Ya Mkapa, Ballali na Jeetu Patel
Januari, 16, 2008
Raia Mwema
"Mr. Clean", Ben Mkapa alikaa Ikulu kama Rais wa Tanzania kwa miaka 10. Katika kipindi hicho 1995 – 2005 Benki Kuu ya Tanzania ilishamiri kwa ufisadi katika kiwango ambacho hakijapata kuonekana katika historia ya nchi.
Zaidi ya Sh. bilioni 133 ziliibwa katika akaunti ya nje ya malipo ya madeni (EPA) peke yake. Mpaka sasa hatujajua kiasi gani kiliibwa kwingineko, lakini kwamba "Mr. Clean" aliamuacha mteule wake, Daudi Ballali kuendelea kuwa Gavana wa benki hiyo kwa miaka takriban minane, ni kitu kinachoibua maswali mengi yanayohitaji majibu.
Je, yawezekana katika kipindi chote hicho "Mr. Clean" alikuwa hajui, au hata kupata fununu, kuhusu ufisadi uliokuwa ukiendeshwa kwa kasi katika benki hiyo?
Na kama alijua au alielezwa, je kiongozi huyo, ambaye "si mvivu wa kufikiri" (kama sisi!), alichukua hatua gani kuhakikisha mabilioni ya pesa za wavuja jasho wa nchi hii hayaendelei kuyeyushwa na mafisadi katika benki hiyo?
Na je, yawezekana kweli ufisadi wa kiwango hicho kikubwa ukaendelea katika BoT bila ya Hazina kufahamu au kupata fununu kwa miaka yote hiyo kumi? Na kama ilifahamu au kupata fununu, ilimtonya "Mr. Clean"? Chama tawala CCM nacho kilikuwa wapi kipindi chote hicho?
Kwa hakika, sakata hili la ufisadi wa BoT ni kama vile mchezo wa kuigiza. Swali moja linachochea kuulizwa swali jingine na jibu moja linaibua swali jingine jipya. Maswali juu ya maswali, majibu juu ya majibu.
Ukweli ni kwamba mtandao wa sakata hili la ufisadi BoT ni mkubwa na unagusa wakubwa, na hivyo kuna shaka kwamba, mwisho wa yote, Watanzania hawatafahamishwa ukweli wote.
Kwa mfano katika ‘igizo' hili, kuna ‘msanii' anayeitwa Jayantkumar Chandubhai Patel (maarufu Jeetu Patel). Huyu, vyombo vya habari vimeripoti kwamba ndiye anayemiliki kampuni sita kati ya 13 zilizotajwa katika taarifa ya ukaguzi kuwa zililipwa Sh. bilioni 90.3 za EPA kwa kutumia nyaraka batili na zilizogushiwa.
Jeetu Patel huyo huyo na washirika wake alianzisha benki inayoitwa Bank M; huku yeye akiwa mmoja wa wanahisa wenye hisa nyingi. Kinachoshangaza zaidi ni kwamba Bank M, ambayo Jeetu Patel ni mmoja wa wanahisa wakubwa, inapangisha katika jengo linalomilikiwa na "Mr. Clean" ambalo zamani lilikuwa ni la umma lakini akalinunua wakati wa kipindi chake cha urais!
Hiyo maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba Jeetu Patel na kampuni zake hizo sita amechota pesa za wavuja jasho katika benki ya umma na kutumia sehemu ya pesa hizo kuanzisha benki binafsi inayopanga katika jengo la Rais mstaafu, "Mr. Clean".
Sasa "Mr. Clean" hatunaye Ikulu. Sasa tuna Rais mpya, Jakaya Mrisho Kikwete. Huyu kauona ufisadi unaotisha wa BoT ambao "Mr Clean" hakuuona kwa miaka 10!
Aliuonaje? Aliuona kwa sababu raia wema waliuanika katika intaneti? Aliuona kwa sababu kina Slaa wa CHADEMA na vyombo vya habari viliuanika hadharani? Vyovyote vile, aliuona na akateua kampuni ya ukaguzi ya kigeni kumfanyia uchunguzi – Ernst & Young.
Kwa nini kampuni ya kigeni? Jibu ni kwamba ni kwa sababu hana imani na kampuni za humu ndani. Na katika hilo huwezi kumlaumu; kwani kwa jinsi mtandao wa ufisadi ulivyo mkubwa, huwezi kuziamini kampuni za humu ndani moja kwa moja.
Sasa Ernest & Young wamemaliza kazi yao na kumkabidhi Rais Kikwete ripoti yake. Rais Kikwete ameisoma. Amekasirika na akaamua kumtimua kazi Gavana Ballali ambaye "Mr. Clean" alimwona ni "msafi mwenzie" kwa miaka minane!
Lakini Rais Kikwete hakuishia hapo. Amewaagiza Mwanasheria Mkuu, IGP na Takukuru, kuchunguza na kuwachukulia hatua za kisheria wezi wote wa pesa za BoT; ikiwa ni pamoja na kutaifisha mali zao.
Hatua nzuri kabisa. Na bila shaka kura ya maoni ingepigwa leo, Rais Kikwete angepanda chati. Lakini swali la kujiuliza ni hili: Ni kweli kwamba, hatimaye, mafisadi hao watafikishwa mahakamani na mali zao kufilisiwa au hatua hiyo ni ya kupunguza tu shinikizo la kina Slaa, wahisani na vyombo vya habari? Si kweli kwamba Ballali ametolewa tu kafara kupoza mambo?
Na je, asasi hizo ambazo Rais Kikwete anataka zichukue hatua - Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Jeshi la Polisi na Takukuru, zilikuwa wapi miaka kumi hiyo ya kipindi cha "Mr Clean" wakati mamilioni hayo yanatafunwa BoT? Hivi zilikuwa zinasubiri zitumwe kazi na Rais?
Pengine jibu ni kwamba hazikuweza kufanya lolote kwa sababu Rais aliyetangulia ("Mr. Clean") hakuwatuma kazi hiyo! Kwa hiyo kila kitu kinategemea Rais aliye madarakani. Rais asipotutuma kazi, basi, tuendelee kulala tu hata kama tuna taarifa kwamba mabilioni ya pesa za umma yanachotwa kwa kasi na mafisadi!
Ninauliza hivyo maana katika kipindi chote cha miaka kumi cha "Mr Clean", na hata katika miaka miwili ya Rais Kikwete Ikulu, hatukusikia hata mtu mmoja akijiuzulu kazi kwavile mkubwa au wakubwa walimzuia kupambana na ufisadi huo!
Hivyo ndivyo tulivyo. Kama Rais wetu habanwi mbavu na kina Slaa na kina Zitto, kama habanwi mbavu na wahisani na vyombo vya habari, basi, hachukui hatua yo yote hata kama ana taarifa zote za ‘usanii' wa mafisadi unavyotumika kuzikausha pesa za umma Benki Kuu!
Na tusisahau kwamba kina Ballali au Jeetu Patel hawako peke yao katika skandali hiyo ya BoT. Yeye anamiliki kampuni sita tu kati ya 13 zilizochota pesa zile za wakulima na wafanyakazi masikini wa nchi hii na kwenda kujijengea mahekalu Oyster Bay, Masaki na kwingineko wanakoishi mamilionea wa nchi hii masikini.
Ndiyo maana tunasema kwamba, kwa tulichokiona katika skandali hii ya BoT, wanyonge sasa tunahitaji kuwa na Robin Hood wetu wa kweli atakayewakaba koo kina Jeetu Patel na kuturejeshea sisi wanyonge pesa zetu zilizoibwa.