Tusisambaze sumu ya udini kwa kivuli cha Membe na OIC
NCHI inakwenda kubaya na tunaitengezea bomu la maangamizi.
Udini utaangamiza taifa, utaleta vita, maafa na hakuna atakayepona, utatuondoa katika mstari wa utaifa wa kupambana na ufisadi na kukuza uchumi.
Mada yangu ya leo ni udini, ambao naona sasa unatupeleka kubaya na hata kutishia kulipasua taifa letu katika mapande mawili.
Nimekuwa nikifutilia vizuri sana malumbano ya kidini nchini kimya kimya. Ukimya wangu unatokana na hofu kubwa kutokana na unyeti wa suala lenyewe. Baada aya kimya cha muda mrefu, nimeona leo nizungumzie suala hili.
Huko nyuma niliwahi kuonya katika safu hii kwamba tunatengeneza bomu la aangamizi katika nchi. Nilichobaini ni kile alichoonya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, miaka 13 iyopita, watu sasa wanazungumza na kujivunia udini hadharani kama alama yao ya utaifa.
Hili limejitokeza kwa kasi sana tangu kuingia madarakani serikali awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete, watu wamekuwa wakizungumza udini kama wendawazimu.
Mjadala huu sasa umepamba moto kufuatia kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe, kwamba Watanzania hawapaswi kuogopa kujiunga na Jumuiya ya Nchi Kiislam Duniani (OIC).
Binafsi, nilikuwapo katika mkutano wa Membe na waandishi wa habari, huyu mtu amefafanua vizuri sana hatma ya Tanzania kujiunga au kutojiunga na OIC.
Kwanza, Membe hakusema kwamba ni lazima Tanzania ijiunge na OIC licha ya kusema hakuna haja ya kuogopa.
Pili, alisema Tanzania haikujiunga na OIC kama watu wanavyovumisha.
Tatu, aliweka bayana kwamba, Watanzania katika maamuzi yao, watapaswa kuangalia mambo mbalimbali katika kufanya maamuzi ya kujiunga au kutojiunga na OIC ikiwezekana hata kuangalia nchi kama Uganda.
Akifafanua hilo, alisema Uganda ambayo asilimia 66 ya wananchi wake ni Wakristo, asilimia 10 Waislam na waliobaki wapagani, ni mwanachama wa OIC.
Lakini, msisitizo mkubwa wa waziri huyo ni kwamba uamuzi huo utakuwa chini ya mamlaka ya wananchi na si vinginevyo.
Baada ya kauli hiyo, mbivu na mbichi zikabainika, wenye kusambaza sumu ya udini katika nchi wakajitokeza, hawa baadhi yao ni wale wanaoitwa viongozi wa dini.
Mstuko unatokana na kuona viongozi wa dini kuwa wenye kuendekeza udini kwa kutoa matamshi makali ambayo hajengi taifa.
Tumesikia na kuona, viongozi wanakaza misuli ya shingo, kuzungumzia OIC kidini badala ya kuzungumzia kitaifa.
Suala la OIC si la Waislamu pekee bali hata Wakristo, hivyo kama linajadiliwa iwe katika misingi ya utaifa, huu ndiyo uzalendo na hata Mungu anapenda.
Hapa hatuko katika vita ya Jihadi au vita ya Msalaba, tuko katika kujadili jambo nyeti linalohusu nchi, hivyo tunapaswa kujadili kama Watanzania wenye akili na utaifa wao.
Kwa mtu mwenye akili timamu, asiye na fikra au chembe za udini kamwe hawezi kujadili jambo nyeti kama hili la kujiunga na OIC akijiita mimi: "Mkristo au Mwislamu"
Hebu tujiulize, Wakristo wakikaza misuli ya shingo kupinga Tanzania kujiunga na OIC, na Waislam nao wakafanya hivyo, matokeo yake ni nini?
Matokeo yake ni kwamba tutatengeneza bomu la maangamizi, na taifa litakuwa kama la Ivory Coast, ambalo limegawanyika kaskazini ya Waislam na kusini ya Wakristo.
Kinachoonekana ni kwamba katika nchi hii kuna watu ambao wanaomba mijadala ya kidini iibuke ili wapate nafasi ya kuonyesha udini wao.
Leo hii baadhi ya watu wenye fikra za udini wanaweza kuhoji uhusiano kati ya Tanzania na Iran, wakisema eti nchi inataka kuingizwa OIC.
Wengine wanaohoji uhusiano na Vatican hadi ubalozi wake kuwa hapa nchini, hizi ni fikra za kimaskini na kijima, nani rafiki mzuri duniani asiye na doa?
Hivi hiyo Marekani inayotoa misaada duniani na hapa kwetu, ina mazuri gani inafanya duniani?
Mbona yenyewe ina madhambi mengi tu, mbona tunakula mabilioni ya dola zao, sasa kwanini Iran iwe kituko na kuanza kuzusha fikra za udini eti tunaingia OIC na Membe ajiuzulu.
Hivi hao wanadhani wankemea udini, wanajua ambayo yamekuwa yakifanywa na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) tangu kuanzishwa na hadi sasa?
Au hivi Ufaransa ina lipi zuri, mbona inaongoza kusaidia mapinduzi ya kijeshi katika makoloni yake, ilidaiwa kuhusika katika mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994 na mbona tunapokea misaada yake?
Tuache fikra za kijima, fikra za kuigawa nchi, hizi ni fikra za hatari ambazo kamwe zikiachiwa haziwezi kumbakisha mtu.
Ukiona mtu ameishiwa sera, ataanza kujitambulisha kwa udini au ukabila, sasa hivi watu wamekosa mambo ya msingi ya kufanya wanasambaza sumu ya udini katika nchi.
Kwa maana, siku zote sipendi kabisa kuona sura au kusikia mawazo ya watu wenye kutaka kuvuruga amani na usalama wa nchi kwa kivuli cha udini.
Hawa ni watu hatari sana. Hivi Watanzania watoto wa taifa moja tunashindwaje kukaa na kutatua mambo yetu kwa amani na utulivu?
Tunaipeleka wapi sifa yetu hii, watu wanakaa na kujivunia umaskini wa mawazo kwa kujiita eti sisi Waislam au Wakristo.
Wengine wanadikiri kuzungumza uchochezi eti Rais Kikwete ni mdini, ukiuliza hupati majibu zaidi ya kuona ni watu wenye hisia tu za kichochezi, hisia za hatari na fikra za kimaskini na kipuuzi.
Leo hii badala kukaa kuzungumza mambo ya msingi kwa pamoja, tunakaa na kutoa matamshi makali yatakayoyumbisha mustakabali wa taifa.
Baadhi ya Wakristo wanasahau kwamba, kutoa matamshi makali kuhusu Tanzania kujiunga na OIC hakuwezi kujenga taifa huku baadhi ya Waislam nao wakisahau kuwa kudai jambo hilo kwa nguvu hakuwezi kufanikiwa.
Nchi hii si ya Waislam wala ya Wakristo kama alivyosema Mwalimu Nyerere, bali wapo wenye fikra za udini wanaofanya mbinu za kuigawa, na ole wao, watakumbana na mkono wa dola!
Halafu cha ajabu baadhi ya wanaojiita viongozi wa dini wenye misimamo mikali kwa kuwa na fikra za kijima, ndiyo wenye kutunza majini nyumbani kwao, wengine wakiwajihusiaha na matukio ya ajabu.
Ndugu zangu Watanzania tusicheze wala tusiruhusu sumu hii ya udini kusambaa, hii itaangamiza taifa na wala hakuna ufundi katika kucheza na jambo hili.
Watanzania tunapaswa kukaa kama taifa moja, kudumisha umoja, utaifa na amani yetu, tusiruhusu watu wachache wenye fikra hatari kuzisambaza katika taifa, tuwakatae, tuwadhibiti na uwezo wa kuwadhibiti tunao.
Aluta Continua!
Ramadhan Semtawa ni mwandishi wa mwananchi:0782-528229:mwanamapinduzi@yahoo.com