Rais Kikwete ahadi za kuitafuta Tanganyika zimefia wapi?
Deogratius Temba
"MUUNGANO una kasoro zake, nilisema tutazimaliza, sikusudii kuunda tume ya kushughulikia kwa sababu kamati zilizowahi kuundwa zimebainisha kasoro za Muungano na namna ya kuzitatua." Hii ni kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Kila mmoja anayefuatilia kwa makini suala la Muungano huu ulioasisiwa Aprili 26, 1964, ataungana na Rais Kikwete kuwa Muungano una kasoro, unaumwa, tena upo taabani.
Ni vizuri kiongozi wa juu anapokiri waziwazi kuwa kuna tatizo na kutaka kuonyesha nia ya kulitatua. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kutamka maneno haya: "Mficha madhara kilio kitamuumbua", hatuna haja ya kukanusha ukweli kama mtu anaumwa tuseme ukweli ili atafutiwe dawa.
Kwa muda wote huo na kwa sababu ya tabia ya kuficha maradhi kwa kigezo, kwani dhambi kuulizia masuala ya Muungano, tunakuwa tukijaribu kutibu tu dalili za maradhi ya muungano badala ya kutafuta chanzo chake.
Si mara moja kumeibuka mifarakano mingi kati ya serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuhusiana na mambo mbalimbali yakiwemo upatikanaji wa mafuta.
Muungano ulianza kukumbwa na misukosuko tangu siku za kwanza ya uhai wake. Tangu wakati huo awamu nne za utawala zimepita na baadhi ya kero ni zile zile kwa miaka 45. Hakuna aliyeweza kuzimaliza lakini napenda kusema kwamba naamini Rais Kikwete atapambana nayo tu.
Waasisi wa Muungano huo, Mwalimu Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume walisimamia Muungano na wakati mwingine ulianza kutetereka na kufikia mahali kutaka kuomba nguvu kutoka nje ya kwa ajili ya kuulinda.
Changamoto nyingi zimewakumba, malalamiko kuhusu kuwapo kwa Muungano huu yanazidi kukua kila siku, inawezekana ilikuwa kosa kuanzishwa kwake lakini pia kuuvunja ni kosa kubwa.
Kuna swali ambalo limejaa vichwani mwa wasomi na wanazuoni, leo wanajiuliza hivi, mawazo ya kuungana yalikuwa ya Mwalimu Nyerere au Sheikh Karume? Na kama yalikuwa ya kwao wenyewe, kwa nini walishindwa kuweka misingi imara ya kuulinda na kuwaweka baadhi ya nyaraka za msingi hadharani ambazo zingeweza kudhibiti mawazo ya baadhi ya watu wanaoupinga?
Ikumbukwe kuwa mwaka huu sherehe za Muungano zimeangukia Jumapili na Muungano huu huu uliasisiwa Jumapili 26, Aprili, 1964, na hicho kilikuwa kipindi cha siku 104, tangu Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.
Siku chache baada ya Muungano, Sheikh Karume alikaririwa na gazeti la Nationalist la Tanganyika akisema: "Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar utatufaidisha sote hautakuwa kikwazo kwa watu wa Zanzibar."
Binafsi nimekuwa nikijiuliza ni kitu gani kilichomsukuma Karume kutamka maneno hayo? ina maana alianza kuhisi kuwa Muungano kamwe hauwezi kuwafurahisha watu wa Zanzibar, licha ya kwamba Watanganyika hawana haja nao.
"Neno hautakuwa na kikwazo kwa watu wa Zanzibar lina maana kubwa linapokuja suala la Uzanzibari na Utanganyika ambao Mwalimu Nyerere aliukataa, lakini mzimu wake ndiyo hivi sa sa unautafuna muungano huu hadi leo.
Tumeona tayari dalili zinaonyesha kuwa kero za Muungano na kasoro zipo Zanzibar tu Watanganyika wamelala fofo, wanasema muungano uwepo usiwepo wao wanasonga mbele.
Kero ya kwanza ilitokea siku chache tu baada ya kuundwa kwake, Jamatatu, Aprili 27, 1964, MwalimuNyerere alitangaza Baraza la Mawaziri alitoa viti vitano kwenda Zanzibar kutoka kwenye baraza hilo.
Hali ilianza kuonekana siku chache na kisha kukatokea mgogoro wa Zanzibar na Tanganyika kuhusiana na suala la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani (GDR), ambapo Zanzibar ilitangaza kuitambua na kutoa utambulisho wake wa kibalozi, wakati Tangayika ilikataa kuitambua, ikawa inaitambua Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani Mashariki.
Jumanne, Mei 4, 1964 ikiwa ni siku nane tu baada ya Muungano na baada ya kuundwa kwa Baraza la Mawaziri, walikaa na kujadili juu ya suala la kuitambua Ujerumani, hawakuelewana ipasavyo, Muungno ukaendelea kutikisika, waasisi wakazidi kutafuta msaada wa nje kuumaliza hasa mataifa ya Marekani na Uingereza ambayo wanadaiwa kuwa ndiyo waliochochea nchi hizi kuungana.
Juni 12, 1964, balozi wa Uingereza Tanzania wakati huo, Wiliam Leonhart, alituma ujumbe kwenda Marekani ukisema anaomba Serikali ya huko imwombe aliyekuwa Rais wa Kenya, mzee Jomo Kenyatta, atumike katika kuimarisha Muungano.
Mdahalo wa kwanza juu mfumo na muudo wa Muungano ulianza kwa njia ya maoni juu ya katiba ya Jamhuri ya Muungano mwaka 1983/84, hapo ilibainika kwa mara ya kwanza viongozi wa juu wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiongozwa na Rais Aboud Jumbe na wale wa serikali ya Muungano wakiongozwa na Mwalimu Nyerere walikuwa na mitazamo tofauti juu ya Muungano huo.
Jumbe na timu yake walitaka Muungano uwe na serikali tatu kwa maana ya serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar iliyopo sasa, na serikali ya Muungano itakayokuwa ikishughulikia mambo ya Muungano tu.
Kutokana na ukorofi na mambo mengine, Sheikh Jumbe alilazimishwa kujiuzulu nafasi zote za uongozi wa nchi kuanzia urais, umakamu wa Rais wa Muungano na nafasi zote za kichama Januari 1984.
Baada ya Sheikh Jumbe kuondoka, hali haikutulia. Kuliibuka tena mambo mengine mapya wakati kundi la wabunge 55 maarufu kama G55, walipojitokeza na kwasilisha bungeni waraka wa kutaka kurejeshwa kwa serikali ya Muungano mwaka 1993.
Ni kweli kuwa Bunge lilikuwa limeshapitisha azimio la pamoja la kuanzishwa kwa serikali ya Tanganyika, Agosti 24, 1993 kwa maana kuwa kuwapo na serikai tatu kama alivyotaka Jumbe mwaka 1983.
Lakini Mwalimu Nyerere akaona kuna hatari ya Muungano kuishilia mbali kama atanyamaza. Aliamua kujitoa mhanga kupambana na kundi hilo hadi kulishinda. Hali hiyo ilisababisha aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, John Malecela, na Katibu Mkuu wa CCM, Horace Kolimba kupoteza nyadhifa zao kwa kile kilichoelezwa kuwa walinyamazia makundi hayo hadi kuingia bungeni.
Leo hii tunapoadhimisha miaka 45, ya Muungano huo, mgogoro kama huo unaonekana katika suala la Zanzibar kutaka kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC) wakati Tanzania haitaki kujiunga nayo. Zanzibar imeanzisha Mahakama ya Kadhi lakini Tanganyika haikuwa tayari kuwa na mahakama hiyo, hizo ni tofauti za kimuungano.
Tumeona jinsi ambavyo hata waasisi walivyoshindwa kuuimarisha ipasavyo Muungano, hebu tujaribu kujiuliza kwa nini Mwalimu Nyerere kila mara alisema ni dhambi kubwa kuuvunja Muungno?
Kwa nini alitumia hata maneno ya kukatisha tamaa ya kusema kuwa ulevi wa madaraka na ujinga wa watu wachache unatawafanya watake kuuvunja Muungano? Aliona hayo tangu awali ikabidi atumie saikolojia ya vitisho.
Mwalimu ameshuhudia makundi kadhaa ya Wazanzibari na Watanganyika kutotaka kuutambua Muungano na kudai kurejeshwa kwa serikali ya Tanganyika.
Tumeona kutokana na magonjwa ya Muungano kutokutibiwa, magonjwa mengine yamekuwa yakiongezeka nakuna kundi limeibuka linataka kusherehekea siku ya Uhuru wa Zanzibar.
Hapo ndipo penye swali, kwa nini Wazanzibari wa leo wanagawanyika? Kwa nini hawataki kabisa kusikia mapinduzi na Muungano?
Hivi karibuni kumeitokeza kundi la wazee kutoka Pemba wakitaka kujitenga yaani Pemba ijitenge ni kisiwa cha Unguja, maana yake kujitenga huo kutaifanya Pemba kutambulika kama nchi au Jamhuri, na wangefanikiwa wangepaswa kutanga uhuru wa visiwa hivyo siku hiyo, wazee hao wamemwandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon, kueleza kilio chao.
Kwa bahati nzuri walipotaka kufanya maandamnao Februari wakati Ban akiwa nchini kuelekea katika ofisi za UN kudai haki hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Muhammed Seif Khatib, akafanikiwa kuwanyamazisha, lakini ieleweke kuwa kunapaswa kutafutwe dawa ya tatizo na si kuwanyamazisha.
Kama anavyosema Rais Kikwete, ambaye anamalizia miaka mitano ya utawala wake, akiwa bado hajaweza kutafauta dawa ya kuutibu Muungano, tunaingia kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, tukiwa na majeraha ya muungano hakuna suluhisho la matatizo.
Migogoro ya kupinga matokeo ya uchaguzi ni matokeo ya kutokutaka kutibu magonjwa ya Muungano, hayo ni moja ya magonjwa yanayouandama Muungano, tyunaelekea kutibu dalili na kuacha kuangalia chanzo cha ugonjwa.
Matumizi mabaya ya dola visiwani humo ni tatizo na ni kero mojawapo ya Muungano, huwezi kuongoza watu kwa kuwashambulia kila wanapopiga kura, wakimaliza unawaacha, haya ndiyo yanayowaumiza Wapemba.
Ni dhahiri kuwa muungano hauna shida kwa Wapemba kama wakipewa haki ya kufanya uchaguzi na kuchagua viongozi wao kwa uangalifu na umakini na wakamweka mtu wanayempenda madarakani, bila serikali ya Muungano kuingilia kati, au kupeleka jeshi la kupambana na raia.
Kero ya kudai kuwa mambo 11 ya Muungano hayako wazi, suala la mafuta, suala la Khatib kutaka kuwa rais si la kusababisha Muungano kuvunjika, kama viongozi wetu watakaa pamoja na kuangalia masuala ya msingi hasa ya Wapemba na kuwajali, kama watu wasio waasi.
Ni kweli kuwa huu ni Muungno wa kihistoria. Hakuna nchi au mataifa yaliyowahi kuungana na yakawa na muungano wa kudumu mzuri kama huu, lakini huu ni mzuri kwa nje lakini ukiingia ndani umejaa magonjwa zaidi ya 22.
Rais Kikwete ahadi zake na kundi lake la G55 za kuitafuta Tanganyika zimeishia wapi?