Stori ya kusisimua - Taxi

Stori ya kusisimua - Taxi

kwa wake wanaoikandiaga bongo movie nafikiri mmejifunza kitu, huyu Bishop ni script writer wa siku nyingi sana na huwa ana story nzuri sana shida inakuwa ni bajeti,kuan watu wanajitahidi ku shoot na ku edit ila kwa hii story ilivyo ukitaka itoke vizuri siyo bajeti ya milioni 5 halafu kushuti kwa week moja,atleast 50 million(kibongobongo) bajeti kitatoka kitu cha kueleweka kama kilivyo
Wasanii wenyewe wepi?
 
Hii sio arosto n
Mkuu, karibu tujumuike kwenye safari hii...


Taxi - (113)

ILIPOISHIA

Tunu alimwangalia kwa makini huku akiendelea kutabasamu na kusema, “Ndiyo, tafadhali unaweza kuniruhusu kuingia ndani?” Tunu alisema kwa sauti tulivu.

Kidogo Lucy akaonekana kusita, hakumwamini mgeni wake. “Unaweza kuniambia hitaji lako?”

“Naomba uniruhusu niinge ndani, ninahitaji kuonana na Winifrida, nimeelekezwa hapa na kaka’ake anayeitwa Sammy,” Tunu alisema na kugeuza shingo yake, akatazama kushoto na kulia kwake kuhakikisha kuna hali ya usalama kisha halafu akamtazama tena Lucy.

Lucy akashusha pumzi. Kimya kifupi kikapita huku Lucy akionekana kutafakari kisha akauma magego na kufanya mataya yake kuchezacheza kama aliyekuwa anatafuna kitu kigumu. Mara ikasikika sauti ya Victoria, “Dada, kwani unaongea na nani?”

Lucy aligeuza shingo yake na kumwona Victoria akiwa amesimama kwenye baraza kubwa ya ile nyumba. “Anasema amekuja kumwona Winifrida, ameelekezwa hapa na Sammy,” Lucy alisema.

SASA ENDELEA...

Victoria alielekea kule getini na alipofika alichungulia nje, akamwona Tunu akiwa bado amesimama pale pale huku tabasamu usoni kwake likiwa halijaenda likizo. Victoria alimtazama kwa makini. “Habari yako, dada?” Victoria alimsalimia.

“Nzuri, anti... naitwa Tunu na...” Tunu aliitikia na kuanza kujitambulisha.

“Ooh, Tunu! Karibu ndani,” Victoria alisema na kuachia tabasamu pana kisha akamgeukia Lucy. “Mfungulie geti aingize gari lake.”

Lucy alishusha pumzi na kulifungua lile geti kubwa akimruhusu Tunu kuingia. Tunu aliingiza gari lake ndani ya uzio wa ile nyumba, akaliegesha kwenye eneo la wazi jirani na banda maalumu la wazi la maegesho ya magari. Ndani ya banda lile kulikuwa na magari mawili, moja lilikuwa Toyota Hilux double cabin la rangi nyeupe na jingine ni aina ya Landcruiser GX V8 rangi nyeusi.

Alitulia kidogo ndani ya gari akiliacha liungurume kwa dakika chache kisha akazima injini na kushuka. Victoria alimwongoza kuelekea ndani ambako walimkuta Pendo akiwa ameketi juu ya sofa, peke yake, akionekana mwenye huzuni. Winifrida hakuwepo.

Wakati Tunu anaingia Pendo alimwangalia pasipo kuonesha tashwishwi yoyote usoni kwake, akili yake ya kitoto ilikuwa inawaza mbali sana. Alikuwa akimwaza mama yake.

“Shemeji Sammy alinipigia simu kunijulisha kuhusu ujio wako, nilipoona muda unazidi kwenda nikajua labda umeahirisha. Karibu sana, Tunu,” Victoria alisema wakati wanaketi juu ya masofa pale sebuleni.

“Ahsante. Kuna mambo fulani yaliingiliana, ikanibidi kwanza niyaweke sawa ndipo nije huku,” Tunu alisema huku akishusha pumzi kisha akaendelea. “Na kwa kuwa nimechelewa kidogo ningeomba twende moja kwa moja kwenye suala lililonileta hapa... shida yangu ni kuongea na Winifrida, sijui yupo?”

“Alikuwapo hapa sasa hivi, nadhani kaingia chumbani maana tangu tukio la jana hawajihisi tena kama wapo salama,” Victoria alisema na kugeuza shingo yake kumwangalia Pendo. “Huyu ni mtoto wa Sammy.”

Okay!” Tunu alisema huku akimtupia jicho Pendo, “Hujambo, mtoto mzuri?”

“Sijambo, shikamoo anti!” Pendo alisalimia, hakuonesha ule uchangamfu ambao amekuwa nao siku zote.

“Marhaba!” Tunu alisema huku akiachia tabasamu pana.

“Pendo nenda kamwite anti Winnie,” Victoria alimwambia Pendo. Pendo akatoka na kuelekea chumbani huku akiita kwa sauti. “Anti Winnie!”

“Nawahurumia sana hawa watoto, hawako sawa kisaikolojia,” Victoria alisema kwa huzuni.

“Mnapaswa kuhakikisha wanaonana na mwanasaikolojia wa watoto ili ajaribu kuwaweka sawa,” Tunu alishauri.

“Ndiyo maana wapo hapa kwani hiyo ndiyo taaluma yangu. Nimeomba ruhusa ya siku saba kazini ili kushughulikia suala hili,” Victoria alisema na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.

“Umefanya vyema. Hili ni suala tata zito sana na watoto hawa hawawezi kulibeba,” Tunu alisema huku akishusha pumzi. “Pia, awali ya kila jambo tunatakiwa kumshukuru Mungu.”

“Kabisa!” Victoria aliafiki na wakati huo huo Winifrida na Pendo wakaingia sebuleni. Winifrida alimtazama Tunu kwa wasiwasi mkubwa, akashusha pumzi na kumsalimia kisha akaketi juu ya sofa.

Victoria na Tunu wakaangaliana kwa muda kisha Victoria akakohoa kidogo ili kusafisha sauti yake. “Winnie, huyu dada anaitwa Tunu, ameelekezwa hapa na kaka’ako, anataka kuongea na wewe,” Victoria alisema na kuinuka, akamshika mkono Pendo.

“Sasa, da’ Tunu, ngoja tuwaache wenyewe muongee kwa uhuru zaidi,” Victoria alisema huku akianza kuondoka.

“Haina shida, dada. Tukimalizana nitakwambia,” Tunu alisema huku akijiweka sawa pale kwenye sofa. Kikatokea kitambo kifupi cha ukimya, kila mmoja alionekana kutafakari. Winifrida alikuwa anamwangalia Tunu kwa jicho la kuibia, uso wake ulionesha wasiwasi fulani.

“Winnie, kwanza nikupe pole kwa yote yaliyotokea jana usiku... Najua hivi sasa unapitia mengi tu na huoni mtu wa kumweleza. Labda si kosa lako. Na sijui ni kwa nini umeshindwa kumweleza hata kaka’ako, au unaogopa?” Tunu alimuuliza Winifrida huku akiwa ameyatuliza macho yake kwenye uso wake.

Winifrida hakujibu, alibaki kimya akiangalia viganja vyake alivyoviweka juu ya mapaja yake. Tunu aliiona hali ya Winifrida kwa jinsi alivyokuwa na hofu, akatabasamu na kutafuta namna ya kuyaelekeza mazungumzo.

“Niko hapa mimi na wewe, wawili tu...” Tunu alisema na kusita, akashusha pumzi za ndani kwa ndani huku akionekana kama aliyekuwa akitafakari nini cha kusema. “Labda nikutoe wasiwasi, mimi nafanya kazi usalama wa taifa na chochote utakachoniambia, kama hupendi kaka’ako ajue kitabaki kuwa siri kati yetu. Nikutoe hofu kuwa wote waliofanya tukio hilo la kinyama watapatikana tu kama utakuwa muwazi...” Tunu alinyamaza kidogo ili maneno yale yamwingie Winifrida.

“Kwa sasa polisi wapo kazini wanawatafuta, mimi pia nimejitolea kusaidia ili kuhakikisha wote wanakamatwa... labda tu nikudokeze kuwa wapo watu ninaowahisi kufanya tukio hilo na ninazo picha zao, kwa hiyo huna sababu ya kunificha chochote unachokijua.” Tunu aliweka kituo, akaminya midomo yake yenye maki na kuficha vishimo vidogo vijitokeze kwenye mashavu yake.

“Sijui umenielewa?” Tunu alimuuliza Winifrida huku akimwangalia kwa makini.

“Nimekuelewa, dada,” Winifrida alisema, akavuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu huku akifanya kifua chake kipande na kushuka. Matiti yake madogo yaliyochongoka yalimiliki vyema eneo la kifua.

Tunu alitoa simu yake ya mkononi, ilikuwa simu nzuri na mpya kabisa aina ya iPhone 11 Pro Max, akaanza kupekuapekua kwenye ile simu kisha akamwonesha Winifrida picha ya Spoiler. “Ulimwona mtu mwenye sura kama hii?” alimuuliza huku akimtazama katika hali ya kumkagua.

Inaendelea

CC the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater Bigjahman moneytalk marybaby nipo2 ram kisukari Smart911 Madame S carbamazepine Astelia culture gal Prisoner of hope Mine eyes kuku mweus Thad hearly Shunie Tumosa Mine eyes Kudo swahiba92 ludist Toyota escudo Clkey macson3 boga la kiangazi LEGE Smart911 Richard irakunda skfull popie Krizy Beat hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami mbududa iron2012 popie Bughy Harry Mlenge Kacheda mjasiliamali Laki Si Pesa cocochanel kinusikwetu big jambo mludego Shupavu Kacheda mjasiliamali Mweweso Songa Heri esiankiki mnadhimu mkuu wa jf red apple the-sniper MR KUO dan oseko Jackal

NB: Litro 👩
Asante Mkuu
Nakufuatilia barabara kabisa
 
Taxi - (116)

ILIPOISHIA

Alipofuatilia aligundua kuwa mapenzi kati ya Omari na Layla yalijaa ukatili na unyanyasaji ambao Layla alishindwa kuvumilia na kuamua kuachana na Omari. Chanzo cha haya yote ni Omari kutokukubali kuachwa.

Omari alikuwa akimnyanyasa sana Layla kingono n ahata kwa vipigo na vitisho vya bastola kuwa angemuua. Miezi miwili kabla ya kifo chake Omari alimchukua kinguvu Layla na kumfungia ndani ya nyumba akimpa vipigo na akiwa hawezi kutoka nje. Tukio hilo liliwafanya ndugu wa Layla kuomba msaada kwa jeshi la polisi ili kumtoa ndugu yao ndani ya nyumba hiyo.

Baada ya kufanikiwa kumtoa walipanga kumwondoa nchini na kumpeleka Kenya ili kusitisha uhusiano huo. Ni katika kipindi hicho Omari alimbembeleza sana Layla amrudie lakini Layla alimshauri atafute kwanza msaada wa kisaikolojia kama alitaka warudiane, kwa kuwa alimwona ni mtu wa hasira kila wakati, vipigo visivyoisha na mbaya zaidi akimtishia kumuua mara kwa mara, kitu ambacho siyo cha kawaida.

Aliendelea kumtaka kuwa akishapata msaada wa kisaikolojia ndiyo angekuwa tayari kuwa naye tena ila kwa muda huo alitaka aachwe kwanza. Omari hakukubali, aliamua kuwatumia watu wa baba’ake; Dulla na Uledi kumteka Layla na hatimaye akatekeleza mauaji hayo. Kisha kwa msaada wa baba yake alitorokea nje ya nchi bila kutiwa nguvuni...

SASA ENDELEA...

Akiwa anaendelea kufanya kazi katika kampuni ya The Splendid Ltd aliweza kugundua mambo mengine zaidi ya kutisha kuhusu biashara za bilionea huyo, washirika wake na mikakati yake ya kutaka kuingia ikulu kwa gharama yoyote ile. Aliweza pia kubaini suala la mateso n ahata mauaji ya wote waliojitokeza kuwa tishio kwa maslahi ya bilionea huyo kama ilivyokuwa kwa Jaji Lutego.

Mawazo yalizidi kupita kichwani kwa Tunu yakimkumbusha moja ya kumbukumbu mbaya sana iliyomfanya aape kuwa lazima siku moja Omari na baba yake Mr. Oduya walipe gharama za uhalifu wao na haki itendeke. Katika uchunguzi wake ndipo likaja sakata la memory card ambayo aliipoteza siku hiyo hiyo, ikaangukia mikononi mwa watu wa Mr. Oduya lakini sasa ilikuwa mikononi mwa Winifrida. Ni kitu kilichomsisimua zaidi. Memory card!

Alishaanza kukata tamaa ya kuipata tena na wakati mwingine alidhani angetumia nguvu kubwa zaidi kuipata, lakini sasa alikuwa ameaminishwa na Winifrida kuwa ndiye aliyekuwa akiishikilia kwa wakati huo na kwamba alikuwa ameiacha kule nyumbani kwa Sammy, akiogopa kutembea nayo kwani ni kitu hatari kuliko hata hatari yenyewe.

Jambo lililomuumiza zaidi kichwa Tunu kwa wakati huo ni jinsi ya kuipata tena hiyo memory card toka nyumbani kwa Sammy kabla haijaangukia tena kwenye mikono ya watu wengine. Alipaswa kuipata haraka iwezekanavyo kabla mtu mwingine hajaipata ila asingeweza kwenda nyumbani kwa Sammy na kuingia ndani pasipo msaada na uwepo wa Winifrida, ambaye kwa wakati huo alikuwa nyumbani kwa Elli na hakutakiwa kutoka nje.

Pia Tunu asingeweza kumwambia Sammy kuhusu kadi hiyo kwa kuwa Winifrida alimsihi sana asimwambie Sammy juu ya uwepo wa kadi hiyo wala suala la yeye kumiliki simu ya mkononi.

Tunu alijikuta akisisimkwa mwili kila alipoifikiria ile memory card akiamini kuwa endapo angeitia mkononi basi angekuwa na ushahidi mzito wa kumfanya Mr. Oduya na genge lake wasalimu amri kwani wasingekuwa na mahali pa kutokea.

Muda wote wa mawazo yale Tunu alikuwa amejiegemeza kwenye siti ndani ya gari lakini macho yake yakiwa yanatazama nje ya gari. Alizungusha macho yake huku na kule kana kwamba alikuwa anatafuta kitu fulani. Alipokosa anachokitafuta, akafumba macho yake na kurejesha mawazo yake kwenye jukumu lililokuwa mbele yake.

Alishtuka akaitazama saa yake ya mkononi, ilimwonesha kuwa dakika therathini na tano zilikuwa zimeshakatika tangu afike mahali hapo walipokuwa wamekubaliana kukutana. Dakika therathini na tano! Tunu alishtuka sana, muda huo kwake ulikuwa ni kama amesubiri kwa siku nzima. Hakuwa na muda wa kupoteza kwa sababu kwake muda ni mali ati!

Aliendelea kuikodolea macho saa yake na kutingisha kichwa chake taratibu kushoto na kulia huku akisonya kwa masikitiko. Laiti ingekuwa ni saa ya kawaida angesema labda ina kasoro. Lakini saa yake, kama ilivyo kwa vitu vyake vingi, haikuwa ya mchezomchezo. Ilikuwa ni saa ghali aliyoinunua nchini Switzerland ikiwa na gerentii ya miaka hamsini.

Hata hivyo, hakuwa na namna nyingine ya kufanya isipokuwa kuendelea kusubiri, akashusha pumzi za ndani kwa ndani na kutoa simu yake, akajaribu kumpigia Victor lakini mlio aliousikia toka upande wa pili wa simu ulimwonesha kuwa simu ile ilikuwa ‘busy’ muda wote. Tunu akashusha pumzi na kuanza kuperuzi kwenye mtandao wa intaneti akisoma habari maana tangu afike jijini Dar es Salaam hakuwa na mud ahata wa kusoma magazeti. Ingalau sasa alikuwa na kitu kilichokuwa kinamsogezea muda.

Baada ya kama dakika kumi, akaliona gari aina ya BMW X6 xDrive 50i lililokuwa likija mbele yake katika barabara ile ya Mikumi likitokea upande wa Mwembechai, aliweza kulitambua vyema kuwa ndilo gari alilokuwa amemwachia Victor. Akamwashia taa mara mbili kama ishara ya kumjulisha kuwa amemuona. Victor naye aliwasha taa mara mbili kisha alimpita kidogo na kuliegesha nyuma ya gari alilokuwemo Tunu, takriban mita ishirini kutoka alipokuwa Tunu. Akashuka haraka na kumfuata Tunu.

“Mbona umechelewa sana?” Tunu alimdaka Victor juu kwa juu baada ya kumfikia, alimuuliza huku akimtazama kwa makini pasipo hata kupepesa macho yake.

“Nisamehe, nilikuwa na ishu fulani nyeti ya kumalizia. Pole sana kwa kusubiri,” Victor alijitetea huku akiachia tabasamu, akatazama kando kuyakwepa macho makali ya Tunu yaliyokuwa yanamtazama kwa makini pasipo kupepesa.

“Dah, n’tafanyaje! Hata nikisema nikulaumu bado haitasaidia. Unajua nina mambo kibao ambayo natakiwa niyakamilishe leoleo, sijui kama nitaweza ku-meet deadline,” Tunu alisema huku akifungua mlango wa gari alilokuwemo na kushuka.

“Kwani una mishemishe gani mjini, naona tangu umekuja uko mbiombio tu na wala hatuelezani!” Victor alimuuliza Tunu huku akimtazama kwa makini katika namna ya kumkagua.

“Nitakueleza, ngoja kwanza niweke mambo fulani sawa kabla hayajaharibika,” Tunu alisema na kupokea ufunguo wa gari lake toka kwa Victor kisha akataka kupiga hatua kuelekea kwenye gari lake lakini akaonekana kukumbuka jambo na kugeuka, akamtazama Victor kwa makini.

“Gari langu halijakuletea usumbufu wowote?” Tunu aliuliza huku akimkazia macho Victor.

“Usumbufu wa vipi labda?” ilikuwa ni zamu ya Victor kuuliza, uso wake ulionesha mshangao.

“Hakuna watu wowote waliokuwa wanakufuatilia?” Tunu aliuliza tena huku akiendelea kumkazia macho Victor.

“Kunifuatilia kuhusu nini? Kwani kuna nini kinaendelea?” Victor naye aliuliza tena swali badala ya kujibu, akaongeza, “Inaonesha una vitu unavijua lakini hutaki kunishirikisha!”

“Nitakwambia siku nyingine, ngoja niwahi sehemu,” Tunu alisema na kuanza kuondoka lakini Victor akamzuia. Wakatazamana moja kwa moja machoni kama vile walikuwa wanasomana mawazo yao.

Inaendelea...

CC the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater Bigjahman moneytalk marybaby nipo2 ram kisukari Smart911 Madame S carbamazepine Astelia culture gal Prisoner of hope Mine eyes kuku mweus Thad hearly Shunie Tumosa Mine eyes Kudo swahiba92 ludist Toyota escudo Clkey macson3 boga la kiangazi LEGE Smart911 Richard irakunda skfull popie Krizy Beat hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami mbududa iron2012 popie Bughy Harry Mlenge Kacheda mjasiliamali Laki Si Pesa cocochanel kinusikwetu big jambo mludego Shupavu Kacheda mjasiliamali Mweweso Songa Heri esiankiki mnadhimu mkuu wa jf red apple the-sniper MR KUO dan oseko Jackal kuku mweus

NB: Litro 👩‍🦱
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom