Serikali imelala usingizi wakati huyu fisadi anaachwa ile asambaze uwongo wake. Lowassa naye alifanya hivyo. Angekuwa amewekwa rumande huu usanii usingetokea
Chenge aanza kujisafisha
* Aenda kujieleza kwa wapigakura wake
* Wapambe wamwandalia mapokezi makubwa
* Wasema ataeleza sababu za kujiuzulu
* Safari kuanzia mkoani Mwanza
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Mwananchi
BAADA ya kukumbwa na tuhuma nzito za ufisadi, Andrew Chenge, sasa ameamua kwenda jimboni kwake Bariadi Magharibi, kujisafisha kwa wapigakura wake.
Mtindo kama huo ulitumiwa pia na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, ambaye baada ya kujiuzulu katika mkutano wa 10 wa Bunge la Februari alikwenda jimboni kwake Monduli ambapo alipokewa na watu na magari mengi, kitendo ambacho kilitafsiriwa kuwa alikuwa anajisafisha kutokana na kashfa ya Richmond.
Ziara hiyo ya Chenge kwenda jimboni ni ya kwanza tangu aanze kuchunguzwa na makachero wa Taasisi ya Kuchunguza Makosa Makubwa ya Jinai ya Uingereza ya Serious Fraud Office (SFO).
Uamuzi huo wa Chenge pia kufanya ziara jimboni kwake umekuja ikiwa ni wiki moja baada ya kuzushiwa kifo.
Habari zilizopatikana kutoka jijini hapa zilisema Chenge alitarajiwa kuwasili Bariadi jana usiku akitokea Mwanza.
Taarifa hizo ziliongeza kwamba, Chenge ambaye alijiuzulu wadhifa wa Waziri wa Miundombinu baada ya kukutwa na Sh1.2 bilioni katika akaunti yake katika kisiwani Jersey, zinazohusishwa na biashara ya kifisadi ya rada, pia atawaeleza wananchi wake sababu za kujiuzulu kwake.
Tumemwandalia mapokezi makubwa, kwanza ni kwa ajili ya kuja kuwathibitishia wapigakura wake kuwa yuko hai, kutokana na uzushi kuwa amefariki dunia," kilisema chanzo hicho na kuongeza:
"Lakini pia kuwaeleza wapigakura wake watapenda kujua sababu ya yeye kujiuzulu kwake, maana yamekuwa yakisemwa mambo mengi,? alieleza msemaji mmoja kutoka Bariadi ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Habari zaidi zilieleza kwamba, Chenge atakwenda katika jimbo hilo ambako baadhi ya watu wanaojiita wafuasi wake wamemwandalia mapokezi makubwa ya kumsafisha na tuhuma za ufisadi zinazomkabili.
Hata hivyo, pamoja na kuandaliwa maandamano hayo, huenda yakageuka mwiba mchungu kwake kwa kuzomewa kwani eneo hilo ni ngome ya chama cha upinzani cha United Democratic (UDP).
Mara baada ya Chenge kujiuzulu, wananchi wa jimbo hilo waliandaa maandamano ya kumpongeza kuachia ngazi kwake. Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, Chenge bado anakabiliwa na wakati mgumu kuweza kujisafisha, kutokana na tuhuma za ufisadi zinazomkabili kuwa kubwa.
Chenge mbali ya kukabiliwa na tuhuma za kujipatia mabilioni hayo ya pesa kwa njia ya rada, pia anatuhumiwa kuiingiza nchi katika mikataba mibovu.
Miongoni mwa mikataba mibovu inayohujumu uchumi wa nchi hadi leo, ambayo Chenge alishiriki ama kutia saini au kushauri akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ni pamoja na Kampuni ya Uzalishaji Umeme ya IPTL, mabilioni ya Kampuni ya Tangold na mengineyo.
Chenge pia katika ziara hiyo atakabiliwa na wakati mgumu kutokana na uamuzi wake wa kuziita Sh bilioni 1.2 alizoficha Jersey kuwa ni 'vijisenti', wakati jimboni kwake, baadhi ya wapigakura hawana huduma za maji safi na salama, uhaba wa huduma bora za kijamii kama afya na elimu.
Hadi sasa uchunguzi dhidi ya tuhuma za Chenge kuhusiana na Sh1.2 bilioni zinazohusishwa na rada, umebaki wiki mbili kukamilika.
Lengo la makachero wa SFO ni kuona kama fedha hizo zinahusiana na kutoa kashfa ya ununuzi wa rada inayodaiwa kununuliwa kwa bei kubwa zaidi ya uwezo na ubora wake.