Taxi - (94)
ILIPOISHIA
Kufumba na kufumbua Sammy akawa amewekwa mtu kati na wale watu walioonekana kudhamiria kumuua. Walizishika vyema bastola zao na kumuelekea Sammy.
Sammy alitweta, ujanja wowote ule ambao angejaribu kuufanya mbele ya silaha zile ungeweza kumgharimu maisha yake kwa kuchakazwa vibaya kwa risasi jambo ambalo hakuwa tayari litokee. Hata hivyo, hakutaka kufa kibudu, alidhamiria kupambana. Alisimama akiwa tayari kwa lolote, aliamini kuwa hawakujua kama walikuwa wanacheza na mtu hatari ambaye hakutakiwa kufanyiwa mchezo.
Kitu alichokuwa anamshukuru Mungu mpaka wakati huo ni kumpa uwezo wa kufikiri na kufanya uamuzi sahihi na wa haraka. Ingawa hajawahi kukumbana na misukosuko mikubwa kama hiyo lakini kila alipojikuta katika sehemu hatari ambayo si rahisi kwa mtu wa kawaida kujiokoa aliweza kutumia uwezo wake wa kufikiri na kuamua kwa haraka ili kujiokoa.
Wakati wakiwa wanaangaliana kwa ghadhabu Sammy akashangaa kumwona Bob Chopa akiachia tabasamu kisha akashusha chini bastola yake.
“Tuondoke, tutatafuta namna nyingine ya kuipata,” Bob Chopa alimweleza yule mwanamume mrefu mwenye mwili ulioshiba. Na hapo wakaanza kuondoka toka eneo lile wakimwacha Sammy katika mshangao.
Alisimama pale pale akiwatazama kwa makini akiwa haamini kama kweli waliamua kuondoka, alidhani ule ulikuwa mtego wao ili wapate kumdhuru lakini akashangaa kuwaona wakizidi kuyoyoma na kupotelea kizani, wala hakujua walikoelekea. Watu hawa ni akina nani? Walikuwa wanataka nini? Na nani aliyewatuma? Sammy alijiuliza bila kupata majibu.
ENDELEA...
Kitu kimoja tu alichokifahamu kwa wakati huo ni kwamba, eneo lile alilokuwa amesimama usiku huo halikuwa eneo salama hata kidogo, hivyo hakutakiwa kuendelea kuwepo pale. Bila kujali kama ule ulikuwa mtego au lah aliingia ndani ya gari lake na kuwasha injini kisha akaligeuza na kuondoka kwa kasi.
* * * * *
Ilikuwa inaelekea kutimia saa tano kamili usiku, gari dogo aina ya
Land-Rover 110 jeupe la POLISI lilikuwa linaendeshwa kwa mwendo wa kasi mno kuelekea mtaa mmoja katika eneo la Tabata Chang’ombe, ndani ya gari lile mbele kulikuwa na askari wawili, mmoja akiwa ndiye dereva wa gari. Nyuma ya gari lile kulikuwa na askari sita waliokuwa wamebebelea bunduki na vifua vyao vimekingwa na mavazi maalumu yanayozuia risasi ‘
bullet proof’. Askari hao walikuwa na sura ya kazi.
Jinsi walivyosimama nyuma ya gari lile ilionesha wazi kuwa mambo hayakuwa shwari kabisa huko walikokuwa wanaelekea.
Gari lile liliingia katika mtaa anaoishi Sammy na kupunguza mwendo baada ya kuikaribia nyumba ya Sammy, kitendo kile kikawafanya polisi watatu waruke kutoka nyuma ya lile gari katika mtindo wa kivita na kujiviringisha barabarani kama maninja kwa namna ya kuonesha kuwa kulikuwa na jambo la hatari, kisha kila mmoja akashika uelekeo wake kuizingira nyumba ile.
Mmoja alikwenda kujibanza mwanzo wa ukuta wa nyumba ya Sammy upande wa kushoto. Mwingine akakimbilia mbele ya geti kubwa la ile nyumba na kujibanza, na yule wa tatu alikwenda kujibanza kwenye kona ya ule ukuta iliyokuwa upande wa kulia. Lile gari
Land-Rover 110 likaongeza mwendo na lilipofika mwisho wa mtaa ule likakata kona na kuuzunguka ule mtaa kwenda kutokea mtaa wa nyuma yake.
Kwenye ule mtaa wa nyuma lilipunguza tena mwendo na kuwaruhusu wale askari watatu waliobakia kule nyuma waruke na kujiviringisha barabarani kama maninja. Kisha lile gari
Land-Rover 110 halikusimama badala yake likaongeza kasi mbele ya na kwenda kutokea tena katika mtaa lilioingilia, kisha likasimama mwisho kabisa wa ule mtaa.
Wale askari walioruka kutoka kwenye lile gari
Land-Rover 110 kule mtaa wa nyuma wakaanza kuusogelea kwa tahadhari ukuta wa ile nyumba ya Sammy huku wakiwa wamezishika vyema bunduki zao mikononi. Watu wawili watatu katika mtaa ule wakaanza kujitokeza wakishangaa, wasijue kilichokuwa kinaendelea.
Dulla na Spoiler ambao walikuwa bado wanawashikilia mateka Joyce na Pendo waliisikia sauti ya gari lile nje ya nyumba lilipopita na kupunguza mwendo kisha vikafuatia vishindo vya watu walioruka. Haraka Dulla akajongea dirishani na kuchungulia nje lakini kwa sababu nyumba ilikuwa imezungukwa na ukuta hakuweza kuona mtu. Akayatega vizuri masikio yake kusikiliza kwa makini, akasikia sauti hafifu za vishindo vya watu waliokuwa wanakimbia sambamba na ukuta ulioizunguka ile nyumba.
Alishtuka sana na kumpa ishara Spoiler kuwa kulikuwa na watu nje ya nyumba kisha akatoka haraka akipitia mlango wa jikoni na kujibanza kwenye kibaraza kidogo cha upande wa jiko, akasubiri kwa dakika moja huku akiwa makini sana kuangalia eneo lote la ule uwa wa nyumba. Mara akawaona wanaume watatu walioshika bunduki na vifua vyao vimekingwa na
bullet proof wakipanda ukuta haraka na kurukia ndani ya uwa bila vishindo. Dulla akashtuka sana na kurudi haraka ndani. “Askari!” alimwambia Spoiler kwa sauti ya chini huku akimwonesha vidole vitatu akimaanisha wapo watatu.
“Mafala hawa! Siwezi kukubali kukamatwa kijingajinga na hawa mabwege,” Spoiler alisema kwa hasira huku akielekea dirishani kuchungulia. Kabla hajafanikiwa kuchungulia dirishani kikatokea kitendo cha ghafla ambacho wote hawakukitegemea. Joyce alinyanyua stuli akampiga nayo Spoiler kichwani. Spoiler alianguka sakafuni huku damu zikianza kumtoka kichwani.
Wakati huo huo Joyce alimnyakua Pendo aliyekuwa amewekwa juu ya sofa na kuanza kukimbilia kule jikoni ilia toke nje lakini Dulla aliachia risasi mbili zilizompata mgongoni. Joyce akipiga yowe kubwa la maumivu na kudondoka sakafuni. Pendo aliangukia kando na kugugumia kwa maumivu. Hakuweza kutoa sauti kwa kuwa alikuwa bado amebandikwa gundi maalumu ya karatasi mdomoni.
Spoiler alinyanyuka haraka akiwa ameghadhabika sana, akatazama upande wa kushoto kwake na kulia akiwa makini, kisha akampa ishara fulani Dulla ambaye alikuwa ameshika bastola tayari kwa lolote. Kitendo bila kuchelewa, wakagawana njia, huyu akaelekea mlango wa jikoni akimruka Joyce na mwingine akaelekea mlango wa barazani.
Spoiler alielekea mlango wa barazani na kuufungua mlengo kwa tahadhari, akawaona askari wawili wakijongea kuelekea pale mlangoni kwa tahadhari, akabana pumzi na kukimbilia kwenda kuichukua ile stuli kisha akazima umeme kwenye swichi kubwa. Eneo lote la nyumba ile likawa kiza, kitendo ambacho wale askari hawakuwa wamekitegemea.
Kufumba na kufumbua Spoiler aliirusha ile stuli katikati ya wale askari wawili ambao walishtuka na kujaribu kuikwepa. Hiyo ilikuwa nafasi ambayo Spoiler alikuwa anaitarajia itokee. Alichomoka kama umeme wakati wale askari walipokuwa katika harakati za kuikwepa ile stuli na kukimbilia upande wa nyuma, akarukia juu ya ukuta wa uwa na kujirusha huku akitua salama nje. Aliusikia mvumo wa risasi zilizomkosakosa.
Alipotua chini aliangaza macho yake pande zote na hakuona mtu yeyote anayemfuatilia, akaanza kukimbia akiambaa na ule ukuta kuelekea kule walipokuwa wameacha pikipiki yao lakini akiwa na tahadhar kubwa, kisu chake kakishika mkononi tayari kwa lolote. Mara akaisikia milio ya risasi zikirindima kule ndani na muda huo huo akamshuhudia Dulla akirukia juu ya ukuta huku akijibu mashambulizi kwa kurusha risasi. Mara akapiga kelele na kuanguka chini baada ya kupigwa risasi kadhaa mgongoni.
Spoiler alishtuka sana na kugeuka nyuma yake, akamwona Dulla akiwa anagugumia kwa maumivu, mita chache tu toka pale alipokuwa amesimama, akamfuata na kumbeba kisha akakimbia naye na kumpandisha kwenye pikipiki akimlaza kifudifudi. Aliiwasha ile pikipiki na kuondoka kwa mwendo wa kasi huku akikoswakoswa na risasi. Mita therathini tu mbele yake akakutana na gari aina ya Cadillac DeVille la Sammy lililokuwa likija katika mwendo wa kasi na kuonekana likiingia upande wake.
Inaendelea...
CC
the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater Bigjahman moneytalk marybaby nipo2 ram kisukari Smart911 Madame S carbamazepine Astelia culture gal Prisoner of hope Mine eyes kuku mweus Thad hearly Shunie moneytalk Tumosa Mine eyes Kudo swahiba92 ludist Toyota escudo Clkey macson3 boga la kiangazi LEGE Smart911 Richard irakunda skfull popie Krizy Beat hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami mbududa iron2012 popie Bughy Harry Mlenge Kacheda mjasiliamali Laki Si Pesa cocochanel kinusikwetu big jambo mludego Shupavu Kacheda mjasiliamali Mweweso Songa Heri esiankiki mnadhimu mkuu wa jf red apple