Richard
JF-Expert Member
- Oct 23, 2006
- 14,939
- 20,400
Naam, ni DP World Luanda Port.
Bandari ya Luanda ni moja ya bandari kubwa nchini Angola kati ya bandari zake zikiwemo za Lobito na Benguela ambazo zipo pembezoni mwa bahari ya Atlantic.
Lakini serikali ya Angola kwa kuona ufanisi mdogo uso na tija kwa uchumi wake ikaamua kutafuta mzabuni ambae ataendesha shughuli za khasa makontena katika bandari ya Luanda ili kuleta tija zaidi na manufaa makubwa ya kiuchumi. Ikaunda kamisheni ambayo itasimamia utekelezaji wa mpango wa kubinafsisha shughuli za bandari na pia kusimamia shughuli zinofanywa na mzabuni DP World kwenye kitengo cha makontena.
Lakini serikali hiyo imeweka masharti yake kwa mzabuni yoyote atakaeshinda na moja ya masharti hayo ni mzabuni kuendesha shughuli zake za usimamizi wa shughuli za makontena kwa miaka 20. Ikifika miaka 20 kama kuna uwezekano wa kuendelea na mkataba basi mkataba utapitiwa upya na mzabuni atapitishwa kuendesha shughuli zake bandarini hapo kwa miaka mingine.
Hatua hii ni sawa na ile ya kubinafsisha bandari ya Lobito kwa wawezekezaji wa ndani na nje kitendo kinoitwa "concession" na benki iitwayo Eagle Stone ya uwezekezaji pamoja na Benki ya Dunia ndo wamekuwa washauri wakuu wa namna ya kurekebisha uchumi wa Angola kwa kuanza na bandari kama hii ya Lobito na ile ya Luanda.
Nifafanue kidogo kuhusu neno "Concession" yaani makubaliano kwamba kwa mfano weye una duka kubwa la bidhaa mbalimbali yaani "departmental store" lakini wakaribisha wauzaji wengine wenye aina zingine za bidhaa tofauti zenye nembo mbalimbali ndani ya duka lako. Wauzaji hawa wengine ambao si waajiriwa wako wao hupanga tu ndani ya duka lako na weye waruhusu wao kujenga duka lao watakavyo ndani humo na kuuza bidhaa zao humo, kuajiri watu wawatakao na pia kufanya mambo yao wanavyoona wao kwa makubaliano ya kukulipa kamisheni inotokana na faida ya mauzo ya bidhaa zao.
Hivyo hapo serikali ya Angola bado ni mmiliki wa bandari zote za Angola lakini imeachia baadhi ya shughuli khasa za kuhusu usimamizi wa makontena ziendeshwe na wabia na makampuni binafsi hususan katika bandari yake ya Luanda ni kampuni ya DP World imeshinda zabuni na sasa ndo yaendesha bandari ya Luanda.
DP World sasa wasimamia kitengo cha makontena cha MPT (multi purpose terminal) na walianza kazi rasmi tarehe 1 March 2021. Bwana Franscisco Pinzon raia wa Panama ndie alieteuliwa na DP world kuongoza MPT akiwa na uzoefu wa miaka 20 katika shughuli za uendeshaji wa bandari na uongozi wake.
Akitoa taarifa ya shughuli za DP world kuanza kazi katika kitengo cha makontena bandarini hapo, afisa mtendaji mkuu na mkurugenzi mwendeshaji bwana Suhail Al Banna amesema DP world wana furaha kuwa nchini Angola na kuendeleza kitengo cha makontena bandarini hapo ili kusaidia kukuza uchumi wa Angola.
Hapa ningependa zaidi msaada wa wanasheria katika kufafanua maana ya maneno yafuatayo: Memorandum of understanding, contract, agreement in principal na agreement. Kisha tufananishe au kulinganisha maneno haya na hili neno "Concession", kwa maana kwamba DP World wamekubaliana na serikali ya Angola kupata uwezo kuendesha shughuli za makontena katika bandari ya Luanda na pia kukifanya kitengo hicho kiwe kitovu cha biashara katika ukanda wa kusini magharibi mwa Afrika.
DP World starts operations of multipurpose terminal at Port of Luanda
Luanda, Angola,
01
March
2021
“
Suhail Al Banna, CEO and Managing Director of DP World Middle East and Africa.We are proud to be in Angola to further develop the terminal as a trade hub in the southern west Africa region, which will support the country’s economic growth objectives by attracting further investment and increased trade.
Serikali ya Angola iliweka ushindani huo wa wazabuni na makampuni kadhaa ya kimataifa yakiwemo kama vile kampuni za Multipaques, Advanced Maritime Transport na China Harbour Engineering Company zilishiriki kupigania zabuni hiyo. Tume maalum ya kutathmini wagombea wa zabuni ambayo iliundwa rasmi na wizara ya masuala ya usafirishaji katika mpango wake uitwao Master Plan, ilikuja na uamuzi kwamba DP World ndo wenye sifa zinofaa na wapewe zabuni.
Sio siri, DP World ni kampuni kubwa yenye uwezo mkubwa na uzoefu wa kazi za kushughulikia makontena yapatayo milioni 70 kwa mwaka. Pia DP World inaweza kulipa kwa mwangalizi (Serikali ya Angola) kiasi cha dola milioni 440 kwa mwaka huku dolali zingine milioni 150 zikilipwa wakati wa utiaji saini na kabla kazi haijaanza!, yaani kwa lugha ingine "Kifunga Uchumba!"
Kwahiyo tumejifunza nini hapo?
Kwanza, tumejifunza kwamba serikali ya Angola bado ni mmiliki wa bandari zote za Angola na imeingia makubaliano na kampuni ya DP World kuendesha shughuli za makontena tu na si vinginevyo katika bandari ya Luanda.
Pili, serikali ya Angola iliweka ushindanishi wa zabuni kwa makampuni mbalimbali yakiwemo ya kimataifa yalotaka kufanya kazi katika bandari ya Luanda. Zabuni hiyo ilitangazwa mwezi December 2019 na DP world ikaja tangazwa kuwa imeshinda zabuni hiyo mapema mwaka 2020. Jambo hilo laonyesha wazi kwamba serikali iliweka jambo hilo wazi na kujulikana wazi kwamba si siri.
Tatu, Serikali ya Angola kupitia wizara ya usafirishaji iliunda tume maalum ya kutathmini zoezi zima la kutafuta wazabuni na kuweka ushindanishi. Hilo pia linalinda heshima kwa serikali (integrity) na imani kwa wnaanchi wake na pia kuonyesha kwamba serikali yajali raia wake na imeweka mbele maslahi ya nchi zikiwemo mali za taifa.
Tumeambiwa kwamba mazungumzo ya mkataba huu yalianza tangia mwaka 2019 hivyo kuwa sawa kabisa na wenzetu wa Angola katika mahckato mzima, je ni wapi tulikwama katika kuhakikisha kunakuwepo ushindanishi wa kupata mzabuni? Au je, kuna tume yoyote iloundwa chini ya wizara ya biashara na viwanda au wizara ya ujenzi au usafirishaji ilohakikisha kuwa kuna uwazi /openness) katika hili na kutathmini mchakato mzima wa kumpata mzabuni?
Je, hili suala ni la kulipeleka Bungeni kwa kuidhinisha tu (rubber stamp) bila kuzingatia maoni ya wananchi au uwepo wa tume hiyo ambayo ingekuwa ikifanya kazi yake kwa niaba wananchi na maslahi ya taifa kwa ujumla?
Je, ni kwanini tumechukua hatua tulizochukua ambazo ni tofauti na hatua ambazo wenzetu na waafrika wenzetu serikali ya Angola imechukua? Je kwanini tusiombe ushauri wa ndugu zetu Angola kwenye hili ili tupate mawazo mazuri ya namna ya kumpata mzabuni hata kama ni DP World kwa kutumia njia sahihi?
Naomba nimalizie kwa kusema yafuatayo:
Hii nchi ni yetu sote na kila maamuzi ambayo serikali yachukua yawahusu watanzania wote na kizazi kijacho, hivyo serikali inawajibika kwa hatua zozote zinohusu maslahi ya taifa hili.
Pia serikali isidharau kauli, ushauri na mijadala mbalimbali kuhusu jambo hili kwani ni fukuto kubwa sana ndani ya mioyo ya watanzania ambao wanazo video zote zinohusu suala la bandari tangia mchakato wake uanze.
Na mwisho, serikali isitishe kuwatumia baadhi ya watu inaoamini kuwa wana ushawishi (influence) kwa jamii hivyo kuweza kusawazisha mambo na kuyapitisha malengo yake yenye kasoro nyingi. Watu hawa ni kweli wana nguvu kubwa ya ushawishi iwe kwenye mitandao ya kijamii, vituo vya redio au televisheni, lakini baadhi yao wamekosa weledi, uwezo wa kufikiri kwa kina na ni waendekezaji mizaha.
Suala linohusu maslahi ya taifa halihitaji mizaha.
Vyanzo vilivyochangia mada hii: Trifigura, DP World Luanda Port, Maritime Institute na vyombo kadhaa vya habari.