Stori ya kusisimua - Taxi

Stori ya kusisimua - Taxi

Taxi - (112)

Akiwa anamalizia kulivuka lile daraja na kabla hajayafikia maeneo yaliyokuwa yamehifadhi makontena ghafla lile lile gari aina yaToyota Alphard jeusi likampita kwa kasi na kumzuia kwa mbele. Kilikuwa ni kitendo cha kushtukiza na Victor hakuwa na namna, akakanya breki huku akilipeleka gari lake kando ya barabara na kulifanya gari lake liserereke kisha likasimama hatua tano toka lilipokuwa limesimama gari aina yaToyota Alphard. Alipiga ngumi kwenye usukani huku akitweta kwa hasira, akalitazama lile gari lililomzuia kwa hasira zilizochanganyika na mshangao.

Kitendo cha haraka sana kikafanyika, Spoiler na Job walishuka toka kwenye gari lao na kulifuata lile gari aina ya BMW X6 xDrive 50i alilokuwemo Victor. Spoiler akauvuta mlango wa dereva. Akajikuta akipigwa na butwaa baada ya kumwona Victor badala ya Tunu! Wakaangaliana kwa sekunde kadhaa kwa namna ambayo ni wao wawili tu walioelewa maana yake.

Shit!” Spoiler alisema huku akishusha pumzi kisha akageuza shingo yake kutazama huku na huko. Tunu alikuwa kawapiga chenga ya akili na mwili.

“Kwani vipi, wazee, mbona sielewi!” Victor aliuliza kwa mshangao huku akiwatazama Spoiler na Job kwa zamu.

“Victor, kwani... hili si gari alilokuwa nalo Tunu leo, au yanafanana?” Spoiler alimuuliza Victor akiwa haamini alichokuwa akikiona mbele yake.

“Ndiyo hili, kaniachia sasa hivi na yeye kachukua la kwangu,” Victor alisema na kushusha pumzi, “Kwani kafanya nini?” akauliza akiwa bado anashangaa.

Muda huo magari mengine yakaanza kupiga honi kumtaka dereva gari aina ya yaToyota Alphard kuliegesha kando ya barabara. Job hakuwa mbishi, aliingia ndani ya gari kisha akalisogeza pembeni kabisa ya barabara ili kuyapisha magari mengine yapite.

“Tayari tumeshachezewa shere!” Spoiler alisema huku kashika kiuno chake kwa mikono yote miwili, alionekana kukata tamaa.

“Haha! Kama mlikuwa mnafuata Tunu, mmeshapotezwa!” Victor aliongea huku akiangua kicheko na kuongeza, “Kwani kuna ishu gani, mzaee, mbona husemi pengine naweza kusaidia.”

“Hayo ndo maneno, ngoja nije nikupe mkanda mzima,” Spoiler alisema huku akizunguka upande wa pili wa lile gari, akafungua mlango na kuingia ndani ya gari, akaketi huku akimkabili Victor.

* * * * *

Saa sita mchana, Pendo na Winifrida walikuwa wamekaa juu ya sofa kwenye sebule ya nyumba moja kubwa ya kisasa ya ghorofa moja katika eneo la Kurasini. Sebule hiyo ilikuwa na samani mbalimbali za gharama kama seti mbili za makochi ya sofa ya kifahari yaliyopangwa kwa ustadi wa hali ya juu katika mtindo wa kuizunguka ile sebule na katikati ya sebule kukiwa na meza fupi ya kioo yenye umbo la yai.

Pendo alikuwa kifua wazi na alikuwa anagombana na Winifrida aliyekuwa anamlazimisha kuvaa shati. Muda huo huo mwanamke mmoja mwenye umbo kubwa kiasi lililokuwa linavutia mno aliingia pale sebuleni baada ya kusikia kelele za Pendo. Alikuwa mrefu wa wastani, mweupe kiasi mwenye mashavu mfano wa chungwa na nywele zake zilikuwa nyingi na nyeusi fii.

Mwanamke yule alikuwa amevaa gauni jepesi na pana kiasi lililoishia magotini na kuifichua miguu yake mizuri huku ikilichora vyema umbo lake maridhawa. Gauni lile lilikuwa linalichora vyema tumbo lake lenye ujauzito wa miezi saba na kiuno chake chembamba lakini imara kilichoshikilia minofu ya mapaja yake iliyokaza kutoka na ratiba nzuri ya mazoezi. Aliitwa Victoria, alikuwa mke wa Elli Kiango.

“Pendo, unagombana nini na anti Winnie?” Victoria alimuuliza Pendo kwa upole huku akiketi karibu yake na kumshika kichwani.

“Eti anti Winnie ananilazimisha kuvaa shati.”

“Sasa kwa nini hutaki kuvaa?”

“Kuna joto, anti.”

“Unasikia joto? Kama unasikia joto sawa,” Victoria alisema kwa upole huku akishusha pumzi. “Lakini...” alitaka kuongeza lakini akakatishwa na sauti ya kengele ya getini iliyoashiria kuwa kulikuwa na mtu nje ya geti.

“Dada!” Victoria alipaza sauti kumwita msichana wa kazi aliyekuwa sehemu fulani mle ndani.

“Abee!” yule mfanyakazi alipaza sauti yake kuitika na baada ya sekunde chache akatokea, alikuwa mdada ambaye kiumri alikuwa na miaka isiyopungua ishirini na tano na hakuzidi miaka therathini. Alikuwa na mwili mpana ila mkakamavu na alivalia gauni refu na kujifunga apron, akionekana alikuwa jikoni akiandaa chakula.

“Hebu kaangalie getini kuna nani!” Victoria alimwambia yule mdada wa kazi.

Yule mdada ambaye aliitwa Lucy alielekea getini, akafungua geti dogo lililokuwa kando ya lile geti kubwa na kuchungulia nje, akamwona mwanadada mmoja mrefu na maji ya kunde mwenye nywele fupi na laini alizozitia rangi. Wakatazamana kwa sekunde kadhaa halafu yule mwanadada akaachia tabasamu lililovifanya vishimo vidogo kwenye mashavu yake vichomoze. Yule mwanadada alikuwa Tunu.

Tabasamu lile likamfanya Lucy naye aachie tabasamu huku akiyatupa macho yake kulitazama gari alilokuja nalo aina ya Toyota Prado.

“Karibu, sijui naweza kukusaidia?” Lucy alimuuliza Tunu akiwa amelifungua lile geti dogo nusu, kichwa kipo nje na kiwiliwili chake chote kikiwa ndani, mkono wake ulikuwa karibu kabisa na mlango kwa lolote ambalo lingetokea.

Tunu alimwangalia kwa makini huku akiendelea kutabasamu na kusema, “Ndiyo, tafadhali unaweza kuniruhusu kuingia ndani?” Tunu alisema kwa sauti tulivu.

Kidogo Lucy akaonekana kusita, hakumwamini mgeni wake. “Unaweza kuniambia hitaji lako?”

“Naomba uniruhusu niinge ndani, ninahitaji kuonana na Winifrida, nimeelekezwa hapa na kaka’ake anayeitwa Sammy,” Tunu alisema na kugeuza shingo yake, akatazama kushoto na kulia kwake kuhakikisha kuna hali ya usalama kisha halafu akamtazama tena Lucy.

Lucy akashusha pumzi. Kimya kifupi kikapita huku Lucy akionekana kutafakari kisha akauma magego na kufanya mataya yake kuchezacheza kama aliyekuwa anatafuna kitu kigumu. Mara ikasikika sauti ya Victoria, “Dada, kwani unaongea na nani?”

Lucy aligeuza shingo yake na kumwona Victoria akiwa amesimama kwenye baraza kubwa ya ile nyumba. “Anasema amekuja kumwona Winifrida, ameelekezwa hapa na Sammy,” Lucy alisema.

Je, Spoiler na Victor wanapanga mkakati gani juu ya Tunu? Victor anafahamiana vipi na kina Spoiler, na je, atamsaliti Tunu? Vipi kuhusu Winifrida, atamweleza ukweli Tunu? Endelea kufuatilia stori hii ya kusisimua...
 
Wakuu, mkiona kimya msihofu, wiki hii nimebanwa kidogo na majukumu fulani ya kikazi✍✍✍. Nadhani kuanzia keshokutwa, Mungu akipenda, tunaweza kuendelea na mtiririko wetu wa hadithi kama kawaida...😜😜😜 wacha niingie tena chimbo...🏃‍♂️🏃‍♂️🏃‍♂️
 
🤣🤣🤣 msihangaike, nimeshatupia mbili. Kwa leo zinatosha...🏃‍♂️🏃‍♂️🏃‍♂️nduki...
😂 😂 😂 😂 pona yako umekimbia maana leo hata arosto haijanitoka ndo kwanza kama nimerambishwa asali kiganjan nataman kuonja tena na tena🤭
 
Wakuu, mkiona kimya msihofu, wiki hii nimebanwa kidogo na majukumu fulani ya kikazi✍✍✍. Nadhani kuanzia keshokutwa, Mungu akipenda, tunaweza kuendelea na mtiririko wetu wa hadithi kama kawaida...😜😜😜 wacha niingie tena chimbo...🏃‍♂️🏃‍♂️🏃‍♂️
Umesomeka mkuu
 
Wakuu, mkiona kimya msihofu, wiki hii nimebanwa kidogo na majukumu fulani ya kikazi✍✍✍. Nadhani kuanzia keshokutwa, Mungu akipenda, tunaweza kuendelea na mtiririko wetu wa hadithi kama kawaida...😜😜😜 wacha niingie tena chimbo...🏃‍♂️🏃‍♂️🏃‍♂️
sawa mkuu
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom