Chenge anafunika ya Mkapa au kamati ya ufundi?
Chris Alan
Tanzania Daima
JANA baada ya Baraza la Mawaziri kuapishwa, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Joseph Mungai, alieleza kufurahishwa kwake na uteuzi wa aliyekuwa Naibu wake, Lawrence Masha, kuwa waziri kamili wa Wizara ya Mambo ya Ndani na Usalama wa Raia, zikiwa zimeunganishwa zilizokuwa Wizara ya Mambo ya Ndani na ya Usalama wa Raia.
Mungai alisema kwamba anajisikia kufarijika kwa kuwa alikuwa amedhamiria siku nyingi kwamba akifikisha miaka 65 atapumzika kazi ya uwaziri na kuganga yajayo.
Alisema kwamba alilala bweni moja na baba yake Masha, Dk. Masha, wakati wakiwa Sekondari ya Tabora.
Kwa maana hiyo si haki kuendelea na uwaziri hata kama watoto wao wana uwezo huo kwa sasa.
Mungai kama walivyo mawaziri wengine wazee kama Kingunge Ngomale - Mwiru, Harith Bakari Mwapachu na Dk. Juma Ngasongwa, ni viongozi ambao wamekuwako madarakani kwa muda mrefu, lakini kwa bahati mbaya wakawa wameshindwa kusoma alama za nyakati kwamba zama za sasa si za huko tulikotoka, kwa maana hiyo walishindwa hata kujipumzisha mapema katika harakati za kisiasa ambazo zinahitaji siha ya mwili na ubongo unaochemka. Siha ya mwili na ubongo unaochemka ni mambo muhimu katika kukabiliana na changamoto za ulimwengu wa sasa.
Kwa maana hiyo kuomba kwa kina Kingunge na Mungai kuenguliwa kwenye baraza la mawaziri hata kabla ya kujua mawazo ya Rais Jakaya Kikwete yalikuwa nini katika kuunda baraza jipya, inaweza kuchukuliwa kama hatua ya kutafuta kustaafu kwa heshima. Tunawapongea, japo walichelewa kutambua hilo!
Kwa maana hiyo, Rais Kikwete alifunuliwa bahati mpya na wazee hawa kwamba si lazima sasa kuendelea kuwarejesha wazee katika baraza jipya. Hii ilikuwa ni nyongeza ya pili ya bahati baada ya wabunge kumpa upenyo wa kufanya mabadiliko ya baraza la mawaziri kutokana na tuhuma za ufisadi.
Ripoti ya Kamati Teule ya Bunge ya Richmond iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe ikichangiwa hisia za wananchi za siku nyingi kama ambavyo zimesemwa kwenye vyombo vya habari, ilikuwa ni fursa ya kipekee kwa Rais Kikwete kupanga kwa umakini mkubwa baraza lake la mawaziri.
Hisia za wananchi kuhusu utendaji wa mawaziri wa Kikwete zilijidhihirisha mwaka jana serikali hiyo ilipotimiza miaka miwili baada ya Taasisi ya Utafiti na Demokrasia (REDET) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kutoa ripoti yake ya utafiti iliyoonyesha jinsi mawaziri wake walivyokuwa wanaboronga.
Kwa maana hii basi, Rais Kikwete alisaidiwa sana jinsi ya kubadili baraza lake la mawaziri, habari ya Richmond kwa bahati nzuri ilikuwa kusaidia tu kumalizia hisia zilizokuwa zimetamalaki mitaani kwamba mawaziri wengi wameoza. Mawaziri wengi wa Kikwete ni mafisadi. Ndiyo, ni mafisadi kama ripoti ya Richmond ilivyokuja kuthibitisha.
Kwa bahati nzuri, Rais Kikwete ametumia fursa hiyo kujaribu kujipanga upya, lakini kwa mshangao wa wengi mtu ambaye kwa miaka na miaka ametajwa kuwa katikati ya matatizo mengi ya mikataba ya nchi hii na sheria nyingine, Andrew Chenge, ameachwa kuendelea kuwa Waziri wa Miundombinu.
Watu wanajiuliza, kwa nini Chenge? Watu wanajiuliza ni kwa jinsi gani Chenge anaweza kujisafisha dhidi ya miswada ya kidikteta na kifisadi iliyowasilishwa bungeni na hatimaye kuwa sheria kama ile ya takrima na ile ya kuzuia kupingwa matokea ya uchaguzi kabla ya kuweka dhamana ya sh milioni tano?
Chenge alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanzia mwaka 1993 hadi mwaka 2005 alipokwenda kugombea ubunge kwenye Jimbo la Bariadi Mashariki.
Chenge ametajwa kuwa mkurugenzi katika kampuni ambayo inatuhumiwa kujinufaisha na fedha za ufisadi kutoka Benki Kuu ya Tanzania; Chenge ametajwa mara nyingi kwamba hakuisaidia sana serikali katika mchakato mzima wa ubinafshaji wa mashirika ya umma.
Akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alishindwa kuisaidia nchi yake isitumbukie katika mikataba mibaya kama ya IPTL. Alishindwa kuisaidia nchi yake isiingie kichwa kichwa katika mkataba wa kuuza hisa za Shirika la Ndege (ATC) kwa makaburu, kitendo ambacho si tu hakikunufaisha nchi, bali kiliiua kabisa ATC iliyobatizwa jina jipya la ATCL.
Chenge alitajwa kwenye orodha ya watuhumiwa wa ufisadi kwenye viwanja vya Mwembeyanga jijini Dar es Salaam, siku orodha ya aibu ilipoanikwa hadharani.
Kwa maana hii watu wanajiuliza, hivi Chenge huyu kwenye baraza la mawaziri jipya anatafuta nini? Anafanana na nani katika baraza hili jipya? Chenge analinda masilahi ya nani ndani ya mfumo wa Serikali ya Awamu ya Nne?
Kwa kuwa kuna kila kielelezo kinachoonyesha kwamba pamoja na mambo mengine, rais safari hii amezingatia usafi wa mtu kabla ya kumteua tena katika nafasi ya baraza la mawaziri, hasa ukiangalia sababu za kuachwa mawaziri kama Zakia Meghji, Basil Mramba, bila kusahau waliojitosa wenyewe mapema, yaani aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa; aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha; Chenge hana sifa za kuendelea kuwa katika baraza jipya.
Hana, kwa sababu anatuhumiwa, hajaweza kujisafisha na kusafishika dhidi ya tuhuma zinazomkabili kwa sasa.
Ni kwa jinsi hii, Watanzania hawana budi kuvaa ujasiri kwa kusema mambo mazito bila kutafuna maneno. Je, Chenge ni nguzo ya kusaidia kufunika maovu ya Serikali ya Awamu ya Tatu?
Hadi sasa ni dhahiri kwamba utawala wa Awamu ya Tatu umethibitika kuhusika na mambo mengi machafu.
Rais mstaafu Benjamin Mkapa amethibitika si tu kufuta sifa yake ya kuwa Mr Clean, bali pia alifikia hatua ya kula njama na mawaziri wake kuhujumu taifa.
Uuzaji wa nyumba za serikali kwa baadhi ya watumishi wake ni kitendo cha hujuma kwa taifa; kitendo cha Rais Mkapa kujianzishia biashara zake akiwa Ikulu kwa kutumia anuani ya Ikulu, kwa kutumia hadhi ya urais na hata kupata mikopo binafsi ya mamilioni kutoka benki bila kuwa na dhamana, ni matumzi mabaya ya wadhifa wa urais.
Yapo mambo mengi ambayo Mkapa hatayakwepa sana, haya hata aamue kuwa bubu kuna siku tu atawajibika kwayo. Tunachosema ni kuomba subira tu na Mungu atafungua njia. Hata Mfalme Suleimani aliyebarikiwa na Mungu alipovunja agano (kiapo), Mungu alimwadhibu, hili kwa Mkapa linasubiri muda tu, mlango utafunguliwa.
Chenge anakumbukwa kwa mengi, ujeuri ulikuwa wake, alipata kuwaambia wabunge kwamba kiti cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali kimejaa, pale alipohojiwa sababu ya kubadili sheria kinyemela bila kuzifikisha bungeni.
Sheria hii ilikuwa ikihusu iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ambayo Serikali ya Awamu ya Tatu bila soni waliitoa bure kwa makaburu.
Inawezekana kwamba watawala sasa wanashindwa kusoma alama za nyakati, kwa maana hiyo ni jukumu la umma sasa kuamka na kusema kwa kinywa kipana kwamba hata kama rais anayo madaraka ya mwisho kumteua yeyote kushika wadhifa huo, asilani haivumiliki watu wenye mikono michafu waruhusiwe kukalia ofisi za umma ambazo zinaendeshwa kwa kodi za wananchi.
Cheo ni dhamana, na wenye dhamana ni wananchi, kama imani kwa kiongozi yoyote imepotea, hakuna sababu ya kusuritishana, kiongozi huyo anawajibika kukaa pembeni. Vinginevyo Rais Kikwete awaeleze Watanzania, Chenge ni wa nini hasa, amemrejesha kwenye baraza jipya, kwani serikalini kuna kamati ya ufundi kama zile za Yanga na Simba ili ieleweke kwamba Chenge ana kazi maalumu ambayo umma hauijui licha ya kukabiliwa na tuhuma zote hizi?