[TABLE="class: contentpaneopen"]
[TR]
[TD="class: buttonheading, width: 100%, align: right"]
[/TD]
[/TR]
[/TABLE]
[TABLE="class: contentpaneopen"]
[TR]
[TD="class: createdate"] Sunday, 15 July 2012 10:00
[/TD]
[/TR]
[TR]
[TD] 0digg
Salma Said, Zanzibar
SERIKALI bado inaendelea kufanya juhudi za kuwashawishi viongozi wa dini na makundi mengine yaliyotishia kususia zoezi la sensa ili kufikia muafaka kabla ya zoezi hilo kufanyika Agosti 26 mwaka huu.
Hayo yamebainika wakati wa mafunzo ya siku tatu ya sensa kwa waandishi wa habari waandamizi na wahariri waliopo Zanzibar ambapo walipata mwelekeo wa sensa hiyo.
Wawezeshaji kutoka ofisi ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar waliwaeleza waandishi wa habari kuwa makundi hasa ya kidini ikiwemo Uamsho hawajapuuzwa na viongozi wa Serikali pamoja na ofisi ya mtakwimu wamekuwa wakifanya juhudi za mara kwa mara kufanya mazungumzo.
Sensa ni muhimu na tunataka kila mtu ahesabiwe, kwa hiyo viongozi wetu wanaendelea na kuwashawishi viongozi wa dini wanaosusia wasifanye hivyo, alisema Mayasa Mahfoudh ambaye ni ofisa mwandamizi wa katika ofisi hiyo ya mtakwimu.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Mohammed Hafidh alisema waandishi wa habari wana mchango mkubwa wa kuhakikisha kwamba sensa ya mwaka huu inafanikiwa kwa kiwango kikubwa.
Tuna changamoto katika kufikia siku ya sensa yenyewe, lakini kwa kushirikiana na wananchi, viongozi katika ngazi zote pamoja na waandishi wa habari tunaweza kufikia malengo na kumfanya kila mtu ashiriki, alisema katika hoteli ya Chavda iliyopo Mji Mkongwe.
Aidha, Hafidh aliwaambia waandishi kwamba maandalizi kwa upande wa Zanzibar yamefikia katika kiwango cha kuridhisha ikiwemo ramani na kuainisha vituo 3,074 vya kuhesabiwa watu.
Alisema changamoto kubwa ni kuhakikisha kwamba wananchi wote wanakuwa na elimu na muamko juu ya umuhimu wa sensa nchini.
Washiriki wa mafunzo hayo kutoka vyombo vya habari mbalimbali walionesha wasiwasi wao juu ya tamko la viongozi wa dini kutoka bara na Zanzibar likiwataka wafuasi wa dini wasusie zoezi hilo.
Walisema tamko hilo linaweza kuleta athari kubwa katika zoezi hilo iwapo viongozi wa Serikali watalipuuza na kushauri umuhimu wa pande mbili hizo kukutana na kukubaliana kwa pamoja ili lengo la sensa litimie.
Ofisa Habari wa Sensa Zanzibar, Salama Njani alitoa wito kwa Vyombo vya Habari kutenga muda na nafasi ya kutoa elimu kwa wananchi licha ya kuwepo upungufu wa fedha za kulipia matangazo katika vyombo hivyo.
Alisema ni wajibu kwa waandishi wa habari kujitolea zaidi kusaidia taifa kwa sababu sensa inalenga katika kuleta maendeleo kwa wananchi. [/TD]
[/TR]
[/TABLE]