Na hili shairi la 'Ujasiri wa Rais Nyerere' katika Tujifunze Lugha Yetu Kitabu cha 9 ndio funga Kazi kwenye Medani ya Propaganda!
1. Sisi Watanzania hakika yatupasa kuwashukuru mashujaa,
Katika nchi yetu wengi walijaribu na kwa kweli walitufaa,
Heko kwa shujaa wetu mkuu Rais Nyerere mwana wa Afrika,
Yeye hakika mjasiri na mtetezi wetu katika Tanzania.
Kibwagizo
Mengi aliyafanya Tanzania,
Na hata katika nchi za nje,
Uingereza, Amerika, pote katutoa,
Tuondoe utumwani.
2. Yeye mwalimu wetu mwana wa kizalendo apendaye ujamaa.
Kazaliwa Musoma mwaka ishirini na mbili kijiji Butiama,
Alijielimisha sana apate elimu bila ya kuchoka,
Mwaka Arobaini na tano, kapata shahada yake ya ualimu.
3. Kuipata shahada mwaka arobaini na tano, kafufua chama TAA.
Chama hiki cha TAA alikitumia kutuunganisha wote,
Alijitolea kufanya kazi zote bila tofauti,
Kukiongoza chama hiki pamoja na kufundisha mashuleni.
4. Kufuzu kwa mwalimu na kupata shahada hakukumtosheleza,
Arobaini na nane alifuzu mtihani chuo kikuu cha London,
Alijiandikisha tena katika chuo kikuu cha Edinburgh,
Na kupata shahada ya M.A. mwaka hamsini na mbili.
5. Kuwa kwake Ulaya, shujaa mwalimu, hakujirudisha nyuma,
Alikuwa tayari katika kupigana na beberu Mwingereza,
Hakuacha kupigania haki na usawa wa binadamu,
Alisema ukweli wote kwa hayo wanayotenda Wakoloni.
6. Vibaraka wakubwa mwaka hamsini na tano walitumwa UNO,
Nia za vibaraka ni kuitokomeza nchi yetu Tanzania,
Viongozi wetu wa TANU, walizitambua hila zao zote,
Naye shujaa wetu Mwalimu, alifaulu na kuwabwaga wote.
7. Aliporudi UNO, alijiuzulu kazi za kiualimu,
Na akajizamisha kwenye chama TANU bila kujali ijara,
Alionyesha ujasiri kufanya kazi isiyo na kipato,
Hakika hiki ni kitendo kilichokuwa cha kishujaa sana.
8. Shujaa wetu Nyerere alikuwa tayari kumshambulia mkoloni,
Alisema ukweli bila kufichaficha mabaya yao vibaraka,
Hakuwajali vibaraka, mabwana shauri wala Magavana,
Ingawa walimshambulia alikurupuka mikononi mwao.
9. Hamsini na nane, wajumbe wa TANU walikutana Tabora,
Kutaka kususia uchaguzi mkuu kwa sababu ya mseto,
Mwalimu akawaelimisha wajumbe umuhimu wa uchaguzi,
Na TANU ilivigombea na kuvinyakua hivyo viti vyote.
10. Hapo sitini na moja Mwalimu Nyerere akawa Waziri Mkuu
Baada ya siku chache hapo Januari alikiacha cheo chake,
Nia iliyo kubwa sana ni kuimarishwa kwa chama cha TANU
Na pia kutoa uhuru kwa aliye tayari kuiongoza nchi.
11. Ushujaa mwingine ni kuiunganisha Tanganyika na Unguja
Aprili sitini na nne, Marais wawili walikubali muungano,
Nao walishikana vema, bila kujali vitisho vyovyote,
Na Muungano uko imara, heko kwa viongozi wa Tanzania.
12. Hakika ya thabiti Rais Nyerere katika kauli zake,
Mwaka sitini na tano, Umoja wa Afrika ulipitisha Azimio,
Kususiwa kwa Mwingereza kutoa Rhodesea kwa Ian Smith,
Nyerere hakurudi nyuma, kawa mmojawapo kuvunja uhusiano.
13. Mjerumani naye wa huko Magharibi alitishia Tanzania,
Iwapo Tanzania itamkaribisha Mjerumani Mashariki,
Shujaa Mwalimu Nyerere hakugutuliwa na usemi wao,
Kawaambia kuviondoa vitu vyao vya Kijerumani.
14. Lengo lake Mwalimu kwa wana Tanzania ni kujenga Ujamaa,
Mwaka sitini na saba, mwezi Februari, Azimio katangaza,
Kuwaondoa wanyonyaji wa kila aina nchini Tanzania,
Makabaila na Mabepari na hao makupe wasionekane.
15. Nasi Watanzania, tuko nyuma yako ewe Mwalimu Nyerere,
Hatutarudi nyuma utuelimishapo na kutuongoza vema,
Twajua utaleta mengi, yenye manufaa nchini Tanzania,
Hata na Afrika ndima na Ulimwengu wote utaelimishwa.