Wizara Katiba Na Sheria
Member
- Feb 28, 2021
- 42
- 84
- Thread starter
- #61
Ndugu Tate Mkuu,1.) Ni kwanini Serikali ya Tanzania inapinga kwa nguvu zote uwepo wa Uraia Pacha huku Nchi nyingine zikinufaika kupitia Uraia Pacha huo huo katika nyanja mbalimbali mfano. Uwekezaji, biashara, michezo, nk?....
Tunaomba tujibu maswali yako kama ifuatavyo:
1. Masuala ya uraia wa Tanzania yanasimamiwa na Sheria ya Uraia Namba 6 ya mwaka 1995 ambayo imebainisha kuwa uraia wa Tanzania upo katika makundi matatu; uraia wa kuzaliwa, uraia wa kurithi na uraia wa tajinisi. Aidha, sheria hii kupitia kifungu cha 7(4)(a)(b) kimeeleza bayana kuwa raia wa Tanzania anaacha kuwa raia kwa kigezo cha kuchukua uraia wa nchi nyingine. Hivyo basi, kutokana na sheria hii na sera ya Tanzania kuhusu uraia ambayo hairuhusu wala kutambua uraia wa nchi mbili, Serikali haiwezi kuweka sheria ya uraia pacha kwa sasa.
Suala hili lilijadiliwa pia wakati wa mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Bunge Maalum la Katiba ambalo lilijadili pendekezo hili liliona Tanzania bado haipo tayari kwa sasa na Bunge hilo Maalum likatoa pendekezo kwamba; “Mtu yeyote mwenye asili au nasaba ya Tanzania na ambaye ameacha kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupata uraia wa nchi nyingine atakapokuwa katika Jamhuri ya Muungano atakuwa na hadhi maalum kama itakavyoainishwa katika sheria za nchi.”
Nukuu hii imebainishwa katika Sura ya 6, Ibara ya 72 ya Katiba Inayopendekezwa ya Oktoba, 2014.
2. Suala la Mgombea Binafsi halipo kwa mujibu wa katiba na sheria zetu. Hoja hii lilipendekezwa kwenye mjadala wa katiba mpya ambayo bado haijakamilika. Hivyo hatuwezi kusema ni lini serikali itaruhusu, labda mpaka pale tutakapokuwa na sheria hiyo.
3. Katiba Mpya ni ajenda ya kitaifa. Ni dhahiri taifa letu linahitaji katiba mpya itakayoakisi mahitaji yetu ya sasa na baadae.
Kwa kulitambua hilo, kama itakumbukwa, mchakato wa Katiba Mpya ulifikia pazuri ambapo serikali kwa nia njema iliitisha bunge maalum la katiba likihusisha wadau wanaowakilisha makundi mbalimbali.
Kwa bahati mbaya, baadhi ya makundi muhimu yanayowakilisha wananchi yaligoma kuendelea kuhudhuria bunge hilo wakati mchakato wa kupatikana katiba mpya ukiendelea, hivyo kukwamisha zoezi zima na serikali kulazimika kusitisha.
Vipaumbele vya Serikali kwa sasa, kama ilivyotangazwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli mara kadhaa, ni kushughulikia kero zinazogusa wananchi moja kwa moja na kuboresha utoaji huduma bora ikiwemo kuweka miradi ya kimkakati itakayokuza uchumi wa taifa letu.
Ajenda ya Katiba Mpya itafikiwa tena pale itakapofika wakati wake kwani Katiba ni hitaji la nyakati.
4. Wizara hairidhishwi na uvunjifu wowote wa sheria unaofanywa na askari au mtumishi yeyote kwani sheria ziko wazi. Makosa ya jinai yote yanashughulikiwa na mahakama zetu kwa mujibu wa sheria bila kuangalia mtendaji ni nani.
Asante.