SoC02 Jibu la kitendawili cha tatizo la ajira nchini kupitia mfumo wetu wa elimu

Stories of Change - 2022 Competition

Philombe Jr

New Member
Apr 24, 2021
4
3
Tatizo la ajira nchini limekua kitendawili kwa muda mrefu sasa bila ya kupata majibu. Taasisi zetu za elimu hutoa wahitimu wengi ambao hutegemea ajira ili waweze kujikwamua kiuchumi. Takriban kila mwaka watu wanaokadiriwa 800000 huwa tayari kuingia kwenye soko la ajira lakini wanaopata ajira hizo hawafikii hata robo ya idadi hiyo.

Kitendawili hiki kimekua kigumu sana kuteguka nchini Tanzania na walio wengi tunajaribu kuangalia kwanza mfumo wetu wa elimu ili kuweza kuona kwa namna gani tunaweza kuboresha mfumo huu wa utoaji elimu. Tunaweza kujiuliza je mfumo wetu wa elimu unalijibu hili swali la ajira, Je hata hao wanaoajiriwa wanachokifanya ndicho kilichotarajiwa?

Je, elimu yetu inamtengenezea mazingira mhitimu kuwaza zaidi au tu inamfunga na kumwambia subiria ajira serikalini? Wapi kuna tatizo ni ajira kuwa chache au tatizo ni elimu yetu kutokutoa mawanda mapana kwa mhitimu kuwaza zaidi juu ya alichobobea au ni astashahada na shahada zetu haziendani na soko la ajira na fursa mbali mbali zinazotolowa? Nikiwa kama mdau wa elimu yetu hapa nchini, tunapaswa kutumia njia hizi ili kwa namna moja ama nyengine tuweze kutatua tatizo hili la ajira.

Kuwalika jopo la wataalamu wa elimu kupitia upya mfumo wetu wa elimu kuanzia ngazi ya chini hadi elimu ya juu.
Mfumo wetu wa elimu ni 2-7-4-2-3+ yaani miaka 2 ya elimu ya maandalizi, miaka 7 ya elimu ya msingi, miaka 4 ya elimu ya sekondari, miaka 2 ya elimu ya juu ya sekondari na miaka 3 ya elimu ya Chuo kikuu. Huu ni mfumo wa elimu ambao unatumika hapa nchini lakini bado haujibu swali la kitendawili chetu cha ajira. Bado haumpi nafasi mhitimu kuweza kufikiria nini afanye badala yake unampa utegemezi wa ajira za serikali tu kitu ambacho ni kigumu sana kwasababu nafasi zinazotoka na idadi iliokuwepo haviwiani. Serikali itakapoamua kuupitia mtaala wetu na kutoa mada zote ambazo zimepitwa na wakati na kumtoa mwanafunzi kwenye elimu ya kukariri kwenda kwenye elimu ya kufikiria basi kutamfanya mhitimu huyo kuweza kufikiria nje ya boksi.

Kimsingi sana mtaala wetu haumpi mhitimu njia mbali mbali za kutumia elimu yake kuigeuza kuwa njia ya kumkwamua kiuchumi, haimuwezeshi kufikiria kujiajiri zaidi na kuacha kuitegemea zaidi serikali, ingelikua elimu yetu inajibu swali hili basi tatizo la ajira lingepungua. Jopo la wataalamu litakapopitia mitaala ya elimu ya maandalizi hadi chuo kikuu na kutoa madhaifu kwa kuongeza vitu ambavyo vinaendana na jamii na soko la ajira basi tutapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la ajira.

Kutambulisha na kutumia somo la Ujasiriamali kwenye mtaala wetu.
Serikali inapaswa kuamua kulitumia somo la Ujasiriamali kwa wanafunzi wote nchini Tanzania kuanzia ngazi ya darasa la 4 hadi Chuo kikuu. Ujasiriamali liwe somo ambalo kila mwanafunzi nchini anatakiwa alisome. Serikali inatakiwa iwekeze kwenye huu ujuzi kwa kutayarisha mtaala na wakufunzi kwa kuwapa elimu iliobora na vitendea kazi vya kutosha. Ujasiriamali ni ujuzi mzuri kwasababu Taifa litafaidika kiuchumi na kumuwezesha mhitimu kupitia elimu na mafunzo kumkomboa kifikra na kiuchumi.

Ujasiriamali utamuwezesha mhitimu kuweza kuitumia akili yake kufikiria zaidi jinsi gani anaweza kuwa mbunifu kwa ambacho kwasasa kinatumika kwa kuweza kukibadilisha na hata kugundua kitu kingine ambacho kitaleta tija kwa Taifa letu. Kupitia somo hili la Ujasiriamali watu wataweza kupata mtazamo chanya juu ya elimu yao na kutoa utegemezi wa serikali. Kutoka kwenye kufanya kazi chini ya serikali hadi kuweza kujiajiri na kuweza kulichangia taifa letu kwa kupunguza wahitimu ambao hawana ajira. Kupitia wakufunzi ambao serikali itawekeza kwa kuwapa elimu bora na ambayo ndio kwasasa soko linataka basi tutegemee Tanzania ambayo itakua na maendeleo kupitia elimu ya Ujasiriamali kwasababu tatizo kubwa huwa wahitimu kukosa maarifa ya kuweza kufikiria zaidi jinsi gani elimu ile inaweza kumkomboa kifikra na kuwa huru kifedha bila ya kuitegemea Serikali.

Kutambulisha na kutumia somo la tehama kwa wanafunzi wote nchini.
Serikali inapaswa kuwekeza kwenye kuwatayarisha wakufunzi kwenye somo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa ngazi ya elimu kuanzia darasa la 5 hadi elimu ya juu. Kwasasa Teknolojia inajibu maswali mengi ya ajira. Kupitia Tehama watu mbali mbali hujiajiri. Elimu ya Tehama ni elimu bora sana kwa maslahi ya taifa hili kwenye kujibu swali la ajira. Serikali inapaswa kuandaa mtaala huu kwa wote nchini na kuweza kuwekeza kwenye kufanikisha miundombinu ya Tehama yanapatikana kwenye maeneo mengi nchini kufanya hivi ni kuwawezesha wanafunzi kuweza kuwa na uelewa wa kuweza kutumia vifaa vya teknolojia kutoka ngazi ya chini ya kutambua hadi kuweza kutumia na kusuluhisha kwa kufanya kazi mbali mbali kwa kutumia vifaa hivyo.

Tunauona umuhimu wa Tehama kwenye kurahisisha utendaji kazi, tutakapofanya hivi kwenye mfumo wetu wa elimu basi tunaitengeneza Tanzania ya kiteknolojia hapo baadae. Elimu ya Tehama ni ujuzi ambao kila mtanzania anapaswa kuwa nao kwani kuwa na ujuzi huu kutamfanya kijana aweze kujiajiri kupitia fursa mbali mbali za kidijidali ambazo kwasasa zipo. Elimu ya Tehama ukijumuisha na elimu ya ujasiriamali itaweza kulisaidia taifa hili kuwa na wabunifu ambao wataweza kugundua vitu mbali mbali ambavyo vitawapa ajira na hata kutoa ajira kwa wengine.

Serikali kuwekeza nguvu nyingi kwenye kuwekeza kwenye masomo ya Sayansi, Uhandisi, Teknolojia,Hesabati pamoja na Afya Biashara na Kilimo.
Tanzania bado imeonesha uhitaji zaidi kwenye haya maeneo ya Sayansi, Uhandisi, Teknolojia Hesabati, Afya, Kilimo na Biashara. Haya ni maeneo muhimu zaidi kwenye kujibu na kutatua matatizo ya ajira nchini. Ni maeneo ambayo serikali inatakiwa kuwekeza nguvu nyingi kwa kuwatengeneza zaidi nguvu kazi ambazo zitaweza kutoa elimu iliobora na inayohitajika kwenye soko la ajira kwa maendeleo ya taifa na ya mtu binafsi. Kupitia elimu hizi kama itakua inatolewa kwa ubora zaidi basi itapunguza swala la ajira kwa kadri muda unavyoenda. Masomo kama Sayansi, Uhandisi, Teknolojia na Hesabati yanapaswa kutolewa kwa kiwango cha juu sana hasa kwenye elimu ya juu kwasababu husaidia kwenye ubadilishaji na ugunduzi kwenye maswala mbali mbali ya kijamii, na kiuchumi. Kupitia teknolojia tunaona watu wanagundua njia za kiteknolojia kwenye biashara, afya, kilimo, kifedha, elimu na maeneo mengine ya kimaendeleo. Hivyo serikali inapaswa kuwekeza nguvu hii kwenye taasisi za kielimu ili kuwawezesha vijana kupata ajira serikalini na hata kwa kujiajiri kupitia ugunduzi mbali mbali.

Serikali kushikamana na wahitimu wanapomaliza masomo yao.
Serikali isiwaache moja kwa moja vijana waliohitimu kwa kuwatupa mkono. Serikali inapaswa kuweka nguvu zao kwa namna moja ama nyengine kwa kundi ambalo linamaliza masomo yao. Serikali itoe mikopo kwa vikundi mbali mbali ikiwa ni moja ya njia ya kutatua tatizo la ajira. Serikali pia inapaswa kuweka maonyesho kila mwaka na kuchukua ugunduzi uliobora kwa kuweza kuwawezesha kifedha ili kuweza kuendeleza mradi huo hii itawapa motisha watu mbali mbali kubuni suluhishi kwenye jamii zetu, na itatoa motisha kwa wengine kufikiria zaidi kutengeneza mradi ambao utatua tatizo la ajira kwao na hata kwa wengine. Serikali inaweza kutafuta wadhamini na wadau mbali mbali kufanikisha hili.
 
Tunaweza kujadili kwenye hili juu ya mitazamo mbali mbali au mnakubaliana na hizi njia?
 
Back
Top Bottom