Kwa wote mtaopata nafasi ya kusoma mawazo yangu,
Bakwata na Basuta wamekosea kwa kweli na hata kama wangekuwa na nia nzuri wangetakiwa watumie hekima. Mojawapo ya sifa kuu ya kuwa kiongozi ni kuwa na hekima na hasa unapo react kwa habari uliyoisikia kutoka upande mmoja. Viongozi wa dini wana jukumu kubwa la kuunganisha jamii lakini kwa muda fulani sasa wamekubali kutumika na wanasiasa kuigawa jamii. Kilichotekea kwa Bakwata na Basuta ni mkokotoo wa madhara ya kampeni za uchaguzi uliopita. Hii kutu haijawatoka viongozi wengi wa dini. Kwa nini viongozi wanatakiwa kutumia hekima hasa kwa kesi hii ya Igunga? Sababu zangu ni hizi zifuatazo:
1. Tukio la mkuu wa wilaya ni tukio la taharuki (chukulia kweli huyu mama alivuliwa hijabu/kilemba/kitambaa/mtandio). Sidhani kuwa watu walioenda pale walienda kwa madhumuni yaliyopangwa (contemplated) kwamba wanaenda kumvua kilemba mwanamke muislamu ili wamdharilishe.
2. Katika matukio ya rabsha/vurugu/hasira/kupambana (kutegemea sababu iliyowafanya wananchi wale waende kumkamata) kitu chochote kinaweza kutokea saa zingine hata kuumia au kupoteza maisha. Huwezi kuhitimisha kuwa wahusika walidhamiria kufanya hayo matokeo. Polisi wanaposhughulikia uhalifu mambo mengi hutokea kupoteza mali, majeruhi au hata vifo. Nivigumu sana kuwatuhumu moja kwa moja kwamba walienda kufanya kile kilichotokea.
3. Sasa hivi Igunga ni wakati wa uchaguzi na hali ya mambo ni tete. Vyama vyote vinavogombania vina wafuasi wa dini mbalimbali ikiwemo na dini yetu ya Uislamu. Makosa yanaweza kutendwa na tasisi, jamii, kikundi au mtu mmoja mmoja. Ndiyo maana hata mahakamani kwa kesi hii wamepelekwa watu kama mtu mmoja mmoja na siyo chama. Kama kweli itadhihirika pasipo shaka yoyote kwamba walitenda makosa hayo basi watahukumiwa kama mtu na siyo chama. Makosa yoyote hutendwa na watu wowote ndiyo maana magereza, polisi, mahakama hakuna dini.
4.Unapotoa tamko kwamba Bakwata na Basuta watawaambia waislamu wote wakiadhibu Chadema ni upotokaji mkubwa wa maadili ya dini. Kabla ya kutoa tamko kama hilo ilitakiwa hekima tu ya kuwaita viongozi wa chama hicho na kuongea nao kupata undani upande wao badala ya kutoa tamko lenye mrengo wa kisiasa na kupendelea chama kingine. Viongozi wa dini wanatakiwa kutenda haki na si kuchukua ushabiki wa kimakundi. Kiimani na kiroho kuwaadhibu chadema (nadhani wana maana waislamu tu tusikipigie kura) kwa sababu ambayo haina uthibisho wa kiroho kuna tija gani kwetu waislamu?
5. Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala ana vipomo vikali kuliko sie wanadamu. Na Yeye huona tofauti kuliko sisi wanadamu na kwa hivyo kwa imani yetu Mungu anajua kwa bayana Yule mama alikuwa anafanya nini pale hata kama atakuja na hadithi ya kuficha. Masheikh wetu hawana undani wa siri ya kile alichokuwa akikitenda pale wengine tunatia shaka tu lakina kwa hakika Maulana anajua nini mama yule alikuwa akikifanya pale. Nina mashaka sana na hukumu ya Maimamu wetu inaweza isiwe hukuma ya Mungu. Na kama hawana uhakika kwa nini basi kujiingiza matatizoni na kuwatia doa ambalo lingeweza kuepukwa?
6. Kama kweli Bakwata na Basuta wana nia isiyo ya kisiasa na ya kutowagawa wananchi kufuata dini zao, kwa nini tamko lao lisingewasihi watu wote bila kujali itikadi zao wakiadhibu Chadema? Je nikisema kwamba wanatumiwa na na chama fulani kukisafishia njia nitakuwa nakosea? Ndugu Nape Nnauye kwenye tamko lake juzi aliweka mbele sana habari ya hijabu waislamu wenye hekima tukajua nini kinachotafutwa hapa na CCM wanafurahi sana Bakwata na Basuta wameichukua hiyo agenda.
7. Viongozi wa Bakwata na Basuta, kama Waislamu wote tutakubali maelekezo yenu tusikipigie kura Chadema na kila mmoja wetu akatii, je tuna hakika nani atashinda kwenye uchaguzi ule? Je, waumini wa dini zingine wakiamua vinginevyo itakuwaje? Je Taswira kwa taifa zima itakuwaje siku za usoni?
Mwisho nawasihi tena viongozi wetu wa dini tuwe na hekima kushughulikia mambo tete kwenye jamii badala ya kusukumwa na jazba za makundi fulani fulani. Tutailinda jamii, na tutaheshimika na viongozi wa kisiasa pia. Viongozi wa siasa nao wawe makini kutowaingiza viongozi wa dini kwenye mirengo ya kisiasa. Tishio walilolitoa Bakwata na Basuta si jambo la kuchekelea hata kidogo, linalenga kubomoa jamii na kuimarisha/kupanua ufa wa udini ambao kwa sasa unaendelea kwenda kina zaidi. Tumwombe Mungu alinusuru taifa hili.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Libya.