Hoja za Makakama ya Kadhi ni Dhaifu - (Makala ya Gazeti la Kulikoni)
Mchungaji/Mwanasiasa Christopher Mtikila amefungua kesi mahakamani kupinga rasmi uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi nchini kwa madai kuwa ni kinyume na Katiba. Mjadala huu siyo mgeni na umekuwepo katika jamii yetu kwa muda mrefu na bila ya shaka ni lazima ufikie wakati ambapo unamalizwa kwa kuanzisha mahakama hiyo kama ndugu zetu Waislamu wanavyotaka au kutoanzishwa mahakama hiyo kama baadhi ya watu wengine wanavyotaka (wawe Wakristu au vinginevyo). Kama Taifa, lazima tujifunze kuanzisha mijadala na kuihitimisha ili tuendelee na mambo mengine. Ni kutotumia muda vizuri kama tutakuwa tunaendelea kuzungumzia jambo lile lile miaka nenda, miaka rudi badala ya kuamua kuzungumza jambo na kulimaliza, hasa linaloweza kumalizika kiungwana, kitaalam, na kidugu kama suala la Kadhi.
Binafsi naamini kuwa hoja ambazo zinatolewa hadi hivi sasa kuhusu haja, ulazima, na haraka ya kuanzishwa kwa mahakama hiyo Tanzania bara ni hoja dhaifu ambazo bado hazina nguvu. Ni mpaka pale watetezi wa uanzishwaji upya wa mahakama ya Kadhi watakapojenga hoja zenye nguvu, ambazo zinaweza kusimama siyo katika kuvutia hisia za watu, bali katika kushawishi akili zao na kuona kuwa ni hoja za msingi na zisizopingika kirahisi, basi kuanzishwa kwa mahakama hiyo nchini kutaendelea kuchelewa na kwa hakika kunapaswa kuchelewa.
Kabla ya kuziangalia hoja hizi na kuonesha udhaifu wake, naomba kwanza niseme mambo machache ambayo ni muhimu kuyazingatia katika mjadala huu. Kwanza kabisa, kesi iliyofunguliwa na Mch. Mtikila kuhusu kupinga uanzishwaji wa mahakama hiyo ni suala la kwake kama raia wa nchi hii. Isichukuliwe hata kidogo kuwa Mtikila anawakilishwa Wakristu wa Tanzania katika kesi hii. Hivyo basi kauli zake zenye kuumiza hisia za Waislamu zichukuliwe kama ni kauli zake na zisichukuliwe kama ni maneno ya Wakristu dhidi ya ndugu zao waislamu. Na kama ilivyokawaida ya viongozi wetu wa Kikristu hakuna aliyetokea hadharani na kupinga kauli za Mtikila kuwa haziwakilishi mawazo au misimamo ya makanisa nchini. Ingekuwa jambo la kupendeza kusikia TEC, CCT, na Muungano wa Makanisa mengine kutoa kauli zao kupinga madai ya Mtikila kuwa kuanzishwa mahakama ya kadhi kutachochea Ugaidi na kuleta vurugu.
Jambo la pili ni kuwa, binafsi sina tatizo na uanzishwaji wa mahakama ya Kadhi Tanzania bara, na sina sababu ya kuwa na hofu ya kuwepo kwake. Nimebahatika siyo tu kuishi na Waislamu bali pia kukulia na kusoma kati yao na kuwa na marafiki wa karibu na wengine imefikia familia zetu kuoleana n.k Siwezi kuamini hata kidogo kuwa Watanzania wenzetu hawa ambao ni Waislamu watageuka na kuwa Afghanistani au Iraq na kuanza kututendea vibaya kisa tu ati mahakama ya kadhi imeanzishwa. Waislamu wa Tanzania ni mfano bora kabisa katika ulimwengu wa mahusiano mazuri kati ya watu wa imani tofauti katika nchi. Ni lazima tujivunie tofauti yetu na hasa pale ambapo tofauti hiyo inatufanya tuzungumze kwa uhuru, kwa heshima, na kwa upendo kati yetu.
Jambo la tatu hapa ni kuwa, utakapofika mwisho wa mjadala huu ni lazima tubakie na heshima na hisia yetu ya Utanzania. Itakuwa jambo baya na la hatari kama tutafikia mwisho wa mjadala huu na kujikuta ni watanzania wapenda Kadhi na Watanzania wapinga Kadhi. Tofauti ya maoni na mitazamo ni kiini cha utawala wa demokrasia kwani kwa kutofautiana ndipo tunapata nafasi ya kupata mawazo mazuri na yenye nguvu zaidi. Kwa sababu hiyo basi, kusiwe na Mtanzania yeyote yule mwenye hofu ya mjadala huu. Wale Mashehe waliozungumza kwenye kipindi cha Jenerali on Monday wasitupe sababu ya kuwa na hisia ya vurugu au uvunjifu wa amani. Katika maneno yao ya mwisho siku ile, ndugu zetu hawa waliwasihi Waislamu nchini kuwa wawe watulivu na kutoleta vurugu. Ni nani kawaambia kuwa Waislamu ni watu wa shari au wanataka kuleta vurugu kwa sababu tu Mtikila kafungua kesi Mahakamani? Ni lazima wao viongozi wa dini waoneshe imani kwa Waislamu wenzao kuwa wanafahamu umuhimu wa utulivu na amani, na wao si chanzo cha uvunjifu wa amani kisa tu ya mjadala wa Kadhi. Na katika hili, ningependa kuona viongozi wengine wa Kiislamu wakiwaweka sawa hawa wenzao ambao waliashiria kuwa Waislamu si watu wa amani na utulivu. Kama vile maaskofu walivyokaa kimya kuhusu Mtikila, vivyo hivyo Maimamu na Mashehe wengine nao wamekaa kimya katika hili.
Baada ya kusema hayo turudi kwenye kichwa cha habari cha hoja ya leo kuwa hoja zinatolewa ili Mahakama ya Kadhi irudishwe Tanzania Bara ni hoja dhaifu. Naomba nieleweke sisemi kuwa hoja hizi ni za kupuuzia (kama watu wengine wafanyavyo wasipoweza kujibu hoja), bali ni hoja zenye kujibiwa. Udhaifu wake unatokana na ukweli kuwa zikiangaliwa moja baada ya nyingine tena kwa karibu zaidi bila hata ya kutumia darubini utaona kuwa zimepotoka ndani kwa ndani (inherently flawed). Kwa muda mrefu sasa nimesubiri kuona kama kuna mtu ambaye atathubutu kuzijibu hoja hizi na kuzionesha kuwa hazifai. Mtu huyo hajatokea na badala yake yupo mtu aliyekimbilia mahakamani. Hetu tuziangalie hizi hoja ambazo hutajwa sana kuwa kwanini Mahakama ya Kadhi ianzishwe tena kwa sheria ya Bunge na uwepo wake uunganishwe katika utaratibu wa mahakama za Tanzania. Kwa maneno mengine, kwanini Waislamu wanataka serikali ianzishe mahakama ya Kadhi Tanzania Bara.
Hoja ya 1: Mahakama ya Kadhi imeahidiwa na serikali ya CCM, hivyo Chama cha Mapinduzi kitimize ahadi yake ama sivyo watakiona 2010.
Nimepata nafasi ya kuangalia Ilani ya Uchaguzi ya CCM, na kuhusu suala la kadhi ahadi waliyoitoa inasema hivi CCM itazitaka Serikali ziendelee na hatua zilizoanza kuchukuliwa ili kuiboresha Sekta ya Sheria kusudi nayo itoe huduma bora zaidi kwa jamii. Yatakayosisitizwa katika kipindi hiki ni pamoja na yafuatayo
. Kulipatia ufumbuzi suala la kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara
Hivyo utaona kuwa CCM haijatoa ahadi ya kuanzisha mahakama ya Kadhi Tanzania bara, bali kulipatia ufumbuzi suala la kuanzishwa kwa mahakama hiyo. Hii ina maana ya kuwa CCM inaweza kabisa kushiriki kwa namna fulani (kwa sera au utunzi wa sheria) kuhakikisha kuwa mahakama ya kadhi inapokuwepo Tanzania bara. Hilo bila ya shaka limechukuliwa kumaanisha kuwa CCM itarudisha Mahakama ya Kadhi kwa kuitungia sheria ya kuianzisha, kuitengea bajeti, na kuiendesha mahakama hiyo. Hii si tafsiri sawa sawa au ya pekee (inawezekana kuwa ni tafsiri mojawapo ya ahadi hiyo) kama nitakavyoonesha baadaye.
Hata hivyo mtu anaweza kusema ahadi hiyo ina maana ya kurudisha mahakama ya kadhi na mimi nimeielewa vibaya. Katika hotuba yake ya bajeti ya mwaka 2005/2006 aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. H. Bakari Mwapachu alisema hivi kuhusu sehemu hiyo ya Ilani, aidha, (kuhusu) suala kadhi, litafanyikwa kazi. Na hata katika bajeti ya wizara hiyo chini ya Waziri Mpya Bi. Mary Nagu na yeye hakutoa ahadi mpya ila iliyokuwemo kwenye ilani ya CCM kuwa katika mwaka huu Wizara yake kwa kutumia Tume ya Kurekebisha Sheria itapitia mambo mengi miongoni mwake ni kulipatia ufumbuzi suala la Uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi, Tanzania Bara.
Kwa kifupi, serikali ya CCM haikuwaahidi waislamu kuanzisha Mahakama ya Kadhi. Ilichoahidi ni kutafuta ufumbuzi jinsi gani inaweza kuanzishwa pasipo kupingana na sheria au kutengeneza sheria itakayowezesha kuanzishwa kwake. Kilichofanyika ni sawa na mtu kuahidi kuwa kwa vile una matatizo ya mahali pa kuishi basi atafanya kila jitihada kukutafuta ufumbuzi wa tatizo lako la makazi ili na wewe uweze kujisitiri na famili yako. Itakuwa ni jambo la kuchekesha kama mtu atatoka na kuanza kudai nyumba kutoka kwa aliyetoa ahadi!!
Sasa haina maana kuwa serikali haitarudisha mahakama ya kadhi bali ina maana katika kutafuta ufumbuzi wa suala la kadhi, kurudisha kwa kutunga sheria inayounda Mahakama ya Kadhi kama zilivyo sheria za Mahakama ya Biashara kwa mfano, ni mojawapo tu ya vitu vinavyowezekana, na kwa hakika siyo jambo pekee.
Hivyo ili hoja hii iwe na nguvu kidogo, ndugu zetu Waislamu wawabane CCM na kuwauliza walichowaahidi hasa ni nini? Je wameahidiwa Kurudishwa kwa Mahakama ya Kadhi au kutafutiwa ufumbuzi wa kurudishwa kwa mahakama hiyo? Baadhi ya Wabunge wa CCM wameoneshwa kukerwa na utata huu wa makusudi na wamehoji iweje ahadi ya kushughulikia suala la kadhi inachukua zaidi ya miaka kumi sasa?
Hoja ya 2. Mahakama ya Kadhi ilikuwepo wakati wa Ukoloni, hivyo kama ilikuwepo wakati wa Ukoloni kwanini isiwepo sasa?
Hoja hii ina nguvu kidogo lakini msingi wake unamashaka. Jambo kufanywa na wakoloni au kuruhusiwa na wakoloni hakulifanyi jambo hilo kuwa jambo sahihi au ambalo tuliendeleze jinsi ile ile. Wakoloni katika nchi mbalimbali walifanya mambo mbalimbali kwa malengo tofauti tofauti. Kuna mambo ambayo wakoloni waliyafanya au taasisi walizozianzisha ambazo sisi kama nchi huru tuliamua kuachana nazo.
Zaidi ya yote, tangu lini tumeanza kutukuza wakoloni? Hivi kweli hoja haiwezi kujenga ikasimama wenyewe hadi tupige magoti na kuonesha kile walichofanya wakoloni. Huku ni kujidhalilisha kusiko kwa lazima. Na kama jambo lilifanywa na wakoloni haina maana jambo hilo lilikuwa sawa. Si hawa hawa wakoloni wanaolalamikiwa na Waislamu kuwa ndio walioweka misingi ya kuwapendelea Wakristu? (soma kitabu cha Hamza Njozi na kile cha Mohammed Said). Si ndiyo hawa wakoloni waliowatenda vibaya waislamu kwa mambo yao kama yanavyosimuliwa katika nyaraka mbalimbali za kihistoria? Ni lazima tukubaliane kuwa kutumia Wakoloni kama msingi wa kujenga hoja ya kadhi ni mkakati mbovu.
Hoja ya 3. Nchi nyingine majirani na za kiafrika zina mahakama ya kadhi kwanini sisi tuogope?
Hoja hii ukiingalia kwa haraka ina nguvu ya kufanana na ushawishi wa ukaribu. Mara nyingi katika hoja hii kauli inayofuatia ni mbona hata Zanzibar Mahakama ya Kadhi ipo kwanini isiwepo hapa Bara? Hoja hii nayo ina msingi lakini haina nguvu ukiingalia kwa karibu. Kwa kuzihusu nchi nyingine hoja hii ina udhaifu mkubwa ufuatao, Tanzania ni nchi huru inayojiamulia mambo yake yenyewe na haishinikizwi kwa namna yoyote ile kufuata kile ambacho nchi nyingine inafanya.
Kuna mambo ambayo nchi nyingine zinafanya na sisi hatufuati. Kuna nchi ambazo zinatambua uwepo wa mahakama ya Kadhi lakini zina mambo mengine ambayo hatuambiwi tuyafuate pia. Afrika ya Kusini inayo Kadhi lakini hao hao wanaruhusu mashoga kuoana. Sasa kama vinavyofanya na sheria za nje ni mambo ya kufuata kwanini tufuate la kadhi tu na tusifuate la kuruhusu mashoga kuoana?
India ambako tuna ukaribu zaidi wa kisheria labda kuliko sehemu nyingine yoyote katika jumuiya ya Madola, wao wanazo mahakama za kadhi lakini hazitambuliki na sheria ya India lakini hazipingwi na maamuzi yake yanakuwa ni ushauri tu usio na nguvu ya kisheria na uamuzi huo hamzuii Muislamu kwenda katika mahakama za serikali. Kwanini tuchague kufuata ya Kenya na siyo ya India? Nchi kama Uturuku ambazo zina Waislamu wengi kuliko Tanzania hazina Mahakama ya Kadhi jinsi zinavyotakwa hapa Tanzania. Wao (Waturuki) ingawa mahakimu wao wanaitwa Makadhi kutokana na sababu za kihistoria lakini hawahukumu kwa sheria za Kiislamu.
Kwa kifupi ni kuwa, suala la kadhi linawahusu Watanzania na ni Watanzania ambao wagonganishe vichwa vyao wakikusanya mangamuzi ya utaalamu wao mbalimbali na kutafuta suluhisho ambalo ni la Watanzania na la Kitanzania.
Itaendelea wiki ijayo kwa kuangalia hoja nyingine zilizosalia na zile hoja zenye nguvu.