Taxi - (115)
“Siwezi kukosa mpango... ninao watu wengi kwenye vyombo vya dola wenye kila aina ya mbinu walio kwenye
payroll yangu,” Mr. Oduya alisema huku akiutazama kwa makini ule moshi wa sigara wakati akiutoa. “Nimeshampa kazi Victor, yule shushushu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, anamfahamu vyema Tunu kwa kuwa ni rafiki’ake mkubwa, yeye ndiye aliyempokea jana wakati anatua kiwanja cha ndege. Kwa kumtumia yeye itakuwa ni kete yetu muhimu ya kumpata. Tukishindwa kuitumia nafasi hii
then we are fucked up!”
* * * * *
Baada ya maongezi yake kwenye simu na Mr. Mafuru, Madame Norah aliwageukia watu wengine na kuwatazama kwa muda kama aliyekuwa anatafuta namna ya kuanza kujieleza. Aliwatazama kwa zamu akianza na Sammy, kisha akamtazama Jengo na baadaye macho yake yakaishia kwa Bi. Pamela.
Wakati akiwatazama kwa zamu Madame Norah alikuwa ameuona mshangao kwenye macho ya Sammy, hali ya kusawajika kwenye macho ya Jengo na chuki ya waziwazi kwenye macho ya Bi. Pamela. Alidhani kuwa pengine Bi. Pamela hakuwa amefurahishwa kabisa na ujio wake katika maisha yao.
Ni kweli. Bi. Pamela alihisi donge la wivu likimkaba kooni, ulikuwa ni wivu wa hofu ya kunyang’anywa vyote; mumewe Jengo na Joyce aliyekuwa amuaminisha kuwa yeye ndiye mama yake.
Hata hivyo, Madame Norah alikuwa na ya kwake moyoni, yeye hakumfikiria kabisa Jengo bali mwanawe Joyce. Hadi muda ule hakuyaamini macho yake wala masikio yake. Alijitahidi kuishirikisha akili yake kikamilifu katika kumletea taarifa za kuaminika. Ni kweli alikuwa amempata mwanawe aliyempoteza miaka therathini na mbili iliyopita!
Mwanawe alikuwa hai ingawa muda huo alikuwa akiyapigania maisha yake kitandani, jambo hilo lilimhuzunisha sana Madame Norah, lakini ingalau alijua kuwa Joyce ndiye mwanawe! Kuna muda alihisi labda yupo ndotoni. Hata hivyo, hakutaka kabisa ile iwe ndoto. Kila alipomtazama Jengo na mkewe aliwaona wakiyaepuka macho yake. Ni Sammy peke yake ambaye, mbali na kuwa na majonzi, alikuwa katika hali ya kawaida japo mshangao ulikuwa haujamtoka.
Eneo lile lilianza kutawaliwa na hali ya ukimya ulioanza kumtisha kila mtu. Madame Norah hakuwa ametegemea kama ingemtokea katika Maisha yake, siku kama hiyo, siku ambayo ilimtaka kusimama kidete ili kuhakikisha anairudisha tena furaha iliyomponyoka kwa miaka zaidi ya therathini. Kuna wakati alitamani mambo hayo yaoze na kuteketea kabisa katika roho yake, bahati mbaya hakuwa na namna ya kuyasahau.
“Yaelekea leo ni siku ya ajabu,” Madame Norah aliwaza. “Hakika leo Mungu kaamua kutenda jambo,” alijikuta akisema kwa sauti na kuwafanya watu wote wamtazame kwa mshangao.
Alipogundua kuwa watu wote walikuwa wanamtazama kwa mshangao, Madame Norah alishauri jambo, “Nadhani ninyi wanaume mnaweza kwenda kupumzika mkatuachia kazi hii sisi wanawake, mimi na bibie,” Madame Norah alisema huku akimwangalia Bi. Pamela. “Mwanamke mwenzangu, naomba tuwe na mazungumzo kidogo, kama wanawake.”
Jengo alimtazama Madame Norah kwa mshangao, alionesha kusita sana. Hata Bi. Pamela pia alionesha kusita. Alijiuliza mwanamke yule alitaka kuzungumza naye kuhusu nini lakini hakuweza kubaini. Iliwachukua takriban dakika kumi na tano kufikia mwafaka wa kuzika tofauti zao ili kuangalia namna ya kumsaidia Joyce aweze kupona na kurudi katika Maisha yake ya kawaida.
Kisha Sammy na Jengo wakaondoka wakiwaacha wanawake wawili ambao waliamua kwenda kuketi katika mgahawa uliomo ndani ya Hospitali ya Rufaa ya Amana kwa maongezi kama wazazi wa Joyce, mmoja akiwa mama mzazi na mwingine mama mlezi.
* * * * *
Saa saba kasorobo mchana ilimkuta Tunu akiwa katika eneo la Magomeni Mikumi, alikuwa ametulia ndani ya gari aina ya
Toyota Prado alilolichukua kutoka kwa Victor, alikuwa akimsubiri Victor waliyekubaliana kukutana hapo.
Kwa kiasi fulani alikuwa amefarijika moyoni mwake baada ya kuanza kupata mwanga wa kile kilichomsumbua kushindwa kukikamilisha kwa miaka mitatu. Katika mazungumzo yake na Winifrida aliweza kupata picha kamili ya nani waliomshambulia Joyce. Jambo lililomtatiza kwa nini walikuwa wanatumia nguvu kubwa kupambana na Sammy?
Jambo moja alilolijua ni kwamba gari la Sammy aina ya
Cadillac DeVille lilikuwa likimilikiwa na Omari Oduya, mtoto wa kwanza wa Mr. Oduya ambaye alikimbilia nchini Marekani baada ya kufanya mauaji akimuua aliyekuwa mpenzi wake, Layla Adil.
Wakati huo Tunu alikuwa amerudi toka Israel na alipopata taarifa za mauaji ya Layla, aliumia sana kwa kuwa alimfahamu vyema Layla kwani walisoma darasa moja katika Shule ya Jangwani. Layla alikuwa chotara wa Kiarabu na mwonekano wake mzuri uliwafanya watu wengi kudhani alikusudiwa kuumbwa malaika badala ya binadamu!
Tunu aliamua kufuatilia sakata hilo ili haki itendeke baada ya kuhisi polisi hawakujishughulisha na kesi hiyo kwa kuwa aliyefanya hivyo alikuwa mtoto wa mtu mzito. Kwa kuwa alikuwa na taaluma iliyohitajika sana ya
Computer System Analysis alifanikiwa kujipenyeza na kupata kazi kwenye kampuni ya Mr. Oduya ya
The Splendid Ltd.
Alipofuatilia aligundua kuwa mapenzi kati ya Omari na Layla yalijaa ukatili na unyanyasaji ambao Layla alishindwa kuvumilia na kuamua kuachana na Omari. Chanzo cha haya yote ni Omari kutokukubali kuachwa.
Omari alikuwa akimnyanyasa sana Layla kingono n ahata kwa vipigo na vitisho vya bastola kuwa angemuua. Miezi miwili kabla ya kifo chake Omari alimchukua kinguvu Layla na kumfungia ndani ya nyumba akimpa vipigo na akiwa hawezi kutoka nje. Tukio hilo liliwafanya ndugu wa Layla kuomba msaada kwa jeshi la polisi ili kumtoa ndugu yao ndani ya nyumba hiyo.
Baada ya kufanikiwa kumtoa walipanga kumwondoa nchini na kumpeleka Kenya ili kusitisha uhusiano huo. Ni katika kipindi hicho Omari alimbembeleza sana Layla amrudie lakini Layla alimshauri atafute kwanza msaada wa kisaikolojia kama alitaka warudiane, kwa kuwa alimwona ni mtu wa hasira kila wakati, vipigo visivyoisha na mbaya zaidi akimtishia kumuua mara kwa mara, kitu ambacho siyo cha kawaida.
Aliendelea kumtaka kuwa akishapata msaada wa kisaikolojia ndiyo angekuwa tayari kuwa naye tena ila kwa muda huo alitaka aachwe kwanza. Omari hakukubali, aliamua kuwatumia watu wa baba’ake; Dulla na Uledi kumteka Layla na hatimaye akatekeleza mauaji hayo. Kisha kwa msaada wa baba yake alitorokea nje ya nchi bila kutiwa nguvuni...
Je, nini kitaendelea katika sakata hili lililoibuliwa na Taxi 🚖? Endelea kuwemo kwani safari bado inaendelea 🚴♀️ 🚴♂️ 🚴♂️ hadi kieleweke 🔚...
NB: Litro 👩