[TABLE="class: contentpaneopen"]
[TR]
[TD="class: contentheading, width: 100%"]Wabunge wajitoa kimasomaso kutetea tuhuma zisizowahusu
[/TD]
[TD="class: buttonheading, width: 100%, align: right"]
Send to a friend [/TD]
[/TR]
[/TABLE]
[TABLE="class: contentpaneopen"]
[TR]
[TD="class: createdate"] Sunday, 04 September 2011 21:42
[/TD]
[/TR]
[TR]
[TD] 0digg
Raymond Kaminyoge
BAADHI ya wabunge wamepinga kuhusika kuandaa mkakati wa kumwondoa madarakani, Rais Jakaya Kikwete, kama angeridhia kurejeshwa kazini Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo.
Walisema taarifa hizo ambazo zilichapishwa wiki iliyopita na gazeti moja la kila wiki (siyo Mwananchi) ni uongo zilizolenga kuwachonganisha wabunge na Rais Kikwete. Mbunge wa Jimbo la Sumve (CCM), Richard Ndasa na Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Azzan Zungu, walisema Dar es Salaam jana kuwa hapakuwa na mpango huo.
Ndassa alisema taarifa hizo zilikuwa na kichwa cha habari kuwa ‘Kikwete chupuchupu', ambayo ilieleza kuwa wabunge walikuwa wakiandaa mkakati wa kumwondoa Rais Kikwete madarakani.
Alisema kwenye taarifa hiyo ilielezwa kuwa wabunge walitaka kupiga kura ya kutokuwa na imani na rais, kwa sababu amekuwa akishindwa kuwachukulia hatua watendaji wenye tuhuma mbalimbali.
"Hapakuwapo na mbunge wala wabunge waliokuwa wakiandaa mkakati huo, hiyo ni habari iliyolenga kutuchonganisha na Rais Kikwete jambo ambalo ni hatari," alisema Ndassa.
Alisema ni Rais Kikwete aliyeamua Jairo kuendelea kubaki likizo muda mfupi baada ya Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, kumrudisha kazini.
"Uamuzi huo wa Rais Kikwete kumrudisha Jairo likizo uliungwa mkono na wabunge, sasa tunashangaa mkakati huo wa kumwondoa madarakani ulikuwa na maana gani?" alihoji Ndassa na kuongeza:
"Kama kuna wabunge waliokula njama ya kuandaa mkakati huo, basi watajwe ili wasitiliwe shaka na wananchi."
Sakata la Jairo, liliibuliwa bungeni na Mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shelukindo, ambaye alisema idara zilizo chini ya wizara ya Madini na Nishati zilichangishwa Sh50 milioni kila moja, kufanikisha kupita bajeti ya wizara hiyo.
Kufuatia kauli hiyo, Luhanjo alimpa Jairo likizo yenye malipo ili kupisha uchunguzi uliofanywa na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).Baada ya uchunguzi wa CAG, Jairo alionekana kutokuwa na makosa hali iliyosababisha Luhanjo kumrudisha kazini ndani ya saa 24.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya kuripoti ofisini akipokelewa kwa mbwembwe na wafanyakazi wenzake, Rais Kikwete aliagiza aendelee na likizo kupisha uchunguzi zaidi.
Nani kawatuma wabunge hawa
Ndassa alisema hawajatumwa na mtu yeyote kukanusha habari hiyo, bali wao wakiwa miongoni wa wabunge wameona hawawezi kukaa kimya na kuwaacha wananchi kuamini kilichoandikwa. "Hatukutumwa na mtu yeyote, tumekuja hapa kama wabunge baada ya kuona habari hiyo ya uongo ni hatari kwa usalama wa nchi yetu," alisema Ndassa.
Jibu la Ndasa lilikuja baada ya kuulizwa na mmoja wa waandishi wa habari kuwa, iweje wazungumzie suala hilo wao wakati kuna wasemaji wa Bunge na ofisi ya rais." Tumekuja hapa kama raia yeyote ambaye anaweza kuona uhalifu ukifanyika mahali na kwenda kutoa taarifa polisi," alisema Zungu.
Hatua hiyo inatiliwa mashaka kutokana na kuwa ya kwanza kwa wabunge kuzungumzia tetesi, ilhali zimekuwapo nyingi kwa muda mrefu zinazohusiana na masuala mbalimbali, lakini hakuna wabunge waliowahi kujitokeza kutoa ufafanuzi kwa niaba ya wenzao bila kutumwa na taasisi hiyo.
Kuhusu hatua zitakazochukuliwa, Ndassa alisema hawatarajii kuchukua hatua zozote za kisheria dhidi ya gazeti hilo, bali wanachotaka ni kubadilika na kufuata misingi na maadili ya uandishi wa habari.
[/TD]
[/TR]
[/TABLE]