Stori ya kusisimua - Taxi

Stori ya kusisimua - Taxi

Taxi - (117)

“Dah! Naona sasa hivi hatuaminiani tena, mshikaji wangu! You don’t trust me any more,” Victor alilalamika huku akiendelea kumkazia macho Tunu.

Don’t be silly... you know the rule of the game. Muda mwafaka ukifika utayajua yote unayotaka kuyajua,” Tunu alisema huku akitaka kuondoka lakini Victor aliushika mkono wake, safari hii aliung’ang’ania.

Wakatazamana tena kwa kitambo fulani kisha Victor akashusha pumzi na kuachia tabasamu. Halikuwa tabasamu la furaha bali lilikuwa limeficha kitu fulani kisichoeleweka ndani yake.

Okay! Nakutakia mafanikio mema, ukihisi unanihitaji unajua wapi pa kunipata,” Victor alisema huku akiendelea kutabasamu.

Tunu alimtazama Victor kwa umakini zaidi, alihisi kugundua kitu kama kebehi katika sauti yake. Naam, aliweza hata kuiona waziwazi katika macho yake ambayo yalikuwa yakimdhihaki waziwazi ingawa mdomo wake ulikuwa hauna dhihaka yoyote.

“Haina shida, nitakutafuta,” Tunu alimjibu kwa sauti tulivu kisha akauondoa mkono wake toka kwenye mikono yenye nguvu ya Victor na kuanza kupiga hatua kuelekea kwenye gari lake. Akasita tena baada ya kuhisi kulikuwa na mtu mwingine wa tatu aliyekuwa anawatazama kwa makini.

Tunu aligeuza shingo yake kuangalia upande wake wa kushoto alikokuwepo yule mwanamume, akamwona mwanamume mmoja mwenye mwili alioshiba akiwa ameketi kwenye kiti cha plastiki katika kibanda cha muuza chipsi. Alikuwa amevaa suti maridadi nyeusi, miwani mikubwa myeusi ya jua iliyoyafunika macho yake na kofia kubwa ya pama. Tunu alimtazama kwa makini lakini hakuweza kumtambua.

Mwanamume yule alikuwa ametulia tuli kwenye kiti chake akiwa ameshika gazeti la Kiingereza la Daily News akionekana kujisomea gazeti lakini Tunu aliweza kugundua kuwa hakuwa akilisoma lile gazeti bali macho yake yalikuwa yakiwatazama kwa kuwachunguza. Mbele ya yule mtu kulikuwa meza ndogo ya plastiki ikiwa na sahani yenye mabaki ya chipsi iliyokuwa tupu na chupa ya soda. Tunu akashangaa sana, kwani kwa muda wote aliokuwa akisubiri eneo lile hakuwa amemwona yule mtu.

“Unamjua?” Tunu alimuuliza Victor kwa sauti ya kunong’oneza huku akimwoneshea kwa ishara mahali alipoketi yule mtu. Victor aligeuza shingo yake na kumtazama yule mwanamume mara moja tu na kisha kuurejesha uso wake kwa Tunu, akatingisha kichwa chake taratibu kukataa.

“Sidhani kama ana lolote la maana la kutufanya tumzingatie, au wewe umeona nini cha ajabu kwake?”” Victor alisema huku akishusha pumzi. Hata hivyo, Tunu aliweza kugundua kitu fulani kisicho cha kawaida kwenye sauti na macho ya Victor. Fadhaa.

Tunu akajifanya kutabasamu na kuzungusha macho yake kutazama sehemu nyingine ingawa akili yake ilikuwa kwa yule mwanamume. “Kuna ubaya wowote mtu kuchukua tahadhari?” akamuuliza Victor huku akishusha pumzi.

“Hakuna ubaya. Nadhani inapendeza zaidi kuwa na tahadhari kwa kila jambo,” Victor alisema na kuachia tabasamu pasipo kuonesha meno yake kisha akaingia ndani ya gari lake na kuwasha injini. “Okay, basi tutawasiliana,” alisema na kuondoa gari pasipo kusubiri jibu la Tunu.

Tunu alizidi kushangaa, alishusha pumzi na wakati huo akili yake ilikuwa inafanya kazi haraka haraka. Alijiuliza yule mwanamume ni nani na kwa nini alionekana kuwachunguza? Kwa nini Victor anaonekana kubadilika na kwa mara ya kwanza kuzipuuza hisia zake? Tunu alihisi kuwepo kwa kitu kisicho cha kawaida kwa Victor. Alihisi kuona kitu kisicho cha kawaida, ila hakujua aliona nini.

Akaelekea kwenye gari lake na kuingia kisha akatulia kwenye usukani wake kwa dakika kadhaa akimchunguza yule mwanamume. Mara akamuona akiitazama kwa makini simu yake ya mkononi iliyokuwa inaita kisha akaipokea na kuipeleka sikioni. Aliongea kwa sekunde kadhaa na kuonesha mshtuko, akageuza shingo yake na kutazama kwa wizi kule lilikokuwa gari la Tunu, kisha akabetua kichwa chake na kuinuka.

Tunu aliendelea kutulia kwenye siti yake akimfuatilia yule mwanamume kwa kila hatua aliyokuwa akiifanya, akamwona akijinyoosha kisha akawa anazungumza na kijana muuza chipsi huku macho yake yakiwa makini kumtazama Tunu. Tunu alichukua simu yake lakini kabla hajafanya chochote akamtupia tena jicho yule mwanamume, hakumwona! Tayari alikuwa ametoweka, na wala Tunu hakujua amelekea wapi.

Aliminya midomo yake, akawasha gari na kuondoka. Alikuwa anaelekea hospitali ya Amana kuonana na Sammy ili ampe tahadhari kutokana na mambo fulani aliyoyagundua. Aliingia barabara ya Kawawa na mwendo wake ulikuwa wa wastani huku akiwa makini kuangalia nyuma kama kulikuwa na gari lolote alilolitilia shaka likimfuatilia lakini hakuona. Akashangaa.

Aliendesha akilivuka bonde la Kigogo, bado mwendo wake ulikuwa ni wa wastani hadi alipofika kwenye mzunguko wa barabara za Kawawa na Kigogo akaamua kuiacha barabara ya Kawawa na kungia kushoto akiifuata barabara ya Kigogo iliyokuwa inapita jirani na Shule ya Msingi Gilman Rutihinda, akachunguza nyuma yake. Hakuona gari lolote lililokuwa linamfuatilia. Akashtuka.

Akahisi kuwa jambo hilo halikuwa la kawaida. Hakujua ni nini kilikuwa kinaendelea lakini hisia zake zilimtanabahisha kuwa hali haikuwa shwari kama alivyotaka kujiaminisha. Siku zote hakupenda kuzipuuza hisia zake, alichukua simu yake na kumpigia Tom, akamweleza kuhusu alichokuwa akihisi na kumpa taarifa za mambo mengine yote kuwa yalikuwa yameenda kama yalivyopangwa.

Inaendelea...

NB: Litro 👩‍🦱
 
Taxi - (118)

Waliongea kwa dakika kadhaa kisha wakakubaliana, alipokata simu akabadili uelekeo, badala ya kuelekea hospitali ya Amana akaelekeza gari lake eneo la Shaurimoyo, Ilala.

* * * * *

Sammy na Jengo walipoondoka pale hospitali ya Amana na kuwaacha Madame Norah na Bi. Pamela, walielekea moja kwa moja katika mgahawa wa kisasa wa Elli’s ili kupata chakula. Wakati wakienda huko hawakujua kuwa walikuwa wanafuatwa. Kulikuwa na gari jingine aina ya Toyota Vanguard jeusi lenye vioo vya tinted visivyomruhusu mtu kuona ndani lilikuwa linawafuatilia.

Walipofika hapo Elli’s Sammy aliegesha gari lake kwenye maegesho, wakaingia ndani ya mgahawa na iliwachukua dakika arobaini na tano kupata chakula na kutoka nje tayari kwa safari ya kuelekea kwenye makazi ya Sammy. Waliagana na Elli kwa ahadi ya kumpitia pale kwenye mgahawa muda wa jioni wakati wanaelekea hospitali ya Amana.

Wakajipaki kwenye gari lao walilokuja nalo na kutimka eneo hilo. Dakika takriban mbili tu tangu waondoke, lile Toyota Vanguard likawashwa na kuanza kuwafuatilia, lakini wakiwa na tahadhari zote, hadi walipofika nyumbani kwa Sammy eneo la Tabata Chang’ombe.

“Karibu sana, baba,” Sammy alimkaribisha baba mkwe wake, Jengo mara tu walipoingia ndani.

“Ahsante sana, mwanangu,” Jengo alijibu huku akijipweteka juu ya sofa. Alionekana kuchoka sana na macho yake yalikuwa yamelewa kutokana na kukosa usingizi.

Sammy aliyabeba mabegi waliyokuja nayo na kuelekea vyumbani akiyapeleka kwenye chumba maalumu cha wageni akimwacha Jengo mpweke. Baada ya kama dakika tano hivi alirejea na kumkuta Jengo akinyemelewa na usingizi pale pale sebuleni kwenye sofa. Miguu yake alikuwa kainyoosha. Alikuwa mchovu aliyechoshwa na mambo mengi, usingizi, safari na mawazo juu ya hali ya binti’ake Joyce.

Sammy alimwangalia kwa makini akamhurumia kisha alimwamsha na kumwelekeza chumba ili akajipumzishe kisha yeye alielekea chumbani kwake na kuingia moja kwa moja bafuni ili kupooza mwili wake. Alijimwagia maji harakaharaka kisha akajirejesha pale sebuleni ambapo alishangaa kumkuta mkwe wake akiwa bado ameketi palepale, sasa usingizi ulikuwa umemchukua kabisa.

Sammy hakutaka kumwamsha, akaketi na kuwasha runinga huku akiweka sauti ndogo akichelea kumwamsha mkwewe. Si kwamba alikuwa anatazana runinga hiyo bali ilikuwa inampa tu ‘kampani’ na kujaribu kumsahaulisha huzuni ya mkasa uliomkuta mkewe. Alijaribu kuwaza mambo kadhaa kuhusu mkasa ule, mara akahisi sauti hafifu ya kishindo ndani ya uwa wa nyumba yake.

Alinyanyuka haraka akatazama dirishani na kisha mlangoni, hakuona mtu. Akaelekea upande wa mlango wa jikoni, patupu! Akatoka nje na kuzunguka kuelekea upande wa mbele alipoegesha gari lake, akabaini kulikuwa na sauti ndogo ya kubipu. Alipata shaka, akatazama huku na kule akisaka na baada ya sekunde kama tano hivi akabaini kulikuwa na kitu fulani kimepachikwa kwenye gari! Akahisi kuwa eneo lile halikuwa salama.

“Bomu!” Sammy akawaza, na hapo akili yake ikafanya kazi haraka sana. Alirudi ndani haraka, akamshtua Jengo kuhusu uwepo wa bomu, wakatoka na kukimbilia upande wa nyuma wa ile nyumba kulikokuwa na geti dogo la dharura. Muda huo bomu lilikuwa limebakia kama sekunde tano tu kulipuka. Hata hivyo alibaini kuwa wasingeweza kufanikiwa kufungua lile geti na kutoka ndani ya muda.

“Baba, lala chini!” Sammy alimwamuru baba mkwe wake huku yeye mwenyewe akijitupa chini na kulala kifudifudi. Sekunde mbili baadaye ukasikika mlipuko mkubwa na kuisambaratisha kabisa nyumba ya Sammy. Sammy na Jengo wakaangukiwa na mabaki ya ile nyumba. Fahamu zikawapotea.

* * * * *

Gari la kifahari aina ya Range Rover Velar la rangi nyeupe liliingia kwenye geti la kuingilia la hospitali ya Amana na kuelekezwa moja kwa moja kwenye viunga vya maegesho, likaegeshwa. Mr. Oduya na Mr. Mafuru wakashuka toka ndani ya gari na kuanza kukatiza eneo lile la maegesho. Mr. Mafuru alitoa simu yake na kumpigia Madame Norah.

“Madame, tayari tumeshafika hapa hospitali ya Amana, uko sehemu gani?” Mr. Mafuru aliongea baada ya simu kupokelewa.

“Njooni hapa kwenye mgahawa, mtatukuta tumeketi hapa,” Madame Norah alisema na mara simu ikakatwa.

Wakati wakielekea pale kwenye mgahawa kama walivyoelekezwa na Madame Norah, simu ya Mr. Oduya ikaanza kuita. Aliitoa na kuiangalia, akashusha pumzi na kuminya midomi yake, kisha akaipokea na kuiweka moja kwa moja sikioni. “Hallo!”

“Mzee, tayari kazi imeisha. Nimeshatekeleza ule mpango mzima na hakuna kilichotoka ndani,” sauti toka upande wa pili wa simu ikasikika.

“Umehakikisha haujaacha kielelezo chochote?” Mr. Oduya akauliza kwa sauti iliyoonesha wasiwasi ili kupata uhakika.

“Usiwe na wasiwasi, mkuu, kila kitu kimekwenda kama kilivyopangwa. Bado yule malaya tu,” mtu upande wa pili wa simu alijibu kwa kujiamini.

“Vizuri, lakini kumbuka yule ni mtu hatari mno na wewe kazi hii ni mpango wa kando, kosa lolote hata dogo linaweza kukugharimu na kitakachofuata kinaweza kuwa kibaya siyo kwako tu, bali kwetu sote, sijui umenielewa?” Mr. Oduya alisema huku akipiga hatua taratibu.

“Kwa hilo wala usijali, mkuu. Niko makini sana,” alisema yule mtu na simu ikakatwa. Mr. Oduya akaachia tabasamu na kutembea haraka kwa kujiamini akimfuata Mr. Mafuru aliyekuwa ametangulia mbele.

Walipotokea jirani na mgahawa wakamwona Madame Norah aliyekuwa anapunga mkono wake kuwaonesha mahali alipoketi akiwa ameketi na mwanamke mwingine ambaye hawakuweza kumtambua. Mr. Oduya na Mafuru wakamfuata, wakawasalimia wote huku wakiwapa pole kwa mkasa ule uliotokea.

Mambo bado ni 🔥🔥🔥 kwelikweli. Naona Mr. Oduya ameamua kufuta kabisa ushahidi. Je, nini kitaendelea? Ndoto ya Tunu kuipata memory card itafanikiwa? Usikose kufuatilia mkasa huu wa kusisimua uliosababishwa na 🚖...

NB: Litro 👩‍🦱
 
Ooh Sammy nyumba tena imelipuliwa kaz hamna mke mahututi askofu unatingisha sana mtima wangu msomaji😩
 
Bishop ee naomba basi nyingine mtunzi mahiri kabsaa japo mbili sjui zisindikize jioni hii njema baba chonde
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom