na haya ndiyo aliyoandika salva. Je, nyie wa san Francisco, haya ndiyo mliyomuuliza rais?
Na Mwandishi Maalum, San Francisco, California, Marekani
Baadhi ya Watanzania wanaoishi mjini San Francisco, Jimbo la California, Marekani, wamezilaumu baadhi ya taasisi zisizokuwa za kiserikali (NGOs) zinazofanya kazi katika Tanzania kwa kujinufaisha tu binafsi baadala ya kuelekeza misaada ambayo zinaipata kwa walengwa.
Watanzania hao wamesema kuwa taasisi hizo zinatakiwa kulenga kuwasaidia walengwa wao na siyo kushibisha matumbo yao kama ilivyo sasa kwa NGOs zilizoko nyingi. Watanzania hao hawakutoa mifano yoyote ya taasisi za namna hiyo.
Lawama na mjadala kuhusu taasisi hizo zimetolewa na kuanzishwa na Mjumbe wa Bodi ya Chama cha Watanzania wanaoishi mjini San Francisco, California, Mama Christine Chacha katika mkutano kati ya viongozi wa chama hicho na Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Mama Chacha alikuwa mmoja wa kundi la viongozi wa chama hicho ambao walimpokea Rais Kikwete baada ya kuwa amewasili mjini San Francisco kuanza ziara yake ya siku nane katika Marekani. Chama hicho kinachoongozwa na Bwana Mwesigwa kina wanachama 100.
Katika mkutano wao na Rais Kikwete kwenye Hoteli ya Four Seasons, mjini humo, Mama Chacha amesema wajibu mkubwa wa taasisi zisizokuwa za kiserikali ni kuwatumikia walengwa wao na siyo kuendesha magari ya kifahari ya Land Cruiser kama ilivyo sasa.
Akitoa kauli yake kwenye mjadala huo, Rais Kikwete amesema kuwa siyo kazi ya Serikali kuingilia shughuli za NGOs kwa sababu hizo ni taasisi za kijamii ambazo ni muhimu katika ujenzi wa demokrasia.
Kazi yetu ni kuzijengea taasisi hizo mazingira mazuri ya kufanya kazi. Siyo kazi ya Serikali kuingilia kazi ya taasisi hizo. Ni taasisi muhimu
hata nyingine zinadai kupewa madaraka kama ya viongozi waliochanguliwa na wananchi, amesema Rais Kikwete.
Katika mkutano huo, viongozi hao wa chama cha Watanzania pia wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kubadilisha sheria, ili kuruhusu Watanzania, wanaopenda, kuwa na uraia wa zaidi ya nchi moja.
Rais Kikwete amewaambia Watanzania hao kuwa suala hilo lina taratibu ndefu kwa sababu litahitaji mabadiliko ya Katiba.
Ameongeza pia kuwa mchakato mzima wa kuanzisha utaratibu wa uraia wa zaidi ya nchi moja unahitaji wananchi kuelimishwa na kuhamasishwa ili wayakubali mabadiliko hayo.
Kuhusu swali kuwa kwa nini makampuni ya madini nchini yanauza hisa zao kwa makampuni mengine baada ya muda mfupi, Rais Kikwete amesema kuwa hayo ni makampuni binafsi yenye uhuru wa kuunza hisa wakati yanapotaka, na wala Serikali haiwezi kuyazuia kuuza hisa na umiliki wa makampuni yao.
Katika mfumo wa biashara huria, ni jambo la kawaida kabisa kwa mwekezaji binafsi kuuza hisa zake wakati wote akipenda ama akiona kuwa akiuza atapata faida. Serikali haiwezi kumzuia kufanya hivyo.
Ends