JanguKamaJangu

JF-Expert Member
Feb 7, 2022
2,308
5,460
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja linawashikilia watu kumi na mbili kwa tuhuma za kukutwa wakila mchana hadharani kipindi hiki cha Mwezi mtukufu wa Ramadhan ambao wanaifanya kuwa idadi ya watu waliokamatwa kwa tuhuma za kutenda makosa mbalimbali kufikia sitini na mbili

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini magharibi Unguja Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Abubakar Khamis Ally amesema kufuatia video iliyosambaa mitandaoni ikiwaonesha baadhi ya watu katika eneo la viwanja vya mnazi mmoja Zanzibar wakila hadharani wakati wa mchana wa Ramadhani, Jeshi hilo lilifanya msako na kuwakamata watu wapatao kumi na mbili wakiwa na vielelezo ambapo amesema wanaendelea na taratibu nyengine ili kuwafikisha Mahakamani.

Aidha ameyataja makosa mengine ni pamoja na unyang’anyi, Madawa ya kulevya na makosa mengine ambapo watuhumiwa wanashikiliwa na Polisi na wengine tayari wameshahukumiwa Mahakamani.

Pia soma:
 
Zanzibar being predominantly Muslim, during Ramadan, everyone is expected to adhere to the Islamic teachings of fasting from dawn to dusk, at least in public. It is not against the law to eat publicly rather considered polite.

Hiki ndicho google inasema.

Lakini sidhani kama kuna sheria ya dini inasema hivyo ni mihemko ya watu kama asemavyo member M Z A N Z I B A R I
 
Kwani zanzibar ni nchi ya kiislam? Huo ni upumbavu kulazimisha watu waamini ujinga. Mungu gani huyo anapambaniwa na watu ili aabudiwe?

Huo upumbavu usifike bara, bara watu wanakula mchana peupe tena malangoni pa misikiti, kuna migahawa kwenye fremu zao na watu wanapata chakula kama kawaida bila kubughudhiwa
 
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja linawashikilia watu kumi na mbili kwa tuhuma za kukutwa wakila mchana hadharani kipindi hiki cha Mwezi mtukufu wa Ramadhan...
Tangu waanze kufunga kuna la maana lipi wamefanya zaidi ya kuweka PAUSE machafu yao, baada tu ya mfungo wana press play. Wanamchezea Mungu. Mfungo focus kwao ni chakula sio mabadiliko ya kiroho, kutwa nzima kusubiri iftar na kupanga iweje. Takataka
 
Zanzibar being predominantly Muslim, during Ramadan, everyone is expected to adhere to the Islamic teachings of fasting from dawn to dusk, at least in public. It is not against the law to eat publicly rather considered polite.

Hiki ndicho google inasema.

Lakini sidhani kama kuna sheria ya dini inasema hivyo ni mihemko ya watu kama asemavyo member M Z A N Z I B A R I
karume ndiye aliendeleza utamaduni huo


Muktasari:
Hii huenda pamoja na kufuatilia kwa karibu zaidi mafunzo na maamrisho ya dini yao, ikiwa pamoja na kuwasaidia wasiojiweza na kujitahidi kufanya mema na kuachana na maovu.

Mwezi mtukufu wa Ramadhani umepiga hodi. Kwa siku 29 au 30 kutegemeana na kuandama kwa mwezi, waumini wa dini ya Kiislamu wanalazimika kwa mujibu wa maamrisho ya dini yao kufunga.

Hii huenda pamoja na kufuatilia kwa karibu zaidi mafunzo na maamrisho ya dini yao, ikiwa pamoja na kuwasaidia wasiojiweza na kujitahidi kufanya mema na kuachana na maovu.

Kufunga katika mwezi huu ambapo Waislamu waliteremshiwa na Mola kitabu chao kitukufu cha Quran ni moja ya nguzo tano za dini hiyo.

Waislamu hufunga kuanzia muda mfupi kabla ya kuchomoza isha za jua kutoka hadi pale linapotua.

Katika funga yao, Waislamu hutakiwa kujiepusha na mengi ikiwa ni pamoja na kula, kunywa, kuvuta sigara na hata kusema uongo au kufanya vitendo vya mahaba hata na wanandoa wenzao.

Kwa Waislamu wengi wa Tanzania funga huchukua kati ya saa 14 na saa 14 na dakika 30 kwa kutegemea funga hiyo unaifanyia sehemu gani ya nchi, lakini wapo wenzao katika baadhi ya nchi ambako usiku huwa mkubwa kutokana na majira ya hali ya hewa na hufunga kwa hadi saa 20.

Katika mwezi huu, Wazanzibar na wageni hutakiwa kuzifuata sheria na taratibu zilizowekwa kisheria na wanaozikiuka hupata adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja usiokuwa na hata siku moja ya msamaha.

Adhabu hii huwakuta watu wazima na wenye akili timamu (bila ya kujali umri).

Hii ni kusema anayekamatwa anakula siku ya tatu ya Ramadhani huenda jela hadi siku ya tatu ya Ramadhani ya mwakani kwa sababu ya kuonyesha jeuri kwa dini ya Kiislamu na kuchezea hisia za Waislamu.

Mara chache huwapo adhabu ya faini kwa makosa haya.

Kwa miaka mingi Zanzibar imekuwa na mwongozo wa mavazi anayotakiwa mtu kuvaa hadharani, lakini sheria hii ambayo imekuwa ikifumbiwa macho kutokana na kile kinachoelezwa kama utandawazi husimamiwa kwa nguvu ukifika mwezi wa Ramadhani.

Kwa mfano, kitendo cha kuvaa nguo fupi sana mwanamke na kuwa mgongo wazi au kuvaa nguo nyepesi inayoonyesha mambo hadharani, kwa mujibu wa sheria za mavazi ya Zanzibar, ni kosa la jinai. Wanaofanya hivyo wanapokamatwa husukumwa jela au kuchapwa viboko.

Katika miaka ya nyuma, watalii waliofika Zanzibar na ‘vinguo’ vifupi walilazimishwa kununua kanga au vitenge na kufunika vizuri maumbile yao. Waliokataa kufanya hivyo walitakiwa kurudi walikotoka kwa sababu Zanzibar haikuwa tayari kuona watu wanakwenda nusu au robo uchi hadharani.

Sheria hii ilikuwapo tangu wakati wa utawala wa Sultani na ilisimamiwa kwa nguvu zaidi wakati wa utawala wa Rais wa kwanza wa Zanzibar baada ya Mapinduzi ya 1964, Abeid Amani Karume mpaka kifo chake mwaka 1972.

Mzee Karume alikuwa akisema mtu yupo huru kwenda uchi nyumbani kwake, lakini akifanya katika barabara za Unguja na Pemba atapelekwa jela akafundishwe kuvaa virago vya gerezani.

Alisema anayependa kuonyesha uzuri wa umbo lake afanye kwenye kioo nyumbani kwake na sio katika barabara za Zanzibar.

Karume alivyodhibiti uvaaji
Siku moja balozi mmoja wa Kiingereza alifika Ikulu ya Zanzibar kuonana na Mzee Karume. Lakini mara tu alipomuona, Rais Karume alirudi ofisini kwake na kuwaambia maofisa wake wamwambie balozi aende kuvaa nguo zenye heshima na stara kwa vile Zanzibar sio nchi ya watu wanaotembea uchi.

Katika mkasa wa pili ulioonyesha namna ambavyo Rais Karume alivyokataa wageni na hata viongozi kuchezea au kukebehi utamaduni wa Zanzibar ni pale Rais wa Liberia, William Tubman alipokuwa afike Zanzibar alipofanya ziara ya Tanzania mwaka 1964.

Siku chache kabla ya Tubman kufika Zanzibar, Karume alitembelewa Ikulu na maofisa wa itifaki wa Liberia kumweleza namna mzee Karume alivyotakiwa kumpokea kiongozi huyo wa Liberia na matayarisho gani amfanyie ili ziara yake iwe ya mafanikio.

Rais Karume alisikiliza kwa utulivu, alitakiwa avae suti nyeusi na afunge tai shingoni na maneno gani atumie kumkaribisha na kwamba amtayarishie kinywaji aina ya whisky wakati wa chakula na mazungumzo.

Baadaye Karume aliangua kicheko na kuwaambia maofisa wa itifiki wa Liberia na Tanzania, kwamba kama Tubman aliamua kutembelea Zanzibar aonyeshe heshima na adabu na lazima avae kanzu na koti, kofia ya baraghashia na viatu vya makubazi.

Vilevile aliwaambia bosi wao afikapo Zanzibar anywe maji ya madafu na kama hakuwa tayari kufanya hivyo asifike Zanzibar. Wakati alipokuwa akitamka hayo Karume alikwishatoa maelekezo kwa maofisa wake kwenda kumnunulia Tubman kanzu, kofia na viatu vya makubazi.

Balaa kubwa lilizuka na mzee Karume alikubali baadaye yaishe na kila mmoja avae vazi lake, lakini hata Rais Tubman hakuruhusiwa kwenda Zanzibar na pombe.

Tubman alifika Zanzibar akiwa amevaa suti na mzee Karume alimpokea akiwa amevaa kanzu maridadi. Hiyo ndiyo Zanzibar ilivyokuwa hapo zamani na hasa katika mwezi wa Ramadhani.

Tahadhari muhimu
Siku hizi hali imebadilika, lakini viongozi wa Zanzibar kila ikifika mwezi wa Ramadhani huwataka wenyeji na wageni, wakiwamo watalii kuuheshimu mwezi huo kwa kufuata sheria na maelekezo yanayotolewa na Serikali.

Nimeeleza haya kuwatahadharisha wageni, wakiwamo ndugu zetu wa Kikristo waliopo Bara wanaofika Zanzibar wakati wa mwezi huo iwe kwa kazi au matembezi kwamba kama wakifanya ‘maraha’ au wakila, kunywa au kuvuta sigara hadharani wanaweza kujikuta katika balaa.

Kila nchi ina sheria zake na zinapaswa kuheshimiwa. Katika baadhi ya nchi ni kosa la jinai kuvaa hijabu na sheria hizo anayezivunja hukiona cha mtema kuni.

Kwa hiyo, isiwe nongwa kwa Zanzibar kuwa na sheria zake na anayeona tabu ni vyema akavumilia au aamue asifike Zanzibar, hasa wakati wa mwezi huu mtukufu.

Nchi nyingi za Magharibi huwaonya raia zake wanaotembelea nchi za Kiislamu na hasa Saudi Arabia na nchi za Ghuba kuwa na hadhari ya kutokula au kunywa hadharani wakati wa mwezi huu kwani kufanya hivyo kutawaweka matatizoni.

Ni vizuri pia zikafanya hivyo kwa wale wanaofika Zanzibar wakati huu kwa sababu mbali ya polisi kuwa ndio msimamizi wa sheria hizi, wakati fulani hata wananchi wenye hasira huchukua sheria mkononi.

Mara nyingi imetokea watu wanaokula hadharani au kuvaa nguo fupi kwenye maeneo ya wazi, hasa mwezi wa Ramadhani kuchapwa na hata kuumizwa na watu wenye hasira ambao huona dini yao inabughudhiwa.

Hata watu wa visiwani wanaofanya hivyo pia hupigwa.

Ni wazi kwamba katika wakati huu ambapo siasa zimewagawa watu, kama kipo kitu unachoweza kusema kimekuwa siku zote kikiwaunganisha Wazanzibari basi ni wakati wa mwezi wa Ramadhani.

Unapokuja mwezi mtukufu wa Ramadhani watu wa Zanzibar wana msemo kama ule wa manahodha usemao, “hii ni meli yangu na sheria zangu zifuatwe” na kwa Ramadhani watu wa Zanzibar wanasema, “hii ni nchi yangu na amri zangu zifuatwe.”

Tushirikiane na wakati kila mmoja anaendelea kuwa na uhuru wa kuabudu dini aitakayo, sio vyema kufanya jambo litalomuudhi muumini wa dini nyingine.

Waislamu na Wakristo kwa miaka nenda, miaka rudi Tanzania Bara na Visiwani wameishi kwa kupendana na kuheshimiana licha ya tofauti zao za kidini. Ni vyema utamaduni huu ukaendelezwa.

 
Back
Top Bottom