Twamshangaa Rostam, lakini makanisa yetu ni machafu
Johnson Mbwambo Julai 16, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo
NIANZE ninachotaka kujadili leo kwa kusema mapema kwamba ingawa sifahamu mbunge wa Igunga, Rostam Aziz ana washauri binafsi wangapi; lakini yeyote aliyemshauri kuutumia Usharika wa KKKT Kinondoni kusafisha jina lake kutokana na tuhuma za kuhusishwa na kampuni ya kifisadi ya Richmond, hakumtakia mema.
Niliamini kwamba mahali pazuri ambako Mheshimiwa Rostam alistahili kujieleza (kujisafisha) kuhusu tuhuma hizo ni kwenye mkutano na vyombo vya habari (press conference).
Huko ndiko mtu unaweza kujieleza kwa mapana na marefu na kisha kuwapa waandishi wa habari fursa ya kuuliza maswali yanayosumbua vichwa vya wananchi kuhusu mahusiano yake na Richmond na hata masuala mengine kama vile EPA n.k
Kanisani hapakuwa mahali pazuri kwake kujisafisha kwa sababu huko unazungumza tu na wala hakuna fursa ya kuulizwa maswali. Na hata kama angetoa fursa ya kuulizwa maswali, hakuna washarika ambao wangemuuliza maswali magumu, kwa sababu sana sana walichomwitia pale ni mchango wake (milioni saba) kwa Usharika huo. Ndiyo maana naamini njia sahihi kwake ni press conference.
Kwa hiyo lilikuwa jambo jema kwake kuitisha Press Conference Jumapili iliyopita na kujieleza. Japo waandishi hawakumbana kweli kweli kwa maswali mazito kama vile ya kumtaka aeleze ni vipi watu ambao wako karibu na yeye kimahusiano walimtaja katika ripoti ya Kamati ya Dk. Mwakyembe kuwa ana mahusiano na kampuni ya Richmond n.k, mwanga kidogo umepatikana.
Japo utetezi wake, kwa namna inayoshangaza, unafanana kidogo na wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa (wivu na kukwamisha uteuzi wa watu katika nafasi mbalimbali za uongozi), bado naamini Watanzania wamepata mwanga kidogo kufahamu iwapo ni haki kumtuhumu Rostam Aziz au ni chuki na wivu tu wa kijinga kama alivyosema.
Lakini mjadala wangu leo si kuhusu Rostam Aziz na tuhuma zinazomwandama; bali ni kuhusu usafi wa Kanisa kwa ujumla.
Nimesema kwamba aliyemshauri Rostam kulitumia jukwaa la KKKT Kinondoni kujisafisha, hakumtakia mema. Nimesema hivyo kwa sababu kama mshauri huyo angelifanya home work yake vizuri; angelijua kwamba uongozi wa Usharika huo tayari umegubikwa na tuhuma za ufisadi, na hivyo kwenda kwake huko kumeongeza tu chumvi kwenye kidonda.
Kwa muda mrefu sasa kumekuwepo na tuhuma za ufisadi dhidi ya uongozi wa Usharika huo, na mwezi uliopita tu ulisambazwa waraka wa wanakwaya kwa washarika uliotumwa kwa uongozi wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ambao uliorodhesha tuhuma mbalimbali za ufisadi unaoendeshwa na uongozi wa Usharika.
Ingawa zilifanyika juhudi za kuzima tuhuma hizo na kuukejeli waraka huo, hali ilikuwa mbaya kiasi kwamba uongozi wa Dayosisi ulilazimika kutuma mjumbe Jumapili moja ili kuwatuliza washarika na kuwaahidi kwamba uchunguzi wa madai hayo unafanyika na kwamba wangepewa taarifa pindi ukikamilika.
Sasa wakati washarika bado wakisubiri mrejesho wa uchunguzi wa Dayosisi kuhusu tuhuma hizo za ufisadi, linaibuka suala jipya la Rostam kualikwa usharikani na uongozi huo huo unaotuhumiwa kwa ufisadi, na yeye Rostam akaamua kuitumia fursa hiyo kujisafisha!
Nina hakika mshauri wa Rostam angeliyajua hayo mapema pengine angemtafutia kanisa jingine salama zaidi kuliko KKKT Kinondoni. Na kama angefanya hivyo (Rostam), pengine kauli yake hiyo ya kujisafisha aliyoitoa KKKT Kinondoni isingekanwa na kutotambuliwa na Dayosisi ya Mashariki na Pwani kama ilivyotokea.
Kwa ufupi, Kanisa la KKKT Kinondoni ambako Mheshimiwa Rostam alichagua kwenda kujisafisha si safi; kwani lenyewe linachunguzwa na Dayosisi kwa tuhuma mbalimbali za ufisadi!
Ninachojaribu kueleza hapa ni kwamba tunaweza kumlaumu Rostam kwa kuutumia Usharika wa KKKT Kinondoni kujisafisha, tunaweza kufurahia tamko la Dayosisi ya Mashariki na Pwani la kumkana Rostam, lakini ukweli unabaki pale pale. Na ukweli huo ni kwamba makanisa yetu yenyewe ni machafu kweli kweli.
Sitaki kuyazungumzia makanisa mengine nchini (na yanaibuka kama uyoga kila kukicha), lakini hili la KKKT Tanzania ambalo mimi ni msharika, nadiriki kusema nalo si safi.
Labda niwaulize Walutheri wenzangu, ni askofu wa kanisa gani aliyeshiriki katika mapokezi ya Edward Lowassa siku aliporudi Monduli baada ya kujiuzulu uwaziri mkuu kutokana na suala hilo hilo la Richmond analotuhumiwanalo Rostam?
Je si kweli kwamba askofu huyo ni Laizer na ni wa KKKT? Si kweli kwamba alipopewa fursa ya kuzungumza, alisema maneno yaliyolenga katika kumsafisha Lowassa? Na kama hivyo ndivyo, kwa nini tushangae ya KKKT Kinondoni?
Ukweli ni kwamba baadhi ya wachungaji na baadhi ya maaskofu wetu wanawapapatikia mno wakubwa; kiasi kwamba usafi wao kimaadili na kiroho unatia shaka.
Nimepata kusali katika makanisa tofauti ya KKKT na katika miji tofauti, lakini ninachokiona huko ni kile kile wenye pesa na madaraka makubwa wanaheshimiwa mno kuliko waumini masikini. Na hili linakwenda hata katika ngazi ya kijiji!
Unapofikia uchaguzi wa wazee wa kanisa utaona jinsi wachungaji wanavyohaha kuhakikisha wafanyabiashara wenye mapesa na wakubwa wenye madaraka serikalini au katika makampuni makubwa wanachaguliwa kuwa wazee wa kanisa; bila hata kujali uadilifu wao.
Wanafanya hivyo kwa sababu wanataka wawe karibu nao kwa kuwa wanatoa mapesa mengi kwenye Harambee za Kanisa; lakini pia kwa kuwa wanataka wawe wafadhili wao binafsi na wa familia zao.
Kwa hakika hata hapa Dar es salaam, kwenye Kanisa Kuu la Azania Front, kuna viti maalumu ambavyo ingawa haijatamkwa rasmi popote, lakini vinafahamika kwamba ni vya wakubwa au matajiri fulani. Utaambiwa hapa ni pa fulani, pale ni pa fulani n.k.
Je, hivyo ndivyo Bwana wetu Yesu Kristo alivyotufunza kubagua kondoo wake kwa misingi ya pesa na madaraka? Je, si kweli kwamba utajiri, uwaziri, ukuu wa mkoa, ubunge, ujaji, ufundi cherehani, ungarishaji viatu, udereva, umakenika na hata umachinga, ni nje ya kanisa, na kwamba ndani ya kanisa wote tu sawa mbele za Mungu?
Na ukitaka kuona ni kiasi gani wachungaji wetu wamepoteza maadili ya kanisa kwa kupenda mno pesa, hudhuria misa za wiki chache kabla ya Sikukuu ya Mavuno. Baadhi ya mahubiri ya wachungaji wa KKKT ya kuhamasisha mavuno yanatia kichefuchefu.
Utasikia Baba Mchungaji akiwahamasisha washarika wake kuleta mavuno kwa kusema: Leteni kila kitu na tutakibariki kwa jina la Yesu. Leteni mavuno yenu yanayotokana na biashara zenu na tutayabariki. Haijalishi kama pesa zako zinatokana na biashara ya baa au ukahaba. Ukishazileta hapa tunazibariki madhabahuni katika Jina la Yesu, na zinakuwa safi! Bwana Asifiwe!
Bila shaka Mchungaji anayetoa mahubiri ya namna hii anachokiona mbele yake ni pesa tu. Hawaonei huruma hao makahaba au wauza pombe, na wala hajali kwamba wajibu wake ni kuwaombea waokoke; bali anachokiona ni pesa zao tu!
Mchungaji anayependa pesa kiasi hicho lazima ni fisadi, na lazima atawapapatikia kupita kiasi waumini ambao ni matajiri; hata kama anajua kwamba ni mafisadi.
Nasikia katika kanisa moja mtuhumiwa wa ujambazi naye ni mzee wa kanisa kwa kisingizio kuwa ameokoka, lakini inadaiwa bado hajaacha shughuli yake hiyo ya zamani.
Aidha, kuna mfanyabiashara mmoja mkubwa jijini, aliye msharika wa KKKT, amechukizwa mno na kitendo cha KKKT Kinondoni kumwalika Rostam Aziz kanisani. Lakini yeye amechukia si kwa sababu Rostam anahusishwa na Richmond, lakini kwa sababu ya kuhofia kwamba Rostam anaweza kumpokonya nafasi yake ya kuwa mchangiaji mkuu katika hafla mbalimbali nchini za KKKT.
Na ukiachilia suala la pesa zake, wala mfanyabiashara huyo aliyeudhiwa na kitendo hicho cha Rostam, mwenyewe hana usafi wowote kimaadili wa kuhalalisha heshima anayopewa na kanisa hilo. Je huo nao si ufisadi?
Nimalizie tafakuri yangu kwa kusema kwamba haitoshi tu kwa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ya KKKT kutoa tamko la kumkana Rostam Aziz; kwani sote tunajua kwamba ufisadi na uchafu wa kila aina umetawala makanisa yake. Kinondoni ni mfano mmoja tu.
Kwa ufupi, makanisa yetu yajitazame kwanza yenyewe usafi wao kabla hayajaanza kuwanyooshea wengine vidole. Si tumefunzwa katika Biblia kwamba tutoe kwanza boriti kwenye macho yetu kabla ya hatujaangalia vibanzi kwenye macho ya wengine?
Tafakari.