SoC02 Tanzania tukiamua, elimu inaweza kuwa silaha dhidi ya maadui watatu wa maendeleo

Stories of Change - 2022 Competition

Polycarp28

New Member
Aug 4, 2022
3
6
Moja kati ya hotuba maarufu sana ya aliyewahi kua muasisi wa taifa letu, Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere ni ile ya mwaka 1995, ambapo kiongozi huyo aliongea kuhusu swala zima la maadui watatu wa maendeleo, ambao ni umasikini, ujinga na maradhi. Katika karne hii ya 21, adui ujinga amekua akipingwa vikali kutokana na kuwepo kwa taasisi mbalimbali zinazotoa elimu katika jamii. Hata hivyo, licha ya kuwepo kwa silaha hii ya elimu, dhidi ua adui ujinga katika nchi hii ya Tanzania, bado jamii haijapata manufaa stahiki kutokana na mchango wa elimu. Hii imetokana na madhaifu mbalimbali yaliyopo kwenye elimu yetu ya Tanzania, ambapo, endapo tuta amua kuyafanyia kazi madhaifu hayo, basi elimu yetu itakua silaha bora katika kupambana na maadui hawa watatu wa maendeleo, na kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa wakati. Madhaifu hayo hameonekana katika maeneo mbalimbali ikiwemo.

Muundo wa elimu ya Tanzania. Kwa miaka mingi nchini, muundo wa elimu yetu umekua ni wa kumzeesha mwanafunzi. Kwa maana kwamba, mwanafunzi amekua akitumia muda mrefu sana shuleni, badala yake angetakiwa amalize masomo mapema ili aweze kulitumikia taifa katika kuleta maendeleo. Mfano, katika elimu ya msingi, mwanafunzi amekua akisoma kwa miak isiyopungua nane (8), katika elimu ya sekondari kwanzia kidato cha kwanza mpaka cha sita, mwanafunzi anatakiwa kusoma kwa miaka sita, na anapofika ngazi ya chuo kikuu, anatakiwa kusoma kwanzia miaka mitatu hadi sita. Hivyo tunapata taswira kua mwanafunzi atatumia zaid ya miaka ishirini shuleni, umri wake pia utakua umesogea, hivyo hata nguvu kazi yake na mchango katika nchi unakua ni mdogo. Hivyo serikali na wizara husika, inapaswa kulitizama swala hili kwa jicho la tatu, kuhakikisha kwamba mwanafunzi hazeeki akiwa shuleni, badala yake azeeke akiwa kazini.


Suala la mitaala ya kufundishia. Suala hili limeonekana pia kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kudhoofisha elimu ya Tanzania, katika vita dhidi ya ujinga, umasikini na maradhi. Mitaala ya elimu ya Tanzania imekua sii mitaala wezeshi katika kuwakwamua vijana wengi wanaohitimu elimu zao. Mitaala ya elimu ya kitanzania imekita zaidi katika elimu ya nadharia zaidi kuliko vitendo, na hivyo kushindwa kumjengea mwanafunzi uzoefu wa kutosha pindi anapokua kazini. Hivyo basi, kungekuwepo kwa mitaala yenye kumpa mwanafunzi muda mrefu wa kujifunza kwa vitendo, ili kimjengea uzoefu na ufanisi, hatimaye aweze kuitumia elimu hiyo katika kuleta mabadiliko katika nchi na katika uchumi kwa ujumla, na ndipo maendeleo yatakapo onekana. Pia katika swala hili la mitaala, kumekua na utaratibu wa ufundishwaji wa mambo ambayo kiuhalisia yamepitwa na wakati kwani hayana mchango wowote katika manedeleo ya nchi yetu. Mfano mzuri ni dhana juu ya historia ya binadamu wa kale, ambapo tunaambiwa binadamu wa kwanza alikua ni sokwe, halafu akabadilika na kuwa binadamu wa sasa. Hii ni dhana potofu na isiyo na uhalisia wowote wala mchango wowote katika uelewa wa mwanafunzi. Na hivyo mada hii pamoja na mada nyingine nyingi ambazo hazina mchango katika elimu na maendeleo kwa ujumla, zingepaswa kuondolewa kabisa katika mitaala ya elimu ya Tanzania, ili kupisha mambo ya msingi na yanayoendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia kuchukua nafasi kwani yana mchango mkubwa sana katika maendeleo.


Suala la mazingira bora ya kujifunzia. Hili ni moja kati ya maswala nyeti sana katika kukua na kuendelea kwa elimu nchini, ili kuweza kuleta maendeleo na kuweza kupambana na maadui hawa watatu wa manendeleo. Kama mazingira ya kupatia elimu yatakua sio rafiki kwa mwanafunzi, elimu pia itakua haina manufaa. Na hii inapelekea matatizo mengi katika jamii ikiwemo watoto kuacha shule na kujiingiza katika makundi mabaya, bila kusahau tatizo la mimba za utotoni ambalo limeota mizizi katika jamii nyingi za kitanzania. Mazingira wezeshi ni uwanda mpana sana kwani unagusa mambo kadha wa kadha. Moja, ni upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia kama vile vitabu na vifaa vya maabara. Katika nchi yetu, vifaa hivi vimekua ni tatizo katika upatikanaji wake, na hivyo kupelekea elimu kua duni kwani wanafunzi wengi wanapata ufaulu wa chini. Lakini pili, ni swala la madarasa. Moja kati ya kero kubwa ni madarasa ambapo watoto wengi wanakosa madarasa ya kusomea na kulazimika kirundikana kwenye darasa moja, na wakati mwingine kusomea chini ya miti. Hivyo ili kutengeneza kizazi cha wasomi wenye tija katika maendeleo ya nchi yetu, ni lazima serikali kuhakikisha kwamba wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia. Tatu, ni upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Hii imekua ni changamoto kubwa sana ambayo imekatisha ndoto za wanafunzi wengi, kwa kushindwa kumudu gharama cha chuo ikiwemo ada. Wanafunzi wengi wanatoka katika familia duni na zenye uwezo mdogo sana, hivyo wanafunzi hawa wanapokosa mkopo kutoka serikalini, wanashindwa kujiendeleza kimasomo. Na hivyo kupelekea kupoteza watu mihimu sana katika nchi, ambao wangezeza kufanya mabadiliko makubwa katika nyanja za kijamii, kiuchumi na kisiasa, na kuchochea maendeleo. Hivyo serikali pamoja na wizara hisika, ingetenga bajeti itakayowanufaisha wanafunzi wengi zaidi ambao ni wahitaji wa mikopo hiyo, kwani tunapoteza wasomi wengi sana na wenye mchango mkubwa katika taifa letu. Yote ni katika kuhakikisha kwamba adui ujinga, maradhi na umasikini wanakua historia katika nchi yetu.

Suala la ajira. Katika miaka ya sasa nchini Tanzania, kusoma kumekua ni jambo moja, ila kupata ajira kumekua ni jambo lingine kabisa!. Swala hili linakatisha tamaa hasa kwa vijana wadogo wenye ndoto za kufanya mabadiliko nchini. Wanafunzi sasa wamekua na wazo kua, kusoma ni lupoteza tu muda kwani hakuna faida yoyte baada ya kusoma, na badala yake, wanapoteza fedha nyingi kwa ajili ya kugharamia masomo yao, lakini mwisho wa siku wanaambiwa "nchini hakuna ajira, vijana mjiajiri wenyewe". Haya ni maneno yenye kuumiza moyo na kukatisha tamaa sana kutoka kwa baadhi ya viongozi wetu tuliowaamini na kuwapa dhamana ya kutuwakilisha huko serikalini. Hii inatupa taswira kwamba, bado hatujajua umuhimu wa elimu yetu, na mchango wake katika maendeleo. Hivyo basi, ningependa kuiomba serikali iliyopo madarakani, pamoja na wizara husika ya kazi na ajira, ambapo sisi wananchi tumewaamini na kuwatuma mtutumikie, kuhakikisha kua tatizo la ajira linatafutiwa mwarobaini, ili kuhakikisha kua elimu iliyopo vichwani mwa vijana wengi, inabadilishwa na kuwa fursa katika kuleta maendeleo nchini, na kuhakikisha kuwa swala la umasikini, ujinga na maradhi linakwisha kabisa kama sio kudhibitiwa kwa kiwango kikubwa.

Hitimisho. Ningependa kuhitimisha chapisho langu kwa kusema kua, elimu bora ndiyo msingi bora wa maendeleo katika nchi yoyote ile duniani. Pasipo elimu bora, ujinga utatawala, umasiki na maradhi yatafwata. Nchi nyingi zilizoendelea na kijikwamua kiuchumi, zilifanikiwa kutokana na kuwepo kwa elimu bora, kwa kuwaajiri wasomi wenye ujuzi mbalimbali katika siasa za uongozi, wafanyakazi wenye ujuzi na weledi katika sekta za kiuchumi kama vile viwanda, kilimo, na sekta za kifedha. Katika nchi yetu ya Tanzania, elimu inapaswa iwepe kipaumbele na kuhakikisha kuwa, madhaifu na changamoto zilizipo kama vile changamoto za kimuundo, mitaala, mazingira bora, pamoja na swala zima la ajiza zinatatuliwa kww haraka ili kuhakikisha kwamba elimu inakua silaha bora na imara katika kupambana na maadui hawa watatu ambao ni umasikini, ujinga na maradhi. Ikumbukwe kwamba, jamii au nchi inapokua na elimu bora, ujinga utaondoka, ujuzi utapatikana kwa kubuni njia mbalimbali za kuongeza pato la nchi na kuinua uchumi, pia kupitia elimu, watu wanapata ujuzi na kusaidia kugundua tiba na chanjo za magonjwa mbalimbali ambayo ni tishio kwa afya zetu na nchi kwa ujumla. Hivyo, maadui hawa watatu wa maendeleo katika nchi yetu watakua ni historia, na ndipo tutakapoyafurahia maendeleo. Ahsante, na kazi iendelee.

MWANDISHI NI POLYCARP P. SILAYO KUTOKA KILIMANJARO, TANZANIA.
SIMU: 0762912431 (Pamoja na WhatsApp).
Email. Silayopolkarpi@gmail.com
 
Back
Top Bottom