SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN --- II -- 12*


ILIPOISHIA
Kwenye majira ya saa sita ya usiku kwa mishale ya saa ya sasa, Roboth akakurupuka kitandani akiwa anakohoa. Hali ya hewa ilikuwa nzito, na kadiri alivyokuwa anahema, ndivyo alivyokuwa anakohoa. Akasikia vishindo vya watu dirishani. Haraka akafungua pazia kutazama. Kwa mbali akaona watu wakiyoyoma.
Hakuweza kuzingatia kwa maana alikuwa anakohoa sana. Mama yake akaamka upesi na kuja kugonga mlango. Akamkuta mwanaye anakohoa na huku akivuja jasho jingi. Akamuuliza nini shida, Roboth akashindwa kuongea kwani alikuwa anakohoa kupita kiasi. Alipokuja kutulia, akamwambia mamaye ameona watu wakiwa wanayoyoma.
Zikapita dakika kadhaa, Roboth akatulia na kumweleza vema mama yake. Hakupata usingizi tena, akajilaza akiwa anatazama huku na huko.
ENDELEA
"Unaendeleaje sasa?" Mama akamuuliza Roboth. Yalikuwa majira ya saa moja asubuhi kijana huyo akitaka kwenda kuhudumia mifugo yao bandani.
"Nadhani naendelea vizuri sasa," akajibu Roboth. "Huna haja ya kuhofia tena mama."
"Lakini ni wakina nani hao waliokuja huo muda? Na nini wanataka hapa?" Mama akauliza.
"Sijui!" Roboth akapandisha mabega yake juu. Mama akamtazama na kumwambia akimkazia macho.
"Robo mwanangu, kuwa makini na tafadhali jiwekw mbali na Tattiana kabisa. Haya yote ni kwasababu ya huyo msichana. Najua tu hiyo ndiyo sababu maana sisi hatuna kitu kuchukiwa na yeyote yule. Sina hata deni!"
Roboth akatikisa kichwa akitazama chini. Hakusema kitu akajiondokea zake mama yake akimtazama akienenda.
"Ndiye kitu pekee nilichobaki nacho. Tafadhali, Mungu nilindie mboni yangu," akasema mama machozi yakianza kujikusanya machoni. Mwanaye alipozama bandani, naye akazama ndani.

***

"Itamchukua muda gani kufika?" Akauliza Sultan. Alikuwa ameketi kitandani miguu yake ipo chini. Ameshika tama akitazama ukuta kwa macho ya mawazo.
Nyuma yake kitandani alikuwa amelala Sultana mdogo akiwa amejifunika shuka mpaka kiunoni. Alikuwa anamtazama mumewe kwa macho ya mazingatio.
"Nadhani leo ndiyo ataingia," akasema mwanamke. Unajua safari toka kule mpaka hapa yachukua muda sana, ukizingatia pia na umri wake. Tumpe muda."
"Lakini muda haupo upande wetu!" Sultan akasema kwa mkazo. "Tukiendelea kungoja mke wangu atafia kitandani. Haitakuwa na maana tena kwake kuja."
"Hatakufa, usijali," Sultana mdogo akamfariji akimpapasa mgongo kwa kiganja chake kilaini.
"Hatakufa?" Sultan akatahamaki. Akamtazama mkewe na macho duwazo.
"Umemuona namna alivyo? Kila siku anakonda na kudhoofika. Analia usiku mzima na analalama siku nzima. Uso wake umekuwa mweusi na hakuna tena nguo inayomkaa mwilini! Amekuwa mtu wa kufunikwa na shuka, wa kulishwa na kunyweshwa kwa nguvu!"
Macho ya Sultan yakawa mekundu. Akayafunika kwa kiganja chake akiinamisha uso wake chini.
"Sikuwahi kujua kama kuna kitu kitakuja kunishinda ingali mimi ni Sultan. Nilidhani ukiwa kiongozi mkubwa, basi utafanya vile unataka, vile unapenda, tena kwa wakati wowote! Hautakuwa na shida yoyote kwani utatimiza mambo kwa kutoa amri tu. Kumbe nilikuwa nakosea. Sikuwa sahihi hata kidogo, na ona sasa ninavyohenyeka. Usultan wangu umeshindwa kufua dafu na sasa namwona mke wangu akifa mbele ya macho yangu nikiwa sina la kufanya."
Sultana mdogo akanyanyuka na kumkumbatia mumewe kwa nyuma. Akamtaka asihuzunike sana kwani yeye yupo na anaamini haya yote yatakwisha kwa kheri.
"Hakuna lisilo na mwisho, laaziz. Litachukua muda lakini litakoma tu. Naamini bibi atamsaidia kabisa akarejea kwenye hali yake."
Japokuwa kinywa cha Sultana huyu kilitoa maneno matamu kama tende, moyoni mwake kulikuwa kuna mgogoro mkubwa. Hakuwa na raha kabisa. Sultan alikuwa kivuli tu mbele ya macho yake.
Tangu amefika mwanaume huyo hajamgusa kwa lolote, hili lawezejanaje na ingali aliweka dawa zake kama alivyoelekezwa na bibi yake? Kwenye pindo la nguo, na hata barabarani?!
Kila alipomtazama Sultan, hakuona kama mwanaume huyo anamtazama kwa mahaba. Kila alipojaribu kumchombeza, kumlaghai ama kumchokomoa kimahaba, hakufanikiwa abadani!
Alishakaa kila mkao, akamgusa kila eneo, lakini mwili wa mwanaume huyo haukufanya kazi. Ni kama vile alikuwa anabonyeza kitufe ambacho waya wake umekata ama ushaota kutu.
Ina maana dawa za bibi zimegoma kufanya kazi? Alikuwa anangoja kwa hamu bibi yake afike na kumuuliza swali hilo. Mwanaume ameshakuja kwenye himaya yake, tena adui yake akiwa hoi, kwanini ashindwe kumpata?
"Unasikia huko nje?" Sultan akamshtua kwa kumtikisa. Akakurupuka na kuuliza.
"Kuna nini?"
"Nadhani kuna ugeni," Sultan akajibu. "Ina maana hujasikia?"
"Hapana! Sijasikia," Sultana akasema akipandisha mabega.
Basi wakanyanyuka na kujiandaa, punde kijakazi akaja na kuwaambia kuna ugeni wa bibi huko sebuleni. Wakiwa wamejiandaa, wakatoka kwenda kukutana na bibi. Wakamkaribisha kwa bashasha na kumpatia pole ya safari.
Bibi alikuwa amevalia gauni lake refu maridadi likiwa na urembo urembo wa maua ya kudarizi.
"Niwape pole nyie mnaouguza. Vipi, hali ni shwari?"
"Hapana!" Akasema Sultan akitikisa kichwa. "Hali si nzuri kabisa!"
Haraka Bibi akaenda kuonana na mgonjwa. Alikuwa amelala kitandani akiwa anapepewa na kijakazi wa kike ambaye alitoka punde baada ya watu kuingia.
Mgonjwa huyo alikuwa amejifunika shuka mpaka mabegani. Nywele zake zilikuwa hovyo, sura yake ilikuwa imekondeana, na macho yake yalikuwa yameingia ndani yakizungukwa na rangi nyeusi.
Alikuwa mdhaifu, hata kugeuza macho ilikuwa shida. Hakuwa na nguvu hiyo! Bibi akamtazama na kumpekua, alipomaliza akaenda kuleta vitu vyake na kisha akaomba apewe faragha afanye kazi yake. Basi Sultan na Sultana mdogo wakatoka ndani. Lakini hawakwenda mbali, wakawa wamesimama kwa umbali mdogo toka mlangoni hivyo wakawa wana uwezo wa kusikia yanayoyukia ndani, japo si kila kitu.
"Unadhani atapona?" Sultan akauliza. Alikuwa amejawa na hofu. Mikono yake ilikuwa inatetemeka kwa mbali.
"Atapona usijali," akasema Sultana japo kinafki.
Wakasimama hapo kwa muda wa kama dakika kumi, mara wakasikia sauti kali ya Sultana ikitoka ndani ya chumba. Alikuwa analia kama mtoto lakini hakudumu muda mrefu, akanyamaza na Bibi akatoka chumbani akiwa anatota jasho. Wakaelekea pamoja sebuleni.
"Pole kwa majaribu haya," Bibi akamwambia Sultan. "Tuna kazi kubwa sana ya kufanya kumrejesha mkeo katika hali yake ya kawaida."
"Ni nini shida?" Akauliza Sultan.
"Unaijua shida, Sultan," akajibu Bibi. "Na kwenye hiyo shida, nawe mkono wako unahusika. Inabidi nawe pia uhusike kwenye kuitafutia ufumbuzi."
"Niko tayari kwa lolote ilimradi mke wangu apone!"
"Safi. Tatizo kubwa tulilo nalo ni kupambana na roho ya ndugu yake ambayo inamuwinda na kumkosesha raha na amani. Anashindwa kulala, kula wala kupumzika."
"Tutapambana vipi na kitu kisichoonekana?" Akauliza Sultan kwa pupa.
"Inawezekana, lakini kazi inakuwa kubwa kwasababu ya roho hii iliyoteketezwa haikuwa na hatia. Na pia, ilikuwa ya mlozi mwenye nguvu!"
Kukawa kimya kidogo. Bibi akaongezea kwa kusema:
"Ngoja tuone kwanza. Kuna dawa nimempatia, tuvute subira kwa siku tatu!"
"Ni dawa gani?" Akauliza Sultan.
"Dawa ya kufukiza kwa ajili ya kukimbiza na kutuliza roho za waliokufa."
Punde Bibi alipomaliza kusema hayo, kukatokea sauti kali tokea chumbani. Sauti hiyo haikuwa ya Sultana tena bali ya mwanaume!
"Ni nani huyo?" Sultana mdogo akalipuka kwa hofu. Bibi akawatuliza na kuwaambia hizo ni roho ndizo zahangaika. Lakini sauti hiyo ya ajabu haikukoma, ikaendelea na kadiri inavyoendelea ikawa inakua na kukua.
Kama haitoshi, mlango ukaanza kubamizwa kwa nguvu sana! Sultan na mkewe mdogo wakawa wanahofia sana. Hata walinzi walikuja na kuuliza kama kuna namna wanaweza kufanya.
"Hapana, tunashukuru!" Bibi akawataka waende nje, na akaagiza mapazia ya madirisha yote yashushwe. Muda kidogo ulivyoenda, mlango wa chumba alichofungiwa Sultana mkubwa ukaanza kuvunjwa!
Hapo Bibi akamwambia Sultan na mke wake mdogo watoke nje upesi wamwache peke yake ndani. Haraka wakafanya hivyo, Bibi akafunga milango yote kwa funguo.
Na punde, Sultana mkubwa akatoka chumbani akiwa ameshamaliza kuvunja mlango wote! Alikuwa anatembea kwa nguvu kamili na macho yake yalikuwa na rangi ya bluu!
Akamtazama Bibi, na kumnyooshea mkono akinguruma kama simba.






*****
 
*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN II -- 13*
*Simulizi za series.*

ILIPOISHIA
"Hapana, tunashukuru!" Bibi akawataka waende nje, na akaagiza mapazia ya madirisha yote yashushwe. Muda kidogo ulivyoenda, mlango wa chumba alichofungiwa Sultana mkubwa ukaanza kuvunjwa!
Hapo Bibi akamwambia Sultan na mke wake mdogo watoke nje upesi wamwache peke yake ndani. Haraka wakafanya hivyo, Bibi akafunga milango yote kwa funguo.
Na punde, Sultana mkubwa akatoka chumbani akiwa ameshamaliza kuvunja mlango wote! Alikuwa anatembea kwa nguvu kamili na macho yake yalikuwa na rangi ya bluu!
Akamtazama Bibi, na kumnyooshea mkono akinguruma kama simba.
ENDELEA
Bibi akasema maneno fulani kwa lugha ngeni. Akayarudia maneno hayo mara tatu huku akihakikisha macho yake hayabanduki usoni mwa Sultana mkubwa. Alikuwa anamtazama ndani ya macho yake ya bluu pasipo na hofu.
Maneno hayo yalipokuwa yanatamkwa, Sultana mkubwa akawa anaghafirika. Anatoa sauti kali ya kilio, lakini hakukoma kumsogelea Bibi. Alikuwa na dhamira ya kutimiza hilo!
Basi Bibi akabadili maneno na kuanza kutamka mengine. Nayo akatamka mara tatu kama yale ya mwanzoni. Mara Sultana akaanza kupepesuka kana kwamba anasukumwa na upepo mkali. Akarudi nyuma hatua tatu, lakini kwanguvu, akapambana na kuendelea na zoezi lake la kusonga mbele!
Sasa alikuwa amebakiza hatua chache kumfikia Bibi! Akanguruma kama simba akiwa amekunja vidole vyake kama waya wa chuma. Mishipa ilikuwa imemsimama kama mabomba ya maji na jasho likimchuruza.
Ungeweza kubashiri ni namna gani angefanya endapo angemtia Bibi mikononi. Alionekama ana njaa ya uhai wa mtu, ama damu ya mtu! Hakuonekana kama mwenye masikhara hata kidogo.
Kwa mara nyingine, Bibi akasema maneno yake ya ajabu:
"Mere na kebu, khakav shindavata meril!" Akarudia tena:
"Mere na kebu, khakav shindavata meril! ... Mere na kebu, khakav shindavata meril!"
Sultana akaanguka chini! Puh! Akatulia tuli kwa muda wa kama sekunde kumi na tano. Ni kama vile hakuwa hai. Hakuonekana kama ana dalili za kuhema. Bibi akamtazama kwa umakini na kwa tahadhari. Alikuwa ameegemea ukuta, macho yake akiwa kayafinya na makunyanzi yake ya uzee.
Baada ya sekunde kumi na tano, Sultan akaanza kuonyesha ishara ya kuhema taratibu. Bibi akaita:
"Samiraa! ... Samiraa!"
Kulikuwa kimya. Sultana alikuwa anaendelea kuhema taratibu akiwa ameegemeshea uso wake chini. Bibi akapiga hatua mbili kumsogelea. Ila bado akiwa kwenye tahadhari, hakutaka kuwa karibu kabisa na mwanamke huyo.
Akaita:
"Samiraa! ..."
Kimya. Akasogea hatua nyingine karibu.
"Samiraa!"
Kimya.
Mara Sultana akaanza kuhema kwanguvu, kwanguvu na kwanguvu! Kabla Bibi hajafanya kitu, Sultana akanyanyuka na kusimama upesi mno kwa haraka ya kufumba na kufumbua, akamsukuma Bibi kwa mbali akitumia mikono yake yenye nguvu!
Bibi akarushwa kana kwamba amepigwa na shoti ya umeme. Akabamiza ukutani na kudondoka chini akilalama kwa maumivu. Si kichwa wala kiuno kilichokuwa muhali.
Basi Sultana ambaye sasa alikuwa amezidi kunenepeana misuli, akapaza sauti yake kwa hali ya juu! Hakuwa binadamu sasa bali mnyama. Rangi yake ya mwili ilikuwa nyeusi, macho yake makubwa rangi ya bluu na mdomo mpana mwekundu.
Alipomaliza kunguruma, akamfuata Bibi aliyekuwa hoi chini, akamkaba kwanguvu huku akilaani kwa maneno ya lugha isiyoeleweka. Bibi akahangaika sana kujikomboa na uhai wake. Lakini nguvu zake hazikuwa kutosha abadani kupambana na jitu lile.
Akaminywa sana koo. Mikono yake ya kizee ikajitahidi kupapasa na kupambana. Macho yake yaanza kutokomea utosini, na mapigo yake ya moyo yakaanza kupungua. Alikuwa anaelekea kufa!
Mikono yake ikaanza kulainika. Ikapapasa mikono ya muuaji wake taritbu ikielekea kuanguka chini.
Lakini kabla zoezi halijafanikiwa, mara pazia la dirisha linafunguliwa na mwanga wazama ndani. Alikuwa ni Sultan anachungulia, na hiyo ndiyo ikawa salama ya Bibi!
Haraka Sultana akamwachia Bibi na kukimbilia kule dirishani. Akapambana na dirisha kwa fujo kana kwamba anapambana na mtu. Sultan akarudishia pazia upesi. Lakini Sultana akalivutia pazia chini, na akaendelea kupambana na dirisha. Afadhali dirisha lilikuwa ni la chuma.
Kadiri Sultana huyo alivyokuwa anapambana hapo, akapoteza nguvu na mwishowe akadondoka chini na kuzirai.
Sultan na mkewe mdogo wakaingia ndani upesi. Wakamkuta Bibi akiwa hajitambui, yupo hoi.

***

"Nadhani ndiyo siku yenyewe. Leo itakuwa hatma yetu," akasema Seth. Wakiwa ndani ya shimo walikuwa wanasikia milio ya ngoma huko nje kwa mbali.
Malkia alikuwa amekaa chini akiwa amejikunyata, Zura alikuwa amejilaza, pamoja pia na Fluffy.
"Sasa tutafanya kitu gani?" Akauliza Fluffy. "Tutaondoka na hao watu kwenda nao Misri?"
"Haiwezekani!" Akadakia Malkia. "Hilo haliwezekani hata kidogo!"
"Lakini kwanini?" Akauliza Seth. "Huoni kama hilo ni bora kuliko kufa hapa?"
"Tutaenda nao mpaka wapi, Seth?" Akauliza Malkia akisimama. "Huoni kama kwenda nao ina maanisha tutakuwa chini yao safari yote? Na hata hicho tunachoenda kufuata huko, kitakuwa ni chao?"
"Malkia, inabidi tufanye kitu. Hatuwezi tukafa hapa!" Akasisitizia Fluffy.
"Muda si mrefu tutakuja kuchukuliwa hapa, hicho mnachowaza mkiseme haraka!" Akasema Seth. Kwa muda kukawa kimya kidogo.
Huko nje, jitu moja kubwa likapewa ishara ya kichwa na mkuu wao. Majitu yote haya yalikuwa yameshakusanyika mbele ya tanuri kubwa lililokuwa linawaka moto wa kijani. Wote walikuwa wamesimama isipokuwa mkuu, yeye alikuwa amekalia kigoda kikubwa mkono wake akiuegemezea juu ya goti.
Basi jitu lile lililopewa ishara likajiondokea kuelekea shimoni walipotiwa mateka Malkia na wenzake. Punde, likatoka na mateka likiwa limewakusanyia kwenye mkono wake mmoja. Likawabwaga mbele ya mkuu!
"Tevtev kashiromata lasopa?" Mkuu akanena akiwa ametoa macho. Alikuwa anamtazama Malkia akiwa anangojea kwa hamu kauli itakayotoka kinywani mwa mwanamke huyo.
"Anauliza umefikia maamuzi gani?" Seth akakalimani kilichonenwa.
Malkia kabla hajajibu, akamtazama Seth na macho ya sisitizo, kisha akamwambia kwa sauti ya pole:
"Nimekuamini." Alafu akamgeukia Mkuu yule wa Azeth, akamwambia kwamba wameridhia kwenda nao kwenye safari ya Misri. Mkuu wa Azeth akatabasamu na kutikisa kichwa chake. Akampomgeza Malkia kwa maamuzi yake, kisha akateua watu wawili wa kuongozana nao kuelekea Misri.
Lakini kabla, akawataka Malkia na wenzake wawapatie faragha, wakasogea kando. Mkuu huyo akawa anateta na watu wake akiwapa maelezo.
"Unadhani atakuwa anawaambia nini?" Fluffy akauliza. Macho yao yalikuwa yakiwatazama majitu hayo yakinong'ona.
"Sijui atakuwa anawaambia nini, ila si kizuri kwetu," akasema Malkia.
Haikupita muda mrefu, wakaitwa. Wakakabidhiwa majitu yale mawili kwa ajili ya kuendelea na safari.
"Seth, una uhakika na kile ulichokisema?" Malkia akauliza.
"Ndio, kwa asilimia zote. Usijali," Seth akasema kwa kujiamini akitikisa kichwa. Safari ikaanza.
Hakukuwa na maongezi sana huko njiani. Kabla hawajakiacha mbali kijiji cha Azeth, farasi wa Malkia akajiri tokea misituni. Malkia akamkumbatia na kumpanda mnyamawe anayempenda.
Lakini walivyotembea kwa umbali mfupi tu, farasi huyo akaanza kulegea na kukosa nguvu. Ghafla akadondoka chini na kupoteza fahamu. Malkia pamoja na wenziwe wakastaajabu nini kilitokea.
Jitu moja, kati ya wale majitu mawili ya Azeth, likampekua farasi huyo kwa kumnusa na kumkagua mwili, kisha likasema:
"Venerdi kashaka!"
"Anamaanisha nini?" Malkia akawahi kuumuliza Seth.
"Amepewa sumu!" Seth akajibu upesi.
"Waulize kama kuna namna ya kunsaidia, tafadhali!"
Seth akafanya hivyo. Malkia akaona majitu yale yakitikisa kichwa.
"Tafadhali, waombe wamsaidie. Tafadhali!" Malkia akasisitiza.
Seth akawaambia. Wale majitu wakamjibu kuwa farasi huyo atakuwa amekula majani ya sumu, au amepewa sumu.
"Na wakina nani?" Malkia akawahi kuuliza.





***
 
Shunie plz would you marry me? I need these stories on bed 😛😛.


Tevtev kashiromata lasopa, Shunie?😀😀
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom