Rais Mkapa Azungumzie utajiri wake na awe mkweli na muwazi!
Tangu kuondoka madarakani kwa aliyekuwa Rais wa Tanzania Bw. Benjamin Mkapa tuhuma na madai mbalimbali yamekuwa yakimuandama mstaafu huyo kila kukicha. Madai ya hivi karibuni ambayo yamekuwa ni kama chumvi kwenye kidonda na mafuta ya taa kwenye moto wa kuni, ni yale ya Bw. Mkapa kujipatia mkopo wa benki na hatimaye kuanzisha kampuni ya biashara wakati akiwa bado katika kiti cha urais. Kabla ya madai haya ya sasa kulikuwa na madai mengine mengi ambayo yanamhusisha Rais Mkapa mwenyewe, mkewe au familia yake ya karibu.
Mara hizo zote, juhudi za kumtaka Rais Mkapa azungumzie na kujibu madai na tuhuma zinazotolewa dhidi yake zimegonga mwamba. Lakini kwa vile Tanzania hatuna wafalme, na viongozi hutawala kwa ridhaa ya watu, na ya kuwa katika nchi ya kidemokrasia kama ya kwetu viongozi huwajibika kwa watu basi hatuna budi kwa mara nyingine tena kumtaka Rais mstaafu Bw. Benjamin William Mkapa kuzungumzia utajiri alioupata akiwa madarakani na kuonesha kwa vielelezo kamili kuwa utajiri wake kaupata kwa njia ya halali na siyo kwa sababu ya kutumia cheo na nafasi yake ya Urais.
Kwa watu wengi ambao wanafuatilia tuhuma zilizotolewa na zinazoendelea kutolewa kwa Rais Mkapa watakumbuka kuwa kati ya tuhuma zote kubwa ya zote ni ile tuhuma ya kuhusika kwake katika ununuzi wa rada ya kijeshi ambayo Benki ya Dunia ilisema ni ghali mno na haikufaa kwa matumizi ya Tanzania. Baada ya mamlaka za Uingereza kuanza kufanya uchunguzi wa kampuni iliyohusika na uuzaji wa rada hiyo, watu na taasisi mbalimbali hapa nyumbani na nje ya nchi walijenga hoja kuwa Bw. Mkapa azungumze na wananchi na awaambie ni kwa kiwango gani alishiriki katika ununuzi wa rada hiyo. Kelele hizo zilipozidi, Rais Kikwete akiwa katika moja ya ziara zake nje ya nchi (Brussels, Ubelgiji) aliingilia kati na kuwauliza Watanzania Hivi mnataka mzee Mkapa atoe sauti, sauti kuhusu jambo gani? Mnataka aseme nini, mimi naona tumwache mzee wa watu.
Suala hili la uanzishaji wa kampuni uliofanywa na Rais Mkapa na mkewe mwaka wa nne tu wa Urais wao umezidi kuzua wasiwasi na hisia za kuwa Rais Mkapa hakuwa mtu msafi kama tulivyofanywa kuamini wakati wa uchaguzi wa 1995. Hata hivi sasa watu na taasisi mbalimbali zinapomtaka Rais mstaafu huyo kuzungumzia miradi yake wakati akiwa katika ofisi ya juu kabisa nchini, kelele za mwacheni mzee wetu zimeanza tena kusikika. Tahariri ya mojawapo ya magazeti ya serikali wiki iliyopita ililitamka bila haya au kigugumizi chochote kile kuwa Mkapa amefanya mengi kwa taifa hili na tumpe nafasi ya kustaafu na kupumzika bila bughudha yoyote.
Kwa baadhi ya watu kumtaka Mtanzania mwenzetu huyo kutuambia na kututhibitishia kuwa hakutumia nafasi yake vibaya alipokuwa madarakani ni bughdha isiyo ya lazima na ni sawa na kumuandama Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu kwa sababu ambazo hazina msingi zaidi ya chuki.. Kwa watetezi hawa wa usiri, kuulizia kiongozi aliyepita katikati yetu na kuomba kura zetu mara mbili akiahidi kupigana vita dhidi ya ufisadi huku akipepea bendera ya "uwazi na ukweli" basi imekuwa tatizo. Tunapouliza ni jinsi gani kiongozi tuliyemweka madarakani kwa kura alitumia ridhaa hiyo na kama hakuitumia ridhaa hiyo kujinufaisha yeye na familia yake imekuwa nongwa.
Ndugu zangu kama waswahili wasemavyo, akutukanaye hakuchagulii tusi. Mtanzania mwenzetu tulimchagua atuongoze kwani tuliambiwa kuwa kati ya wale wote walioonesha nia ya kutaka kwenda Ikulu mwaka 1995 yeye ndiye aliyekuwa msafi. Nakumbuka alivyonadishwa na Mwalimu Nyerere pale uwanja wa Nyamagana. Tukamchagua na kumpa dhamana ya uongozi wa nchi yetu. Miaka kumi baadaye Mtanzania huyo anaondoka Ikulu akiwa Bilionea na watetezi wake wanatuambia tusiulize kazipataje, kweli woga mwingine! Kiongozi ameondoka akiwa na majumba bwelele ya kupanga na makazi, ndani na nje, akiwa na akaunti za fedha hapa nyumbani na ugenini, na akiendelea kutesa kiulaini kwa pensheni na mafao kadha wa kadha yanayotokana na ofisi yake iweje kumuuliza kuwe kosa? Kumuuliza mzee utuambie umevipataje vitu hivi vyote ndani ya miaka 10, wakati yule aliyetawala nchi yetu miaka 25 hakuweza tunaambiwa ati tunambughudhi mzee. Hoja nyingine ni za kutupa zinapotolewa tu hadharani.
Ukweli ni kuwa watetezi wa Mkapa wanatutaka tukae kimya kwa vile hata tuulize vipi hatutapewa majibu. Binafsi naona kuwa wale wanaotutaka tunyamaze tusiulizie utajiri wa Rais Mkapa wanatumia visingizio vya "Amani ya Tanzania", "Kubadilisha uongozi kwa ustaarabu" na "uzee wa Mkapa" kama mbinu ya mazingaombwe ili tusione viini macho vinavyotendeka au vilivyokwisha tendeka. Mbinu zao hizo zinatokana na hofu moja tu, nayo ni hofu ya ukweli. Watetezi wa Rais Mkapa wanaogopa ukweli kujulikana na watu wa kawaida kwani sifa zote za "amefanya mengi kwa Taifa hili" zitapeperuka hewani kama vumbi kwenye jani kavu lipeperushwapo na upepo. Watetezi hawa siyo tu hawako tayari kuuacha ukweli ujulikane bali hawawezi kustahili kuona ukweli huo! utawaumbua.
Kuhusu hili suala la Rais kupewa mkopo wa dola laki tano na kuweza kuanzisha biashara akiwa ofisini na kutajwa ati huo ni mfano mzuri wa kukopa kutoka benki na klipa. Wazo hilo kwanza linatuchekesha na linasikitisha mno. Kama alikuwa ni mfano mbona hatukuambiwa wakati anakopa na kurudisha fedha hizo ili tumuige? Kwanini awe mfano baada ya siri kufichuka? Hivi wanataka Watanzania tuamini kuwa Rais Mkapa alikwenda mwenyewe benki kimya kimya au waseme tu kuwa benki ilimfuata Ikulu.
Sitashangaa kabisa kuwa imekuwa vigumu kwa Rais Mkapa kufuatilia kwa makini na kwa uzito unaostahili tuhuma na madai yote yanatolewa dhidi yake binafsi na familia yake. Hili linawezekana aidha kutokana na wingi wake au kwa sababu nyingine yoyote, nimeona nijitolee basi kwa moyo wangu wa ukarimu kuorodhesha tuhuma na manunguniko ambayo yamejaa mitaani kuhusu utawala wake na hasa kwenye suala hili la kujitengenezea utajiri wa haraka haraka ndani ya miaka kumi ya kukalia kiti urais wa jamhuri yetu. Madai hayo ni haya:
Kwamba akiwa Rais na kwa kutumia nafasi hiyo aliweza kujipatia mkopo mkubwa kutoka benki miaka minne tu ya utawala wake tena alifanya hivyo wakati watanzania wako katika kumuuguza baba wa Taifa. Kwa mtu aliyepewa kwa dezo nafasi hiyo na Mwalimu Nyerere kitendo hicho kinaonekana ni cha kisaliti na kuvunja vunja kila ambacho Mwalimu alisimamia.
Kwamba katika kipindi chake hicho kifupi aliweza kukusanya fedha kiasi cha kujenga jumba Lushoto, kufanyia matengenezo nyumba ya Sea View, kujenga jumba jipya Msasani, na kununua nyumba/hoteli huko Afrika ya Kusini na ikadaiwa alimuomba mzee Madiba aipe baraka zake, na mzee huyo akamkatalia.
Kwamba ilikuwa ni kutokana na baraka zake Taifa letu likaingia kwenye Mkataba wa kununua rada ya kijeshi ambayo kwa mujibu wa Benki ya Dunia ilikuwa ni ghali na kwa Tanzania haifai. Baadaye imekuja kugundulika kuwa dalali aliyeshiriki kutuuzia rada hiyo alimegewa karibu dola milioni 12 kwa kazi yake huku akiwagawia watu wachache serikalini. Je yeye (Mkapa) alijua kuhusu mgao huu kwa namna yoyote ile.
Kwamba ilikuwa ni katika uongozi wake Taifa letu likaingizwa kwenye mikataba ya ajabu ya uwekezaji na ile ya ubinafsishaji. Ilikuwa vipi yeye kama Rais kushindwa kabisa kuweka maslahi ya Taifa mbele hadi mrithi wake anapokuja ndipo makosa yanaonekana hadi kudaiwa kuwa Tanzania hatuna wataalam wa mikataba? Kama alijua wataalam wetu hawajabobea katika mikataba hii mikubwa ya biashara kwanini hakuomba msaada mapema hadi leo tunalazimika kuwaomba watuonee huruma na kuanza kupitia tena mikataba?
Kwa vile alianza biashara zake na ujasiriamali akiwa bado Rais, ni kwa jinsi gani shughuli zake hizo ziliingilia utendaji kazi wa ofisi yake au yeye mwenyewe na hivyo kuathiri matokeo ya kazi zake alizoapishwa kikatiba. Je, haoni kuwa wazo la Rais kuanza kufanya biashara kubwa akiwa ofisini inaleta picha mbaya na hasa kuonesha mgongano wa maslahi?
Kama kweli katika kufanya biashara hizo akiwa Ikulu alitaka kuwa mfano kwa Watanzania wengine ni kwanini Watanzania hawakuambiwa kuwa Rais wao ni mjasiriamali na ameanzisha biashara kama wengine, na kwanini hakujitolea kuwa mfano wa kukopa kutoka benki na kulipa?
Kwamba, kwa kutumia vyombo vya dola alilazimisha mali ya Watanzania kuendeshwa na wageni ambao baadaye tukagundua kuwa hawakuwa na uwezo wa kutuendeshea kampuni yetu. Je haoni haja ya kuwaomba wananchi msamaha kwa kutudhalilisha kiasi hicho wakati mapolisi na mitutu yao walipowaingiza kwa nguvu watendaji wa Tanesco toka Afrika ya Kusini?
Kwamba, alipokuwa kwenye mkutano wa baraza la kiuchumi kule Davos, Uswisi ilipigwa haramba iliyoongozwa na mcheza filamu maarufu Bi. Sharon Stone ambapo kiasi cha dola milioni moja zilichangwa ndani ya dakika tano ili kumpa Rais Mkapa katika juhudi za nchi yake kupambana na ugonjwa wa Malaria. Aliporudi na hata baadaye, Watanzania hatujaambiwa ahadi ya kiasi hicho ilitimizwa vipi? Ni kiasi gani kiliweza kupatikana taslimu na fedha hizo zilitumiwa vipi na kikundi gani katika juhudi za kuangamiza ugonjwa wa Malaria? Kwanini hakutuambia wakati huo?
Basi, hayo ni maswali machache ambayo yako mitaani na Watanzania kwa kweli wangependa wasikie majibu yake kwa ukweli na uwazi. Kwa kufanya hivyo atajijengea heshima kwa wananchi na kuonesha mfano wa ujasiri wa kiongozi kutoogopa maswali. Hata hivyo kama ataendelea kuwa kimya (kama ilivyo kawaida ya baadhi ya viongozi) basi anawapa Watanzania idhini ya kujaribu kutafuta ukweli kwa njia yoyote ile zikiwemo njia za kisheria. Itakuwa ni jambo la kusikitisha sana na la aibu endapo kesi itafunguliwa katika mahakama ya nyumbani au nje ya nchi ili kutafuta ukweli wa utawala wa Rais Mkapa. Viongozi wetu lazima waanze kubadilika kwani Watanzania waliowazoea miaka ya nyuma waoga oga hivi na wasiothubutu sasa hivi wameanza kuamka.
Kuendelea kukaa kimya na kupuuzia madai dhidi yake Rais Mkapa hajitendei fadhila, hawatendei haki wananchi waliomweka madarakani na haimsaidii kitu zaidi ya kuanza kuonekana amejiunga na jumuiya teule ya viongozi wa kiafrika ambao kwa nguvu zote wameingia Ikulu wakiwa masikini na wakatoka matajiri. Kwa kuendelea kuwa bubu kuhusu madai dhidi yake na familia yake Rais Mkapa ataanza kuonekana ni mmoja wa viongozi wa kiafrika waliotumia nafasi zao kujitajirisha kupitia migongo ya wananchi wao. Licha ya sifa ambazo amezipata nje ya nchi, wakati umefika "mzee wetu mstaafu" azungumze na wananchi wenzake ili aonekane mwenye hekima na siyo kiburi.
Vinginevyo sisi Watanzania wenzake tutaanza kupata jibu la lile swali alilouuliza Mwalimu wakati wa vuguvugu la uchaguzi wa mwaka 1995 baada ya vigogo wengi wa CCM na upinzani kujitokeza kutaka kugombea nafasi ya kuingia Ikulu. Mwalimu aliuliza "watu wengi wanakimbilia Ikulu, Ikulu kuna nini?" Hatujui kama Rais Kikwete naye ameshaanza biashara huko Ikulu au ana mpango huo, hata hivyo inaonekana Rais Mkapa ameanza kutupa jibu la hicho kilichoko Ikulu ambacho "watu wengi wanakimbilia". Tulichobaki kushangaa ni kama ule "utakatifu" wa Ikulu bado upo au uliondoka na Mkapa.
Wasiliana nami:
mwanakijiji@jamboforums.com
Piga Simu: +1248 686 2010