Leo nimekuja across na hii article nikaona niiweke hapa, kama ilishawekwa then samahanini !!
KUNA msemo usemao kuwa ukitaka kumfahamu mtu mwangalie marafiki zake. Wengine wanasema, ndege wenye manyoya yanayofanana huruka pamoja. Naam, wako wasemao Waarabu wa Pemba hujuana kwa vilemba.
Siku ya Alhamisi tarehe 15 Machi 2007, Rais Jakaya Kikwete alifanya ziara ya siku moja nchini Zimbabwe. Taarifa zilizotolewa na Ikulu sambamba na vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa, vilithibitisha kuwa ziara hiyo ya rais ilikuwa ni kwa nafasi yake kama Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa nchi za Jumuia ya SADC. Pamoja na Tanzania, katika kamati hii, zipo nchi za Namibia na Lesotho.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, azma kuu ya msingi ya ziara hii, ni sehemu ya jitihada za Rais Kikwete kumaliza mgogoro wa kisiasa nchini Zimbabwe, kati ya Rais Robert Mugabe na chama chake cha ZANU-PF kwa upande mmoja na vyama vya upinzani vikishirikiana na wadau mbalimbali wa harakati za haki za binadamu kwa upande wa pili. Baadhi ya vyombo vya habari vimemnukuu Rais Kikwete akisema kuwa, sehemu ya mazungumzo hayo, yalikuwa kumfahamisha Rais Mugabe jinsi suala la nchi hiyo lilivyojitokeza kwenye mazungumzo yake na viongozi wa nchi kadhaa za Ulaya, wakati wa ziara yake katika nchi mbalimbali za Jumuia ya Ulaya, hivi karibuni.
Habari zaidi ambazo hazikutolewa na ofisi ya rais kwa vyombo vya habari, zinaeleza kuwa, ziara ya rais Zimbabwe ilitanguliwa na ziara ya Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa nchini Tanzania, Rashid Othman.
Inasemakana, Othman alifanya mazungumzo na wakuu mbalimbali wa vitengo vya usalama nchini humo. Alizungumza vilevile na viongozi wa serikali. Jambo hasa walilojadili, bado halijawekwa bayana.
Kitendo cha mkurugenzi wetu wa usalama wa taifa kutembelea Zimbabwe na kufanya mazungumzo na maofisa wa idara nyeti kabla ya ziara ya rais, pamoja na mambo mengine, inathibitisha ukaribu wa kikazi baina ya Serikali ya Tanzania na utawala ulioua maelfu na bado unawatesa mamilioni ya Wazimbabwe. Mara baada ya mazungumzo ya marais hawa, yanayosemekana kuchukua saa tano, kila mmoja kwa upande wake alizungumza na vyombo vya habari.
Rais Kikwete hakutaka kutoa taarifa yoyote ya kina ila alisema: Tumekubaliana mambo mengi namna ya kwenda mbele, tupeni muda. (We agreed on the way forward on a number of issues. Give us time!). Ameomba apewe muda, lakini hakuwa tayari kubainisha wazi kuwa muda huo ni wa kufanya nini! Kama kawaida, rais wetu amezungumza, lakini hakuzungumza kitu. Kaelea juu juu bila kutanabaisha dira yake na msimamo wa Tanzania kuhusu hali ya kusikitisha ya Zimbabwe.
Wachambuzi wa mambo wanatafakari hali hii kama a lot of style but no substance. Kwa Kiswahili, tunaweza kusema; mbwembwe nyingi bila chochote cha maana. Ni vyema tukumbuke kuwa, mara baada ya kuchaguliwa, Rais Kikwete alitembelea Zimbabwe na kuutetea kwa nguvu zote utawala wa Mugabe.
Kabla ya Kikwete, Rais mstaafu Benjamin Mkapa, naye alimtetea Mugabe kwa nguvu zote. Wote walidai, Waafrika waachiwe mambo yao wenyewe. Huu ni unafiki mkubwa uliotolewa na watu ambao wenyewe kucha, kutwa wanatembeza bakuli nchi za Magharibi kuomba misaada ya kuwezesha serikali zao kuendelea kutawala. Kauli zao, sambamba na ukimya na unafiki wa viongozi wengine wa Afrika, zilimpa na zinaendelea kumpa Mugabe jeuri ya kuumiza na hata kuua wananchi wake. Damu za Wazimbabwe, zitawalilia watawala wetu kama hawatatubu!
Kwa upande wake, baada ya kikao na Rais Kikwete, Rais Mugabe alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa, kinachoendelea Zimbabwe leo, si chochote zaidi ya fitina za kibeberu za nchi za Magharibi sambamba na vyombo vyake vya habari katika kutetea watu wanaovunja sheria, akimaanisha wapinzani wake. Akamalizia kwa kusema, hatishiki na kelele hizo na wanaolalamika wanaweza kwenda kujinyonga (
can go hang!).
Siku za karibuni nchini Zimbabwe, viongozi kadhaa wa vyama vya upinzani walisulubiwa na mwingine kuuawa na vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama nchini humo wakati wakijaribu kufanya mkutano wa hadhara wa kuiombea nchi yao kutokana na majanga kibao yanayoikabili. Mkutano huo wa sala ulijumuisha pia makundi kadhaa ya wanaharakati mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini. Mikutano ya hadhara imepigwa marufuku nchini Zimbabwe.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, Rais Mugabe bado ameendelea kuzitaka nchi za Afrika kuungana kutetea bara lao dhidi ya ukoloni mamboleo na ubeberu wa nchi za Magharibi. Kauli za kizalendo kama hizi zimekuwa silaha ya muda mrefu ya Rais Mugabe, iliyomwezesha kutetewa na nchi kadhaa za dunia ya tatu. Tanzania imekuwa kinara wa muda mrefu sana na mtetezi wa utawala wa Mugabe.
Taarifa hizi kutoka vyanzo mbalimbali, vinanijengea msingi wa tafakuri yangu ya leo. Swali la kwanza kabisa linalonikereketa roho yangu, ni pamoja na kutaka kujua dira au vision inayoongoza uhusiano na urafiki wa Tanzania na Zimbabwe! Najiuliza, je ni urafiki na mahusiano ya wananchi wa nchi hizi mbili? Je, ni uhusiano na urafiki wa vyama vinavyotawala nchi hizi mbili vya CCM na ZANU-PF? Je, ni mwendelezo wa kurithishana wa kimahusiano na kirafiki baina ya viongozi wakuu wa nchi hizi tangu Baba wa Taifa, Mwinyi, Mkapa na hatimaye Kikwete kwa upande mmoja na Robert Mugabe pekee kwa upande wa pili?
Je, huu ndiyo utekelezaji wetu wa sera ya diplomasia ya kiuchumi? Je, balozi wetu Rajab Adadi, ambaye alikuwa namba mbili katika utawala wa polisi nchini kwenye utawala wa Mkapa na hivyo kuwa mstari wa mbele katika kulinda mikakati haramu ya kuhakikisha CCM inashinda kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 na 2005, kapelekwa Zimbabwe kujenga mahusiano ya kiuchumi au kuendeleza mkakati wa kumlinda Mugabe na utawala wake?
Je, Tanzania , ambayo damu ya watu wake ilimwagika katika kusaidia kuondoa utawala wa walowezi nchini Zimbabwe, imepata neema gani kwa uhusiano huu wa miaka 27 na utawala wa Rais Robert Mugabe? Hivi kweli Serikali ya CCM inaweza kuwaambia Watanzania jambo moja tu zaidi ya hisia za uzalendo wa kiafrika (sense of African nationalism) ambalo nchi yao imevuna chini ya utawala wa Mugabe?
Na kama tuliwapigania wananchi wa Zimbabwe, je, nao wamefaidika nini na utawala wa mtawala huyu pekee tangu uhuru wa nchi yao mwaka 1980? Je, utayari wa viongozi wetu kumlinda na kumtetea Mugabe umetuwezesha kupata maslahi gani ya kiuchumi na kijamii kiasi cha kuwa tayari kutetea utawala ambao umeua raia wake zaidi ya 10,000 katika kipindi cha miongo miwili na nusu iliyopita?
Ni wendawazimu gani au mchawi gani anawaongoza watawala wetu kiasi cha kutokuwa na mshipa wa aibu au huruma kwa wananchi wa Zimbabwe? Leo mfumko wa bei (inflation) umefikia kiwango cha asilimia 1,700 na sasa nchi hii haina tena fedha za kudumu! Kiwango hiki ni historia na rekodi ya dunia.
Ni limbwata gani ambalo watawala wetu wamelishwa hadi kufumbia macho ukweli kuwa sasa zaidi ya robo ya wananchi milioni 15 wa Zimbabwe wameikimbia nchi yao na kusambaa kote duniani kwa sababu mbalimbali zaidi zikiwa za kiusalama na hali ngumu ya maisha? Watanzania tuna uelewa mdogo sana kuhusu hali halisi katika nchi nyingine za Afrika. Miundombinu ya upashanaji habari katika bara la Afrika haijawa ajenda iliyojengewa mkakati wa makusudi katika maazimio kadhaa ya Umoja wa Afrika. Huu pekee ni ushuhuda kuwa Umoja wa Afrika una safari ndefu.
Kwa kiasi kikubwa, Afrika bado hutegemea taarifa nyingi kutoka vyombo vya habari vya nje ya bara letu. Ni dhahiri basi, vyombo hivi vitaripoti yale yanayogusa maslahi yao kwanza. Kila chombo cha habari cha kimataifa kina chimbuko lake ambapo hatimaye maslahi yake yatajikita. Lakini hili halifanyi kila linaloripotiwa na vyombo hivi kuwa yasiyotakia bara letu mema!
Kwa Watanzania walio wengi, Zimbabwe ni nchi rafiki. Vyama vinavyoongoza nchi hizi, ZANU-PF kwa upande wa Zimbabwe na CCM kwa upande wa Tanzania, ni marafiki wa muda mrefu. Aidha, Rais Mugabe anachukuliwa kama mtu makini na mzalendo wa kweli miongoni mwa jamii ya Watanzania. Walio wengi wanamfahamu Mugabe na ZANU-PF kwa historia ya harakati za ukombozi kusini mwa Afrika. Alikuwa rafiki wa Mwalimu, mpigania uhuru na mkomunisti. Tanzania imekuwa sehemu ya waangalizi wa uchaguzi wa SADC ambao walisimamia chaguzi za Zimbabwe mara kadhaa ikiwamo uchaguzi wa mwisho mwaka 2002. Katika kile kilichoshangaza dunia, waangalizi hawa walisema uchaguzi ulikuwa huru na haki.
Ukweli ni kuwa uchaguzi ulitawaliwa na kila aina ya vurugu, mauaji, kutekana nyara, kuibiana kura na kila aina ya uchafu, mambo yanayosemekana kufanywa wazi na vikosi kadhaa vya ulinzi vya serikali vikishirikiana na vikosi vya kiharamia vya umoja wa vijana wa ZANU-PF. Mugabe aliyeingia madarakani miaka 27 iliyopita si wa leo. Tanzania tumeendelea kumkumbatia bila kusoma alama za nyakati sambamba na matendo yake. Kidogo tulichoelezwa, ni kuwa ugomvi wake ni kutaka kuchukua (na kuchukua) ardhi kubwa iliyomilikiwa na Wazungu wachache na kuigawa kwa Waafrika walio wengi.
Kwa wale wanaopenda kusoma, ukipekua na kusoma vitabu na majarida mbalimbali yanayohusu historia na hali ilivyo sasa ya kisiasa, kiuchumi na hata kijamii katika bara hili, utagundua kuwa tuna tatizo kubwa kuliko wenyewe tunavyoliona. Vitabu na majarida mengi yameandikwa na waandishi wa nchi za Magharibi. Wengi wa waandishi hawa wamejaribu kuielimisha dunia kuhusu ufujaji na ulimbukeni wa kutisha wa viongozi kadhaa wa nchi za Kiafrika.
Kwa sababu ya hisia za Uafrika wetu, mengi ya maandishi haya yametuudhi. Tumewalaumu waandishi wake kuwa ni wazushi, wambeya, wakoloni nk. Hata pale mambo ya ukweli na uchafu wa viongozi wa nchi za Kiafrika yanapoandikwa na waandishi kutoka katika bara la Afrika, tafsiri rahisi na ya kipropaganda itakayotolewa ni kuwa, mwandishi ni kibaraka wa Wazungu.
Baada ya kuona hakuna faida yoyote ya kijamii na hata kiuchumi inayotokana na mahusiano haya, basi ni dhahiri kuwa lililobaki ni maslahi ya kisiasa. Yako mambo mengi yanayoshabihiana kati ya CCM na ZANU-PF. Moja, vyote ni vyama vilivyoshiriki kwa njia moja au nyingine kupigania uhuru katika nchi zetu. Ni vyama vilivyojenga mitandao ya awali kabisa kutokana na shauku ya wananchi kupata uhuru toka kwa Wakoloni.
Baada ya uhuru katika kila nchi, vyama hivi vyote vilijitahidi kuua upinzani na hivyo vyote kujenga mfumo wa chama kimoja cha siasa. Ni vyama vilivyojaribu kujenga mifumo ya kijamaa kwa upande wa Tanzania na kikomunisti upande wa Zimbabwe. Ni vyama vilivyoshindwa kuwaletea wananchi wao matunda halisi ya uhuru. Ni vyama vilivyopunguza uwezo wa wastani wa kuishi wa wananchi wao. Ni vyama vilivyoongeza umasikini wa wananchi wao.
Ni vyama ambavyo vimelazimishwa na mifumo ya dunia kukubali tena mfumo wa vyama vingi vya siasa. Ni vyama ambavyo serikali zao bila misaada haziendi popote. Ona hali ya Zimbabwe leo! Ni vyama ambavyo vimedhihirisha kwa vitendo kuwa, viko tayari kuua ili kubaki madarakani. ZANU-PF imeua sana nchini Zimbabwe hasa Jimbo la Matabele ambako ilionekana kuna nguvu kubwa ya upinzani kutoka chama cha mpigania uhuru mwingine wa Zimbabwe, Joshua Nkomo na chama chake cha ZAPU na sasa MDC. Wapinzani wamefanyiwa kila aina ya vitimbi ili kuwadhoofisha.
Kwa upande wa Tanzania, Serikali ya CCM inatumia mbinu zote chafu na safi maeneo yale yanayoonekana kuwa na upinzani wa nguvu. Kama hawakuuawa watu, basi vitimbi na mateso mengi vimewafika wapinzani. Mifano rahisi ni pamoja na Pemba, Zanzibar, Tarime, Kilimanjaro, Kigoma, Bukoba, Bariadi nk. Kuna kila dalili ya vyama vya CCM na ZANU-PF kuendelea kubadilishana uzoefu wa kuhujumu chaguzi na hata mikakati ya kudhibiti wapinzani. Tofauti kubwa kati yao ni nguvu ya upinzani na wanaharakati wengine katika nchi zao.
Kama ilivyokuwa dhahiri kwenye maeneo ambayo wapinzani wameonekana kuwa na nguvu kama vile Pemba, siku Tanzania Bara itakuwa na upinzani wa aina ya Pemba, tutegemee mauaji mengi ya kutisha. CCM ni ruthless kweli kweli inapokuwa na uhakika kuwa upinzani una nguvu ya kutosha katika eneo fulani. Hata hivyo, somo la Zimbabwe na liwafundishe CCM kuwa kuua, kuumiza, kudhalilisha na kutesa upinzani kamwe hakuwezi kuzima azma ya binadamu kutetea anachokiamini. Utamchelewesha, lakini hutamzuia hatimaye.
Viongozi wengi wa nchi za SADC nao wameonyesha udhaifu wa kutisha katika kukabiliana na udhalimu wa utawala wa Mugabe. Ni rais mmoja tu wa Afrika, Levy Mwanawasa wa Zambia aliyesema waziwazi kuwa hali ya Zimbabwe haikubaliki na utawala wa Mugabe umeizamisha Zimbabwe. Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini naye ameshona mdomo.
Anasahau kuwa, kama si jumuia ya kimataifa kuushinikiza utawala wa makaburu huko nyuma, leo asingekuwa na fursa ya kuwa rais. Watawala wengi wa Afrika wameonyesha waziwazi kuwa udhalimu ukifanywa na weupe kwa weusi ni mbaya, lakini ukifanywa na weusi kwa weusi ni halali! Aibu gani hii!
Kisingizio ni kuwa nchi za Afrika zinatumia kile zinachokiita Quite diplomacy, yaani diplomasia isiyo na kelele, ya chini kwa chini, ya ndani kwa ndani. Unafiki mkubwa. Watu wanauawa nyie mnafanya diplomasia ya kimya kimya kwa kunywa mvinyo na kuonyeshana ufahari wa madege! Ni mkakati wa unafiki na ulioshindwa. Mazingira yote yanasababisha kuhofu kama kweli Rais Kikwete na serikali yake ni wasuluhishi wa kweli (honest brokers) wa mtafaruku wa Zimbabwe .
Aidha, Rais Kikwete asifumbie macho yanayofanywa na chama chake hapa nchini kwani kila dalili inaonyesha utekelezaji wa uharamia kama wa Zimbabwe. Uharamia huu umeanza kuonekana tangu uchaguzi wa mwaka 2005 na hata uchaguzi mdogo wa Tunduru hivi majuzi.
Kikwete na serikali yake, ni marafiki wa Mugabe na serikali yake, hivyo tunawajibika kuhoji dhamira ya rais wetu. CCM na ZANU-PF ni ndege wa unyoya mmoja, nao basi wako njia moja na wanaruka pamoja. Ni kwa maana hii basi, namtaka Rais Kikwete asimame na awe tayari kuhesabiwa kwa kumwambia ukweli Mugabe kuwa, Watanzania hawakumwaga damu zao ili naye amwage za Wazimbabwe.
Tutafakari usanii uliojengeka ndani ya sera yetu ya mambo ya nje iliyoasisiwa na Kikwete akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inayoitwa diplomasia ya kiuchumi.
Tuonane wiki ijayo
source:
http://www.freemedia.co.tz/daima/2007/3/28/makala2.php