Mimi siku zote husimamia haki na daima huwa upande wa wanyonge dhidi ya maovu. Ila kamwe siwezi kuunga mkono uvamizi wa mgodi wa North Mara na kuwaita waliouwawa wanamapinduzi -- hapa tunachezea maana halisi ya wanamapinduzi.
Wote hapa hatujui nini haswa kilitokea, lakini based on police statements ni kuwa kundi la watu 800 mpaka 1,000 walivamia mgodi wa North Mara wakiwa na mapanga, marungu na silaha zingine za jadi wakawa wanataka kuiba gold ore kwa lengo la kwenda kuiuza na kujinufaisha wao wenyewe.
Sawa, wananchi wa Nyamongo wana manung'uniko yao ya muda mrefu kuhusu mwekezaji kupewa eneo hilo lakini kisheria Barrick ni mmiliki halali wa mgodi huo. Hivyo watu 8 au watu 800 wakiingia ndani ya mgodi huo kinyume cha sheria kwa lengo la kuiba mawe ya dhahabu watu hao ni wezi au wavamizi tu, kamwe si wanamapinduzi.
Ni kama wewe ukiwa na shamba lako lenye hati umeuziwa na serikali ya kijiji, umejenga ukuta na kuweka geti. Sasa wakaja wanakijiji 800 na kuvamia eneo hilo kwa lengo la kuiba ng'ombe wako utawaita hao wanakijiji wanamapinduzi au wezi? Ndiyo maana wengine wameweka vibao kwenye mashamba yao kuwa "Trespassers will be shot!"
Kama wanakijiji wa Nyamongo wana malalamiko kuhusu mgodi huo ni vyema CHADEMA na wanasiasa wengine wakawafundisha utaratibu mzuri zaidi wa kudai haki zao, si kuvamia na kuiba mawe ya dhahabu kwani Barrick watakuwa na haki ya kulinda mali zao.
Nadhani polisi walitumia excessive force kama wanavyofanya kila siku wanapouwa watuhumiwa wa ujambazi au wananchi wasio na silaha kwenye maandamano kama ya Arusha.
Hatuwezi kuunga mkono uvunjaji wa sheria hata kama wananchi hawa wana madai halali, pia serikali itaonekana ni ya kipuuzi mbele ya wawekezaji wa kimataifa kama itashindwa kulinda mali za wawekezaji kutoka kwa wavamizi.