Zitto azua jambo bungeni
Basil Msongo, Dodoma
Daily News; Tuesday,July 01, 2008 @00:04
MBUNGE wa Muleba Kusini, Wilson Masilingi (CCM), ametaka ufanyike uchunguzi kuhusu kauli za Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema) kuwa viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) hawaelewani, na kwamba fomu za mali za viongozi zilizopo kwa Spika wa Bunge zinatofautiana na zilizopo katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Amesema ikithibitika ni uongo, Mbunge huyo aombe radhi. Masilingi alisema kauli ya Kabwe kuhusu Takukuru lazima itolewe maelezo na akahoji Kabwe amefahamu vipi kuwa kuna mgawanyiko mkubwa na mgongano baina ya wafanyakazi wa taasisi hiyo wakati hafanyi kazi huko.
Masilingi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, alisema anaamini Kabwe ana uhakika na aliyoyasema na kwa kuwa hafanyi kazi Takukuru lazima wafanyakazi wa taasisi hiyo wamemueleza hayo. Alisema lazima pia uchunguzi ufanywe kufahamu Kabwe amefahamu vipi kuwa kuna fomu za mali za viongozi wa umma zilizopo katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambazo zinachezewa na ni tofauti na zilizopo katika Ofisi ya Spika wa Bunge.
Masilingi aliyasema hayo baada ya Kabwe kumaliza kuchangia hoja ya makadirio ya matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa mwaka wa fedha 2008/2009 iliwasilishwa jana bungeni mjini Dodoma. Kabwe alisema taarifa za mali za viongozi wa umma zinachezewa katika sekretarieti hiyo na hivyo suala hilo lichunguzwe pamoja na kuchunguza tofauti ya fomu zilizopo huko na zile alizonazo Spika wa Bunge.
Siri zetu zote, mali zetu zote, madeni yetu yote zinafahamika.... alisema Kabwe na pia akawaeleza wabunge kuwa kuna umuhimu wa kuiangalia upya Takukuru kwa kuwa kuna matatizo makubwa ndani ya taasisi hiyo. Kwa mujibu wa Mbunge huyo, viongozi wa taasisi hiyo hawaelewani na watumishi wa chini, kuna Kamati ya kuwawinda wanaoisema Takukuru na kwamba mgawanyiko huo unasababisha Takukuru ishindwe kushughulikia kesi za ufisadi.
Pia alisema Bunge linapaswa kupitia upya sera na Sheria ya Usalama wa Taifa kwa kuwa hivi sasa Idara hiyo hairuhusiwi kuchukua hatua, inatoa ushauri tu. Pesa za EPA ziliibwa kwa cash, Idara ya Usalama wa Taifa ilikuwa inafahamu, alisema Kabwe na kusema kuwa Meremeta haihusiani na Usalama wa Taifa hivyo serikali kupitia Bunge lazima iwaeleze ukweli Watanzania akidai kuwa Meremeta ni wizi wa waziwazi.
Masilingi alisema anavyofahamu hakuna tofauti ya rushwa kubwa na rushwa ndogo, anafahamu kuna watu wanaoichukia Takukuru na isipokuwapo taifa litaangamia. Alisema watu wanawatuhumu wenzao kuwa ni mafisadi nao wachunguzwe wasije wakasakwa wanaotuhumiwa kumbe wengine wapo, na akasema kuna mafisadi na vifisadi.
Mimi sichukii mtu akisema fisadi fisadi, tusije tukasema fisadi fisadi tukawapita mafisadi, alisema Masilingi na kuitaka Takukuru ichunguze kwa makini kabla ya kuwakamata watuhumiwa. Alisema watumishi wa umma wanapaswa kujiamini, wasiogope kujenga maghorofa au kununua magari ya kifahari kwa sababu ya hofu ya kuitwa mafisadi.
Msemaji wa Kambi ya Upinzani katika wizara hiyo, Grace Kiwelu alisema wananchi wengi hawaamini kuwa Takukuru ni chombo cha kupambana na rushwa, bali taasisi ya kulinda mafisadi.
Kambi ya upinzani inaitaka serikali ianzishe mchakato wa kuichunguza Takukuru yenyewe kwa lengo la kujisafisha, kuona kama yenyewe ni safi, jambo ambalo kimsingi linaashiria kuwa haiko safi ndiyo maana inashindwa kuchukua hatua kwa watuhumiwa mbalimbali, alisema.
Mbunge wa Kibaha Mjini, Dk. Zainab Gama (CCM), alisema inapaswa kufuatilia taarifa za rushwa serikalini, mahakamani na kwamba hata kama zinawahusu wabunge wachunguzwe. Dk. Gama alisema kuna umuhimu wa kuwa na kamati ya Bunge inayoshughulikia rushwa kama ilivyo kwa Kamati ya Bunge ya Ukimwi, na pia Takukuru wawe wanatoa taarifa bungeni kuhusu utendaji wao.