Kungekuwa na jinsi ya kuongeza "thank you" kwenye post moja ningekupa nyingi sana Bubu! you just nailed it!
Ndugu zangu;
Ngoja niende kwenye falsafa kidogo(rector wangu pale Peramiho atafurahi LOL)
Kuna vitu ambavyo tunaweza kuchagua na vitu ambacho hatuna uwezo wa kuchagua hata kama tungetaka vipi. Vitu hivi ambavyo tunavyo lakini hatukuvichagua ni vitu ambavyo sheria za fizikia, kemia, na elimuviumbe zinakataza. Vitu hivi ambavyo hatukuwa na uchaguzi navyo mara nyingi tunajikuta hatuvipendi na tunatamani tungepewa uchaguzi wa aina fulani. Lakini kanuni zijulikanazo ambazo zinatawala ulimwengu zinatukatalia uchaguzi huo.
Ni kwa sababu hiyo basi hatuna uchaguzi wa wapi tutazaliwa. Ni wengine na mazingira yanayochagua wapi tutazaliwa. Tungekuwa na uchaguzi wengine tusingependa kuzaliwa nyumbani ingekuwa bora hospitalini; wengine tungependa kuzaliwa angalau nyumbani kuliko ndani ya basi (I witnessed one of those); lakini katika hali zote ni watu wengine waliamua au mazingira yaliamua tukazaliwa tulikozaliwa; Sisi wenyewe hatukuwa na uchaguzi.
Hatukupewa uchaguzi wa mji na nchi gani tungezaliwa au Taifa gani tungezaliwa. Labda wengine tungetamani "angalau" tungezaliwa watu weusi hivi hivi lakini tungezaliwa Marekani au Ulaya. Lakini tusingependa kuzaliwa weusi huko India au China! Wengine tunaona ingekuwa bora kama tungezaliwa tukiwa wazungu maana kuwa mzungu kuna "kaujiko" na "ubora" wa aina fulani. Bahati mbaya, hatukupewa uchaguzi huo.
Ningeweza kuorodhesha mengine mengi ambayo yanathibitisha kuwa kuna mambo katika maisha yetu ambayo hatuwezi au hatukuweza kuyachagua na tunajua kuwa kama tungekuwa na uchaguzi basi tungechagua kitu tofauti.
Ukweli huo kuwa kuna vitu ambavyo mwanadamu hana uwezo wa kuchagua (ingawa anaweza kumchagulia mwingine) ni ukweli ambao unakubalika kuwa ni kweli ukienda China, Alaska au Amazoni. Lakini pia kuna vitu vingine ambavyo mtu mwingine anaweza kutuamulia nacho ni kama tuko huru au la, tunaishi vipi n.k
Hata hivyo kuna kitu kimoja ambacho mwanadamu ana uchaguzi nacho na hakuna pingu, au mawingu yoyote yanayoweza kumuondolea. Kitu hakijalishi kama huyo mtu yuko Sahara au Kalahari. Kitu hicho ambacho mwanadamu anaumiliki kamili hakijalishi kama huyo mtu ni mtumwa au huru, mweusi au mweupe, msomi au simsomi. Kitu hicho ni uwezo wake wa kufikiri na kuamua yeye anajitambuaje (self perception)
Mtu anaweza kujiona duni na mnyonge; anaweza kujiona hafai na hastahili, anaweza kujiona dhaifu na asiyeweza. Kujiona huko kunatokana siyo na matendo ya nje lakini na fikara zake za ndani. Katika mfano wa Kunta Kinte hapo juu utaona kuwa Kunta hakukubali kuitwa "Toby" licha ya mijeredi mingi. Yeye alijitambua kama "Kunta Kinte". Lakini baada ya kufanywa duni na vitendo vingine alizisalimisha fikara zake kwa kukubali kuwa yeye ni "Toby". Kwa kufanya hivyo alizisaliti fikara zake kwa ajili ya kukwepa maumivu.
Mtu anayekubali fikra za kujiona duni hujikuta anajenga hisia ya ya kujiona duni (inferiority complex). Mtu anayejiona duni anakubali vitu jinvi "vilivyo" na anaona chochota anachokipata (chema au kibaya)) kuwa ni mastahili yake. Akiona barabara mbaya anasema "ndivyo tulivyo"; bodi ya mikopo iliyo mbovu anasema "ndivyo tulivyo"; wanaiba EPA anasema "ndivyo tulivyo"; n.k yaani mtu mwenye fikra za kujiona duni haoni mwanga mbele yake bali giza tu! Huyo ukimpa watu awaongoze atawaongoza shimoni kwani hivyo ndivyo ilivyo!
Mtu huyo mwenye fikra hizo za "ndivyo tulivyo" hawezi kuongoza na siyo tu hawezi kuongoza hastahili kuongoza. Kwani na yeye ni mtu ambaye hawezi kubadili kitu. Kwanini abadili kitu wakati "ndivyo tulivyo"? Mtu mwenye mawazo ya kukubali hali halisi na ambaye anaona kuwa siyo tu ni vigumu kubadilika bali amechagua kukaa pembeni na kuona wengine wabadili hali hiyo ili aone "proof" kuwa sivyo tulivyo!
Ni kweli kuwa baadhi ya viongozi tulionao leo hii katika utumishi wa umma na hata sekta binafsi wana mawazo hayo yaliyosalimu amri. Mawazo ya mtumwa aliyekubali kuitwa Toby!
Lakini mimi ndugu zangu sijasalimisha mawazo yangu kwenye kambi ya waishio katika ulimwengu wa "ndivyo tulivyo". Mawazo yangu na fikra zangu ziko huru na hazitegemei matukio nje yake kuweza kuulinda uhuru wake. Mimi na nyinyi bila ya shaka tunaangalia vitu vile vile lakini tunafikia mahitimisho tofauti. Ya kwenu ni ya ya watu waliokubali kushindwa na kusalimu amri. Ni mawazo ya watu waliokata tamaa kuwa situ vitu jinsi vilivyo bali kuwa "ndivyo sisi tulivyo".
Na hapa suali la Bubu hapo juu lina uzito wake. Kama sisi ndivyo tulivyo kwanini tunasimama kukosoa na kutoa mapendekezo ya kufanya vitu tofauti? Kwanini tunasisitisha kuona mabadiliko wakati tumeshasema kuwa "ndivyo tulivyo". One can not predict the obvious! You can not prophecy and go out to fullfil that prophecy. Kama ndivyo tulivyo juhudi zetu zote na mazungumzo yetu yote na mijadala yetu yote hapa hasa ile inayohusu mabadiliko ya uongozi ni bure tu!
Na hapa naweza kuyasikia maneno ya Lowassa kuwa "nimeonewa" yanapokuwa na ukweli. Kama ndivyo tulivyo kwanini Lowassa kajiuzulu na Baraza kuvunjika? Kama ndivyo tulivyo kwanini tunataka watu wa EPA wasiishie kurudisha fedha tu bali pia watiwe pingu? Kama ndivyo tulivyo kwanini tunataka Balali arudi na kutiwa pingu asimame Kisutu?
Nyinyi mliokubali kuwa ndivyo mlivyo hiyo ni haki yenu na hizo ni fikra zenu ambazo kama nilivyosema hapo juu mmezichagua na kuzikubali. Ni haki yenu kuzitetea na kuzisimamia kwa sababu kama hivyo ndivyo mlivyo hamuwezi kubadilika na hivyo mnathibitisha wenyewe kwa kauli zenu kuwa ndivyo mlivyo.
Kwa vile hivyo ndivyo mlivyo hakuna mtu anayeweza kuwashawishi vinginevyo au kusababisha mtazame vitu kwa namna nyingine ya matumaini zaidi na ya kutaka mabadiliko ya kweli. Hakuna hoja au vioja vinavyoweza kusababisha mabadiliko ya fikra ndani yenu isipokuwa nyinyi wenyewe mtakapoona kwenye ushawishi wa fikra zenu kuwa vitu vinaweza kubalishwa na kama vinaweza kubadilishwa basi sivyo tulivyo!
Mimi, Fundi, Bubu, na wengine ambao tumekataa maxim hiyo ya "ndivyo tulivyo" tumechagua katika fikra zetu kutowekwa kwenye chupa na kufungiwa humo! Tumekataa kuwekwa kwenye kisanduku kibovu cha "ndivyo tulivyo" na kuambiwa ati hatutoki humo. Kwa ghadhabu na makelele, na kama watu walio na kisasi tunakataa, tunapinga, tunakejeli, na kudharau fikra hizo dhaifu ambazo hazina msingi katika ukweli.
Hatuwezi kuwa wazungu, hatuwezi kubadili nasaba zetu. Lakini tunachagua fikra zetu kuwa na sisi ni watu sawa, wenye haki sawa. Ndiyo maana mapambano haya yanaitwa mapambano ya kifikra siyo mapambano ya nani mzuri, nani anaweza n.k Ndiyo maana nilisema huko nyuma kabla ya kuwashinda kwenye sanduku la kura ni lazima tuwashindwe kwenye fikra!
Lakini kama wapo watu wengi wenye mawazo ya "ndivyo tulivyo" basi ni rahisi kuelezea kilichotokea Kiteto; ni rahisi kuelezea vijana pale barabara ya Nyerere karibu na Scania watu wanafanya biashara hadi barabarani na hakuna Polisi anayeweza kuwaondoa; ni rahisi kuelezea kwanini badala ya kuwafikisha wahalifu mahakamani tunakaa meza moja na kujadiliana nao ni adhabu gani tunaweza kuwapa!
Ni lazima tushinde kwenye fikra kwanza kabla hatujaweza kushinda kwenye ofisi zao na kubadili mikataba; ni lazima tushinde kwenye fikra kwanza kabla hatujadhaminiwa kuongoza nchi. Kabla hamjaona vitendo vinavyoonesha mabadiliko ni lazima mabadiliko ya fikra yatangulie kwanza kwa sababu wazo hutangulia kitendo!
Msitarajie kuona mabadiliko ya utendaji kama hakuna mabadiliko ya fikra. Ninatoa mwaliko huru na kwa wote ambao bado wamefungwa na minyororo ya "ndivyo tulivyo" kuivunja na kuikana na kuungana na fikra za "sivyo tulivyo" ili kwa pamoja tuweze kuanza kubadili mtu mmoja baada ya mwingine!
Ninawakaribisha kwenye mapambano ya kifikra ambako hakuna kusalimu amri wala kurudi nyuma ni mbele kwa mbele hadi Watanzania wote wanajiamini, wanatambua kuwa wanaweza, na wanaanza kutenda wakijua kuwa wanastahili vitu vizuri na viongozi wazuri!!!
M. M.