CHADEMA yamgeukia Lowassa
na Tamali Vulu
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemwandikia barua Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kikimtaka atoe tamko kuhusu kuhusishwa kwenye tuhuma za rushwa kwa wajumbe wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge zilizotolewa na Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo.
Barua ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Wilbroad Slaa ya Januari 15, 2006, kwenda kwa Lowassa, inaeleza kushangazwa na ukimya wake pamoja na tuhuma hizo nzito zilizotolewa na Ndesamburo.
Taarifa za uhakika ambazo gazeti hili limezipata kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu zinaeleza kwamba, barua hiyo imeshafika katika meza ya kiongozi huyo wa tatu kimamlaka serikalini, baada ya Rais na Makamu wa Rais.
Hata hivyo jitihada za gazeti hili kuwasiliana ama na Lowassa mwenyewe au mwandishi wake wa habari, Said Nguba, ili kupata maoni yake kuhusu suala hili, zimekuwa zikigonga ukuta kwa takriban wiki moja sasa tangu Ndesamburo alipotoa tuhuma nzito wiki iliyopita, sambamba na kutangaza kujiuzulu ujumbe wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Ofisa mmoja wa juu serikalini aliyezungumza na Tanzania Daima kwa sharti la kutotajwa jina, alisema Waziri Mkuu amekaririwa akiyaelezea maneno hayo ya Ndesamburo kuwa yasiyo na ukweli wowote.
Alipotakiwa na Tanzania Daima aeleze hatua ambazo Lowassa amepanga kuzichukua dhidi ya suala hilo ambalo kauli yake inahusishwa, ofisa huyo alisema, vyombo vinavyohusika vitalishughulikia.
Sisi tunajua ni kwa nini Ndesamburo kasema maneno hayo. Tunajua kila kitu kinachoendelea kuhusu jambo hili. Ni vyema tukanyamaza. Waziri Mkuu anajua anachofanya, hawezi akasema maneno ya namna hiyo. Ipo siku ukweli utabainika, alisema ofisa huyo wa serikali.
Badala yake, ofisa huyo wa serikali alieleza pia kushangazwa kwake na ukimya wa Mengi ambaye ndiye aliyetajwa na Ndesamburo kumwambia maneno hayo kuendelea kukaa kimya pasipo kutamka hadharani, iwapo ni kweli alifikisha maneno hayo au la.
Ninyi mnamtafuta Waziri Mkuu atoe tamko, mbona hatujasikia Mengi akisema hadharani ni kweli kuwa alimwambia Ndesamburo maneno haya? Si yuko na anapatikana, mbona amekaa kimya? alihoji ofisa huyo.
Slaa katika barua aliyomwandikia Lowassa anasema: Pamoja na uzito wa tuhuma hizi na hasa ukizingatia uzito wa nafasi yako ya Uwaziri Mkuu mpaka sasa hujajitokeza wewe mwenyewe kukanusha au kukubali taarifa hii.
Kwa vyovyote ukimya wako katika suala hili kadiri unayoendelea, unaweza kuwafanya wananchi kupoteza imani kuhusu msimamo wako katika vita dhidi ya rushwa na jihihada za kuleta utawala bora nchini.
Kama kweli wewe ulifahamu kuwa kuna mtu ametoa rushwa kwa wabunge na hukuchua hatua zinazostahili, kwa vyovyote ni kinyume cha sheria, maadili ya uongozi, na dhamira ya Mheshimu Rais Jakaya Kikwete ya kupambana na rushwa bila kumfumbia macho mtu.
Kwa upande mwingine, tuhuma kwamba mhimili wa serikali unaingilia mhimili wa Bunge zinakuelekea wewe (Waziri Mkuu) moja kwa moja kama kiongozi wa shughuli za serikali bungeni. Suala hili ni kinyume na utawala bora na mgawanyiko wa madaraka uliomo katika sheria na katiba ya nchi ambayo umeapa kuilinda, ilieleza sehemu ya barua hiyo ambayo nakala yake imepelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete na Spika wa Bunge, Samuel Sitta.
Tayari Spika amemwandikia barua Ndesamburo akimtaka kumwandikia kwa maandishi tuhuma za rushwa alizozitoa dhidi ya kamati hiyo.
Wiki iliyopita, Ndesamburo alitangaza kujiuzulu ujumbe katika kamati hiyo kwa madai kuwa alielezwa na Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi, kuwa aliambiwa na kiongozi mwandamizi serikalini kwamba, wajumbe wa kamati hiyo wamepewa rushwa kutoka kwa mfanyabiashara, Yusuf Manji, ili asitendewe haki kwenye kesi yake na Mbunge wa Mkuranga, Adam Malima.
Ndesamburo alieleza kuwa anahofia usalama wa maisha yake na hataki kuhusika na maamuzi ambayo yanagubikwa na tuhuma za rushwa, huku akitaka kuitwa na Mengi na kiongozi huyo ili kuthibitisha madai hayo.
Akichangia bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Malima alimtuhumu Mengi kwa kujipa muda mwingi kujitangaza kwenye matukio yanayomhusu huku akitoa muda mfupi katika matukio yanayomhusu Rais na Waziri Mkuu.
Kutokana na tuhuma hizo, Mengi alilalamika kwa Spika kuwa Malima hakumtendea haki kumtuhumu sehemu ambako hawezi kujitetea.
Baada ya malalamiko hayo, Spika alipeleka mashauri hayo kujadiliwa kwenye kamati hiyo, hatua iliyozusha malalamiko kutoka kwa baadhi ya wabunge kuwa haikuwa haki.
Tayari Manji ameshatoa tamko kukanusha kuhusika kwa namna yoyote kuwapa rushwa wabunge na amemtaka Ndesamburo aeleze kile ambacho alidai kinafichwa katika suala hilo zima.