Mafuta yakipatikana, tumkaribishe Mwenyezi Mungu atuwakilishe kwenye mikataba!
Na Julius Samwel Magodi
WIKI hii pamoja na kutawaliwa na mabomu ya wabunge bungeni ambao walikuwa wakilipuana wenyewe kwa wenyewe kutokana na tuhuma za ama kushiriki katika ubadhirifu wa fedha za walipa kodi au la, kulikuwa na habari ambazo ninaweza kuziita za neema, yaani zile za kupatikana kwa mafuta.
Ingawa wabunge wetu walikuwa bize wakirushiana makombora mazito mazito, lakini Watanzania wengi wanaofuatilia tuhuma zinazoibuka nchini, hawakuona kitu kipya kwani wanajua kashfa kama hizo siku zote hapa nchini huvuma na kisha kuyenyuka mithili ya mafuta ya mgando yaingiapo katika moto.
Sijui kuna nini kinatufanya sisi Watanzania tusichukuliane hatua kali pale ambapo ubadhirifu wa wazi unapojitokeza au kujionyesha. Kigugumuzi hiki cha serikali kushindwa kuwaadhibu watu ambao wanahusika na ufisadi wa fedha za walipa kodi, ndio kitu ambacho kimekuwa kikiwatia hasira wananchi na kushindwa kuwaelewa viongozi wao wakiwamo walioko serikalini.
Hebu acha nirejee katika mada yagu ya leo, baada ya Uganda kugundua akiba yamafuta na huko Kenya kusikika kwa dalili hizo, sasa dalili njema zimeanza kunukia kwa Watanzania baada ya kupata visima vitatu vyenye kuashiria kuwapo kwa mafuta katika eneo la Mnazi Bay, mkoani Mtwara.
Wiki hii, Kamishna wa Nishati na Petroli katika Wizara ya Nishati na Madini, Bashir Mrindoko aliutangazia umma kuwa visima vitatu vilivyochimbwa na Kampuni ya Artumas inayochimba gesi eneo hilo vimiminika vilivyochukuliwa vimeonyesha dalili za kuwepo mafuta machafu.
Alisema vimiminika hivyo, vina kila dalili za kuwepo kwa mafuta na kwamba, kazi inayofanyika ni kubaini kiwango cha vimiminika hivyo na eneo halisi.
Majaribio yaliyofanywa kuhusu eneo la Mnazi Bay, yanaonyesha lina akiba ya kutosha ya gesi asili na bidhaa zingine za nishati.
Vimiminika vilivyopatikana vinaonyesha kiwango cha kati ya 25 na 27 ya ubora, ambavyo kawaida huambatana na mafuta machafu.
Kazi inayofanyika sasa ni kupima kiwango cha mafuta hayo kama yapo ni kiasi gani na yako wapina kwamba sampuli za mapipa 90 zimechukulwa kufanyiwa utafiti huko Marekani.
Kwa hakika kupatikana kwa vimiminika hivyo, kumechochea changamoto ya kuendeleza utafiti wao kwenye eneo hilo.
Ikumbukwe kwamba gesi ya Mnazi Bay iligundulika mwaka 1982, lakini kazi ya uendelezaji ilianza mwaka 2003, serikali ilipotiliana saini na Kampuni ya Artumas kwa ubia na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPC).
Hii ni neema myingine ambayo Mwenyezi Mungu ametujalia tena Watanzania baada ya kutupatia raslimali nyingi mno kama vile madini ya karibu kila aina, wanyamapori, ndege adimu, milima, maziwa na bahari na kutupatia misitu tele ambayo mpaka sasa mingine haijawahi kukanyagwa na mtu tangu duniani iwepo.
Rasilmali zote hizi watu wengi katika mataifa mbalimbali wamekuwa wakitushangaa kwa nini Watanzania tumebakia kuwa masikini, wakati vitu vyote hivi wanavyo wao? lakini jibu la haraka linaloonekana ni kuwa ufisadi umetujaa mno, hatuna uzalendo na hatuwezi kulinda raslimali zetu.
Ni nchi chache sana duniani hujaliwa sana kuwa na rasilmali zote hizi, lakini kinachosikitisha ni njisi ambavyo tumeshindwa kuvifanya viweze kutupatia maendeleo.
Je, hii ni laana ya Mwenyezi Mungu au ni nini? Hawa walafi ambao wanatukwamisha tunashindwa nini kuwakandamizia jela kama anavyosema Masanja Mkandamizaji wa maarufu kama akina Ze Komedi ili wengine waweze kujua kuwa hilo ni fundisho au viongozi wetu nao wanalambishwa utamu wa ufisadi huu?
Mafuta haya ambayo sasa yanaelekea kupatikana, ninaamini kuwa hatayataweza kutunufaisha sisi kutokana na rekodi zetu za nyuma za kuingia mikataba chakavu, yenye usiri mkubwa, mibovu ambayo inaishia kwa baadhi ya maafisa wetu wa serikali kujinufaisha.
Mifano ya mikataba mibovu ambayo serikali iliingia lakini imeshindwa mpaka sasa kuwanufaisha Watanzania ni pamoja na kampuni ya kuzalisha umeme wa mafuta ya IPTL, kuuzwa kwa mashirika mengi ya umma, gesi ya Songosongo, mikataba ya kuzalisha umeme wa dharura mwaka juzi na jana, ile mingi ya madini na kadhalika.
Kama kawaida yetu Watanzania tusitegemee kupata nafuu na mafuta hayo ambayo huenda yatachimbwa hapa nchini kwetu kutokana na ugonjwa wetu wa kuingia mikataba kama vile haiwahusu Watanzania, huku wenzetu wachache wakigeuka kuwa mabilionea.
Nadhani safari hii Watanzania wachache, wenye macho, masikio, tunaoona viziuri, kamwe tusikubali kuingizwa tena mjini na wajanja, rasilmali yetu iachwe iliwe na watu wengine badala ya kuwanufaisha Watanzania wenyewe.
Hivi kweli inaingia akilini mwa mtu kwamba mgeni uliyempa kibali cha kukodisha shamba lako la mahindi kwa ubia kulima, baada ya kuvuna yeye achukue kila kitu halafu wewe uambulie kupewa mabua kwa ajili ya kuezekea ua, mahindi yote achukue!
Ni nchi chache sana duniani ambazo unaweza kupata bahati kama hiyo, ya kupewa ruksa ya kuichezea serikali kadri unavyotaka kwa maana ya kuweka mazingira ambayo unaweza kuwanunua maafisa wanaohusika na masuala ya uwekezaji.
Watanzania sasa tunaitaka serikali katika suala hili la mafuta, mkataba wa kuingia na mchimbaji lazima uwe wa wazi na ambao upate ridhaa ya wananchi kupitia wawakilishi wao wabunge.
Siamini, kama mwekezaji huyo ataweza kuwanunua wabunge wote ili aweze kuiweka nchi katika kona ya ulingo ili aweze kuibia kadri anavyotaka.
Nasema hivyo kwa sababu taratibu za sasa za mikataba kuwa siri na kupitishwa na baraza la mawaziri hakika sio sahihi kwa sababu watu hawa ni wachache ambao hatuamini kama wanaweza kutoa maamuzi siku zote yaliyosawa.
Mikataba karibu yote hii inayoiliza nchi hivi sasa imepitia katika baraza la mawaziri kwa maana nyingine tunaomba mkabata wa mchimbaji wa mafuta mkataba wake upitie katika mikono mingine ambayo ni Watanzania wote au pengine kupitia wawakilishi wao, kama wabunge, madiwani na kadhalika.
Tukichezea hata mkataba wa mafuta, tukifanya uzembe hapo tujue tumekwisha na kwamba hilo jambo linaweza kutuingiza katima vita vya kupigania mafuta.
Ni wazi kuwa watanzania walio wengi hawatakubali kuona kuwa mafuta yanachimbwa hapa nchini lakini hawanufaiki nayo badala yake yananufaisha watu chache.
Ipo mifano mingi ya nchi ambazo zimeingia katika vita kutokana na mikataba ya wawekezaji kushindwa kuwanufaisha. Napendekeza kama vigogo wataendelea kutaka kuikumbatia mikataba hii basi, wananchi tuwaombe wenzetu serikalini watukubalie tumchague Mungu ndiye awe mwakilishi wetu ili tusije tena kuingizwa katika matatizo makubwa ambayo tunayo hadi leo.
Mwandishi wa safu hii ni mhariri wa habari maalum, Anapatikana kupitia baruapepe;
juliusmagodi@yahoo.com, simu, 0754 304 336