Kwanza alitaka kuizima lakini akakwama. FISADI Mkubwaaaaaaa
Chenge akwama kuzima hoja ya Richmond
na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Miundombinu, Andrew Chenge, jana alijaribu bila mafanikio kuzima hoja ya kuwasilishwa kwa taarifa ya kamati teule ya Bunge iliyochunguza mchakato wa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura ulioipa ushindi Richmond Development Company LLC ya Houston, Texas, Marekani mwaka 2006.
Orodha ya shughuli za Bunge kwa kikao cha saba jana, ilionyesha kuwa kabla ya kipindi cha maswali na majibu, kamati hiyo iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe (CCM), itawasilisha taarifa yake.
Baada ya dua, taarifa ya kuwasilisha ripoti hiyo ilisomwa na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Stela Manyanya (CCM).
Lakini, baada ya kipindi cha maswali na majibu, baada ya Spika kumuomba Katibu alieleze Bunge shughuli inayofuata, huku ratiba ikionyesha kuwa huo ulikuwa ni wakati wa kuwasilishwa kwa ripoti kamili ya Richmond, Chenge alisimama akitaka mwongozo wa Spika.
Alipopewa nafasi, Chenge alisema wakati wa kikao cha kupewa maelezo ya shughuli za mkutano wa 10 wa Bunge kilichofanyika Januari 28 mwaka huu, wabunge walielezwa kuwa kulikuwa na miswada sita ya serikali itakayowasilishwa.
Akitumia kifungu cha 30(4) cha Kanuni za Bunge, Chenge alisema kuwa kwa kawaida shughuli za serikali hupewa kipaumbele katika mkutano wowote wa Bunge.
Chenge alisema kuwa kama yalikuwepo mashauriano baina ya Ofisi ya Spika na Serikali, hakuwa na taarifa kuwa miswada ya serikali ilikuwa imemalizika kujadiliwa na hivyo kushangaa kwa nini inaletwa ripoti ya kamati kabla miswada ya serikali haijajadiliwa yote.
Lakini akijibu hoja hiyo, Spika, Samuel Sitta, alisema kwa mujibu wa kifungu cha 34 cha kanuni hizo hizo, utaratibu wa shughuli za Bunge unaongozwa na maamuzi ya Kamati ya Uongozi ya Bunge.
Alisema katika kikao cha kamati hiyo, ambacho Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), alishiriki kikamilifu, kiliamua kuwa hoja hiyo iletwe bungeni, hasa kwa kuzingatia mazingira yaliyotokana na mjadala katika semina ya wabunge iliyofanyika Jumapili iliyopita.
Awali, Spika alisema mjadala wa semina hiyo, ambao kupitia kwayo wabunge walikataa kuwasilishwa kwa miswada miwili kuhusu nishati, ni moja ya sababu kadhaa zilizomfanya asitishe safari yake ya nchini Marekani.
Alisema katika semina hiyo wabunge walionyesha kuwa suala la ripoti ya Richmond lilikuwa muhimu mno kiasi kwamba ilimlazimu yeye kuahirishaa safari hiyo, ili kuhakikisha kuwa suala hilo linafikishwa bungeni haraka iwezekanavyo.
Alisema kwa kuwa alikataza masuala hayo kujadiliwa wakati hayupo, hakuona sababu ya kuendelea na safari, wakati dalili zote zikionyesha kuwa suala hilo linapaswa kujadiliwa haraka.
"Spika ambaye anakimbia wakati huku nyuma nyumba inaungua, hafai," alisema na kubainisha kuwa kukataza kwake masuala hayo kujadiliwa wakati hayupo ilikuwa ni aina ya kuonyesha uwajibikaji wake yeye kama Spika.
Alisema Spika ndiye anayewajibika kwa masuala yote yanayolihusu Bunge, hivyo isingekuwa busara kumwachia Naibu wake, Anne Makinda, kusimamia mijadala ya masuala nyeti kama hayo.
Hata hivyo, Sitta aliomba radhi kwa lugha aliyoitumia wakati akitangaza suala hilo wiki iliyopita, ambayo kwa kiasi fulani ilionyesha dharau kwa naibu Spika.
Baada ya Dk. Makyembe kuwasilisha taarifa hiyo, Spika aliliahirisha Bunge hadi leo, ili kuwapa nafasi wabunge kuisoma taarifa hiyo yenye zaidi ya kurasa 160 pamoja na vielelezo vingine kadhaa, kabla hawajaanza kuijadili leo baada ya kipindi cha maswali na majibu.
Kwa kuonyesha kuwa hataki kuwabana wabunge katika kuijadili hoja hiyo, Spika alisema anatoa siku mbili, leo na kesho kwa wabunge kuijadili hoja hiyo.
Mara baada ya kuahirisha Bunge, mawaziri kadhaa, wakiongozwa na Waziri Mkuu, Edward Lowassa, walionekana wakiwa katika majadiliano mazito ndani ya Bunge, huku wabunge wengine wakitoka nje.
Hata hivyo, chanzo cha habari kililieleza gazeti hili kuwa Karamagi ameshaandika barua ya kujiuzulu, lakini alikuwa bado hajaiwasilisha sehemu husika.
Akizungumza na gazeti hili nje ya Ukumbi wa Bunge, Waziri Mkuu mstaafu na Mbunge wa Mtera, John Malecela, alisema ameipokea ripoti hiyo kwa furaha.
Alisema ripoti hiyo inaeleza mambo mengi ambayo pamoja na masuala mengine, yanatoa nafasi kwa Watanzania kujirekebisha na kutafuta njia muafaka ya kwenda.
"Kama alivyowahi kusema Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, huu ni wakati, si kwa serikali ya CCM tu, bali kwa Watanzania wote, kujirekebisha," alisema Malecela ambaye pia alikuwa makamu mwenyekiti wa CCM kwa muda mrefu.
Dalili kuwa jana ilikuwa siku ya kihistoria kwa Bunge la Tanzania, kwa mara ya kwanza msafara wa Spika na makatibu wake kuingia bungeni asubuhi, uliongozwa na mpambe mwanamke.