Habari Zinazoshabihiana
*Apewa kinga ya Bunge na atoboa siri zote
*Vigogo waandaliwa kuburuzwa mahakamani
WAZIRI wa zamani wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Bi. Clare Short, amelithibitihia Bunge la nchi hiyo, kuwa upo ushahidi mzito kuwa rushwa ilitumika katika kuchagiza Serikali ya Tanzania kununua rada iliyogharimu zaidi ya sh. bilioni 40 mwaka 2002.
Bi. Short ambaye alipinga kwa nguvu zote ununuzi wa rada hiyo akisema ni mzigo mkubwa na usio na manufaa kwa nchi changa kama Tanzania, alivuta hisia za wabunge wengi, alipokuwa akichangia mjadala huo, juzi usiku.
Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian la Uingereza toleo la jana na taarifa kutoka Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Bi. Short kabla ya kutoa ushuhuda huo mzito, kwanza aliomba kuhakikishiwa kinga ya Bunge ya kutoshitakiwa kwa maneno ambayo angeyasema.
Akilihutubia Bunge hilo, Bi. Short alisisitiza kuwa suala la kutumika rushwa katika ununuzi huo lilikuwapo na kwamba alipewa siri za ndani kutoka Idara ya Kuchunguza Makosa ya Ulaghai (SFO) ya Uingereza inayochunguza suala hilo, ikithibitisha.
"SFO wamemthibitishia Clare Short kuwa kuna nyaraka nzito zinazoonesha kwamba rushwa ilitumika katika uuzaji wa rada kwa Serikali ya Tanzania," lilisema The Guardian likinukuu alichokisema mwanasiasa huyo bungeni na kusema upo uwezekano wa baadhi ya vigogo kufunguliwa kesi.
Bi. Short alikaririwa zaidi akisema hata baadhi ya viongozi wa Serikali ya Uingereza walijihusisha katika kufanikisha ununuzi huo.
Aliuita ununuzi huo kuwa ni 'uchafu' na kuomba wabunge waunganishe nguvu zao kutaka sheria kali zaidi zitungwe kuibana Serikali katika aina ya mauzo ya vifaa vya kijeshi itakayopaswa kuruhusu siku zijazo.
"Serikali ya Tanzania ingefurahi kama Serikali ya Uingereza (ili kuonesha kwamba nayo haikufurahi juu ya mauzo ya rada hiyo) ingewanyima wauzaji hao (BAE) leseni ya usafirishaji, kwa kigezo kwamba ingeathiri maendeleo ya Taifa hilo changa (Tanzania)," alikaririwa akisema Bi. Short.
Bi. Short alisisitiza kuwa hata mkopo ambao Tanzania iliupata kutoka benki ya Barclays ili kununua rada hiyo, ulikuwa na walakini, kwani Benki ya Dunia ilidanganywa hasa juu ya ukubwa wa mkopo wenyewe.
Bw. Andrew Mitchell ambaye ni Waziri kivuli wa Wizara ya Maendeleo ya Kimataifa, naye alitilia nguvu maoni ya Bi. Short kwa kuiponda rada hiyo, akisema Tanzania imeuziwa mtambo wa kizamani ambao hautaweza kuisaidia kama inavyodhani.
Alipobanwa katika kikao hicho, Waziri wa sasa wa Maendeleo ya Kimataifa ambaye mwaka 2002 alikuwa msaidizi wa Bi. Short, Bw. Hilary Benn, alikataa kuzungumzia chochote juu ya tuhuma, kwamba kuna kamisheni ya sh. bilioni 12 iliyotolewa na kampuni ya BAE Systems, ili kuchagiza ununuzi wa rada hiyo, ila akatetea kuwa Tanzania haijaathirika kiuchumi.
"Kabla ya kuuziwa hiyo rada, Serikali ya Tanzania iliulizwa kama kusingekuwa na madhara makubwa kwenye uchumi wao, ikasema hakuna," alisema Bw. Benn huku akikwepa pia kuzungumzia suala kuwa rada hiyo ni mbovu na teknolojia yake imepitwa na wakati.
Katika hatua nyingine, ilibainika kupitia kikao hicho cha Bunge kwamba tayari kampuni ya BAE imeanza kuchunguzwa pia nchini Afrika Kusini, inakodaiwa kutoa kamisheni zinazofikia zaidi ya sh. bilioni 100 kwa wanasiasa wa ANC, ili kupata mikataba na zabuni mbalimbali kuanzia mwaka 1995.
Tayari Idara ya Uendeshaji wa Mashitaka na Upepelezi ya Afrika Kusini, Scorpions, imeanza kushirikiana na wenzao wa Uingereza kufanya uchunguzi huo.
Mbunge wa chama cha upinzani cha Independent Democratic, Bi Patricia de Lille, amejitolea kwenda London, Uingereza, kutoa ushahidi wa vitendo hivyo vya rushwa kati ya BAE na baadhi ya maofisa wa ANC