Ubaguzi kwa walioambukizwa ndio chanzo cha woga
WOTE tumesikia juu ya kampeni ya kitaifa ya kupima UKIMWI, ambayo, chini ya uongozi wa Jemadari Mkuu katika vita hii ya kitaifa, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilianza rasmi mnamo Julai 15, mwaka huu.
Ndio. Kampeni inaanza rasmi siku hiyo huku kukiwa na dalili zote za kutofanikiwa kwa kampeni hiyo, kutokana na sababu nyingi ambazo tayari zimeanza kujidhihirisha. Ninafahamu dhahiri kwamba Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Kampeni hiyo imesheheni wataalam waliobobea kwenye fani zao, wakiwa madaktari na wataalam mbali mbali. Ninafahamu dhahiri kwamba wataalam hao wameteuliwa kushika nafasi zao muhimu kwenye kamati hiyo kutokana na umahiri wao katika utekelezaji wa kazi zako, hususan katika kufanikisha kampeni hiyo. Hata hivyo, wataalam hao wataniwia radhi kwa kusema kwamba, hata kabla ya kuanza rasmi kampeni hiyo, tayari wamekwishashindwa kutekeleza wajibu wao katika kufanikisha kampeni hii.
Labda nitaonekana mwenye kibri au mwenye dharau, kwa kusema kwamba wataalam bingwa wameshindwa kufanikisha Kampeni ya Kitaifa ya Kupima Virusi vya UKIMWI, hata habla ya kuanza rasmi kwa kampeni hiyo. Je, mimi nina uwezo mkubwa zaidi yao? La hasha. Hata hivyo, ninakiri kwamba mimi si mtaalam wa afya wala sijawahi kuingia kwenye darasa linalofundisha mambo yanayohusiana na UKIMWI. Sijawahi kuchukua mafunzo yoyote juu ya ushauri nasaha kwa watu wanaotaka kupima afya zao, hususan kubaini kama wameambukizwa Virusi vya UKIMWI (VVU). Lakini, kama mtaalam wa sekta ya habari na mawasiliano, ninaweza kabisa kukuhakikishia wewe msomaji kwamba, vita dhidi ya janga hili la kitaifa tayari imekwama, kutokana na sababu zifuatazo.
Mosi: Elimu ambayo ilitakiwa kutolewa kwa wananchi, kubainisha UKIMWI ni nini, kisayansi, haijawahi kutolewa hata siku moja. Kumekuwa na mkazo wa kuupiga vita UKIMWI lakini bila ya kuwaelimisha watu kwa ufasaha wanaupiga vita kwa sababu gani. Asilimia kubwa ya ujumbe ambao umeenezwa kwa wananchi ni kwamba kiwango kikubwa cha maambukizo ya VVU hupatikana kwa njia ya kujamiiana, hivyo, watu wanapaswa kutumia kinga wakati wote wa kujamiiana. Haikuwahi kutolewa elimu kuwaeleza wananchi UKIMWI ni nini, jinsi mtu anavyoweza kuambukizwa, VVU vikoje, na kadhalika. Hakukuwahi kuwapo na mpango wa kisayansi wa kuwaelimisha wananchi kwa ufasaha, UKIMWI ni nini. Kama kungekuwapo na mpango wa kisayanzi wa kuwaelimisha wananchi kwa ufasaha UKIMWI ni nini na namna ya kuupiga vita, tusingelazimika kuendesha kampeni ya kitaifa ya kupima VVU, kwani, watu wangekuwa wakimiminika wenyewe kwenye vituo vya ushauri nasaha na kupima endapo wameambukizwa VVU kwa hiari yao wenyewe! Kama elimu hiyo ingekuwepo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania asingelazimika kuwa Mhamasishaji Mkuu wa kampeni hii. Kama... lakini elimu hiyo haikuwepo, haijakuwepo, na nina uhakika kwamba asilimia kubwa ya wajumbe waliopo kwenye kamati hiyo walikuwa na majukumu ya kutayarisha na kutekeleza mikakati ya elimu hiyo, kitaifa, jambo ambalo halikufanyika. Mpango huo, kwa uwajibikaji, ulikuwa chini ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (NACP), lakini haukutekelezwa. Mpango wa Elimu ya UKIMWI kwa Umma (National Public AIDS Awareness Educational Campaign) haukuandaliwa wala kutekelezwa. NACP walikuwa wapi?
Pili: Vita ambayo imekuwa ikipiganiwa juu ya UKIMWI imekuwa kujikinga na UKIMWI, sio kuwaelimisha wananchi ambao ndio askari muhimu katika vita hii kali kwamba unapoambukizwa VVU sio mwisho wa maisha yako. Kumekuwa na matukio mbali mbali ya kuwabagua, kuwanyanyasa na kuwatenga watu ambao wameambukizwa VVU, kiasi kwamba hofu kubwa imetanda miongoni mwetu. Watu wameshuhudia wanaobisha wamwulize Dk. Sebastian Ndege, anayeendesha kipindi cha redio cha Njia Panda kwenye kituo binafsi cha redio cha Clouds FM jinsi ambavyo watu walioambukizwa VVU wamekuwa wakitengwa, hata na ndugu zao! Watu wameshuhudia jinsi wazazi walivyowatenga vijana wao, wake kwa waume, kwa kosa la kuambukizwa VVU. Watu wameshuhudia jinsi ambavyo jamii imewatenga na kuwazika wakiwa hai watu ambao wameambukizwa VVU, kiasi ambacho hofu kubwa imejengeka miongoni mwetu. Hofu hii imesababisha watu kuogopa, ama kwenda kupima VVU kwa kuhofia kupata majibu mabaya, au kujitangaza pale ambapo wanapobaini kuambukizwa VVU, kwa kuhofia kutengwa na kuhesabiwa kuwa wamekufa, huku, pengine, bado wangeweza kuwa na maisha mazuri, ya kawaida, kwa miaka kadhaa. Hofu hii imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza kiwango cha maambukizi kutokana na kwamba, watu ambao tayari wameambukizwa na hawajui kama wameambukizwa wamekuwa wakiendelea kujamiiana na watu wengine ambao hawajaambukizwa, bila kupima afya zao. Watu hawa wamekataa kupima kutokana na woga, woga wa kutengwa, kunyanyaswa na kubaguliwa na wenzao katika jamii.
Tatu: Pengine, itastaajabisha, jambo ambalo limewekewa mkazo mkubwa zaidi, yaani, matumizi ya kinga kondomu dhidi ya UKIMWI, nalo pia limekumbwa na utata. Tumekuwa tukipata ripoti kadhaa juu ya kukosekana kwa silaha hizi muhimu, kiasi kwamba kuna sehemu kadhaa ambapo watu wamekuwa wakiwakodisha watu wanaotaka kujamiiana silaha hizi ambazo tayari zimekwishatumika, na hazifai kutumika tena, ili kwenda kuzitumia katika kupambana na UKIMWI. Inaweza kuonekana kama mzaha, lakini, kuna baadhi ya vijiji ambavyo viko mbali, havifikiwi mara kwa mara na watendaji husika, jambo ambalo limewafanya wananchi wanaoishi kwenye maeneo hayo kujihisi kwamba, labda, vita hiyo haiwagusi wao, na wala wao hawahusiki na vita hiyo. Huu sio mwelekeo sahihi. Ni ajabu, lakini hata baada ya vyombo vya habari kueleza kwa kina tatizo hili la uhaba mkubwa wa silaha za kupambana na UKIMWI, yaani kondomu, kwenye maeneo hayo ambayo hayafikiwi kwa haraka kwa sababu ya kutokuwapo miundombinu sahihi kama vile barabara, vyombo vilivyopewa dhamana ya kupigana vita hii vimelipuuzia tatizo hili. Wananchi wanaoishi sehemu hizo wameendelea kutumia vifanyio kwa kukodishana, jambo ambalo ni dhahiri limechangia kasi ya maambukizi mapya ya VVU.
Jambo lingine ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa Watanzania kupata maambukizo ya VVU kwa kiwango kikubwa ni dhana potofu juu ya UKIMWI. Leo hii, UKIMWI unaonekana kuwa ni malipo ya dhambi ya zinaa. Kwa kiwango kikubwa, Watanzania wanauchukulia UKIMWI kwamba ni malipo kwa watu wanaofanya zinaa, huku wakisahau kwamba, mosi, kuna vijana wadogo kabisa wanaosoma shule za msingi, sekondari na haya kwenye vyuo vya juu, ambao wameambukizwa VVU tokea wakiwa tumboni mwa mama zao. Wapo pia walioambukizwa wakati wakinyonyeshwa maziwa na mama zao. Je, na hao pia walifanya zinaa, kwa hiyo wanastahili adhabu hiyo? Je, na wale ambao waliambulikizwa VVU kwa kuchomwa sindano ambazo hazikuwa safi, kwenye zahanati za mitaani ambazo hazizingatii kanuni bora za afya? Je, na hao pia wana dhambi, ndio wastahili adhabu hiyo?
Mtazamo huo potofu, wa kuufanya UKIMWI kuwa ugonjwa wa ajabu na wa kuogopwa, na wa kumhukumu kila ambaye ameambukizwa VVU kuwa mhalifu ni jambo ambalo limechangia, kwa kiwango kikubwa sana, kwa watu kuendelea na hamsini zao bila kujali kwenda kupima kama wameambukizwa, na wale ambao wameambukizwa kuendelea na vitendo vya ngono bila kutumia kinga, hivyo kuendelea kuwaambukiza watu wengine bila ya wao wenyewe kujua.
Pia, kuna watu ambao wanafahamika kwa ushahidi wa mazingira kwamba wameambukizwa VVU, lakini kutokana na utajiri wao, haswa kwa wanaume, wamekuwa wakibadilisha wanawake kama wanavyobadilisha mashati yao. Watu hawa, tena kwa makusudi kabisa, wamekuwa wakitumia visu vyao kutembea na wasichana wadogo wadogo, na kuwaambukiza VVU, kwa kuwapa zawadi zenye thamani kubwa pamoja na kuwastarehesha. Kuna waliodiriki hata kuwachukua wasichana hao wadogo wadogo na kwenda kustarehe nao nchi za nje, kisha kuwazawadia vitu vya thamani kubwa, kama vile magari madogo aina ya baloon, au simu za mkononi zenye thamani kubwa. Kutokana na tamaa zao, wasichana wadogo wamekuwa wakibabaika kila wanapowaona wenzao wakipewa zawadi hizo, hivyo kujirahisisha kwa wazito hao, wakisababisha kukua kwa mtandao wa maambukizi mapya ya VVU.
Sasa mtaniuliza: Nini kifanyike?
Wote tunajua kwamba, unapokwenda vitani, lazima kwanza ufanye utafiti kumjua kwa undani adui yako. Lazima umjue yeye ni nani, marafiki au washirika wake ni nani, anaishi wapi, ana fikra gani, mbinu zake za kivita ni zipi, ikiwezekana, ujue kila anachofanya kwa muda wote, ili kuweza kujua ni wakati upi utakaokuwa sahihi kumvamia na kumpiga bila ya yeye kuweza kujipanga. Hizi ni mbinu za kijeshi ambazo hufanywa na wanajeshi wote duniani, kabla ya kwenda vitani. Kumchunguza adui yako uweze kufahamu udhaifu wake.
Tumeingia kwenye vita dhidi ya adui UKIMWI bila kumjua kwa undani adui yetu. Hatujamchunguza, yeye ni nani, marafiki au washirika wake ni nani, anaishi wapi, ana fikra gani, mbinu zake za kivita ni zipi, na hatujajua ni wakati gani muafaka wa kumshambulia ili asiweze kujipanga na kujibu mashambulizi yetu. Tumekwenda kumpiga vita adui UKIMWI bila ya kuwa na dira, bila ya kuwa na mpango, tumepoteza muda mwingi na fedha nyingi, huku askari wetu wengi wakiteketezwa na adui huyu. Bado tunataka kuendelea na vita hii?
Mimi ninawasifu sana watu wa Uganda, kwani, wakati UKIMWI ulipogunduliwa, vijana wengi sana wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo walipukutika kama majani, kwa vifo vilivyosababishwa na UKIMWI. Vilio vilitanda kila kona ya nchi ya Uganda, sio mijini pekee bali hata vijijini.
Wananchi wa Uganda wakashtuka, wakasema: Hapana! Tutajipanga upya!
Mikakati ya kuwafundisha wananchi, kuanzia ngazi ya kijiji, kuufahamu UKIMWI, kwa undani wake, ilifanyika. Watu wakafahamu UKIMWI ni nini, wakabadilika kitabia na kifikra. Wakaacha kuwabagua, kuwanyanyasa na kuwatenga watu wengine walioambukizwa UKIMWI. UKIMWI ukaonekana kuwa ugonjwa wa kawaida tu!
Hilo ndilo jambo la msingi kuufanya UKIMWI uonekane kuwa ugonjwa wa kawaida tu! Hapo, ubaguzi uliisha, kutengwa kukakoma, na hakukuwa na vitendo vya kuwanyanyasa watu walioambukizwa UKIMWI. Kila mtu aliendelea na shughuli zake za kawaida, lakini kwa makini zaidi. Watu walikwenda kupima UKIMWI kila mara, bila ya kuwa na hofu wala woga, wakijua kwamba, kama walikuwa wameambukizwa, wangeendelea kuishi bila matatizo yoyote. Hali ilikuwa shwari. Ukichunguza takwimu za maambukizi ya UKIMWI nchini Uganda leo, katika nchi zote za Afrika Mashariki, Uganda ina maambukizi mapya machache kuliko nchi zote za Afrika Mashariki. Uganda imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kwenye vita dhidi ya UKIMWI.
Tujiulize. Kinachotutofautisha sisi, Watanzania, na wenzetu, majirani zetu, Waganda, ni kipi? Kwa nini wao waweze kufanikiwa kwa kiwango kikubwa huku sisi tukiwa watazamaji? Kwa nini sisi hatutaki kubadilika?
Tunaweza kubadilika, na tunaweza kufanikiwa, iwapo tutaweka mikakati thabiti, ya, kwanza, kuyajua yote ambayo tunapaswa kuyajua juu ya UKIMWI.
Tunao madaktari, ambao wanaweza kushirikiana na wataalamu wa sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEKNOHAMA), kutayarisha makala kwenye magazeti na majarida, pamoja na vipindi maalum ambavyo vitaoneshwa kwenye luninga au kutangazwa kwenye redio. Vyombo vya habari vina nafasi kubwa na muhimu ya kutoa mchango wa elimu katika vita dhidi ya UKIMWI, kupitia majarida na magazeti, vipeperushi, mabango, luninga, redio, na pia, wasanii wa fani mbali mbali, kama vile fasihi simulizi na fasihi maandishi. Kwenye fasihi simulizi kuna tamthilia (maigizo, nyimbo, ngoma za jadi, n.k.) wakati kwenye fasihi maandishi kuna viandiko (majarida, magazeti, vitabu, mabango, vipeperushi, n.k.). Kama ikibidi, wasanii wa maigizo kwenye luninga walipwe chini ya mpango maalum wa dharura ili waweze kutunga michezo ya kuingiza itakayowaelimisha watu juu ya UKIMWI, namna ambavyo mtu anaweza kuambukizwa VVU, jinsi ambavyo mtu anaweza kujikinga dhidi ya maambukizo, na kadhalika. Mchango wa vyombo vya habari tayari umeonekana, kwa mfano, mpango wa kitaifa ambao umekuwa endelevu, katika kuelimisha na kuchangia vita dhidi ya saratani inayowaathiri wanawake (kwa uwingi wao) na hata wanaume (kwa uchache wao). Mchango mkubwa ambao umekuwa ukitolewa kwa Chama cha Madaktari Wanawake wa Tanzania (MEWATA) usingefanikiwa kama vyombo vya habari visingeshirikishwa kwenye kampeni hiyo. Kampeni kama hiyo inaweza pia kufanikiwa, katika vita dhidi ya UKIMWI, kama vyombo vya habari vingeshirikishwa ipasavyo. ITV na MEWATA wameonesha njia, TACAIDS na NACP wameiona?
Wengi wetu hatujui A wala B kuhusu UKIMWI. Binafsi, ukiniuliza kuna aina ngapi ya VVU sitaweza kukujibu. Nenda sehemu yoyote ya Uganda leo, waulize watoto wadogo, watakutajia aina zote za VVU. Ala? Hivi kuna zaidi ya aina moja ya VVU? Mlikuwa hamjui?
Wataalam wa teknolojia ya habari na mawasiliano wako tayari kuandaa vipindi maalum ambavyo vitawaelimisha wananchi kupitia luninga na redio, kinagaubaga, ili waweze kuujua UKIMWI. Wasanii wataweza kuandaa michoro, kutokana na maelezo ya madaktari na wataalam wa afya, ili kuweza kuonesha mifano ya maumbile ya VVU. Katika kuelezea UKIMWI, kupitia mbinu za kisayansi, tutaweza kuujua UKIMWI na tutaweza kuubomoa.
Hakuna elimu ya kutosha kwa sasa juu ya UKIMWI. Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI, katika miaka yake yote tokea ulipoanzishwa, haujaandaa kipindi hata kimoja, ambacho kingerushwa kwenye luninga au kutangazwa kwenye redio, kuwaelimisha wananchi kisayansi, UKIMWI ni nini. Ninakumbuka, mwanzoni kabisa, mabango yaliyokuwa yakielimisha wananchi juu ya UKIMWI yalikuwa na michoro ya watu waliokondeana, wakionekana dhahiri kuwa na afya mbaya. Jambo hili liliwatisha watu wengi, ikaonekana ni makosa. Lakini ile dhana kwamba ukiambukizwa UKIMWI ndio mwisho wa maisha yako, kwa kusema UKIMWI UNAUA ilikuwa tayari imejengeka. Bado, kuna maandishi kadhaa kwenye machapisho mbali mbali, yanayosema UKIMWI NI HATARI. UNAUA. JIHADHARI NA UKIMWI! Machapisho haya yanawatisha watu, yanaogopesha, yanakwamisha vita dhidi ya UKIMWI!
Kwa mtazamo wangu, lazima tukubali kwamba tulifanya makosa, na sasa bado tuna nafasi ya kujirekebisha. Sisemi kwamba tuurembe UKIMWI kwa kuufanya uonekane kwamba sio hatari. La hasha. Tuwe na mtazamo kwamba unapoambukizwa sio mwisho wa safari ya maisha yako. Watu wanaoishi na VVU wana nafasi kubwa katika vita hii, kwani wao ni mfano tosha kwamba unaweza kuwa umeambukizwa lakini ukaendelea kuishi maisha ya kawaida. Wao ndio walimu wetu katika vita hii, tuwape nafasi ya kutuelimisha. Hata hivyo, licha ya kukubali kwamba kuambukizwa UKIMWI sio mwisho wa maisha, hakuna maana kwamba tuache kujikinga na kuwa makini wakati wote. La hasha. Tunatakiwa tuongeze bidii katika vita hii.
Ninampongeza Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa kusimama kidete na kuwashauri wananchi kwenda kupima UKIMWI. Nimewahi kupima UKIMWI na nitapima tena siku hiyo. Nitayakubali matokeo yoyote yale. Kwani kuambukizwa UKIMWI sio mwisho wa maisha yangu.
Lakini tukumbuke: Je, tumejipanga vizuri katika vita hii kubwa kuliko zote?
Mungu Ibariki Tanzania.
Mungu Ibariki Afrika.
Naomba kutoa hoja.