...au Fisadi Mkapa alijivisha ngozi ya "Mr Clean" kumbe ni fisadi wa hali ya juu!?
Nyerere hakumjua Mkapa
Absalom Kibanda
Tanzania Daima
TAIFA liko katika msukosuko. Hali hii imesababishwa na mtikisiko uliothibitika, unaohusu ufujaji mkubwa wa fedha za umma, ambao dalili zote za awali zinaonyesha bayana kuwa ni kazi mahususi iliyoratibiwa kifisadi na baadhi ya viongozi na maofisa wa juu serikalini.
Ripoti ya ukaguzi uliofanywa na kampuni ya kimataifa ya Ernst & Young imebaini upotevu wa fedha zinazokadiriwa kufikia shilingi bilioni 133 ambazo zililipwa kupitia kampuni 22.
Kwa viwango vyovyote vile, kiasi hicho cha fedha kilichofujwa kutoka katika akaunti moja tu ya malipo ya madeni ya nje (EPA), iliyokuwa ikisimamiwa na kuratibiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ni kikubwa na cha kushtua.
Ni kwa sababu hizo basi, ndiyo maana watu ambao uadilifu wao hauwezi kutiliwa shaka hata kidogo, mmoja mmoja au kupitia katika taasisi, wameeleza kushtushwa na ubadhirifu huo ambao habari zake zilipoanza kusikika kwa mara ya kwanza zilionekana kuwa ni ama mzaha, uzushi, ufitini na mambo mengine yanayofanana na hayo.
Wapenzi wa soka wanasema kwamba, kiasi hicho cha fedha kilikuwa na uwezo wa kujenga viwanja viwili vya kisasa, mfano wa kile kimoja tulichonacho na tulichokijenga kwa takriban shilingi bilioni 56.4.
Kwa sababu hiyo basi, leo hii taifa lingeweza kuwa na viwanja vitatu vya soka vya kisasa badala ya kile kimoja tulichonacho na wakati huo huo tungejikuta tukibakiwa na albaki ya shilingi bilioni 20.
Kama hilo lingewezekana, basi Watanzania huenda tungeweza kuwa miongoni mwa mataifa 20 yaliyokusanyika Ghana katika kinyanganyiro cha fainali za Mataifa ya Afrika.
Wataalamu wengine wa masuala ya kitaaluma wanasema kwamba iwapo fedha zilizofujwa BoT zingeingizwa katika mfumo wa elimu, basi zingeweza kufanikisha kujenga shule (si madarasa) zaidi ya 1,000 ama za msingi au sekondari.
Si hivyo tu, mabilioni hayo ya BoT yaliyofujwa yalikuwa na uwezo wa kujenga takriban madaraja matatu kama Daraja la Mkapa, ambalo lilikamilika miaka kadhaa baada ya mipango iliyokwishakuwapo ya kulijenga kushindwa kukamilika zama za uongozi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere (1961-1985), na baadaye enzi za mzee wetu, Ali Hassan Mwinyi (1985-1995).
Kwa maneno rahisi, Kashfa ya EPA ni fedheha ya taifa na kimsingi ni aibu ya serikali na pengine kielelezo cha wazi cha kushindwa kazi kwa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, ambaye uoza huu unaoanza kujulikana leo hii ulizuka zama zake.
Ukifikiri sawasawa unaweza ukaona namna Kashfa ya EPA inavyozidi kuongeza utandu kama si ukungu katika utendaji wa serikali ya Mkapa ambaye zama zake alijitambulisha kama mtu muwazi na mkweli.
Kwa hakika Kashfa ya EPA imezidi kuifanya kaulimbiu yake ya uwazi na ukweli kutiwa madoa, na sina shaka kabisa kwamba idadi ya wananchi wanaoendelea kumuangalia kiongozi huyo kwa jicho na tafsiri hasi inazidi kuongezeka kila kukicha.
Kashfa hii ya sasa imebadili akili yangu. Imefuta imani ya kipekee niliyoijenga kwa miaka mingi kwa Mkapa ambaye zama zile alipokuwa akipingwa na kukosolewa na watu wengi, binafsi niliendelea kumuona akiwa shujaa wa taifa hili na mwanafunzi wa kweli wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Naweza kusema bayana kabisa kwamba, hili suala la EPA limeturudisha nyuma hatua kadhaa, hali ambayo kama Watanzania, tunalazimika kugeuka nyuma na kufanya tathmini ya wazi na ya kweli kuhusu viongozi wetu wakuu waliolifikisha taifa letu hapa tulipo.
Katikati ya viongozi hao wakuu ni lazima atawekwa Mkapa, ambaye lundo la uvundo wa kiutendaji ambao umekuwa ukifukuliwa tangu mapema mwaka jana limeanza zama akiwa rais na hususan kabla kidogo au baada ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.
Hili halihitaji ushahidi, liko wazi. ANBEM, kampuni ya kibiashara inayomilikiwa na rais huyo mstaafu, ambayo katika miaka ya hivi karibuni imezua maneno mengi, ilianzishwa mwaka huo huo wa 1999. Hili ni moja ya mambo yaliyosababisha Joseph Butiku, Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere atoe kauli nzito dhidi ya rais huyo wa tatu wa Tanzania.
Leo hii maneno ya Butiku dhidi ya CCM na Mkapa ukiyaainisha na kuyaweka katika mizania ya Kashfa ya EPA yanakuwa na nguvu zaidi na mantiki kuliko ilivyokuwa wakati alipoandika barua ya kulalamika kwenda kwa rais huyo mstaafu, kwa mara ya kwanza Agosti 10, mwaka 2005, na baadaye akayarudia mwaka jana.
Butiku kupitia katika barua yake hiyo alimtaka Mkapa kutambua kuwa CCM, chama alichokuwa akikiongoza wakati huo kilikuwa kikiendeshwa katika misingi ya kibaguzi.
Baadhi ya mambo aliyomweleza mwenyekiti huyo ni kuporomoka kwa misingi, maadili ya chama na ubaguzi uliojionyesha wazi wakati wa harakati za uchaguzi ulioiweka madarakani Serikali ya Awamu ya Nne.
Katika barua yake hiyo ya kurasa 14, Butiku katika sehemu moja anaandika: Mimi naamini CCM sasa imeanza safari ya kuelekea kwenye KIFO chake-imekumbatia jambo ovu-Rushwa, ambayo imeua viongozi wazuri wengi, vyama vya siasa na serikali makini duniani. CCM imeanza kushindwa kusema na kutetea HAKI na UKWELI; Imeanza kuvumilia na kutetea UBAGUZI.
Mbali ya hilo, Butiku katika barua yake hiyo alisema CCM (ya Mkapa) na hii ya leo, imeanza kujenga matabaka miongoni mwa viongozi wake hata kuifanya mali ianze kuchukua nafasi ya uzalendo.
Aidha, alisema pia kwamba, hali hiyo imeanza kuchukua sura mbaya zaidi kutokana na viongozi wakuu wa chama hicho kukaa kimya wakishindwa kutetea maovu.
Alichokisema Butiku wakati huo kilikuwa kimepata kusemwa zama hizo hizo za Mkapa na marehemu Horace Kolimba, ambaye siku chache kabla kifo hakijamchukua, alikielezea chama alichopata kuwa katibu mkuu wake kama kilichopoteza dira.
Leo hii miaka kadhaa baada ya Baba wa Taifa kutabiri kuhusu hatari ya CCM kuporomoka na baadaye Kolimba na Butiku kuonya kuhusu kupoteza dira kwa chama hicho, kumeibuka Kashfa ya EPA inayotoa mwelekeo dhahiri wa kukitafuna chama hicho.
Maneno yanayosikika mitaani, tena yakizungumzwa na watu wazito wanaokosa ujasiri wa kujitokeza hadharani kusema kwa uwazi, yanaihusisha kashfa hii ya EPA na matumizi ya fedha chafu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.
Kama alivyopata kunukuliwa akisema Dk. Willibrod Slaa, ushahidi wa mazingira unatufanya baadhi yetu tujikute tukilazimika kuyakubali maneno haya mazito yanayosemwa na kisha kuyatafakari.
Tunapofikia hatua hiyo ndipo tunapojikuta tukimuona Mkapa, kiongozi mwenye mbwembwe nyingi na jeuri kubwa kimatamshi, akiwa amesimama katikati ya uvundo huo wa ufisadi.
Katika hatua hii, Mkapa anageuka na kuwa mtu anayekosa ile jeuri yake ya kimamlaka aliyokuwa nayo iliyokuwa ikimpa fursa ya kutamba kuwa yeye ni muwazi na mkweli, ilhali akijua wazi kuwa hakuwa mkweli na kimsingi alikuwa msiri wa kweli kweli.
Anayeonekana hapa ni Mkapa ambaye zama akiwa rais, takwimu za ukutani zilikuwa zikionekana kuneemeka na kukua kwa uchumi wa taifa katika maeneo takriban yote, ilhali hali za wananchi walio wengi zikiendelea kubakia za kifukara.
Mkapa wa EPA anayeonekana leo hii ni yule ambaye taswira yake inaonyesha dhahiri kuwa mtu aliyejiandaa kuchuma utajiri kwa namna na kwa njia za namna yake kwa gharama za kuruhusu mikopo ya ajabu ajabu kutoka katika mifuko ya pensheni, kuuza na kunununua nyumba za serikali na hatimaye kubariki ajenda ya siri ya kufukarisha wengi na kutajirisha wachache.
Katika hili, wajihi wa Mkapa ndio ambao leo hii unatufanya baadhi yetu tujikute tukihaha kutafuta njia bora kabisa ya kumuomba radhi mzee wetu, Ali Hassan Mwinyi na mkewe, Mama Sitti, ambao zama wakiwa madarakani walizushiwa kila aina ya uchafu wasiostahili kubebeshwa.
Leo hii miaka zaidi ya 10 tangu atoke madarakani, maisha anayoishi mzee huyo na wake zake wawili ni ya kawaida, yasiyo na makuu, maswali au shaka yoyote machoni mwa Watanzania wenzao, tofauti kabisa na ilivyo kwa Mkapa.
Auhitaji ushahidi kulithibitisha hili. Nyumba pekee ya Mkapa isiyo na maswali wala shaka machoni mwa Watanzania leo hii ni ile aliyoijenga kijijini kwake Lupaso, Masasi, huku nyingine mbili; ya kwanza ikiwa ni ile ya Lushoto na ile ya Ocean Road - Dar es Salaam zikidai maelezo mengi.
Binafsi sina uhakika ni jibu gani atakalowapa Watanzania wakamuelewa leo hii iwapo atatakiwa kutoa maelezo ya namna alivyozipata nyumba hizo mbili, ambazo umiliki wake haufanani kwa namna yoyote na zile za watangulizi wake, Mwinyi na Mwalimu Nyerere. Katika hili, zama akiwa madarakani angesema ni wivu wa kijinga.
Ninapofika hatua hii, ndipo ninapolazimika kukikumbuka kiapo cha urais alichokula Mkapa mwaka 1995 na baadaye mwaka 2000, kilichogawanywa katika sehemu tatu:
Kiapo cha kwanza ni cha utii alichoapa Mkapa, ni kile cha kuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuitumikia kwa moyo wake wote, na kwamba ataihifadhi, kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Anapaswa kujipima na sisi kumpima kama alikitimiza kiapo hiki.
Kiapo cha pili alichoapa ni kile cha kuahidi kuwa, atatenda kazi zake za urais kwa uaminifu na kutimiza wajibu wa kazi hizo kwa bidii na moyo mkunjufu, na kwamba atawatendea haki watu wote kwa mujibu wa sheria, mila na desturi za Tanzania bila woga, upendeleo, huba wala chuki.
Mkapa pia katika kiapo chake cha tatu aliahidi; kudumisha Muungano na kudumisha umoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Watanzania tunapaswa kurejea viapo hivi vya rais na kuangalia iwapo Mkapa alivitimiza akiwa madarakani na iwapo alikiuka, ni hatua gani basi anaweza kuchukuliwa?
Kutokana na somo hili tulilojifunza kutoka kwa Mkapa, Watanzania wa leo hatuna budi kufanya kila linalowezekana kutafuta namna bora ya kuchukua hatua madhubuti za kisheria na kikatiba ili kulinusuru taifa hili kuingia katika mtego tulionaswa na serikali ya Mkapa.
Juu ya yote hayo, Watanzania wana kila sababu ya kuanza kuamini kuwa, Mkapa aliyepigiwa chapuo la urais na Baba wa Taifa mwaka 1995, si yule aliyeondoka madarakani mwaka 2005. Sasa naamini tena kwa dhati kwamba, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere hakumjua Mkapa.