Zanzibar: Dkt. Biteko ashuhudia utiaji Saini mikataba ya kuwezesha upatikanaji wa Gesi Asilia

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameshuhudia uwekaji saini Mkataba wa Mauziano ya Gesi Asilia itakayozalishwa katika eneo la Ntorya Kitalu cha Ruvuma na uwekaji saini hati ya Makubaliano kwa ajili ya kuanzisha mahusiano ya kujenga miundombinu ya kusambaza Gesi Asilia kwa Teknolojia ya miundombinu midogo ya kubadilisha Gesi Asilia kuwa kimiminika (Mini-LNG).

Hafla ya utiaji saini imefanyika leo Januari 10, 2024, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo Mkataba wa Mauziano ya Gesi Asilia itakayozalishwa eneo la Ntorya umesainiwa kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kampuni ya ARA Petroleum ya Oman na Ndovu Resources ya Uingereza.

Hati ya Makubaliano kwa ajili ya kuanzisha mahusiano ya kujenga miundombinu ya Gesi Asilia imesainiwa kati ya TPDC na Kampuni ya KS Energy.

abf76bc4-c223-4c79-b7a2-0957dcb971ba.jpeg
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Biteko amesema Mkakati wa Wizara ya Nishati ni kuhakikisha inasimamia ipasavyo Sera ya Nishati ya Mwaka 2015 na kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa nishati safi ambayo itawafikia wateja mbalimbali kwa urahisi na bei nafuu.

Amesema lengo la nchi ni kuwa na nishati inayotokana na vyanzo mbalimbali ikiwemo Jua, Upepo, Gesi na Maji ili Gesi Asilia iliyopo itumike pia kwa kiasi kikubwa kwenye maeneo mengine kama viwanda na majumbani badala ya kutumika kwa kiasi kikubwa kwenye umeme na pia kupunguza matumizi ya mafuta.

“Mkakati wetu ni kubadilisha suala hili la Gesi Asilia kutumika zaidi kwenye umeme ambayo ni takriban asilimia 80, tunataka kuwe na nishati mchanganyiko nchini ili gesi itumike kwenye viwanda na majumbani na pia tupunguze utegemezi wa mafuta,” amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza, TPDC sasa wana mkakati utakaowezesha kuwa na mgawanyo wa matumizi ya Gesi Asilia ambapo matumizi kwenye umeme itakuwa asilimia 38, majumbani na viwandani itakuwa asilimia 32 na asilimia 10 itabaki majumbani tofauti na ilivyo sasa ambapo matumizi ya Gesi viwandani na majumbani ni asilimia 28 na asilimia iliyobaki kwa kiasi kikubwa inaenda kwenye umeme.

Kuhusu hati iliyosaniwa ya miundombinu midogo ya LNG, Dkt. Biteko amesema nchi ina kilometa za mraba 945,000 na kwamba pamoja na uwepo wa Bomba la Gesi Asilia nchini njia rahisi ya kufanya Gesi iwafikie watu wengi ni kuigeuza gesi kuwa kimiminika na kusafirisha kwa magari kwenda kwenye maeneo ambayo watu watatumia hivyo kutiwa saini kwa makubaliano hayo kutawezesha Gesi kuwafikiwa Wananchi wengi zaidi.

e0767d67-3a78-41a6-bf4b-fa1f9928db58.jpeg
Amesema Serikali iko tayari kushirikiana na wawekezaji hao ili kuwafikishia Wananchi nishati ya uhakika kutoka vyanzo mbalimbali huku akitolea mfano utekelezaji wa mradi wa megawati 50 unaotokana na Jua wilayani Kishapu, Mkoa wa Shinyanga na ujenzi wa miradi mingine ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme.

Ameeleza kuwa, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anafuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya nishati nchini kwani anachotaka ni watu wapate umeme wa uhakika pamoja na nishati nyinginezo.

Vilevile, amesema Serikali haitaki urasimu katika utekelezaji wa mipango inayojiwekea kwani nia ni kwenda na wakati na kufanya vitu vitokee kwa manufaa ya kizazi cha sasa na cha badaye.

Amesema Serikali inaangalia vitu muhimu ambavyo vitaondoa watu kwenye umaskini kwa haraka zaidi ikiwemo uwepo wa miundombinu ya barabara, anga, reli, Bandari na uwepo wa nishati ya uhakika ambapo kwa upande wa Wizara ya Nishati, zinafanyika kila jitihada ili kuwe na nishati ya kutosha na ya uhakika.

Upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema kuwa, mradi miradi hiyo ina umuhimu mkubwa ikiwemo katika mikoa ambapo rasilimali hiyo inazalishwa na kwamba watahakikisha wanaisimamia kwa ajili ya maendeleo ya Mtwara na nchi kwa jumla.

Amemshukuru, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati mkoani Mtwara ikiwemo ya utafutaji na uzalishaji wa Gesi Asilia.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame alisema Mkataba wa mauziano ya Gesi Asilia uliosainiwa utawezesha kuongeza gesi iliyogunduliwa nchini ambapo mradi huo unategemea kuzalisha kiasi cha kuanzia futi za ujazo milioni 60 kwa siku hadi kufikia futi za ujazo milioni 140 kwa siku katika kipindi cha miaka 3.

Ameongeza kukamilika kwa mkataba huu kutawezesha shughuli nyingine za uendelezaji kufanyika kama vile, ujenzi wa miundombinu ya kukusanya gesi kutoka visimani, ujenzi wa miundombinu ya kukusanya gesi kutoka visimani, ujenzi wa miundombinu ya usafishaji wa awali ikiwemo kutoa maji na ujenzi wa bomba la kilometa 34 la kusafirisha gesi asilia hadi kiwanda cha kuchakata gesi kilichopo Msimbati, Madimba mkoani Mtwara.

Ameeleza katika kitalu cha Ruvuma Gesi iliyogunduliwa na kuhakikiwa ni futi za ujazo bilioni 1.6.

Kuhusu Hati ya Makubaliano kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu midogo ya kubadilisha Gesi Asilia kuwa kimiminika (Mini-LNG), ameeleza kuwa, mradi utakuwa wa kwanza kufanyika nchini na utawezesha kupunguza kiu ya watanzania kutumia Gesi Asilia hata kwa maeneo yaliyo mbali na miundombinu ya mabomba na hivyo kuchochea matumizi ya nishati safi nchini.

Hafla hiyo ya utiaji saini makubaliano imehudhuriwa pia na Wabunge Mkoa wa Mtwara, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mohamed Fakihi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC, Balozi Ombeni Sefue na Menejimenti ya TPDC.
 
Kama wewe Mwananchi imekusaidiaje gesi asilia ya songosongo?
 
Back
Top Bottom