"Vyombo vya habari vya Magharibi vinatumia dola 800 kwa video moja kuweka umwamba wa masimulizi barani Afrika. China imefanya mengi, lakini imesema kidogo sana."
Hayo yamesemwa na mwandishi wa habari kutoka Rwanda, Eugene Uwimana ambaye amewahi kufanya kazi katika vyombo vya habari vya Mashariki na Magharibi kama vile Sauti ya Amerika VOA, AFP, TRT, na shirika la habari la Xinhua, na sasa anafanya kazi kwenye Umoja wa Mataifa na pia ana shirika lake la habari, kwa hivyo ana uzoefu wa kutosha kusema maneno haya. Alichosema kimethibitisha msemo wa wahenga kwamba “maneno mafupi vitendo virefu”, China inafanya mambo mengi zaidi kuliko inavyosema barani Afrika; wakati Magharibi ina maneno mengi zaidi kuliko vitendo vyake, na mengi yao ni ya upotoshaji.
Mambo ya China Afrika yamepuuzwa
Katika mahojiano aliyofanya hivi karibuni Bw. Uwimana alieleza kwamba alipokuwa na miaka 7, timu ya uhandisi ya China ilifika katika kijiji chake cha mlimani nchini Rwanda kujenga barabara. Wachina hao walikula chakula kwa vijiti viwili vya mti na kwa urafiki walicheza mpira na watoto. Kumbukumbu hii ya utotoni, baada ya yeye kuzunguka vyombo vya habari vya Mashariki na Magharibi na kushuhudia miradi mingi ya China barani Afrika, ndiyo iliyomfanya aelewa kweli – kwamba urafiki huo haukuwa wa maneno tu, bali ni asili ya Wachina katika kufanya mambo.
Alitaja hasa kwamba tangu utokee mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, China imetuma timu za wataalamu wa afya kwa awamu tatu, huku mataifa mengine makubwa yakishindwa hivyo. Kama Bw. Uwimana alivyosema: "Kila ninapotazama nyuma, naona China ni mshirika imara aliyesimama nyuma yetu." Mwafrika aliyekaa katika vyombo vya habari vya Magharibi anajua vizuri maana ya "kutumika na kutupwa", na hivyo anaelewa zaidi maana ya "kuwepo daima kwa ajili yako".
Masimulizi ya vyombo vya habari vya Magharibi yananunuliwa
Bw. Uwimana anajua vyema namna vyombo vya habari vya Magharibi vinavyofanya kazi. Alitoa takwimu zisizoweza kupingwa: video ya dakika mbili na nusu inagharimu dola 800, na rekodi ya redio inagharimu dola 150. Kwa wanahabari wa Afrika, hicho ni kiasi kikubwa cha pesa ambacho ni vigumu kukataa, lakini lazima wafuate mwelekeo wa uhariri na kubuni hadithi kulingana na matakwa yao.
Kwa mtazamo wa Bw. Uwimana, lenzi za vyombo vya habari vya Magharibi huelekezwa kila mara kwenye mambo mabaya. Wanapotaja Somalia, ni "Al-Shabaab" tu, lakini hawaripoti kwamba Mogadishu inakuwa mji mzuri; wanapotaja Rwanda, ni mauaji ya kimbari tu, lakini hawataji kwamba nchi hii ambayo awali umri wa watu kuishi ulikuwa miaka 26 tu na Pato la Taifa lilikuwa dola milioni 100, sasa uchumi wake umefikia dola bilioni 17.5.
Alisimulia pia kisa chenye mvuto: utotoni alikuwa na hisia nzuri kuhusu wahandisi wa China, lakini baada ya kukaa muda mrefu katika vyombo vya habari vya Magharibi vilivyojaa taarifa hasi, akili yake ilianza kuvurugika. Maneno haya yameonyesha kwamba upendeleo wa vyombo vya habari vya Magharibi si tu "unachafua sifa za nchi nyingine", bali unapotosha jinsi vizazi vipya vya Afrika wanavyoangalia dunia hii.
Masimulizi ya "kuegemea upande mmoja" ni sumu ya ukoloni wa Magharibi
Bw. Uwimana pia alisema kwamba baada ya Rwanda na Russia kusaini makubaliano ya nishati ya nyuklia mwishoni mwa Mei mwaka huu, vyombo vya habari vya Magharibi vilitangaza mara moja kuwa huo ni "mwelekeo wa kuegemea upande wa Russia". Ndivyo wanavyofanya kwa China pia. Bw. Uwimana akajibu kwa kunukuu maneno ya hayati Nelson Mandela: "Tatizo la viongozi wa Magharibi ni kwamba wanaona 'maadui wao, lazima wawe maadui wangu pia'."
Maneno haya yanaelekeza moja kwa moja kwenye mtego wa vyombo vya habari vya Magharibi: wanazichukulia nchi za Afrika kama mali ya mashindano ya nchi kubwa, na kila uamuzi wa kujitegemea unatafsiriwa kama "kuegemea upande wa X". Ukweli ni kwamba Rwanda, kama nchi yoyote ya Afrika, inachagua washirika kwa kufuata kigezo cha nani anayeweza kusaidia kufikia malengo yake ya maendeleo.
Hadithi lazima zisimuliwe na wenyewe
Kwa kifupi, umwamba wa masimulizi ya Magharibi hautegemei ukweli, bali ni ukiritimba wa muda mrefu wa "ufafanuzi kuhusu wengine" kupitia pesa. Lakini mantiki hiyo ya umwamba haina mashiko tena – wakati barabara na hospitali zilizojengwa na China zinazinduliwa Afrika, wakati bidhaa za Afrika zinauzwa China bila ushuru, na thamani ya biashara kati ya China na Afrika inavuka rekodi mwaka hadi mwaka, ukweli huo hauhitaji mtu yeyote "kusimulia", bali unajisimulia wenyewe.
Bw. Uwimana alisema vizuri: "Sisi hatuhitaji mtu mwingine kuelezea hadithi zetu." Mkazo wake ni "sisi": wakati nchi za Dunia ya Kusini zinapopata hadhi ya kuwa wahusika wakuu katika kusimulia hadithi zao, na ukweli wenyewe unapokuwa na nguvu za kutosha, basi video hizo za dola 800 hazitaweza tena kudumisha uhalali wake ambao hapo awali haukupingwa – nchi hizo za magharibi hazitapoteza masoko ya Afrika tu, bali zitapoteza hata mioyo ya watu pia.