Nikiri kuwa japo nimekuwa nikirambaza ndani ya hili baraza kwa muda sasa, bado najiona kuwa Mwanagenzi kwa kujilinganisha na waliotangulia kujiunga na kwa michango yao mzo mzo katika mada na mijadala mbalimbali.
Mpaka sasa, nadiriki kusema kuwa baraza linavutia kwa mijadala ya wanabodi na pia malumbano, vibwagizo na vijembe vya hapa na pale, ambavyo ni kama chachandu katika pilau.
Pamoja na hayo niseme kuwa bado tuna nafasi ya kuliboresha baraza letu kwani ubora hauna kikomo.
Kwa maoni yangu, tujaribu kuepuka yafuatayo:
1. Kutuhumu na kushutumu kwa nguvu kabisa (siyo kwa namna ya mzaha) baadhi ya waanzilishi wa hoja (wachokozi) au wachangiaji kuwa ni wanachama, wafuasi, wapenzi, wakereketwa, wafurukutwa, au washabiki wa chama fulani cha siasa ilhali wao hawajatuambia hivyo. Daima tuzingatie hoja na si nani katoa hoja.
2. Kutuhumu na kushutumu baadhi ya wachangiaji kuwa "wametumwa" na kikundi cha watu fulani na hata serikali. Hata kama hilo linawezekana, na huenda baraza halina haja wala jinsi ya kulizuia, hoja iwe kuchangia, kukosoa, kupinga, kurekebisha nk "hoja", badala ya kutoa madai ya kijumlajumla. Isitoshe kwa nini mtu uamini kuwa fulani katumwa? Kwani huyo mchangiaji hawezi kuwa na mawazo yake binafsi kama wajumbe wengine? Kwani watoao madai kama hayo wao wanakuwa "wametumwa" na nani? Naamini wengi, kama si washiriki wote, barazani ni wazalendo na wana uchungu na nchi hii. Vinginevyo hatuna kipimo cha kujua nani mzalendo na nani siyo (si hata baadhi ya viongozi wa taifa letu wanaonekana kuwa si wazalendo?).
3. Kujenga dhana kuwa kuna makundi ndani ya baraza, na kwamba hoja hutolewa kwa kufuata makundi, au kuunga mkono hoja za kina fulani tu, na kupinga za wengine. Tuaminiane kuwa washiriki ni watu wazima, wenye uwezo wa kupima mantiki za michango mbalimbali, na kwamba wanashiriki barazani
kwa hiari yao, na wanajiwakilisha wao na nafsi zao.
4. Kama ambavyo imekuwa ikisisitizwa, tuepuke lugha ya matusi, na kumlenga mchangiaji binafsi badala ya hoja yake. Hoja ijibiwe kwa hoja. Kama Mwalimu alivyotuasa, "Tutumie nguvu ya hoja badala ya hoja ya nguvu, na tupingane bila kupigana", kwani sote tuna nia ya kuchangia ujenzi wa Tanzania yetu.
Kwa kumalizia , nadhani ni muhimu tupitishe kanuni na tuziheshimu. Naamini baraza hili ni bora na tusilibomoe kwa mikono yetu wenyewe!
Mungu libariki Baraza,
Mungu Ibariki Afrika,
Mungu Ibariki Tanzania!