Ushuhuda: Jinsi mwenye nyumba alivyoshughulikia Chanagamoto ya mpangaji wake ya uharibifu wa nyumba

Aliko Musa

Senior Member
Aug 25, 2018
156
240
Mwezi wa disemba mwaka 2021 nyumba nilipokea simu kutoka kwa msimamizi wa nyumba ya kupangisha.

Hitaji la msimamizi na mwenye nyumba huyu lilikuwa ni kujifunza mbinu bora za kupambana na wapangaji waharibifu.

Aliendelea kutoa maelezo kuwa hajawahi kutana na changamoto ya kutolipwa kodi ya nyumba lakini karibu kila mpangaji hupelekea uharibifu wa nyumba.

Uharibifu huu hupelekea kutumika kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya ukarabati. Hii humfanya ashindwe kufurahia kodi anayokusanya kutoka kwa wapangaji wake.

Wapangaji wake walikuwa wanapigilia misumari kwenye kuta za nyumba kiasi kwamba kila mpangaji akiondoka ni lazima ufanye ukarabati.

Wengine walikuwa wanachafua rangi za kuta za nyumba kiasi kwamba rangi hupoteza kabisa mvuto kutoka kwa wapangaji wengine.

Aliendelea kusisitiza kuwa amechoshwa na tabia hii kiasi kwamba haoni tena umuhimu wa kumiliki nyumba za kupangisha.

Swali; je utafanyaje ili kukabiliana na chanagamoto za wapangaji waharibifu wa nyumba au vyumba walivyopanga?.

Mbinu Za Kuboresha Usimamizi Wa Nyumba Za Kupangisha.

Moja
Mkataba Wa Upangishaji.

Unatakiwa kuandaa mkataba mzuri ambao una manufaa kwa pande zote mbili. Lakini uwe ni mkataba ambao utasaidia kutatua migogoro kati ya wapangaji na msimamizi wa nyumba au mwenye nyumba.

Kwenye mtandao huu wa UWEKEZAJI MAJENGO nimeandaa zaidi ya mikataba mitano (5) ya upangishaji. Kupitia mikataba hii utaweza kujifunza mambo ya msingi ya kuzingatia kwenye mikataba yako.

Hakikisha mkataba wako wa upangishaji umepitiwa na wakili mzoefu kwenye uwekezaji huu.

Pia, manufaa ya kifedha unahitaji kumshirikisha mshauri mbobezi ili akushauri vipengele muhimu vya kuifanya nyumba yako iingize kipato kizuri.

Mbili
Mahusiano Bora Na Wapangaji.

Chanagamoto nyingi sana zitachelewa kukifikia kwa sababu ya mahusiano mabaya yaliyopo kati yako na mpangaji wako.

Hii itapelekea hasara kwa baadhi ya chanagamoto ambazo ulitakiwa kuzitatua haraka.

Jenga mahusiano mazuri na wapangaji wako. Hii itakusaidia kufahamu mambo mazuri na mambo mabaya.

Mfano; mwenye nyumba mmoja alikuwa anaishi kwenye nyumba na familia yake. Nyumba ya nyumba hiyo ziliunganishwa fremu tano (5) kwa ajili ya biashara.

Kwa muda wa miezi kumi (10) alikuwa hafahamu ni aina gani ya biashara ambayo hufanywa na wapangaji wake hao watano.

Mpangaji mmoja alikuwa ameanza kufanya biashara ya madawa ya kulevya. Hii ni biashara ambayo sio halali kwa hapa Tanzania.

Hatimaye shauri lilifunguliwa dhidi ya mpangaji na mwenye nyumba kuhusu biashara hiyo haramu.

Kujenga mahusiano mazuri kati yako na wapangaji husaidia hata kuwafanya wapangaji wako wawe na amani kuendelea kuishi kwenye nyumba yako.

Mahusiano mazuri hugusa sehemu ambayo mkataba hauwezi kugusa. Kuwa na mkataba wa upangishaji haindoi ule umuhimu wa kujenga mahusiano mazuri na wapangaji wako.

Vilevile kuwa na mahusiano mazuri haiondoi umuhimu wa kuandaa na kusaini mikataba rafiki kwenu wote.

Haijalishi una mahusiano mazuri kiasi gani na wapangaji wako unahitaji kuwapangisha kwa kuingia makubaliano mazuri ya kimaandishi ambayo kwa lugha nyingine tunaita mikataba ya upangishaji.

Tatu
Kufanya Ukarabati Wa Mara Kwa Mara.

Usisubiri wapangaji waanze kuvujiwa na maji ya mvua ndio uanze kutafuta mafundi ya ukarabati wa paa nyumba.

Nyumba ambayo hufanyiwa ukarabati mara kwa mara itakuwa na kasoro chache zinazohitaji kufanyiwa ukarabati.

Nyumba inayovutia na yenye thamani kubwa itakaliwa na wapangaji wanaojielewa na wenye kujiheshimu. Ingawa hii haiwezi kuwa mara zote kwa sababu tabia ya mtu haingalii cheo wala kiasi chake cha kipato.

Nne
Kuwafanyia Tathimini Wapangaji Wanaotaka Kulipia.

Wapangaji wengine wameshindikana kabisa hawawezi kusaidiwa kwa mkataba mzuri wala mahusiano mazuri.

Wao ni sikio la kufa. Wapangaji hawa hawana dawa. Dawa pekee inayowafaa ni kutowakubali wawe wapangaji wako.

Jambo hili limekuwa gumu kufanyika kwa mazingira yetu ya Tanzania. Lakini pale inapowezekana kupata taarifa sahihi za wapangaji walioshindikana, usiwe mtu wa kuwaonea huruma.

Haya ndiyo mambo yanayoweza kukusaidia kuboresha usimamizi wa nyumba zako za kupangisha.

Tukio La Mpangaji Na Mwenye Nyumba.

Siku ya tarehe 08-februari-2022 nilipigiwa simu na mteja wangu ambaye alikuwa ni mwenye nyumba.

Mteja alitaka kunijulisha kuhusu mpangaji wake ambaye aliamua kutoroka kwenye chumba huku akiwa hajamalizia kodi ya miezi miwili (2).

Mpangaji huyu alikuwa na historia ya kutokuwa mwaminifu wa kulipia kodi ya chumba kwa wakati unaotakiwa.

Mbaya zaidi mwenye nyumba alikuwa anafahamu usumbufu wa mpangaji huyo hata kabla hajawa mpangaji wake.

Aliamua kumhurumia kwa sababu alifukuzwa kwenye nyumba ya karibu yake. Mpangaji alikuwa na mke mwenye ujauzito na mtoto mmoja mdogo.

Mke wake hakuwa na kazi ya kueleweka akaamua kuwakubalia ila aliwaonya wawe waaminifu wasiwe na tabia walizokuwa nazo kutoka kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi kabla.

Huyu ndiye mpangaji ambaye aliamua kutoroka na jumla ya kodi ya nyumba ya miezi miwili (2).

Pia, mpangaji aliamua kubeba kila kifaa kilichotumika kwenye kusuka waya za umeme. Mpangaji huyo aling'oa hata soketi na waya zote zinazopitisha umeme.

Alifanya matukio yote haya muda wa saa nne kasoro usiku. Mwenye nyumba aligundua kuwa mpangaji wake ametoroka siku iliyofuata.

Mwenye nyumba akaamua kuachana naye na kuandelea na kutafuta wapangaji wengine.

Lengo la kukushirikisha tukio hili ni kukuandaa wewe unayependa kujenga utajiri mkubwa kupitia nyumba za kupangisha.

Kwa kufahamu haya utaweza kujifunza kupitia makosa ya wawekezaji wengine. Utaweza kujiandaa kisaikolojia juu ya chanagamoto za wapangaji na jinsi ya kukabiliana nazo.

Ni vigumu zaidi kusimamia nyumba kuliko hata kununua kwa sababu jambo la kununua au kujenga nyumba ni la mara moja wakati jambo la kusimamia wapangaji ni jambo la maisha yako yote.

Rafiki yako,

Aliko Musa.

WhatsApp; +255 752 413 711
 
Habari mkuu,Naomba unielimishe juu ya yafuatayo......... 1.Namna bora ya kumbana mpangaji wa aina hiyo asiweze kufanya uharibifu wa nyumba kwa kutoboa toboa kuta za nyumba,uharibifu wa rangi na vinginevyo. 2.Njia bora kuzuia kitendo cha mpangaji kukimbia na deni lako wewe mwenye nyumba kama ulivyo elezea hapo juu kwenye hicho kisa kilicho mkuta mateja wako
 
Back
Top Bottom