Rostam aliangukia kanisa
na Martin Malera
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
MBUNGE wa Igunga, Rostam Aziz (CCM), amesema taifa liko kwenye wakati mgumu kisiasa na kijamii, hivyo amewaomba wananchi watumie makanisa kulirejesha katika mstari ulio sahihi.
Rostam alitoa kauli hiyo jana katika sherehe ya uzinduzi wa albamu ya kwaya ya Amkeni ya Kanisa la Kilutheri Tanzania, iliyofanyika katika viwanja vya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Usharika wa Kinondoni, Dar es Salaam, ambapo alikuwa mgeni rasmi.
Huku akishangiliwa na umati wa waumini waliohudhuria uzinduzi huo, mbunge huyo anayeandamwa na jinamizi la ufisadi, alisema waumini wa dini hawamtuhumu mtu, hawamshutumu, hawapendi wenye wivu na wenye chuki bali wanapenda haki.
Akionekana kuwashangaza waumini kutokana na maneno yake ya ucha Mungu, Rostam alisema ana watoto watatu ambao aliahidi kanisani hapo kwamba anataka awalee katika misingi ya dini ili wawe wananchi bora na waadilifu hapo baadaye.
Nawashukuru kwa kuamua kunialika kuwa mgeni rasmi leo, hii ni ishara kwamba mmeamua kupuuza viji-maneno na upuuzi wa vijiweni. Nafurahi kuwa miongoni mwenu
hamtuhumu, hamshutumu, hampendi wenye wivu na wenye chuki, mnapenda haki. Ninao watoto watatu na nataka niwalee katika misingi hii, alisema Rostam huku akishangiliwa na umati wa watu walioshiriki hafla hiyo.
Alisema hivi sasa nchini, watu wameanzisha tabia ya kuchukiana mpaka kuzushiana uchawi na kuombeana vifo, na kusisitiza kuwa wananchi watumie makanisa kukemea vitu hivi.
Ingawa katika kauli hiyo hakutaja mtu, lakini mbunge huyo ambaye hajawahi kupata mpinzani katika jimbo lake, alikuwa akizungumzia tukio la hivi karibuni bungeni, ambako Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge (CCM) na ofisa mmoja mwandamizi wa Bunge, walituhumiwa kuweka vitu aina fulani ya uchawi au sumu ya kisasa ndani ya ukumbi wa Bunge.
Hata hivyo, suala hilo hadi sasa bado linashughulikiwa na vyombo vya dola, ambako Spika wa Bunge, Samwel Sitta, alikabidhi mikanda inayodaiwa kuonyesha picha za wahusika walipokuwa wakiwanga bungeni.
Rostam aliendelea kuwaambia waumini hao kuwa mbali ya matatizo ya kisiasa, pia kuna matatizo ya kijamii kama vile ndoa kuvunjika kila kukicha, watoto wa mitaani kuongezeka, madanguro na dawa za kulevya kukithiri, ambayo alisema yanasababishwa na mmomonyoko wa maadili, hivyo kusisitiza wito wake wa kutaka makanisa kuiombea nchi ili kurejesha katika hali ya matumaini, upendo na amani.
Katika hafla hiyo, Rostam alitoa mchango wa sh milioni tano kuchangia seti za vyombo vya muziki kwa kwaya ya Amkeni pamoja na jenereta yenye thamani ya sh milioni 2.6.
Katika siku za hivi karibuni, Rostam amekuwa akiandamwa na jinamizi la ufisadi kiasi cha baadhi ya wabunge na wananchi kutaka achukuliwe hatua za kisheria.
Wakati wa mkutano wa 10 wa Bunge, baadhi ya wabunge walitaka Rostam awajibishwe kutokana na kutajwa kuwa ndiye mmiliki wa Kampuni ya Richmond inayodaiwa kuihadaa serikali katika makubaliano ya kuzalisha umeme wa dharura.
Wakichangia ripoti ya Kamati Teule ya Bunge juu ya mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura wa Richmond bungeni, Februari mwaka huu, baadhi ya wabunge walisema kitendo cha mbunge huyo kugoma kutoa ushahidi katika kamati hiyo iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe kuwa ilikuwa ni dharau kwa Bunge na kwa Spika aliyeiunda.
Hatuwezi kuhoji kwa sasa kwamba Richmond ni ya akina nani. Ukweli uko wazi kuwa ni wale walioshinikiza kampuni hiyo ipewe mkataba, alisema Mbunge wa Sikonge, Juma Mkumba (CCM).
Alisema Rostam katajwa kuwa na uhusiano na Richmond na pia anatajwa kuwa na uhusiano na Kampuni ya Dowans iliyokuwa inaendesha shughuli za Richmond kabla ya serikali hivi karibuni kuamua kuvunja mkataba wake.
Mbunge mwingine ambaye aliwahi kuchangia kutaka kuwajibishwa kwa Rostam ni Godfrey Zambi (CCM), Mbozi Mashariki ambaye alisema ni vyema achukuliwe hatua, kwa vile ni kiongozi wa CCM na yuko kwenye Halmashauri na Kamati Kuu ya chama hicho.
Alisema kitendo cha Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, kunukuliwa akimtaja Rostam kuwa na uhusiano na Richmond ni ushahidi wa kutosha.
Wakati wabunge wakitoa shutuma hizo, Rostam alijiandaa kujibu bungeni, lakini katika hali isiyo ya kawaida, Spika wa Bunge, Samwel Sitta aliikataa hoja yake kwa kile kilichoelezwa kuwa kama angetoa maelezo hayo ni wazi kwamba angelitikisa Bunge.
Inadaiwa kuwa Rostam baadaye aliamua kuyapeleka maelezo yake kwenye Kamati ya CCM ambako yalijadiliwa na kumzuia mbunge huyo wa Igunga kuyasema bungeni.
Hivi karibuni, Rostam ambaye kwa mara mbili mfululizo amekuwa akipita bila kupingwa kwenye jimbo lake la uchaguzi, alitangaza kutowania tena ubunge, hali ambayo inaweza kuwa na uhusiano na tuhuma zinazomwandama kuhusu ufisadi.