Kikwete: Vigogo wa dawa za kulevya jisamilisheni
Na Ramadhan Semtawa, Songea
SIKU chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza kuwa ana majina ya vigogo wa dawa za kulevya nchini, amewataka wanaojihusisha na biashara hiyo kujisamilisha vinginevyo watanaswa na msako mkali utakaoanzishwa dhidi yao.
Akihutubia katika kilele cha Mwenge na hitimisho la wiki ya Vijana Taifa juzi, Rais Kikwete alisema msako wa vigogo hao utakuwa mkali kuliko ule ambao unaendeshwa dhidi majambazi.
Alisema dawa ya vigogo hao ni kujisalimisha kwa kuacha biashara hiyo au vinginevyo watakabiliana na mkono mrefu wa dola.
Alisema sasa umefika wakati kwa 'Wazungu wa Unga' kuamua kujisalimisha kwa kuachana na biashara hiyo au wakabiliane na mkono wa dola.
"Naomba vijana muache kukubali kutumiwa, mkikataa mtakuwa mmesaidia serikali kuukata mzizi wa fitana wa 'wazungu wa unga', naomba nichukue fursa hii kuwaonya kwamba, tutawaendeshea operesheni kama ile dhidi ya majambazi," alionya Rais na kuongeza.
"Ni jukumu lao kuamua kuacha au kukabiliana na nguvu za dola, hawa ni watu hatari, lakini vita hii tutaweza kufanikiwa ikiwa vijana mtashirikiana na serikali yenu, ungeni mkono serikali," alisisitiza Rais.
Alisema vijana wengi ambao ni nguvu kazi ya taifa wanaathirika kutokana na matumizi ya dawa za kulevya na kuonya kwamba serikali haitakaa kimya kukubali hali hiyo iendelee.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete imeungwa mkono na Kamishna wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Christopher Shekiondo ambaye amesema sambamba na mpango huo kuna mkakati wa kubadili sheria ya dawa za kulevya ili kuwabana zaidi vigogo wa mihadarati.
Shekiondo alisema sheria ya sasa ina upungufu kwani inatoa mwanya na kwa wafanyabiashara wakubwa kuendelea kufanya biashara ya dawa za kulevya bila kukamatwa na ushahidi ingawa majina yao yanaweza kupatikana.
Kwa mujibu wa Shekiondo, udhaifu uliopo katika sheria ya sasa unatokana na adhabu ya faini kwa watuhumiwa ambao mara nyingi si vigogo wenyewe bali ni wale waliotumwa hivyo huwa rahisi kwa vigogo wakubwa kulipa faini hizo.
Shekiondo alifafanua kwamba, wafanyabiashara wakubwa au vigogo wanapotuma vijana wao kwenda nje au kuuza katika soko la ndani huwasisitizia kwamba hata wakikamatwa wasithubutu kuwataja kwani watatolewa kwa dhamana hivyo wakiwataja watakosa watu wa kuwatoa kwa dhamana.
"Ni kweli dawa za kulevya huingizwa nchini na wafanyabiashara wakubwa, lakini inakuwa vigumu kuwakatamata hawa, hawa hutumiwa vijana wao, lakini huwaeleza kabisa kwamba hata wakikamatwa wasithubutu kuwataja kwani wao ndiyo watakaowatoa kwa dhamana," alisema Shekiondo na kuongeza:
"Sasa ndiyo maana unaona kijana anakamtwa na mzigo kutoka nje lakini hamtaji bosi wake kwa sababu anajua atatolewa kwa dhamana, ni kweli kama mtu ana mzigo wa Sh100milioni na kijana wake anatakiwa kutolewa kwa dhamana ya Sh10milioni unafikiria atashindwa kumtoa."?
"Haya ni mapungufu ndiyo maana tunaangalia jinsi ya kupendekeza kuwepo mabadiliko katika sheria hii ili iwe na meno zaidi iwabane wafanyabaishara wakubwa na wanaotumiwa hasa kwa kuangalia masharti ya dhamana kuyafanya kuwa magumu zaidi."
Shekiondo alifafanua kwamba, dawa za kulevya bado ni tatizo kubwa nchini kiuchumi na kijamii na kuongeza kwamba hivi sasa kuna changamoto kubwa ya kudhibiti matumizi na biashara ya dawa hizo hasa kuwa makini na biashara hiyo kutoka Marekani ya Kusini kuelekea Afrika Magharibi.
Kamishna huyo alisema hivi sasa kuna wimbi kubwa la uingizaji dawa za kulevya kutoka Marekani ya Kusini kuingia Afrika Magharibi hasa kwa dawa za viwandani kama heroine, coceine na mandrax na kuongeza kwamba ingawa dawa hizo zinalengwa kupelekwa Ulaya lakini hata nchi za Afrika Mashariki zinaweza kukumbwa na hatari hiyo.
Akizungumza na wahahariri Ikulu hivi karibuni Rais Kikwete alikiri kupokea barua ya majina ya vigogo 58 wa dawa za kulevya iliyoandikwa na vijana 15 wazalendo.
Alisema mbali ya kuyapokea majina pia vyombo vya dola vimeaanza kuyafanyia kazi
Wala rushwa walipewa muda wa kubadili tabia,sasa wazungu wa unga wanaombwa wajisalimishe.This President can't be serious,can he?