NCHI YETU INA LAANA YA NANI?
Kila mahali utasikia CCM wabaya bwana! CCM hatari sana, CCM mafia! Yaani leo tunaiogopa CCM kuliko maisha yetu na vizazi vyetu! Hebu fikiria: Huyu CCM tunayemwogopa ni nani hasa?
Mambo haya na mengine mengi yananifanya nifikirie upande wa pili wa shilingi. Najiuliza, mfumo wa vyama vingi vya siasa umeisaidia nchi hii au umeiingiza kwenye matatizo zaidi? Hii ndiyo tafakuri yangu ya leo!
Yako mawazo yatakayokinzana kuhusu hoja hii. Wako watakaosema kuwa vyama vingi ni tunda la fikra za Mwalimu Nyerere kwani alikuwa wa kwanza kutamka hadharani umuhimu wa CCM kuona ulazima wa kuukubali mfumo huu. Hii ilikuwa mwaka 1991.
Wengine watadai ni zao la mabadiliko ya mifumo ya kisiasa duniani kufuatia kumalizika kwa vita baridi (cold war). Vita baridi ilikuwa mvutano wa kiitikadi na kisera duniani. Mataifa ya Magharibi yakiongozwa na Marekani, yalisimamia itikadi za kibepari na sera za uchumi wa soko. Zile za Mashariki zikiongozwa na Urusi, zilisimamia itikadi za kijamaa/kikomunisti na sera za uchumi hodhi.
Mataifa mengi duniani yaliamua kuwa upande mmojawapo wa mvutano huu. Yapo yaliyodai kuwa "hayafungamani na upande wowote" (Tanzania ikiwemo), lakini dhana hii iliishia zaidi kuwa ya kinadharia kuliko vitendo. Ukweli Tanzania ilifungamana zaidi na nchi za Mashariki.
Wengine watadai vyama vingi ni zao la shinikizo la nchi za Magharibi kwa nchi za dunia ya tatu, kufuatia ushindi wao katika vita baridi. Utawala wa demokrasia ya vyama vingi, sambamba na mabadiliko kadhaa ya kisera sasa, yalitumiwa kama chambo ili kuwezesha nchi hizi za dunia ya tatu (zilizokuwa hoi kiuchumi), Tanzania ikiwamo, kupata misaada mbalimbali.
Vyovyote iwavyo, vyama vingi tunavyo. Sasa hebu tuangalie historia inatueleza nini kuhusu chimbuko la ufisadi wa kutisha baada ya mfumo huu kuanza.
Wakati wa utawala wa awamu ya kwanza, hasa baada ya Azimio la Arusha, nchi hii ilikuwa na itikadi iliyoeleweka. Ilikuwa ya Ujamaa na Kujitegemea, chini ya mfumo wa chama kimoja. Kiongozi Mkuu, Mwalimu Nyerere, aliweza kutoa dira iliyotokana na sera na falsafa alizoziasisi na kuziamini. Kama sera na falsafa hii ilikuwa sahihi, si shabaha ya tafakuri yangu leo.
Pengine kwa sababu ya uadilifu wa Mwalimu, awamu hii haikufanya masihara na mafisadi. Watu walichapwa viboko hadharani. Viongozi waandamizi na wafanyabiashara hawakupewa fursa ya kuwa mawakala wa kiongozi mkuu, yaani rais. Tukiacha mambo ya nje, agenda za vikao zilikuwa ni wananchi na mustakabali wa taifa. Hakuna historia ya ufisadi.
Awamu ya pili chini ya Rais mstaafu, Mzee Ali Hassan Mwinyi, ilikuwa awamu ya mpito na hapa nchi ilianza kupoteza dira kiitikadi, kisera na hivyo kimwelekeo. CCM ilizika kimya kimya itikadi na sera za kijamaa na kukumbatia sera za kibepari na uchumi wa soko. Unafiki wa kisiasa hapa sasa uliota mizizi.
Itikadi na sera za ujamaa, zilionekana kupendwa zaidi na wananchi, lakini zilipigwa vita na wafadhili. CCM iliegemea upande wa wafadhili, ikazika itikadi ya ujamaa na kuanza kubadilisha sera zake za kiuchumi kuwa za soko. Wananchi hawakushirikishwa. CCM ikaendelea kudanganya mpaka leo kupitia katiba ya nchi kuwa, nchi hii ni ya Ujamaa na Kujitegemea. Hata ndani ya chama chenyewe, wanachama wameendelea hadi leo kudanganywa chama chao kina itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea – eti kwa mtindo wa kisasa!
Viongozi wakuu ghafla wakaanza kuwa na washirika wa karibu. Ikulu ikavamiwa na wapambe ambao wanabadilishana viti kila serikali ikibadilika. Uswahiba na watawala vikawa sera isiyo rasmi hadi leo. Wako wengi wametajirikia Ikulu na jamii kamwe haiwajui hawa. Madalali hawa wa nchi wapo na wamebana kimya. Muda utasema. Wametumika kama kinga kwa viongozi wakuu.
Awamu hii ilisimamia uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi. Wananchi wengi hawakuwa na hofu bado. Ilikuwa almanusra CCM iende na maji. Wamshukuru Mwalimu Nyerere.
Awamu ya tatu ya Benjamin Mkapa iliingia madarakani kwa nguvu ya ziada. Michubuko ya uchaguzi wa vyama vingi ilimtesa kwa kipindi chote cha utawala wake.
Aliweka misingi mibaya ya uhasama wa kisiasa. Alibariki vyombo vya serikali katika azma ya kuzima kukua kwa demokrasia ya vyama vingi. Alitumia vyombo vya dola hasa usalama wa taifa na Jeshi la Polisi kudhibiti wapinzani ambao sasa walionekana adui wa serikali na chama chake na si wadau muhimu katika mustakabali wa kusimamia haki na ustawi wa nchi. Wapinzani walichukiwa na kutengwa. Hapa ndipo hofu ilipojengwa kwa nguvu zote.
Awamu hii iliwajenga madalali wa nchi kwa nguvu zote. Wengine Ikulu haikuwatosha, wakajipenyeza na kwenye chama tawala, CCM. Hawa wameshiriki vilivyo katika kuuza nchi, huku wakikinga biashara chafu za viongozi wakuu tuliowapa dhamana ya kutuongoza.
Mikakati ya makusudi ya kiharamia ilifanywa kudhibiti na kudhalilisha wapinzani. Dola ilitumika kunyima upinzani rasilimali watu na rasilimali mali. Wafanyabiashara waliounga mkono vyama vya upinzani, walishughulikiwa na kufilisiwa. Wenye roho nyepesi (ambao ni wengi) walilazimishwa kimazingira kuvikimbia vyama hivyo. Wasomi nao hali kadhalika. Mapambano ya kisiasa sasa yakawa mapambano ya kitabaka.
Matajiri wafanyabiashara wa ndani na nje wakaiteka CCM. Wasomi nao kwa mfumo huu tegemezi wakatangaziwa kuwa vyeo na kinga ya ajira viko CCM. Wakatimka. Yeyote aliyependa fadhila, utajiri na cheo, akaingia CCM. Yeyote aliye na cha kuficha akapata kinga CCM. Nchi ikageuzwa "shamba la babu" ambamo kila mwenye nguvu anachuma kadiri ya uwezo wake na babu hana uwezo wa kuzuia.
Fedha ikawa itikadi ya CCM. Nchi ikakosa mwelekeo wa kisera. Fedha, ya wafadhili wa nje au wa ndani ndiyo ikawa sera na mhimili wa taifa na maendeleo yake.
Awamu ya Mkapa, iliendeleza sera za uhuru wa soko - fikra na dira zikitoka kwa wafadhili. Uchumi sasa ukashikwa rasmi na wageni. Wazawa wakatelekezwa na kurushiwa "mapanki." Akatokea "mwenzao" Iddi Simba akatetea wazawa! We! Cha moto alikiona!
Utandawazi ukachukua nafasi kubwa katika agenda za kiongozi mkuu. Wizi (wa viongozi na wafanyabiashara wa ndani na nje) ukashamiri kwa mgongo wa ubinafsishaji na uwekezaji. Wenye kuitetea nchi wakaonekana si mali kitu! Wengine hata uraia ukawa matatani. Siasa ndani ya CCM sasa ikawa biashara chafu. Fedha ni fedha, iwe ya dawa za kulevya, iwe ya rushwa nk haijalishi. Hapendwi mtu wala nchi hapa – ‘fweza tu!!'
Bunge nalo halikuachwa nyuma. Huko nyuma nililiita mchezo wa kuigiza. Nikafunguliwa mashitaka. Nikajitetea kwani sikubali kuwa kondoo. Niliamini nilichokisema. Narudia leo: ‘Bunge limegeuzwa kitanzi cha haki na sasa limekuwa kisagio cha kodi za wananchi na baraza la kuhalalisha ufisadi.' Wapinzani wanasema, lakini serikali sasa inatumia wingi wa wabunge wa CCM kuhalalisha uharamia. Watanzania "wanafaidi" matunda ya ushindi wa tsunami.
Sasa tuna awamu ya nne ya Jakaya Kikwete. Haina jipya. Itikadi hakuna. Sera mpya hakuna. Fikra mpya hakuna! Ni awamu mahiri kwenye mambo ya sanaa na mahusiano - mbwembwe, ndoa na vyombo vya habari, mashairi, sherehe, vibwagizo na kaulimbiu tamu tamu, ziara, ahadi, nk.
Nikiri, walikuwa makini katika kampeni! Walikuwa hawana "mswalie mtume" – kuanzia wenyewe kwa wenyewe hadi wapinzani. Umahiri wao wa sanaa ulionekana tangu hapa. Fikra zao ziliishia siku ya kuingia Ikulu. Wamefanikiwa! Watanzania bado wanajipa matumaini kuwa ari, kasi na nguvu mpya ni sera!! Ya wapi… Muda utahukumu.
Rais Kikwete kakiri, hana jipya na viatu vya Mkapa ni vikubwa kwake!! Ataendeleza yale yote mazuri ya Mkapa?! Hajatuambia mabaya ni yapi na atayafanyaje! Sasa tutegemee nini? Mkuu keshakata tamaa?
Chama kinachotuongoza kiko vipande vipande! Kinajua bila dola hakipo. Bila mikwara, hofu haitaendelezwa. Kimepata wapiga zumari wasioweza kueleza itikadi yao, kwani hawana. Wana agenda moja: NYONGA UPINZANI LAKINI USIUE. Ukiua, misaada ya kimataifa hakuna. Ukiua, kinga ya ndani ya ufisadi wao haipo! Hii ndiyo dhana ya upinzani kufanywa kinga ya ufisadi wa watawala!
Wote wako kwenye utando wa buibui, hawana jinsi, lazima walindane. Kinachowaunganisha hawa si itikadi, kwani haipo, ila ni kuwa kila mmoja ana kapu na yuko tayari kuvuna ndani ya "shamba la babu."
Tuonane wiki ijayo!
Source:
http://www.freemedia.co.tz/daima/2007/1/31/makala3.php