Nyiye waandishi, mwacheni babangu
2008-06-13 09:28:35
Na Godfrey Monyo
Mtoto wa Rais mstaafu, Bw. Benjamin Mkapa, Steven Mkapa, amevishutumu vyombo vya habari kwa kumwandika vibaya baba yake kuwa ni fisadi.
Alisema kuwa kinachofanywa sasa na vyombo hivyo ni kumshushia baba yake heshima na utu alionao katika jamii.
Mtoto huyo ambaye alijigamba kuwa kinachotafutwa na waandishi wa habari katu hakiwezi kupatikana kwa kuwa uelewa wao ni mdogo.
Aidha, Bw. Steven, aliwashangaa waandishi hao pamoja na watu wengine wanavyopoteza muda wao kukaa na kumjadili baba yake badala ya kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Aliyasema hayo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na Nipashe wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa na kampuni inayojishughulisha na utengenezaji na usambazaji wa vifaa vya maji ya ERV East Africa.
Bw. Mkapa, anadaiwa kufanya biashara akiwa Ikulu ambapo mwaka 1999 ilianzisha kampuni iliyoitwa ANBEM.
Aidha, anadaiwa kuchukua mkopo wa dola za Marekani 500,000 katika Benki ya Biashara (NBC) bila ya kuweka dhamana yoyote.
Pia Bw. Mkapa maarufu kama ``Mr.Clean`` anadaiwa kununua mgodi wa Kiwira Coal and Power Limited kwa bei ya ``kutupa`` ya Sh. milioni 70 wakati mgodi huo unathamani ya Shilingi bilioni nne.
Aidha, anadaiwa kumiliki baadhi ya majumba ya kifahari sehemu mbalimbali hapa nchini sambamba na kumiliki ekari 600 ya miwa huko Mtibwa mkoani Morogoro.
Aidha, kiongozi huyo hajawahi kukanusha taarifa za kuwa yeye ni mshiriki wa Benk M.
Bw. Steven alionekana wazi kuwa na ghadabu na waandishi wa habari kutokana na kile alichodai kuwa wanatumiwa na watu wachache kumchafua baba yake.
Alisema kuwa waandishi hao wamekuwa wakipewa fedha kidogo na kutumia muda mwigi kuhangaika na baba yake, jambo ambalo alisema katu hawataweza kupata kitu.
``Najua na wewe ni miongoni mwao kati ya wale wanaotumiwa kumchafua baba lakini hamtaweza kitu hizi ni namba zingine,`` alisema Bw. Steve.
Mtoto huyo wa Mkapa ambaye anajulikana zaidi kwa jina la ``Merinyo`` alisisitiza kuwa maneno yake yanatoka moyoni na anazungumza kwa kujiamini bila ya kuogopa kitu na hivyo wahusika wapatiwe taarifa ili watafute kazi zingine za kufanya.
``Wewe unakuja kunichora hapa maswali mengi ... Nikikuuliza mimi unanijibu kwa kuniuliza swali maana yake nini? kama umekuja kunijulia hali mzee anaingia vipi kwenye mazungumzo yetu?`` Alihoji Merinyo.
Merinyo ambaye pia alionekana kukerwa sana na madai kwamba baba yake ni mimiliki wa mgodi wa Kiwira alihoji kwa nini habari za Kiwira haziishi katika vyombo vya habari.
Hata hivyo, alipolulizwa kwa sasa anajishulisha na kazi gani ambayo inampatia kipato alisema kwa hasira kuwa anafanya kazi katika mgodi wa Kiwira.
``Najua unataka niseme nini... Nenda kaseme, nafanya kazi Kiwira... Kwa sababu nadhani nyiye bila Kiwira na Mkapa hamna cha kuandika,`` alisema Merinyo huku akinyanyua glasi yake tayari kwa kunywa.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Mark Bomani, ambaye alikuwa mgeni rasmi aliishauri serikali kuwa wepesi kukubali ushauri unaotolewa na watalamu.
Jaji huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa kiwanda cha bia cha Serengeti ambayo ndio ilikuwa moja ya wadhamini wa hafla hiyo, alisema yapo mambo mengi ambayo kama serikali ikikubali ushauri yataweza kuiletea faida kubwa nchi na hivyo kuongeza pato la taifa.
Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na kutumia vifaa vinavyopendekezwa katika kutoa huduma za maji kama vile vipuri vya kusambazia maji.
``Yapo maji mengi yanapotea njiani lakini kama kungekuwa na vifaa imara vinavyotumika yasingepotea kiholela,`` alisema Jaji Bomani.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ERV East Africa Bw. Phillemon Ntahilaja, alisema kuwa wanakusudia kuwapatia mafunzo zaidi wataalamu wao.
Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuweza kuboresha zaidi huduma zao na kwa watanzania kwa ujumla.
SOURCE: Nipashe