2007-09-19 08:37:14
Na Raymond Kaminyoge
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Siasa na Uhusiano wa Jamii, Bw. Kingunge Ngombale-Mwiru amesema kashfa zinazotolewa na wapinzani dhidi ya viongozi ni kutapatapa baada ya kushindwa uchaguzi na kulitumia Bunge.
Bw. Kingunge aliyasema hayo jana Ikulu, jijini Dar es Salaam katika mkutano na vyombo vya habari uliomshirikisha pia Waziri wa Habari, Michezo na Utamaduni, Bw. Mohamed Seif Khatib.
Alisema serikali haitachukua hatua yoyote itawaacha waendelee kuzunguka huku ikiendelea kutekeleza ahadi zake kwa wananchi.
Kauli ya Bw. Ngombale-Mwiru, imekuja siku nne baada ya umoja wa vyama vya upinzani unaoundwa na TLP, CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi, kutangaza majina ya vigogo waliodai kuhusika na ulaji na ubadhirifu wa fedha za umma zikiwemo za ujenzi wa majengo pacha ya Benki Kuu Tanzania (BoT).
`Wameshindwa uchaguzi wa 2005, wameshindwa kulitumia Bunge kumaliza hoja zao, sasa wanapita mitaani kuwachafua viongozi, lakini sisi hatutawafuata Mwembeyanga badala yake tunaendelea kuwaletea wananchi maendeleo,` alisema.
Aliongeza kuwa, Bungeni ndiyo mahali ambapo vyama vya upinzani vinatakiwa kuichachafya serikali, lakini siyo mitaani.
Alisema mafanikio ya serikali ya awamu ya nne, ndiyo yanayowafanya wapinzani kuona njia pekee ya kusikilizwa na wananchi ni kuwapaka matope viongozi wake.
Alisema kutaja majina ya viongozi, hakusaidii badala yake kama kuna ushahidi wa tuhuma zifikishwe mahakamani.
Alisema serikali ya CCM imeweka wazi kuwa, yeyote atakayekuwa na ushahidi wa kiongozi kuhusika na rushwa, atoe taarifa.
Aliwaambia wapinzani kuwa, wamesahau kwamba, demokrasia wanayoitumia ya kuwachafua viongozi ilianzishwa na CCM.
Bw. Ngombale-Mwiru alisema serikali haijazipata nyaraka zinazodaiwa kuwa ndiyo ushahidi wa baadhi ya viongozi kuhusishwa na ufisadi na rushwa na kuongeza kuwa zikiwafikia watatoa taarifa.