SoC03 Hizi ndizo fursa zilizopo vyuo vikuu, enyi wanafunzi wa vyuo vikuu tumieni fursa hizi kutengeneza ajira zenu baada ya chuo

Stories of Change - 2023 Competition

Lidafo

JF-Expert Member
Sep 26, 2019
551
747
Tatizo la ajira nchini linazidi kuwa kubwa na hii ni kutokana na wingi wa wanafunzi wanaohitimu kila mwaka huku serikali ikishindwa kutoa ajira kwa wahitimu wote, Katika kukabiliana na tatizo hili serikali imekuwa ikipendekeza njia ya kujiajiri na sio kusubiri kuajiriwa swali la msingi hapa ni je vipi kijana ataweza kujiajiri na hana mtaji wa kutosha? Kwani kozi nyingi ambazo zinafundishwa vyuoni zinahitaji mtaji mkubwa ili uweze kujiajiri.

Katika kutafakari nimeona kuna fursa kubwa sana ambazo wanafunzi wengi wa vyuo vikuu wanazichezea ama kuzipuuza wanapokuwa vyuoni na endapo wataamua kutumia fursa hizo kisawasawa zitawasaidia kupata ujuzi ambao wanaporudi mtaani hawatahitaji mtaji mkubwa kuanza biashara lakini pia itakuwa ni rahisi kwao kupata ajira.

Fursa zlizopo vyuoni ni pamoja na uwepo wa maktaba, Upatikanaji wa intaneti ya bure, Uwepo wa wahadhiri wa daraja za juu kielimu ,Uwepo wa maabara zenye vitendea kazi, Uwepo wa fani na kozi nyingi zinazotolewa na chuo. Kwa muda ambao mwanafunzi amekaa chuoni anaweza kutumia hayo yote kujitengenezea ajira baada ya kuhitimu mafunzo chuoni.

Niende moja kwa moja kuelezea ni jinsi gani fursa hizo zinaweza kutumika kumtengenezea ajira mwanafunzi wa chuo kikuu kama ifuatavyo:-

1. Mwanafunzi anaweza kupata ujuzi ambao ni tofauti na kozi anayesoma ambao utamsaidia anaporudi mtaani mfano, Mwanafunzi anayesoma shahada ya ualimu au sayansi ya mimea anaweza kutumia muda wake wa ziada kujifunza jinsi ya kutumia programu mbalimbali za komputa kama data base, Microsoft office zote, kuchapa, kutumia barua pepe kibiashara, kujifunza miundo ya picha kwa kutumia adobe illustrator, Photoshoot na programu nyingine nyingi.

Kivipi atatengeneza ajira kupitia ujuzi huo?

Anapo rudi mtaani mwanafunzi huyu asisubiri kuajiriwa bali afanye mpango wa kupata milioni moja na nusu anunue mashine ya kuchapa, kutoa nakala na komputa yake na afungue ofisi ndogo awe anatoa huduma za kuchapa,kutoa nakala, kuunda kadi na matangazo n.k haya yote ataweza kuyafanya yeye mwenywewe hivyo hatakuwa na haja ya kulipa mtu kumfanyia kazi au kwenda tena kujifunza bali tayari atakuwa na ujuzi wake, Lakini kama itashindikana yeye kupata mtaji anaweza kuomba kazi makampuni binafsi na kwakuwa ana sifa za ziada hii itamfanya kujiweka katika nafasi nzuri ya kuajiriwa kulinganisha na wahitimu wengine.


2. Kufanya tafiti na chunguzi mbalimbali na kuandaa miradi kazi Kwa wanafunzi wa kada za sayansi lakini pia kuandaa makala, Machapisho na Uchambuzi wa maswala ya kijamii kwa wanafunzi wa kada za sanaa. Chunguzi ambazo zitapelekea ugunduzi au utatuzi wa changamoto katika jamii jambo hili ni lazima mwanafunzi alifanyie kazi toka mwaka wake wa kwanza chuoni kwa msaada wa wahadhiri wake na wataalamu wa maabara


Kivipi fursa hii itamsaidia kupata ajira?

Katika jamii kuna matatizo mengi sana yanayohitaji ufumbuzi kuna maswala yanahitaji ufumbizi wa kisayansi kama sekta ya kilimo,mifugo na viwanda kuna maswala yanahitaji ufumbuzi kupitia sayansi ya siasa na sanaa ya ustawi wa jamii kama maswala ya kupambana na rushwa , Utawala bora na mengine mengi, Matatizo na changamoto hizo ni fursa kwa mwanafunzi kwakuwa atakuwa ameandaa tafiti na Makala mbalimbali ambazo zimepitiwa na wataalamu chuoni, Huu utakuwa ni muda wake kuwasilisha taarifa zake na kazi zake katika taasisi za uchunguzi na tafiti kama TPRI, TAWIRI,TARI na makampuni binafsi pia anaweza kupeleka mawazo ya kibiashara ikiwa ni mwanafunzi wa masomo ya biashara cha muhimu ni kuwa tafiti, Chunguzi, Mipango kazi na mawazo yote anakuwa ameshayandaa toka akiwa chuoni na hivyo anakuwa anapeleka kitu chenye uhakika kwani anakuwa amekifanyia kazi kwa muda mrefu lakini pia amekipitia vya kutosha hii itamfanya yeye kuajiriwa kama mchambuzi,muelekezaji ama mshauri katika makampuni na taasisi lakini pia itamtengenezea jina na wasifu mzuri na kumuweka sehemu nzuri na anapohitimu chuo anakuwa na pakuanzia.


3. Kuwa karibu na wakufunzi na kuwatumia kuchota maarifa lakini pia kuishi nao vizuri na kwa nidhamu kubwa, Ewe mwanafunzi wa chuo kikuu leo nakuibia siri kuwa kamwe usidharau wakufunzi na wahadhiri wako kumbuka hao ni watu wenye mtandao mkubwa na wanajuana na watu wengi hapo ulipo chuoni upo na maprofesa tena maprofesa kweli, Hao ni mtaji kwako jifunze kupitia wao waheshimu na waombe ushauri pale unapokwama, Kumbuka kufanya hivyo kuna kupa nafasi ya wewe kujifunza mambo mengine tofauti na kozi unayosoma lakini pia wengine hapo ni watu wanamiliki biashara kubwa na wanaendesha miradi mikubwa hapo wapo wahadhiri ni washauri wa serikali ,Wengine ni watu wa vitengo muhimu serikalini hivyo juhudi zako na jitihada zitawafanya wakuangalie kwa jicho la pekee na ukafaidika nao. Wahadhiri wana michongo ya jinsi ya kupata udhamini na ufadhili wa masomo, wanafuatwa na watu wa serikali wapendekeze wanafunzi gani bora ili waingie kufanya kazi muhimu za serikali lakini pia wanaweza kukupa nafasi ya kufanya kazi katika miradi wanayosimamia na kukupendekeza katika kazi mbalilmbali wanazopata hivyo usidharau uwepo wao na kuona hao ni watu wa kupita, Lahasha! hao ni mtaji mkubwa sana kwako.

Mwisho niseme kuwa Kuna kasumba moja ambayo vijana wengi wa chuo wanayo nayo ni kupuuza mambo ya msingi, Uvivu katika kujifunza, Kudharau wahadhiri na kuendekeza mambo yasiyo na msingi jambo hili ndio linalopelekea wanafunzi wengi kulalamika wanaporudi mtaani kwani wanatoka vyuoni wakiwa na uwezo mdogo huku tegemezi kubwa likiwa ni ajira kutoka serikalini, Niwakumbushe kuwa iwe ni serikali au kampuni binafsi wanahitaji mtu aliye na uelewa mkubwa na anaye fanya kazi kwa bidii hivyo jijengee uwezo huo unapokuwa chuoni ii ukija mtaani uwezo huo ukusaidie kupunguza ukali wa maisha na kukuweka sehemu nzuri sana ya wewe kujiajiri ama kuajiriwa. Lakini pia serikali ifanyie kazi tatizo hili la ajira na ije na majibu ni jinsi gani wananchi wataweza kujiajiri lakini serikali yenyewe ndio iwe ya kwanza kutengeneza miradi na kutengeneza mazingira rafiki kwa sekta binafsi ili kuunda ajira nyingi kwa watanzania.
 
Back
Top Bottom