Hongera serikali kwa kuitosa Dowans
2009-03-16; 10:24:26
Na Mwandishi Wetu
Baadhi ya wabunge waliokuwa wajumbe katika Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mchakato wa utoaji wa zabuni ya kufua umeme wa dharura kwa Kampuni ya Richmond, wameipongeza serikali kuachana na mpango wa kununua mitambo ya kufua umeme ya Kampuni ya Dowans.
Mbunge wa Nzega CCM, Lucas Selelii, amesema anapongeza uamuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kujitoa katika ununuzi wa mitambo ya kufua umeme ya Dowans kwa sababu ilikuwa ni kashfa kubwa.
Alisema iwapo matakwa ya kununua mitambo hiyo yangetekelezwa, kitendo hicho kingeleta picha mbaya.
Alisema Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPRA) ya mwaka 2004 hairuhusu kununua vifaa, mitambo au mashine ambazo zimekwishatumika, hivyo, kufanya uamuzi tofauti na sheria hiyo ni sawa na kuhalalisha kashfa.
Selelii, hata hivyo, alisema serikali inaweza kukodi mitambo iliyokwishatumika lakini sio kuinunua.
Alisema uamuzi huo ni wa busara na umechukuliwa kwa ujasiri hivyo ni vema kama utaendelea kuwa thabiti.
Akifafanua azma ya kununua mitambo hiyo na ile ya kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Selelii alisema kuna tofauti kubwa kati yake.
Alisema uamuzi wa kununua mitambo ya IPTL uliridhiwa na Bunge wakati uamuzi wa kununua mitambo ya Dowans ulikuwa ni wa watu binafsi na wa siri.
``Nia hiyo ilikuwa ni ya mtu binafsi, haikuridhiwa na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na wala Bunge lenyewe, lakini uamuzi wa kununuliwa kwa mitambo ya IPTL uliridhiwa na Bunge,`` alisema na kuongeza kwamba IPTL tayari ilikuwa inauza umeme wake kwa Tanesco kwa bei mbaya na nia ya kununua mitambo yake ilikuwa na lengo la kupunguza `maumivu`.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum, Stella Manyanya, alipongeza hatua hiyo akisema: ``Naunga mkono serikali kujitoa katika ununuzi wa mitambo hiyo, kinachotakiwa sasa ni kuzingatia hatua mbalimbali zilizoainishwa na Waziri Ngeleja mwishoni mwa wiki za kuhakikisha kwamba nchi inapata umeme wa kutosha... Taifa lina vyanzo vingi vya umeme, hivyo, vizingatiwe,`` alisema.
Manyanya alisema hoja ya mitambo ya Dowans imemchosha na asingependa kuizungumzia mara kwa mara na badala yake aliwataka wadau na wajasiriamali mbalimbali, hasa wa ndani, kujitokeza kwa wingi kuwekeza katika sekta ya umeme.
Alisema wadau hao wakiwa kama makampuni au watu binafsi, wanayo nafasi kubwa ya kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo vingi vya umeme vilivyopo nchini na kuwauzia wananchi moja kwa moja, badala ya kila mmoja kutaka kuuza umeme wake kwa Tanesco.
Alisema kwa kufanya hivyo, kutakuwa na ushindani katika utoaji wa huduma hiyo na kuleta ushindani unaowiana kama ilivyo katika makampuni ya simu nchini.
Alisema kujitokeza kwa wajasiriamali wengi katika huduma ya umeme kutaondoa ukiritimba wa muda mrefu wa kutegemea shirika moja tu kuzalisha na kusambaza umeme, hali ambayo inasababisha kuleta ugumu katika kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri Ngeleja, alitangaza uamuzi wa serikali wa kujitoa katika ununuzi wa mitambo hiyo, uamuzi ambao ulitangazwa siku kadhaa baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Dk. Idris Rashid, kutangaza kuwa shirika hilo limeamua kuachana na ununuzi wa mitambo hiyo.
Wakati Dk. Idris akitangaza uamuzi wa Tanesco kusitisha mpango wake, alitishia kuwa nchi itaingia gizani na kusema kuwa Tanesco isije kulaumiwa.
Hata hivyo, Ngeleja alipinga madai ya mtendaji huyo mkuu wa Tanesco kuwa nchi itaingia gizani.
SOURCE: Nipashe