KWA KIASI KIKUBWA AHADI NYINGI ZA KIKWETE ZILIKUWA ZINATOKA BILA MANTIKI YOYOTE. MOJAWAPO NI HILI LA KUTENGENEZA AJIRA WAKTI SERIKALI IMESHAUZA MASHIRIKA YOTE NA KUJITOA KATIKA BIASAHARA YA AINA YOYOTE. AHADI NYINGINE AMBAYO NINAITAZAMA KWA MAKINI NI ILE YA KUJENGA SHULE ZA SEKONDARI 500 KILA MWAKA.
=====================
Kikwete Atahadharishwa
*ILO yasema ajira milioni moja kufikiwa ni kazi
*Yasema njia bora ni kuimarisha uchumi wa nchi
Na Mkombe Zanda, Morogoro
SHIRIKA la Kazi Duniani (ILO), limeitaka Serikali ya Tanzania kuchukua tahadhari kubwa katika mpango wake wa kuzalisha ajira milioni moja nchini, kwa kuimarisha kwanza uchumi wake, kwani bila kufanya hivyo kamwe mpango huo hautafanikiwa.
Mshauri wa Ufundi wa ILO, Profesa Vremudia Diejomaoh, aliitaka Serikali kutambua kuwa mpango huo hauwezi kufanikiwa wala kuwa endelevu na wenye manufaa kwa wananchi wa kawaida nchini, endapo uchumi wa Taifa hautakuwa imara na wenye uwezo wa kukabiliana na mahitaji halisi ya uanzishaji wa ajira hizo.
Profesa Diejomaoh alisema ili ajira hizo ziweze kupatikana ni lazima kwanza Tanzania iwe na uchumi madhubuti utakaokuwa na uwezo wa kutoa fursa za upatikanaji wa kipato cha uhakika kwa wananchi, hali ambayo pia itatoa fursa ya kuanzishwa kwa ajira nyingine za kuwasaidia Watanzania.
Alisema uchumi imara ndiyo njia pekee ya kuimarisha na kuzalisha zaidi ajira kwa wananchi wa kawaida, hivyo aliitaka Serikali kuzingatia kwanza msingi huo katika utekelezaji wa mpango wake.
Profesa Diejomaoh alitoa tahadhari hiyo juzi mjini hapa katika mkutano wa siku mbili wa vyama vya wafanyakazi nchini, wa kujadili upatikanaji ajira.
Kimsingi aliitaka Tanzania kutambua kuwa mazingira yaliyopo hivi sasa nchini, hayatoi fursa nzuri katika utekelezaji wa maazimio mbalimbali ya kimataifa, kuhusu upatikanaji wa ajira nyingi kwa wananchi wa kawaida, hali ambayo imeendelea kuwa vikwazo katika utengenezaji wa ajira kwa wananchi.
Aidha, Profesa Diejomaoh aliishauri Serikali kuipa kipaumbele zaidi sekta binafsi kwenye utekelezaji wa mpango huo, kwani hiyo ndiyo sehemu inayomiliki soko kubwa la ajira nchini.
Kutokana na hali hiyo, aliitaka Serikali kurekebisha kasoro hizo ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na fursa nzuri zaidi katika kuwawezesha raia wake kujipatia ajira mbalimbali zenye uwezo wa kuwakwamua kimaisha.
Miongoni mwa marekebisho hayo, Profesa Diejomaoh aliyataja kuwa ni kukuza fursa za kiuchumi na biashara, kuboresha mfumo wa utawala bora, kuboresha miundombinu hasa vijijini, kupunguza masharti ya uwekezaji na kuboresha mfumo wa elimu kwa raia wake.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania(TUCTA), Bw. Nestory Ngulla, aliitaka Serikali kuhakikisha kuwa mpango wa ajira milioni moja unatilia mkazo zaidi katika utengenezaji wa ajira zenye uwezo wa kumkwamua mwananchi wa kawaida, kutoka kwenye hali duni ya kiuchumi aliyonayo hivi sasa.
Ni lazima tuhakikishe mpango wa ajira milioni moja unatengeneza ajira bora na si bora ajira. Tunataka ajira zenye kumwezesha Mtanzania kukabiliana na changamoto za sayansi na teknolojia zilizopo hivi sasa, ili aweze kujikwamua kiuchumi.
Mkutano huo wa siku mbili unatarajiwa kutoa mapendekezo kwa Serikali kuhusu namna ya upatikanaji wa ajira kupitia sekta binafsi nchini.
Kabla na baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Rais Jakaya Kikwete, alitoa ahadi za Serikali yake kutengeneza ajira milioni moja katika kipindi cha miakamitano ya uongozi wake.
Wakati huo huo, Ramadhan Libenanga anaripoti kwamba Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya vijana Kapteni mstaafu John Chiligati, amesema Serikali katika utekelezaji wa ahadi zake kwa wananchi, tayari kwa kipindi kifupi imetoa jumla ya sh. bilioni 10.5 kati ya sh. bilioni 21 zilizotengwa kwa kila mkoa, kupewa sh. bilioni moja na
tayari zimewasilishwa katika Benki za CRDB na NMB nchini.
Waziri Chiligati alisema Serikali pia imeanzisha utaratibu wa kutambua na kurasimisha rasilimali na biashara za Watanzania wanyonge walio katika sekta iliyo rasmi kupitia mpango wa MKURABITA wenye lengo la kuandikisha na kutoa vyeti vya umiliki kwa rasilimali hizo na kutumiwa kwa vyeti hivyo kama dhamana na ya mikopo kwenye mabenki.
Akifungua mkutano wa Jumuiya za Wafanyakazi kuhusu Programu ya Ajira ya
Taifa mjini hapa jana, Waziri alisema hiyo ni moja ya jitihada za Serikali iliyopo madarakani kutekeleza ahadi yake iliyotolewa na Rais Kikwete wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka jana kuhusu kutoa ajira milioni moja kwa kipindi cha miaka mitano 2006-2010.
Alisema Serikali, imechukua hatua mbalimbali za kusaidia kukua kwa uchumi na hivyo kuongeza ajira ikiwamo kuanzishwa kwa mpango wa kuendeleza sekta ya kilimo (ASDP) ambapo wakulima wadogo watapewa pembejeo, zana za kilimo na masoko.
Kwa mujibu wa Waziri Chiligati kuwa katika mpango huo, jumla ya sh. trilioni 2. 5 zimetengwa katika bajeti ya mwaka huu kwa ajili hiyo.
Mbali na hayo Waziri Chiligati alisema ukosefu wa ajira ni tatizo sugu na linaloleta kero kwa nchi zote zinazoendelea ikiwamo Tanzania.
Alisema kulingana na taarifa za utafiti wa nguvukazi uliokuwa ukifanywa, mwaka 2000 na 2001 kiwango cha ukosefu wa kazi nchini kilikuwa ni asilimia 12.9 na ulibainisha kwamba kila mwaka watu wapatao 700,000 huingia katika soko la ajira na kundi linaloathirika zaidi ni vijana na wanawake.
Waziri Chiligati alisema tatizo linalochangia kupunguza kasi ya kukuza ajira ni uwekezaji finyu kwenye sekta zenye uwezo mkubwa wa kukuza ajira kama vile kilimo.
Aidha, alisema hivi sasa asilimia 82 ya Watanzania wote wanategemea kilimo kwa maisha yao na kwa ajira ambapo suluhisho ni namna ya kuboresha kilimo na sekta iliyorasmi ili nafasi nyingi zaidi ziweza kupatikana.
Chiligati alisema kuwa njia nyingine ya kukuza uchumi ni kuwekeza zaidi katika maeneo ambayo yatahitaji nguvu kazi kubwa kama shughuli za viwanda, ujenzi wa barabara, nyumba viwanja vya ndege na mabwawa.
Alisema suala la kukuza uchumi na kuongeza ajira linahusu jamii yote na hasa sekta binafsi ambayo ndiyo sekta itakayotoa asilimia kubwa ya ajira nchini