KASHFA ya Richmond iliyomlazimisha aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa na mawaziri wengine wawili kujiuzulu na baadaye kuvunjika kwa Baraza la Mawaziri imeendelea kuchukua sura mpya kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele.
Ushahidi wa ukweli huu unathibitishwa na kuibuka kwa mambo mapya kila kukicha, kubwa kati ya hayo likiwa ni lile la jana usiku la Televisheni ya Taifa kukatisha ghafla mahojiano yale na Lowassa.
Tukio hilo la jana usiku lililokuja wakati usiotarajiwa linaweza likafungua ukurasa mpya wa kisiasa kwamba, viongozi wa juu serikalini huenda sasa wameanza kuhofia kwamba Lowassa anaweza akaibua masuala mengine yanayoweza kuhatarisha amani au kuimega serikali.
Aidha kukatwa kwa mahojiano hayo kunaweza kukafungua ukurasa mpya wa hoja kwamba, sasa ni wazi kuwa, Lowassa ameanza kutengwa waziwazi na viongozi wakuu serikalini ambao amefanya nao kazi kwa muda mrefu, kiasi kwamba hakuna aliye tayari kumuona mwanasiasa huyo akijaribu kujijenga upya kisiasa au kujisafisha kwa gharama za kufichua kila anachokijua kuhusu sakata la Richmond.
Hadi wakati TvT wakikatisha ghafla mahojiano hayo jana usiku, tayari Lowassa alikuwa ameshaeleza mambo mengi ambayo pia alikuwa ameyasema jana jioni wakati wa mkutano wake wa hadhara alioufanya nyumbani kwao Monduli alikokwenda kuwaleza wapigakura nini kilitokea bungeni hata akalazimika kujiuzulu.
Aidha, mbali ya hayo, wiki hii imeshuhudia kuanza kufunguka au kufichuliwa kwa masuala mengine mapya yanayozingira sakata hilo la Richmond ambalo mbali ya Lowassa, lilisababisha aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ibrahim Msabaha, kuondoka madarakani kutokana na majina yao kutajwa katika mzingo wa sakata zima la Richmond.
Katika hatua nyingine, kauli zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete na Sheikh Yahya Hussein kuhusu Richmond zimeanza kuzua mijadala huku baadhi ya wadadisi wa mambo wakiziona kuwa zilizo na ajenda mahususi za kuweka mambo sawa.
Wakati Kikwete akionekana kujaribu kunawa mikono dhidi ya lawama zinazoelekezwa kwake za kuwatelekeza marafiki zake wa siku nyingi, Lowassa na Rostam Aziz, wakishutumiwa vikali hata kutakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria, matamshi ya Sheikh Yahya yanaonekana kuchukua mwelekeo wa kuwa na ushawishi wenye malengo mahususi.
Wadadisi wengine wa mambo wanaiona kauli ya Kikwete aliyoitoa kwa wazee wa Dar es Salaam akimsafisha Lowassa kuwa ilitolewa na mkuu wa nchi ambaye alishindwa kusoma alama za nyakati ambazo zilikuwa zikimtaka kutoonyesha kufungamana na upande wowote katika masuala yanayohusu ufisadi.
Katika hatua ambayo huenda haikutarajiwa na baadhi ya watu, baada ya kimya cha siku kadhaa, Lowassa na Karamagi, wameanza kutoa kauli ambazo zinatoa mwelekeo wa kuanza kujibu mashambuli makali yanayoelekezwa kwao tangu Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe, ilipowasilisha ripoti yake ya uchunguzi kuhusu mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura kati ya Kampuni ya Richmond Development Company na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Wakati Lowassa akitoa kauli, kwanza kupitia katika mahojiano aliyofanya na Televisheni ya Taifa (TvT) yaliyorushwa jana usiku na pia katika mkutano wa kwanza wa hadhara alioufanya nyumbani kwao Monduli jana hiyo hiyo alasiri, Karamagi yeye ametoa kauli yake katika mahojiano ya ana kwa ana aliyofanya na gazeti hili.
Wakati hayo yakitokea, Karamagi naye katika mahojiano na gazeti hili wiki hii, alitangaza nia yake ya kupambana na watu aliodai kuwa walihusika kuchafua jina lake kwa kumhusisha katika kashfa ya Richmond.
Alisema hatakaa kimya dhidi ya tuhuma zilizoelekezwa kwake na wajumbe wa Kamati Teule ya Bunge, iliyochunguza mchakato wa upatikanaji wa zabuni ya uzalishaji umeme wa dharura ulioipa ushindi Richmond.
Akizungumza kwa kujiamini, Karamagi alisema hakubaliani moja kwa moja na ripoti ya kamati hiyo kwa sababu baadhi ya aya zilizomo katika ripoti, zinaonekana kuwekwa makusudi kwa ajili ya kumchafua, yeye pamoja na baadhi ya viongozi wenzake waliolazimika kujiuzuru nyadhifa zao baada ya kutajwa kuhusika na kashfa hiyo.
Baadhi ya maeneo katika ripoti hiyo sikubaliani nayo kabisa, yalipotosha hali halisi ilivyokuwa, yalilenga kunichafua na kunidhalilisha mbele ya jamii, mimi pamoja na wenzagu tuliojiuzuru.
Kamati ilisikiliza na kuruhusu maneno ya umbea kuingizwa katika ripoti, inaonekana wajumbe wa kamati walifurahia kuingiza umbea katika ripoti yao. Hili lilivuruga kabisa hata yale mazuri yaliyokuwa katika ripoti hiyo. Ni wazi yalichomekwa kwa ajili ya kutuchafua, alisema Karamagi.
Akizungumza kuhusu kutohusika na kashfa hiyo, alisema alihamishiwa Wizara ya Nishati na Madini Oktoba 19,2006 na alipoingia ofisi alikuta barua kutoka Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO iliyoandikwa Oktoba 13, 2006, siku sita kabla ya kuingia katika ofisi hiyo ikielezea hali halisi ya tatizo la umeme nchini na ilitoa ushauri wa nini kifanyike ili kukabiliana na hali hiyo.
Barua hiyo ambayo Tanzania Daima Jumapili iliiona, imesainiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurungezi wa TANESCO, Balozi Frugence Kazaula pia inaeleza kutambulika kwa utapeli uliokuwa ukitumiwa na kampuni ya Richmond kuihadaa serikali juu ya kuwasili kwa mitambo hiyo ya kufua umeme wa dharura.
Bodi ya Tanesco ilikuwa imeiandikia serikali ikieleza utapeli wa Richmond, hatua za kuchukua kukabiliana na tatizo la umeme na ilishauri kujiepusha na malumbano yoyote kwa wakati huo na kampuni hiyo kwa sababu yangeweza kuharibu mambo.
Mimi nilianza kuifanya kazi barua hiyo baada ya kushauriana na wenzangu na kuona tulikuwa na kila sababu ya kufanyia kazi mapendekezo yaliyokuwa katika barua hiyo. Sikuhusika na kusaini mkataba wa Richmond wala kushinikiza ipewe upendeleo wowote, nilikuta imeshachukuliwa na imeshangulika ni ya kitaperi.
Ajabu ninatajwa katika kamati kuwa nilishikiza Richmond au dada yake Dowans kuendelea na kazi.Inaumiza sana kuona mtu mzima anakuzulia jambo la ajabu namna hiyo, alisema Karamagi.
Karamagi ambaye mahojiano yake yamechapishwa ndani ya gazeti hili leo, alieleza kushangazwa na kitendo cha kamati hiyo kutotumia barua ya Bodi ya Tanesco iliyokuwa ikiishauri serikali cha kufanya katika kukabiliana na tatizo la umeme licha ya kuwasilisha barua hiyo kwa Spika wa Bunge Samuel Sitta, badala yake ilitumia barua ya Mwakilishi wa Net Group Solutions.
Hata hivyo alisema hata baada ya kutokea mambo hayo yeye binafasi hana tatizo na chama chake, Chama Cha Mapinduzi: Sina tatizo na CCM, nina tatizo na baadhi ya watu ambao wameamua kuacha kusema ukweli, wameamua kusema uongo kwa malengo na dhamira wanazozijua wao.
Hawa wataleta matatizo ndani ya CCM na hata katika serikali. Wamenichafua, hawakusema ukweli kuhusu mimi. Nitapamba, kuna vikao vyetu, nitasema ukweli kuhusu watu hawa. Nayasema haya ili Watanzania waelewe ukweli ulivyo. Si kwa sababu nataka kurudi katika uwaziri, alisema Karamagi.
Akizungumza kuhusu sababu za kampuni yake ya TICTS, inayohusika na kupakua kontena bandarini kuongezewa mkataba wa miaka 15 kabla ya ule kwanza kumalizika alisema muda uliongezwa kufuata taratibu.
Alisema kampuni yake iliomba kwa serikali kuongezewa muda huo baada ya kuonekana ulazima wa kupanua shughuli za bandari pamoja na kuongeza mtaji katika uwekezaji eneo hilo.
Alisema maombi hayo yalifanyiwa kazi na serikali likiwemo baraza la mawaziri ambalo baada ya kukubaliana na hali halisi liliielekeza Tume ya Kurekebisha Mashirika ya Umma, PSRC kushaurina na TICS namna ya kuongeza mkataba huo kwa ajili ya kuboresha shughuli za bandari.
Kuhusu kutajwa kwa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kuwa aliibeba TICS kuongeza mkabata huo wa miaka 15, alisema wakati kampuni hiyo ianongezewa muda hakuwa akifahamiana wala hakuwa na mahusiano ya aina yoyote na Mkapa.
Wakati Lowassa na Karamagi wakitoa kauli hizo za kujitetea kwa mara ya kwanza, wiki hii pia, mnajimu maarufu Sheikh Yahya Hussein alizungumzia kashfa hiyo ya Richmond akisema wahusika katika sakata hilo ndani ya serikali walikuwa ni wengi kuliko mawaziri watatu waliojiuzulu.
Katika hatua ambayo bado inaacha maswali mengi, Sheikh Yahya alisema alikuwa ana uhakika kuwa siku moja Lowassa atarejea katika madaraka ya kiserikali baada ya ukweli kamili kuhusu sakata hilo la Richmond kubainika.
Kauli hiyo ya Sheikh Yahya ilikuja siku chache tu baada ya Rais Kikwete kuwahutubia wazee wa Dar es Salaam na kueleza namna alivyoguswa, kushtushwa na tukio la kujiuzulu kwa Lowassa na kutajwa kwa watu wengine kadhaa ambao alisema amekuwa na uhusiano nao wa kijamaa na kikazi kwa miaka mingi.