Taxi - (105)
Ilipoishia
Saa tatu na nusu asubuhi Sammy alikuwa ameketi nje ya chumba cha uangalizi maalumu katika hospitali ya Amana, alikuwa amefika hapo mara tu alipoweka mambo sawa nyumbani kwake. Kwa kushirikiana na Elli, Sammy aliwahamisha Winifrida na Pendo na kuwapeleka Kurasini, nyumbani kwa Elli.
Alichokikuta pale hospitali baada ya kufika kilimmaliza nguvu. Joyce alikuwa amewekewa mashine maalumu ya kumsaidia kupumua baada ya hali yake kubadilika ghafla. Muda ule madaktari na wauguzi walikuwa wanahangaika kuokoa maisha yake, Sammy huruhusiwa kuingia wodini.
Endelea...
Akiwa ameketi pale nje ya chumba alimolazwa Joyce mara simu ya Joyce ikaanza kuita, simu hiyo alikuwa nayo Sammy akiwa ameichukua asubuhi ile. Aliitoa toka mfukoni na kuitazama kwa makini, akaliona jina la mpigaji na kushusha pumzi. Ilikuwa ni simu kutoka kwa Madame Norah.
“Hallo!” Sammy alisema mara tu alipoipokea na kuiweka sikioni huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.
“Hallo!” Madame Norah alisema kwa sauti iliyoonesha shaka kidogo baada ya kuisikia sauti ya kiume ikizungumza badala ya sauti ya Joyce, “Madame Norah hapa, sijui nazungumza na nani?” akauliza kwa mshangao.
“Sammy, mume wa Joyce,” Sammy alijibu kwa sauti tulivu huku akilamba midomo yake.
“Ooh, Sammy! Hujambo baba?”
“Sijambo, mama, shikamoo!”
“Marhaba! Samahani kwa usumbufu nahitaji kuongea na Joyce sijui yupo karibu?” Madame Norah alisema kwa sauti iliyojaa wasiwasi.
“Bila samahani, mama, nipo hapa hospitali ya Amana, Joyce alipigwa risasi usiku wa kuamkia leo,” Sammy alisema huku akijitahidi kuzuia machozi yaliyokuwa yakimlengalenga machoni.
“
Oh my God!” Madame Norah alimaka kwa mshtuko, kisha kikatokea kitambo fulani cha ukimya. Alihisi dunia yote ikizunguka kwa kasi ya ajabu na kumtia kizunguzungu. “Nani kampiga risasi?” Madame Norah alimudu kuuliza baada ya kitambo fulani cha ukimya.
“Bado haijafahamika nani waliompiga risasi na kwa sababu gani?” Sammy alisema, Madame Norah akavuta pumzi ndefu.
“Vipi hali yake?”
“Hali yake si nzuri, anapumua kwa msaada wa mashine maalumu ya kumsaidia kupumua.”
Madame Norah alitaka kusema lakini maneno hayakutoka, alihisi donge fulani likimkaba kooni, akashusha pumzi na kubaki kimya. Alihisi kupata pigo kubwa sana kwa kuwa alimtegemea sana Joyce kwenye mradi wake mpya. Alishindwa kuvumilia, akaanza kulia. Alikuwa analia kilio cha kwikwi kilichosikiwa vyema na Sammy. Sammy alipigwa na butwaa, hakujua afanye nini.
Wakati huo huo gari dogo la kifahari aina ya
BMW X6 xDrive 50i jeusi lilikuwa linapita kwenye geti la kuingilia la hospitali ya Amana na kwenda hadi katika viunga vya maegesho vya hospitali hiyo, likaegeshwa hapo jirani na gari la Sammy aina ya
Cadillac DeVille. Gari hili liliendeshwa na Tunu.
Alibaki kwenye gari kwa dakika chache huku gari likiunguruma kisha akazima inji na kufungua mlango, akashuka huku akilitazama kwa makini gari la Sammy aina ya
Cadillac DeVille kisha akatazama pande zote kuhakiki usalama.
Alipohakikisha kuwa kulikuwa na usalama wa kutosha akaanza kupiga hatua taratibu kuelekea katika jengo la mapokezi. Kabla hajafika mapokezi aligeuza shingo yake kutazama kule kwenye maegesho na kuridhika kuwa hali ilikuwa shwari. Akashusha pumzi. Tunu alikuwa amevaa suti ya kike ya bluu ya kitambaa ghali na shingoni alivaa mkufu wa dhahabu wenye kidani chenye herufi “G”.
Pale mapokezi aliwakuta wahudumu kadhaa akawauliza mahala kilipo chumba cha wagonjwa mahututi walio katika uangalizi maalumu, akaelekezwa na bila kupoteza muda akaelekea huko. Alipokuwa mbali alimuona Sammy akiwa ametulia, simu ikiwa kwenye shavu.
“Sammy!” Tunu alishindwa kujizuia akaita hata kabla hajamfikia.
Sammy alishtuka na kumtazama Tunu kwa makini, akamtambua na kuinuka huku akimkodolea macho kwa mshangao.
“Gift!” Sammy alisema kwa sauti ya chini iliyojaa simanzi.
“Pole sana kwa yote yaliyotokea,
I feel sorry for you,” Tunu alisema kwa huzuni huku akimkumbatia Sammy katika namna ya kumfariji. Wakakumbatiana kwa kitambo huku Sammy akilengwa na machozi, kisha akambusu Tunu kama shukrani ya kwenda hospitali kumfariji.
Baada ya maongezi mafupi ya kujuliana hali Sammy alimsimulia Tunu yote yaliyomtokea siku iliyotangulia, tangu walipoachana pale katika mgahawa wa Elli’s, njiani akatekwa na watu waliokuwa wanatafuta
memory card hadi alipofika nyumbani na kukuta askari wametanda nyumbani kwake baada ya kupewa taarifa za uwepo wa watu hao nyumba yake. Alimweleza Tunu pasipo kubakisha kitu hadi jinsi alivyopishana na watu waliompiga risasi mkewe na kukosa kuwagonga kwa gari, na baadaye kumkuta mkewe kalalia dimbwi la damu baada yakupigwa risasi.
Tunu alimsikiliza Sammy kwa makini, alihisi donge la huzuni likimkaba kooni kwake. Machozi yalimlenga machoni na alijikuta akitamani sana kumweleza ukweli Sammy kuhusu akina Bob waliomteka kuwa ni yeye aliyewatuma, lakini si kwa nia mbaya.
“Pole sana!” hatimaye Tunu alimudu kutamka, na kuendelea, “Wakati mkeo anapigwa risasi hakukuwa na watu wengine nyumbani?” Aliuliza huku akiyatuliza macho yake kwenye uso wa Sammy akijaribu kuyasoma mawazo yake.
“Mbali na mke wangu, pia walikuwepo mtoto wangu wa miaka mitano, Pendo na mdogo wangu Winifrida anayesoma kidato cha nne,” Sammy alisema.
“Vipi kuhusu wao, hawakudhuriwa?” Tunu aliuliza kwa wasiwasi huku akimkazia macho Sammy.
“Hawakudhuruiwa ingawa Pendo walimfunga plasta mdomoni ili asipige kelele. Winifrida hawakumwona kwani aliwahi kujificha juu ya kabati la ukutani kabla hawajaingia chumbani na aliweza kusikia baadhi ya maneno ya vitisho waliyokuwa wakiyatoa...”
“Alibahatika kuwaona sura zao?”
“Tumejaribu kumuuliza lakini haelezi vizuri, ni kama vile kuna mambo anaogopa kuyasema au pengine hana uhakika!” Sammy alisema kisha akamsimulia
“Kwani ni nani aliyewajulisha polisi kuhusu uwepo wa watu hao nyumbani kwako?” Tunu alizidi kumsaili Sammy akionesha shauku ya kutaka kujua.
“Hapo ndipo penye kizungumkuti, hajulikani nani aliwapigia simu, tumemuuliza Winifrida lakini amekana kupiga simu, ingawa polisi wanadai kuwa mpigaji alikuwa mwanamke na aliwaambia kuwa alikuwa amejificha ndani ya nyumba hiyo iliyovamiwa!”
“Kwani Winifrida ana simu?”
“Hana,” Sammy alijibu pasipo kufikiri.
“Una uhakika?” Tunu aliuliza kwa sauti iliyoonesha shaka fulani, bado alikuwa ameyatuliza macho yake usoni kwa Sammy katika namna ya kuyasoma mawazo yake.
Sammy alifikiria kidogo na kushusha pumzi, akatingisha kichwa chake taratibu kushoto na kulia kukataa. “Hata sijui!”
“Kwa hiyo polisi wanasemaje, wamekwisha wabaini waliofanya tukio hilo?” Tunu aliuliza baada ya kufikiria kwa kitambo kidogo.
“Bado wanaendelea na upelelezi, ila nilipozungumza nao leo asubuhi walisema kuwa wamebaini vitu vichache, hususani alama za viatu walivyokuwa wamevaa watu hao na maganda ya risasi.”
Itaendelea...
CC
the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater Bigjahman moneytalk marybaby nipo2 ram kisukari Smart911 Madame S carbamazepine Astelia culture gal Prisoner of hope Mine eyes kuku mweus Thad hearly Shunie Tumosa Mine eyes Kudo swahiba92 ludist Toyota escudo Clkey macson3 boga la kiangazi LEGE Smart911 Richard irakunda skfull popie Krizy Beat hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami mbududa iron2012 popie Bughy Harry Mlenge Kacheda mjasiliamali Laki Si Pesa cocochanel kinusikwetu big jambo mludego Shupavu Kacheda mjasiliamali Mweweso Songa Heri esiankiki mnadhimu mkuu wa jf red apple the-sniper MR KUO dan oseko