Vita ya ma-DAS, ma-DC yaichefua Serikali

Oldmantz

JF-Expert Member
Jan 24, 2023
430
996
Dodoma. Ungedhani baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuwaonya wateule wake kuhusu kuendekeza migogoro kazini, hali hiyo pengine ingekoma. Lakini hali sivyo ilivyo.

Migogoro isiyokwisha ya makatibu tawala wa wilaya na wakuu wa wilaya kwa baadhi ya wilaya nchini, imeibua hasira ya Serikali iliyotoa onyo la mwisho kwa watakaobainika kuendeleza hali hiyo.
Hali ya kuwapo kwa migogoro hiyo ambayo viongozi wa juu serikalini wamekuwa wakiikemea mara kwa mara, ilibainishwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Angellah Kairuki wakati wa mafunzo ya siku tatu kwa makatibu tawala wa wilaya zote za Tanzania Bara jijini Dodoma.

Alisema kuna migogoro na kesi nyingi ambazo amekuwa akisuluhisha kwa vigogo hao wa wilaya.
Kairuki alisema uvumilivu na kuwanyamazia sasa itakuwa basi na kwamba kuanzia sasa watakaobainika, watapelekwa kwa mamlaka ya uteuzi kwa uamuzi.

Rais Samia Juni 6, 2023 alifanya uteuzi wa makatibu tawala wapya 72, na kuwabadilisha vituo vya kazi 51 na 11 kuachwa katika vituo vyao vya kazi. Akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu, Kairuki alisema baadhi ya makatibu hao ama kwa makusudi au kutojua, wamekuwa wakianzisha mivutano na wakuu wa wilaya kwa kisingizio kuwa na wao ni wateule wa Rais.

"Kuanzia sasa watakaoshindwa kubadilika, nasema kuwa siwezi kuwavumilia, tutakwenda kushauriana na mamlaka zilizowateua. Tumechoka kusuluhisha migogoro yenu, tunaangalia akaunti zenu kwenye mitandao pia hamfanani kama viongozi, kwani mnazungumza vitu vya ajabu kabisa, maadili na tabia lazima ziakisi nafasi zenu," alisema Kairuki.

Waziri huyo alisema mara nyingi anatembelea akaunti za viongozi na kile anachokutana nacho siyo mambo ya maendeleo, bali kila wakati anaona wanavyoendeleza malumbano yasiyokuwa na msingi mzuri wa kimaendeleo na ndiyo maana waliamua kuwaita ili wawape mafunzo.

Kingine aliwaagiza kwenda kufanya kazi ya maofisa masuhuli wakisimamia kila mchango utakaokuwa unaingia au kutoka kwenye halmashauri ili wawe na taarifa sahihi za kila kinachoendelea.

Migogoro ya watendaji
Kauli ya Waziri Kairuki imekuja zikiwa zimepita wiki mbili tangu Rais Samia alipoeleza sababu ya kutengua uteuzi wa aliyekuwa Kabidhi Wasii Mkuu, Angela Anatory na kumteua Frank Kanyusi, akisema ni ugomvi usiokwisha ulioshusha utendaji kazi katika ofisi ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).

Pia Rais Samia alimteua Irene Lesulie kuwa Naibu Kabidhi Wasii Mkuu, akichukua nafasi ya Lina Sanga.
“Kabidhi Wasii Mkuu na naibu wako nimewateua baada ya kuwaondoa viongozi wote wawili waliokuwepo pale, nilikuwa nategemea wananchi wapate huduma za kuridhisha ndani ya ile ofisi, lakini kilichokuwa kinatokea ilikuwa ni ugomvi.

“Nikasema labda kwa kuwa wote walikuwa kinamama ndiyo maana kulikuwa na ugomvi mkubwa, lakini ukiangalia kwa ndani kulikuwa na kutokutekelezeka kwa kazi vizuri, mwingine akisema huyu anakasirika, mwingine akirekebisha mwingine anachafua, kwa hiyo nikaamua kuwaondoa wote wawili watapangiwa kazi nyingine, sasa nendeni ninyi,” Rais aliwaagiza wateule wapya.

Ugomvi wa wateule wa Rais katika halmashauri pia ulijitokeza katika utawala wa awamu ya tano na miongoni mwao ni ule wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, Sada Malunde na aliyekuwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Wende Ng’ahara.

Akiwa ziarani Mkoa wa Kagera Februari 20, 2019, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwataka wamalize tofauti zao.

“Mkurugenzi unagombana na DC wako, DAS nawe umeingia kwenye mgogoro, mnagombana mpaka mnatumiana uchawi,” alisema.

“Mmeanza kuhama na ofisi, mtakimbia wilaya. Mnagombana nini? Ninyi viongozi mnashindwa kukaa na kumaliza mambo hayo? Ninazo habari zote za migogoro yenu, halafu mnagombana wakubwa, wadogo wapo wanaangalia, ni vituko, badilikeni.”

Hata aliyekuwa Rais wakati huo, hayati John Magufuli aliwahi kuzungumzia migogoro kwa viongozi aliowateua akitaja mmojawapo uliokuwa wilayani Gairo alikosema kulikuwa na sintofahamu ya vigogo wake.
“Pale Dodoma, mkurugenzi wa jiji na DC walikuwa wanagombana, nika-send message (nikatuma ujumbe) kwamba ‘endeleeni kugombana tu, mtagombania vijijini siku moja. Wamenyamaza naona yameisha,” alisema Rais akiutaja mgogoro mwingine.

Alichosema Majaliwa
Katika hatua nyingine, akifungua mafunzo hayo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikiri kuna baadhi ya watendaji hao wa wilaya, wanafanya vitu ambavyo Serikali isingetamani kuona vikifanyika na wengi wao wanatumia muda mwingi kwenye mitandao.

Majaliwa alisema suala la migogoro na wakuu wa wilaya na watendaji wengine katika halmashauri wanazoziongoza, ni jambo linalotia aibu kwa watu wanaotegemewa kama hao.
Waziri Mkuu alisema nafasi ya katibu tawala ni kubwa isipokuwa wengi wanashindwa kutambua wadhifa huo na kuwa chanzo cha migongano na viongozi wengine.

Alisema ni lazima kuwe na mabadiliko hasa kwa waliopata nafasi ya kushiriki kwenye mafunzo, ili waendane na uhalisia wa watumishi wao na kuonyesha njia kwa wengine wapate kuwaiga.

"Kikubwa muwe watu wa kutunza siri na nyaraka za Serikali, haiwezekani mpo halafu tunaona kila wakati mnashinda kwenye mitandao bila faida, pale mlipo sisi tupo, tunawaona. Wekeni kifuani baadhi ya mambo mnayokutana nayo kwenye kamati za ulinzi ambako mnasaidiana na DSO (Ofisa Usalama wa wilaya).”
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, ni aibu kiongozi wa ngazi ya katibu tawala kujisifu kuwa anafanya kazi wakati anashindwa kusimamia hata watumishi na wananchi, ikiwemo kutomaliza migogoro angalau ya mipaka ya vijiji.

Agizo kwa ma- Das
Katika hatua nyingine Majaliwa aliagiza matumizi ya masurufu yanayopelekwa kwenye halmashauri, makatibu tawala hao wajitahidi kujua kila shilingi imefanya nini na kama kuna mchango watambue wilaya au halmashauri imeingiza kiasi gani.

Aliwaagiza kwenda kusimamia vyama vya siasa bila kupeleka migogoro, wabebe ajenda za kitaifa wakati wote, kujenga uhusiano mzuri na watendaji wao na migogoro yao isitoke nje ya kuta za majengo yao.
“Usijipendekeze viti vya mbele, andaa mazingira mkuu wa wilaya aketi kwanza ndipo nawe ukae, lakini heshimuni maamuzi ya viongozi. Tuna mfano wa mkuu wa wilaya hapo Kilimanjaro aliipiga marufuku moja ya taasisi kutokana na mafundisho yake kuwa kinyume na maadili yetu, lakini wakawabeba watumishi kwenda kuwafunda Zanzibar, katibu tawala asijue wanachofanya watumishi wake,” alisema.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene alisema mafunzo kwa makatibu tawala hao, yatakuwa na tija kwa sababu yatapeleka mchango wa uwajibikaji kwenye nafasi walionazo.

Simbachawene alisema Serikali imekuwa na imani kubwa kwa makatibu tawala katika kutafsiri maana halisi ya Serikali za Mitaa na Serikali Kuu, hivyo wanapaswa kuwa ni watu wa kujifunza wakati wote.

Aliwataka washiriki kwenye mafunzo hayo kujiamini, kwani watakwenda kufanya kazi iliyotukuka, huku wakitimiza dhamira ya aliyewateua katika nafasi hiyo ambaye ni Rais.

CREDIT: MWANANCHI
 
Back
Top Bottom