Huduma za Kimataifa za Injili bado ni jambo geni sana katika nchi yetu ya Tanzania kwa sababu tuna Wahubiri wachache sana wa Kimataifa walio na neema ya kufanya Mikutano ya Injili ya malaki ya watu katika nchi nyingine duniani kama ilivyo kwa wahubiri wengine wa Kimataifa kwa mfano, Reinhard Bonnke, Benny Hinn n. k. Kwa sababu hii watu wasioelewa jinsi Huduma hizi zinavyofanya kazi, ndiyo wanaoweza kufikiri kwamba Kanisa la FULL GOSPEL BIBLE FELLOWSHIP limebadili jina na kuwa BISHOP ZACHARY KAKOBE INTERNATIONAL MINISTRIES, kutokana na kukosa uelewa.
Kanisa la FULL GOSPEL BIBLE FELLOWSHIP halijawahi kubadili jina lake wala halitabadili jina lake, na waumini wa FGBF, wote tunajua jambo hili. Hata hivyo ni muhimu kufahamu kwamba wito wa mwasisi wa Kanisa hili, Askofu Mkuu Zachary Kakobe sio kuhubiri Tanzania tu bali kuhubiri kote ulimwenguni. Katika maono hayo, Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship linahubiri Injili Tanzania na kufungua makanisa kote nchini. Hata hivyo katika kuenenda ulimwenguni kote, huko hatuendi kuanzisha Makanisa ya Full Gospel Bible Fellowship kila nchi, kwasababu muda uliosalia kabla ya Yesu kurudi ni mchache mno. Biblia inasema katika WAEBRANIA 10:37, "Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye anakuja, wala hatakawia. " Kwa sababu hii, badala ya kufungua makanisa ya FGBF nchi nyingine ulimwenguni, Mtumishi wa Mungu, Askofu Kakobe hushirikiana na madhehebu yote ya Kiinjili ya nchi hizo katika kuwaleta watu wengi kwa Yesu. Hufanya hivyo, kwa kufanya Mikutano Mikubwa ya Injili, inayokwenda sambamba na Konferensi za Wachungaji, ambao hufundishwa jinsi ya kukuza Makanisa yao, na kuwekewa mikono, ili kuchochea karama zilizomo ndani yao.
Mikutano hii Mikubwa ya Injili, katika baadhi ya nchi hizo, hukusanya makumi elfu elfu ya watu mahali pamoja, kama picha mbili hizi hapa chini zinavyoonesha sehemu ya umati wa watu waliokuwa wakihudhuria kila siku, na pia kukata shauri kuokoka, katika Mkutano alioufanya Askofu Kakobe, Oktoba mwaka jana 2013, huko Congo (DRC), katika Jiji la LUBUMBASHI:
Sasa basi, ni muhimu kufahamu kwamba, ni vigumu kwa Kanisa moja kutoka nje ya nchi kuandaa Mkutano unaoweza kukusanya watu wengi kiasi hiki, katika nchi nyingine. Kwa mfano, Mkutano huu wa Lubumbashi uliandaliwa na Makanisa tofauti zaidi ya 300. Mamia ya Maaskofu na Wachungaji hukusanya nguvu, na kuunda kamati mbalimbali za maandalizi. Mambo mengi huhitajika kufanikisha Mkutano wa Injili kama huu, ikiwemo upatikanaji wa maelfu ya Wahudumu, kutoka katika mamia ya Makanisa.
Ni muhimu pia kufahamu kwamba, kama Mhubiri atakwenda katika Jiji fulani, lililoko nchi fulani, kwa jina la dhehebu au Kanisa lake, kwa mfano FULL GOSPEL BIBLE FELLOWSHIP, halafu akataka mamia ya Maaskofu na Wachungaji pamoja na Makanisa au madhehebu yao tofauti tofauti, kumpa ushirikiano kuandaa Mkutano Mkubwa wa Injili, ni vigumu kwa Watumishi hao kumpa ushirikiano. Hofu yao kubwa, huwa ni Mhubiri huyo kutaka kuanzisha Kanisa lake katika mji huo, kwa kutumia mgongo wa Watumishi hao wa Mungu, na Makanisa yao. Mamia ya Makanisa, huwa tayari tu kumpokea Mhubiri kama watajua kwamba siyo tu karama mbalimbali hutenda kazi ndani yake, bali pia Mhubiri atahakikisha kwamba haendi huko kuanzisha Kanisa, bali anakwenda kuyasaidia Makanisa yao kuimarika, na kwamba waumini wapya katika Mkutano huo, watajiunga na Makanisa yao. Watumishi wa Mungu, hupenda kuipokea huduma ya yeye Mhubiri kama yeye tu, na siyo Kanisa au dhehebu lake.
Kwa sababu hiyo, kote ulimwenguni, Wahubiri wakubwa wa Kimataifa, huenda wao kama wao, kuhubiri katika nchi nyingine, na hawaendi huko kwa jina la Makanisa au madhehebu yao, ili wakubalike kwa Wachungaji wa madhehebu yote. Kwa mfano, Mhubiri wa Kimataifa kutoka Marekani, BENNY HINN, ni Mchungaji wa Kanisa lake linaloitwa WORLD HEALING CENTER CHURCH, lakini anapoenda kuhubiri ulimwenguni, haendi kwa jina la Kanisa lake, bali huenda kwa huduma ya yeye kama yeye, BENNY HINN MINISTRIES. Asipofanya hivyo, hawezi kupewa ushirikiano na Watumishi wa madhehebu tofauti. Vilevile Mhubiri mwingine wa Kimataifa kutoka Marekani, ERNEST ANGLEY, huyu ni Mchungaji wa Kanisa lale la GRACE CATHEDRAL, lakini anapoenda ulimwenguni kote kuhubiri, huenda kwa huduma ya yeye Mhubiri kama yeye, ERNEST ANGLEY MINISTRIES, ili apokewe na madhehebu yote, n.k. Miezi michache iliyopita alikuja Tanzania, Mhubiri wa Kimataifa, REINHARD BONNKE. Huyu naye hakuja kama Kanisa, angefanya hivyo, isingekuwa rahisi kukubalika kwa madhehebu yote. Wahubiri wa Kimataifa kote duniani, hufanya hivihivi.
Kwa msingi huu sasa, Askofu Kakobe anapokwenda kuhubiri kote ulimwenguni, mbali na Tanzania, huenda kwa huduma ya yeye Mhubiri, kama yeye, BISHOP ZACHARY KAKOBE INTERNATIONAL MINISTRIES. Likienda kama Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, haliwezi kupokelewa na madhehebu mengi tofauti. Yadhuru nini, hatuko hapa kujenga ufalme wa dhehebu, bali Ufalme wa Mungu. Furaha yetu ni kuona wengi wanampokea Yesu kila mahali duniani, na wengi wakiongezeka katika Ufalme wa Mungu. Huduma ya BISHOP ZACHARY KAKOBE INTERNATIONAL MINISTRIES imesajiliwa Marekani na pia Canada. Kutokana na sheria za nchi hizo, mambo mengi ya Injili hayawezi kufanyika mpaka huduma husika ya Injili iwe inatambulika kwao kisheria. Nchi hizo, na hata nchi nyingi nyingine zilizoendelea, huwa ni vigumu kuipokea huduma iliyosajiliwa katika nchi za Afrika, kwa sababu huidharau Afrika, na kujiona wao ndiyo watawala wa dunia. Unaweza kupata mengi zaidi kuhusu utendaji wa huduma ya BISHOP ZACHARY KAKOBE INTERNATIONAL MINISTRIES, kwa kutembelea
http://www.bishopzacharykakobe.org